Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 1/22 kur. 21-23
  • Ni Nani Ataeneza Evanjeli Katika Uingereza?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ni Nani Ataeneza Evanjeli Katika Uingereza?
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Msingi Usio Hakika
  • Kufafanua Malengo
  • Jukumu Tata
  • “Habari Njema”—Chanzo Chayo
  • Alama za Ukristo wa Kweli
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
  • Je, Watahubiri Mlango kwa Mlango?
    Amkeni!—1995
  • Uenezaji wa Evanjeli—Mahali Pao Katika Ibada ya Kweli
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1983
  • Kanisa—Mabadiliko na Mvurugo
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 1/22 kur. 21-23

Ni Nani Ataeneza Evanjeli Katika Uingereza?

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA

UHAI wa makanisa ya Uingereza unapungua kwa kiasi cha karibu washirika 1,500 kwa juma, laripoti The UK Christian Handbook. Wachanga wanaliacha kanisa, The Times lapiga mbiu, “kwa sababu wao waliona kuwa lenye ukimwa na upweke.”

Ingawa makanisa ya Kianglikana yafunga kazi kwa kadiri ya moja kwa juma, kuna “maelfu ya watu wanaotafuta maana na kusudi la maisha zao,” lakiri Church Times la Kanisa la Uingereza.

Kwa kukabiliwa na shida kubwa hii, makanisa ya Uingereza yaliungamana katika 1990 kuendeleza “Mwongo wa Uenezaji Evanjeli.” The Scotsman lilisema miaka ya 1990 “huenda hata ikawa ndiyo mwongo ule ambamo uenezaji evanjeli warudishwa na Makanisa ya kimapokeo, yaliyoimarishwa ili kujaribu kuongezea ushirika uliopunguka kwa kadiri ya kusikitisha na ili kubadili ule mwelekeo wa kugeukia mambo ya kilimwengu.”

Ni tumaini lenye thamani kubwa—lakini laweza kutimizwa? Ni nini limetendeka miaka michache iliyopita?

Msingi Usio Hakika

Makasisi wa Kanisa la Uingereza hawakutokeza idili nyingi kwa ajili ya ule “Mwongo wa Uenezaji Evanjeli” kwenye Mkutano Mkuu wao wa 1989. Kwa kielelezo, mwenyekiti wa Church Union’s Mission and Renewal Committee alikazia hivi: “Matayarisho ni ya maana kabisa,” lakini akaongezea hivi kwa tahadhari: “Katika visa fulani, huenda hiyo ikachukua mwongo wote.”

Askofu Gavin Reid alitabiri hivi: “Itakuwa kampeni yenye usumbufu baada ya miaka mitano.”

Bila kukata tamaa, Waanglikana walifanyiza upesi sera ya muungamano pamoja na Wakatoliki wa Kiroma, waliokuwa wamejianzishia “Mwongo wa Uenezaji Evanjeli” katika 1988. Madhehebu mengine yaliyo mengi yalikuwa na shaka fulani. “Ni lazima nikiri kuwa nahisi wasiwasi juu ya ule Mwongo wa Uenezaji Evanjeli. Huo ni mtajo wenye kusikika ukisifika sana, lakini wamaanisha nini?” akauliza Paul Hulme, mhudumu wa Kikanisa cha Wesley katika City Road, London. “Ni nini tupaswalo kuwa tukifanya tusilolifanya tayari?”

