Uvumbuaji wa Jeni ya Binadamu
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
“MRADI wa biolojia wa kwanza ‘wa sayansi ulio mkubwa sana,’” wa sita kati ya “staajabu saba za ulimwengu wa kisasa”—yote hayo ni mafafanuzi ya Mradi wa Jenomu ya Binadamu, jaribio la kimataifa la kukuvumbua wewe! Jenomu ni nini? Ni jumla ya mfanyizo wa jeni zako, sehemu moja iliyorithiwa kutoka kwa baba yako na sehemu ile nyingine kutoka kwa mama yako bali sasa kwa kifani ni wako.
Wanajeni Sir Walter Bodmer na Robin McKie wauita mradi huo wa jenomu “kile Kitabu cha Mwanadamu.” Lakini kukisoma si kazi rahisi. “Kamwe hakuna vitabu vingine vilivyoandikwa vya maagizo vitakavyopatikana na jamii ya binadamu,” adai James Watson, mmoja wa wanasayansi wasifikao kwa kuvumbua umbo la ile molekuli ijulikanayo sana kuwa DNA. “Hatimaye itakapofasiriwa,” yeye asema, “jumbe za jeni zilizopangiliwa ndani ya molekuli ya DNA yetu zitaandaa majibu ya msingi kwa ubuni wa kikemikali wa kuwapo kwa binadamu.”
Kama ilivyo na mradi wowote mkubwa na wenye gharama nyingi wa sayansi, ule Mradi wa Jenomu ya Binadamu una wanaoamini na walio na mashaka. “Mradi wa Jenomu ungeweza kuwa ukiukaji wa hali ya juu wa usiri wa binadamu,” aonya mwandishi wa sayansi Joel Davis, “au ungeweza kuwa ufunguo usio na kifani kwenye uhai uliofanywa upya, kwenye afya, kwenye uponyaji.” Lakini lolote utakalofikia, yeye aamini kwamba “litabadili kabisa taaluma ya jeni” na kwamba “huenda likabadili kabisa asili ya Homo sapiens.” Huko nyuma katika 1989, George Cahill, naibu wa rais kwenye Howard Hughes Medical Institute, alikuwa chanya. “Utatueleza kila kitu,” yeye alisema. “Mageuzi, maradhi, kila kitu kitategemezwa kwa kile kilichoko katika ukanda huo wenye fahari uitwao DNA.”
Jukumu Kubwa Mno
Katika 1988 kikundi cha kimataifa cha wanasayansi kilianzisha HUGO (Human Genome Organization) ili kutoa uangalifu wa kazi ya watafiti wa jenomu katika nchi zinazoshiriki. Wakiwa na matumizi yapatayo dola bilioni 3.5, HUGO huwakilisha matokeo yao katika kompyuta tata. Ingawa kompyuta sasa zaweza kufahamu vijenzi vya habari zilizo nazo, jenomu ni tata mno kiasi cha kwamba wanasayansi hawatazamii kukamilisha kuzisanifu hadi wakati fulani kwenye karne ya 21. Gazeti la Scientific American lakadiria kwamba ikiwa jenomu zingechapishwa katika aina ya kitabu, ingechukua “theluthi moja ya wakati wa maisha” ili kukipitia kwa kusoma.
Baada ya mjadala mwingi wanasayansi waliamua juu ya mkakati ufuatao. Kwanza, wanuia kupangilia jenomu ili kupata zilipo jenasi 100,000. Ikifuatwa na utaratibu ujulikanao kuwa uratibu jenomu, watumaini kuvumbua ule mpangilio wa protini zifanyizazo kila ya jenasi hizi. Lengo lao la mwisho ni kuratibu ile asilimia 95 hadi 98 nyingine ya jeni za mwili wetu.
Je, kufikia yote haya kutavumbua yote yaliyopo ili kujua kuhusu uhai wa binadamu? Je, jenomu ina ‘uandishi wa vitabu vya maagizo vilivyo muhimu sana’ mwanadamu hajapata kuviona? Je, Mradi wa Jenomu ya Binadamu utatoa maponyo ya magonjwa yote ya binadamu? Makala zifuatazo zachunguza maswali haya.