Kuutazama Ulimwengu
Visa Vingapi vya Utoaji-Mimba?
“Ulimwenguni karibu visa milioni 33 vya utoaji-mimba ukubaliwao na sheria hutukia kila mwaka, na ikiwa visa vyote vya utoaji-mimba usiokubaliwa na sheria vingeongezwa kwenye hivyo, jumla ingekuwa kati ya milioni 40 na milioni 60,” lasema gazeti la asubuhi la Buenos Aires Clarín. “Asilimia 76 ya idadi ya watu wa ulimwengu huishi katika nchi ambako utoaji-mimba wa makusudi hukubaliwa na sheria.” Idadi ya maisha zikomeshwazo kwa kutolewa mimba ni zaidi ya idadi ya watu wa Argentina na yalinganika na kufutilia mbali idadi nzima ya watu wa nchi moja kama vile Afrika Kusini, Italia, Misri, Ufaransa, Uingereza, au Uturuki kila mwaka. Yalingana na watu waliouawa katika miaka yote sita ya vita ya ulimwengu ya pili, wakadiriwao kuwa karibu watu milioni 50.
Ndipo Mahali Bora Zaidi pa Kuishi?
Kanada imeamuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa ndipo mahali bora zaidi pa kuishi ulimwenguni. “Ndiyo mara ya pili katika muda wa miaka mitano faharisi imekusanywa kuonyesha kwamba Kanada imeshika nafasi ya kwanza katika orodha ya nchi 173,” laripoti The Toronto Star. Laongezea kwamba hii “haimaanishi, hata hivyo, kwamba Wakanada ndio wenye kiwango cha juu zaidi cha maisha ulimwenguni.” Kwa nini Kanada ilionwa kuwa ndipo mahali bora zaidi? Ripoti hiyo, iliyotayarishwa na Shirika la Maendeleo la UM, huzipa nchi namba kwa kutegemea mambo matatu yakiunganishwa pamoja: mapato ya wastani, utimizo wa kielimu, na utarajio wa maisha. Wakanada walishika nafasi ya sita katika urefu wa maisha, wakiwa na wastani wa muda-maisha wa miaka 77.2. Kanada ilikuwa karibu na nafasi ya kwanza kwa habari ya fedha zilizotumiwa kwa elimu na utunzaji wa afya, na pia katika kumiliki vitu kama vile televisheni na magari.
Vikundi vya Kihindi vya Brazili
“Brazili ingali ina vikundi vya Kihindi 59 vikaavyo peke yavyo kabisa, au vyenye kuonana na watu weupe mara kwa mara tu tena bila urafiki,” laripoti O Estado de S. Paulo. “Kati ya jumla hii, ni vikundi tisa tu vimetambuliwa tangu mwanzo wa miaka ya 1980 na National Indian Foundation.” Makabila mapya yaendelea kupatikana katika misitu ya Amazon. Walio wengi wa Wahindi wakaa-peke-yao huishi katika vikundi vya watu 150 au wachache zaidi. Brazili ina maeneo ya Kihindi 532, vikundi tofauti 180 vya kikabila, na Wahindi elfu 260. Wao hukaa katika jumla ya kilometa za mraba 909,705—karibu asilimia 11 ya eneo la Brazili—ingawa nusu ya maeneo haya hayana mipaka iliyothibitishwa. Katika jitihada ya kusaidia makabila yaimarishe vifungo vya mahusiano na kuokoka maingilio ya ulimwengu wa kisasa, waanthropolojia wamekuwa wakifundisha washirika wa kikabila jinsi ya kutumia kamera ya video ili waweze kurekodi desturi za kijiji na kushiriki tepe hizo na vikundi vingine vya karibu. Majuzi, baada ya kuona filamu za kikundi hiki na hiki, Waiapi na Zo’é walikutana. Wakisema lahaja zifananazo, walizungumza mapokeo na desturi zao, na pia njia zao za kuwinda, kuponya, kupika, na kufuma kwa uzi.