Kufafanua Malengo

Kueneza evanjeli ni kuihubiri gospeli, au habari njema, kugeuza wasikiaji wafuate Ukristo—jambo linalotofautiana sana na lile ambalo viongozi wa kanisa wangetaka kuona. “Si kazi yetu kugeuza watu wafuate Ukristo,” akapiga mbiu Dakt. Newbigin wa United Reformed Church. “Hiyo ni kazi ya Mungu.” Ni nini kilichochochea taarifa hiyo isiyo ya kawaida? Ni ule mkazo unaoongezeka wa jamii ya watu wa Uingereza yenye makabila mengi ikiwa na dini za kikabila zisizo za Kikristo. Fikiria yanayofuata:

“Ule Mwongo wa Uenezaji Evanjeli huenda ukanoa kama miongo mingineyo,” alisema rekta Mwanglikana Neil Richardson, “lakini uendeleapo kuwapo kwa kujikokota, huo ni kikengeushi cha kuondoa fikira kwenye suala linalohitaji kushughulikiwa haraka linalokabili makanisa na kila mtu mwingineye: mkabiliano wa dini mbalimbali uwezao kuzusha mfoko mkali katika majiji yetu yote.” Akionyesha tatizo lenyewe hasa, aliendelea kusema: “Mahusiano kati ya sehemu za jumuiya ya kidini yahitaji kuwa juu ya msingi wa uhakika imara kwamba hakuna mtu anayetafuta kugeuza au kuongoa watu.”

Akijua vema juu ya hali hii ‘iwezayo kuzusha mfoko mkali,’ George Carey, Askofu-Mkuu wa Canterbury, aliutangaza “Mwongo wa Uenezaji Evanjeli” kuwa “mtajo ovyo” kwa sababu viongozi Waislamu na Wayahudi walihisi walikuwa wakilengwa na “waevanjeli sugu.” “Ni kosa,” alisema baadaye, “kusema kama wengine wafanyavyo kwamba jukumu la kwanza la kanisa ni kueneza evanjeli.”

Askofu Michael Marshall, kwa upande ule mwingine, ashikilia kwamba uhitaji wa msingi ni kwamba Kanisa la Uingereza ‘ligeuzwe kuwa Kanisa la Mungu katika Uingereza,’ huku Waislamu na wengine wakiletwa ndani ya zizi la Kikristo. “Ule mwito wa kuuvutia Uislamu uje upande wa Kristo umewekwa katika mjadala,” akapiga mbiu, akionya kwamba mfikio wa jinsi hiyo “pasipo shaka utahusisha mwongo wa mkabiliano.”

Namna gani Wayahudi? “Uenezaji Evanjeli wa Kweli Lazima Utie Ndani Wayahudi,” kikasema kichwa kikuu cha Church Times. Lakini David Sheppard, askofu wa Liverpool, alikataa kwa uthabiti. “Lengo kuu la ule Mwongo wa Uenezaji Evanjeli lazima liwe ni kuelekea wale ambao wamepotoka katika imani au wasiopata kamwe kujua maana ya kuamini katika Mungu,” akasema. Je, hili lawezekana? Neil Richardson, akiandika chini ya kichwa kikuu “Hasara za Uenezaji Evanjeli” cha The Guardian, ashikilia hivi: “Kila mtu [katika Uingereza] amekuwa na fursa ya kutosha kukadiria thamani ya madai ya Ukristo. Ni wazi kwamba walio wengi wameamua kwamba hauwafai.”

Je, makanisa ya Uingereza yametayarishwa kwa vifaa ili kueneza evanjeli katika jumuiya ya jinsi hiyo yenye imani nyingi sana na tamaduni za kikabila?

Jukumu Tata

Aliyekuwa askofu-mkuu Dakt. Runcie alitangaza hivi: “Maofisa wetu katika uenezaji evanjeli ndio maaskofu na makasisi, wamishonari wetu ndio watu wa kawaida.” Mweneza-evanjeli wa siku nyingi Gilbert W. Kirby alisema hivi: “Kila mkristo apaswa kuweza kueleza mwingine mambo ya msingi ya ile imani. Kila mkristo apaswa kufundishwa jinsi ya kuongoza mwingine kwenye Kristo. . . . Shabaha yetu yapasa iwe kuwa na washirika wa kanisa waliofundishwa. . . . Ni kazi bure kuwaambia watu waeneze evanjeli bila kuwaonyesha jinsi ya kufanya hivyo.” Yaani, maaskofu na makasisi ni lazima watoe uongozi katika kuonyesha makundi yao jinsi ya kueneza evanjeli.