Shughuli Yenye Mafanikio
Kikiwa na “fahari halali kabisa,” lasema gazeti la Kiitalia La Stampa, kikoa cha kitiba kilichompasua Papa John Paul 2 katika Aprili kilitaarifu kwamba ule upasuaji wa kiuno “usingaliweza kuwa bora kuliko ulivyokuwa.” Lakini mapasuo aliyofanyiwa papa wa wakati wa sasa hayajawa na matokeo bora zaidi sikuzote. Alipopasuliwa kufuatia lile jaribio la 1981 la kumuua, John Paul 2 alilazimika kukaa hospitalini kwa miezi miwili ili atibiwe ambukizo zito mno la virusi zenye kunenepesha chembe lililoletwa na mitio-damu mishipani. Hivyo, haishangazi kwamba, ingawa safari hii, kulingana na La Stampa, “potezo la damu lilikuwa jingi,” hakuna mitio-damu iliyofanywa. Badala ya hivyo, lasema gazeti hilo, “damu ya Papa ilirudishwa, ikahasishwa, na kutiwa upya mishipani wakati wa upasuaji huo.”
Hakuna Ponyo la UKIMWI Lionwalo Karibuni
Kongamano la 10 la Kimataifa Kuhusu UKIMWI, lililofanywa katika Japani katika Agosti wa mwaka uliopita, lilitambua kwamba jitihada za kufanyiza chanjo ili kuzuia UKIMWI na kufanyiza dawa za kuutibu zimeshindwa sana-sana, na hakuna zozote zitarajiwazo kupatikana kufikia mwishoni mwa mwongo huu. “Tuko kwenye mwanzo tu wa kipuku cha H.I.V. ulimwenguni,” akasema Dakt. James Curran wa Centers for Disease Control and Prevention katika Atlanta, Georgia. Watu wapatao milioni 17 ulimwenguni pote walisemwa kuwa wameambukizwa, hao wakiwa ni milioni 3 zaidi ya mwaka uliotangulia. Kwa kuhuzunisha, milioni moja kati ya idadi hii walikuwa watoto. Ikiwa kadiri iyohiyo itaendelea, jumla ya watu kutoka milioni 30 hadi 40 wataambukizwa kufikia mwaka 2000, lasema Shirika la Afya Ulimwenguni. Visa vilivyopevuka kabisa vya UKIMWI viliongezeka kwa asilimia 60 katika muda wa miezi 12, vikileta ile jumla ya katikati ya 1994 iwe milioni nne, kutia na wale ambao wamekufa. Yaweza kuchukua hadi miaka kumi kati ya wakati wa kuambukizwa HIV na mwanzo wa dalili za UKIMWI. Kwa sababu ya maendeleo ya polepole katika kupambana na kipuku kikubwa kinachoongezeka, ilitangazwa kwamba kongamano hilo la UKIMWI lingefanywa kila miaka miwili badala ya kila mwaka, huku mkutano ufuatao ukiratibiwa uwe Julai 1996 katika Vancouver, British Columbia, Kanada.
Watoto Waathiriwa Mapema Maishani
“Mwelekeo wa mapema wa mtoto kuhusu ulimwengu hutegemea kwa kadiri kubwa kipimo cha ulezi ambao yeye hupokea kabla ya umri wa miaka 3, jambo ambalo nalo huathiri ukuzi wa mishipa ya fahamu na uhakika wa mtoto na uwezo wa kutatua matatizo kwa njia yenye ubuni,” laripoti The Globe and Mail la Toronto. “Vijana wanaoishi katika hali zilizoshuka za kiuchumi na za kijamii wana nafasi haba ya kukua wawe watu wazima wenye matokeo na waliorekebika vema.” Kulingana na Dakt. Fraser Mustard, msimamizi wa Canadian Institute for Advanced Research, watoto kama hao huelekea zaidi kuacha shule mapema na huegemea kutatua matatizo kwa jeuri. “Kadiri yako ya kukuza stadi za kukabili hali ina uzito mkubwa juu ya uwezo wako wa kujipatanisha na mfumo,” akasema. Globe lataarifu kwamba uchunguzi mbalimbali uliofanywa na Chuo Kikuu cha Yale na Chuo Kikuu cha Montreal waonyesha kwamba “uhusiano wenye maana wa kimzazi pamoja na watoto ni wa manufaa kubwa sana kwa ukuzi wa kijana wa kimwili, wa kutambua mambo na wa kihisia-moyo.”
Uwe Mwangalifu Unaposafiri
Unaposafiri, toa uangalifu kwa yale yanayotendeka kukuzunguka. “Wezi wa mizigo na wa mfukoni wana upendelevu usiozuilika wa wasafiri wenye kujisahau kiakili,” laarifu gazeti Claúdia la Brazili. Vivyohivyo, “mtu yeyote akikugonga au akumwagie kitu katika mavazi yako, kaa macho. Hizi ni hila zenye sifa mbaya za kukengeusha uangalifu wako.” Pia, kaa macho ikiwa mtu fulani aomba habari au msaada. Ukengeufu kidogo tu wa fikira huenda ukakuletea hasara ya mizigo yako. Kulingana na Adriano Caleiro wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa São Paulo, uangalifu maalumu wahitajiwa unapotoa mikoba ya nguo katika kituo cha uchunguzi kwenye uwanja wa ndege, unapotia hati sahihi kwenye kaunta za kukodi magari, unapoingia au kuondoka katika hoteli, unapotayarisha watoto kuingia katika teksi, unapotazama madirisha ya maduka, au unapokunywa kikombe cha kahawa. Gazeti hilo lakuonya ubadili kufuli mara hiyo ikiwa funguo zako zimeibwa. Huenda mwizi akasema alipata mizigo yako na hata kurudisha vyote vilivyopotezwa, lakini huenda akawa alitengeneza fungu la funguo za nakala ili aweze kuvamia nyumbani kwako baadaye.
Hakuna Madhara Yaliyokusudiwa
Wageni wanaozuru Japani waonao ishara zikisema “Wageni Hawaruhusiwi” hawapaswi kuudhika wala kukasirika, lasema shirika Helpline la Japani, lichunguzalo malalamiko. Zilizo nyingi za ishara hizo husimamishwa na watu ambao kwa kweli wanajaribu kusaidia. Kielelezo cha njia hii ya kufikiri ni elezo lililotolewa na mwenyeji wa duka dogo la elektroni katika eneo la Akihabara la Tokyo: “Kwa kuwa mimi siwezi kusema [lugha za kigeni] zozote, nimekuwa nikitatiza watu wengi wasiosema Kijapani wajao ndani ya duka langu. Niliwaza jambo bora zaidi ambalo ningeweza kufanya lingekuwa kusimamisha ishara ya jinsi hiyo ili watu wasilazimike kutatizika.” Liliripoti hivi Asahi Evening News: “Katika visa vilivyo vingi ubaguzi hutukia kwa watu ambao wamekuwa na mwonano kidogo na watu wasio Wajapani na ambao kwa hiyo hufikiri kukataa ndiyo njia bora zaidi ya kushughulika na hali hiyo.”
Wapiga-Filimbi-Rangirangi Walioelimishwa
Likitangaza ili kujazia nafasi 76 za cheo cha waua-panya, Shirika la Manispaa ya Bombay walitatizika. “Walio wengi wa waomba-kazi 40,000 na kitu ni wahitimu, waandikishwa-chuoni na walioacha koleji mapema, hali takwa la kielimu kwa muua-panya ni elimu ya shule ya msingi tu,” laripoti Indian Express. “Tungewezaje kumweka rasmi mhitimu awe muua-panya?” ofisa mmoja akauliza. Panya hutafutwa usiku na kuuawa kwa rungu kwa malipo ya rupia 100 (zaidi kidogo kuliko dola 3, za Marekani) kwa kila panya 25 waliouawa sasa hivi. Shirika hilo linatafuta “mpango mzuri zaidi wa kutafuta wafanya-kazi.” Lakini hili silo tatizo pekee ambalo mamlaka za miji zimekuwa zikikabili. Zina tatizo la kidini pia. Washirika wa dini ya Jain, na pia wengine wasioamini yafaa kuua wanyama, wamekuwa wakiwahonga wafanya-kazi wawaachilie panya kwa sababu za huruma ya kibinadamu.