Akisema wazi katika “Mhadhara wa Ukumbusho wa Priestland” wa BBC, mtangazaji wa redio Brian Redhead alisema: “Wenye vichwa vilivyofunikwa kwa shela za kipadri wapaswa kuukubali uhakika wa kwamba wameupoteza uwezo wa kuvuta uangalifu wa watu wasiojali dini . . . Ni lazima watie mkazo mkubwa zaidi juu ya ustadi wa kuhubiri.” Na hili lapasa kufanyiwa wapi?

Mwanzoni mwa karne hii, William Wand, aliyekuja baadaye kuwa Askofu wa London, alipokea mazoezi yake ya mapema katika Lancaster, Uingereza, wakati ilipokuwa kawaida ya wachungaji kuzuru watu. “Nafikiri kwamba hesabu kubwa zaidi ya milango niliyopata kubisha hodi katika alasiri yoyote ile ilikuwa arobaini,” akaandika baadaye. “Vikari huyo alikuwa mwenye bidii sana pia kuangalia mahitaji ya watu wachache waliokuwa hawaelekei kamwe kuja kanisani. Alihangaikia kufanya ule uitwao sasa ‘mpenyo’ dhidi ya utepetevu na ubaridi huu.”

Ingekuwa tofauti isiyo ya kawaida kwelikweli ikiwa kasisi yeyote angefanya mwonano huo wa kibinafsi leo katika Uingereza! Makanisa ya Uingereza yanatambua yakiwa yamechelewa mno kwamba hakuna njia iliyo badala ya kuenezea watu evanjeli katika nyumba zao, katika njia ambayo Yesu na wanafunzi walifanya hivyo.

“Ni mtu aliyejitoa kwelikweli peke yake awezaye kuvuta wengine kwa Mungu,” laonelea Evangelism and the Laity. “‘Fanya kazi ya mhubiri wa Injili’ [2 Timotheo 4:5] . . . ni amri ambayo lazima itiiwe kwa njia fulani na kila Mkristo ikiwa Kanisa litatimiza kusudi lalo katika kizazi chetu.”

“Habari Njema”—Chanzo Chayo

John Taylor, mwandishi mkuu wa Mgawanyo wa Huduma za Kanisa la Kimethodisti, aliandikia The Times la London juu ya “wajibu wetu wa kushiriki habari njema.” Alisema: “Kwa hiyo ni lazima kanisa litafute njia mpya na zenye matokeo zaidi za kuwalea na kuwafundisha washirika walo lenyewe. Hata ndani ya kanisa mna ukosefu mkubwa ajabu wa kuyajua maandiko ya Kikristo.” Ukosefu huu wa ujuzi umeongoza washirika walo kwenye nini?

“Waevanjeli kadhaa vijana mashuhuri . . . wasisitiza kwamba uanafunzi wa Kikristo wadai kuwe na aina mahususi za hatua ya kijamii na ya kisiasa,” aeleza Rachel Tingle katika Another Gospel?—An Account of the Growing Involvement of the Anglican Church in Secular Politics. Hii “Theolojia ya Ufalme,” kama vile itajwavyo kuwa, hushikilia kwamba Ufalme wa Mungu hutanuliwa kufika duniani wakati amani, haki, na “uadilifu wa kijamii” zianzishwapo kwa njia za kisiasa. Bila shaka, hii ni “Theolojia ya Ukombozi,” au “Usoshalisti wa Kikristo” wa kale uliojivika kisingizio cha kisasa.

Kufikiri kwa jinsi hiyo kwapatanaje na taarifa ya Yesu mwenyewe: “Ufalme wangu si sehemu ya ulimwengu huu. . . . Ufalme wangu si kutoka chanzo hiki”? (Yohana 18:36, NW) Au na maneno ya nabii mmoja wa mapema zaidi: “Katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele”?—Danieli 2:44.

Angalia kwamba Ufalme huu waanzishwa na mikono ya Mungu—si ya mwanadamu. Ukombozi kutoka kwenye vita, kutoka kwenye ukosefu wa haki, na hata kutoka kwenye kifo chenyewe utakuja kutoka kwa Yehova kupitia Mfalme wake aliyewekwa rasmi, Yesu Kristo—si kutoka kwa mwanadamu. Kweli hiyo ni habari njema ihitajiyo kupigiwa mbiu!—Ufunuo 21:3, 4.

Leo, Mashahidi wa Yehova, ambao idadi yao ni karibu 130,000 katika Uingereza pekee, hushiriki usadikisho huohuo. Wakiwa wamevutwa kutoka vikundi vyote vya kitaifa na imani za kidini, wao wameungamana wakiwa Wakristo. Wao ni waeneza-evanjeli waliozoezwa vema wakiwa na hamu nyingi ya kuishiriki habari njema pamoja na wote watakaosikia. Kwa kusudi hili wao hutumia kila njia ipatikanayo, na wengi wananufaika kutokana na huduma yao yenye matokeo.

[Sanduku katika ukurasa wa 23]

Waevanjelisti wa Uingereza

Dondoo linalofuata limetolewa katika gazeti la kila juma la Katoliki ya Kiroma ya Uingereza, Catholic Herald, Oktoba 22, 1993, ukurasa 8.

“Ni nini kilichopata ule mwongo wa uenezaji evanjeli? Kweli ulipatwa na nini! Miaka miwili iliyopita mwezi ulikuwa haumaliziki bila huo kufanyika na ilikuwa vigumu juma moja kupita kabla haujatajwa katika matbaa. Leo je? Kimya kabisa. . . .

“U wapi ule uharaka uliowasilishwa na Yesu wakati Yeye alipokuwa akituma wanafunzi Wake wakaeneze evanjeli katika vijiji vilivyowazunguka? Au uliowasilishwa na Mt Paulo: ‘Ole wangu nisipoihubiri Injili! (1 Ko 9:16).’

“Pia kuna lile tatizo la kwamba Wakatoliki wengi hawathamini kwamba uenezaji evanjeli si hiari bali ni amri iliyoagizwa na Kristo Mwenyewe: ‘Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi’ [Mathayo 28:19]. . . .

“Ni Wakatoliki wangapi ambao huelewa imani yao vya kutosha kuwafanya wakabiliane na watiaji shaka? . . . Ni ajabu kama nini kwamba, Mwana wa Mungu akiisha kuja duniani, ni wachache sana kati yetu hujihangaisha kujifunza aliyoyasema Yeye. . . .

“Sasa mimi sitetei Mashahidi [wa Yehova]. . . . Lakini lifikirie kidogo jambo hili kwa upande ule mwingine. Msimamo wao wa kiadili, ambao msingi wao ni imani katika viwango vya Mungu vyenye mamlaka kamili, hauwezi kutiliwa shaka. Kuongezea hilo, kila Shahidi alitoa kitu kama jioni tatu ziwe za mafundisho, funzo la Biblia lenye utaratibu, na maisha ya Kikristo yenye kutumika siku kwa siku, mara nyingi wakiwa katika nyumba za mtu na mwenzake.

“Si hilo tu, bali pia kila Shahidi hufundishwa kwamba, kutokana na wito wake wenyewe, yeye kwa lazima ni mishonari. Yeye hufundishwa njia za kikazi zihitajiwazo kutokeza ujumbe wake. Kubisha hodi mlangoni, kwenda nje wawili-wawili, ni sehemu kuu ya maisha yake. Mashahidi ni wenye bidii pia katika kuwatunza maskini na wahitaji.

“Kwa ufupi, . . . ni vigumu kutokukumbushwa juu ya Kanisa la mapema kama lionyeshwavyo katika matendo ya Mitume. Na mwungwana ni kitendo. Ukuzi wao umekuwa wa kishindo. Upigaji mbiu wa wazi waweza kufanya mambo!”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki