Malengelenge—Kukabiliana na Maumivu
“Maumivu makali mno yaliyokuwa nyuma ya jicho langu yalinitia hofu,” akumbuka Ann. “Nilikuwa na wasiwasi kwamba uvimbe wa ubongo ulikuwa ukikua.”
“Nilipoamka nikiwa na umivu lisilo la kawaida upande mmoja wa fumbatio, niliwaza kwamba ni lazima uwe ni mchochota wa kibole,” Jean hukumbuka.
“Nilikuwa nimepata harara mbeleni,” asimulia Dilip, “lakini nilishangaa kwa nini hii iliuma mno ngozini.”
MALENGELENGE (shingles) hasa ni nini? Katika mtajo wa watu wa kawaida kwa maradhi haya yaonekana hutoka kwa neno la zamani la Kiingereza sengles (likimaanisha “kizingo” au “mshipi”) litokanalo na neno la Kilatini cingulum, likimaanisha “ukanda.” Hivyo, neno hilo halina uhusiano na viezekeo.
Kitiba, yajulikana kuwa herpes zoster (kutokana na mtajo wa Kigiriki herʹpes, ambao umetolewa kutoka herʹpo, ukimaanisha “kutambaa” na zo·sterʹ, ikimaanisha “kuzinga.”) Katika tabia ifananayo na jina, virusi ya herpes ambayo husababisha malengelenge hutambaa kupitia mishipa ya kuhisi na mara kwa mara huzinga kiwiliwili ikiambatana na mfululizo wenye mapindi ya miwako yenye umivu. Maumivu ya mshipa uliochochota mara nyingi yaweza kuwa maumivu yenye kuumiza mno, hivyo mtajo “umivu kali” utumiwao na baadhi ya madaktari.
Dalili za mapema za malengelenge, kama vile homa, kutetemeka kwa baridi, kwa ujumla kujihisi huna afya, mara nyingi huhusisha mafua lakini huenda ikafikiriwa kuwa mshiko wa moyo, uvimbe wa ubongo, au baadhi ya hali nyingine mbaya. Kufa ganzi, kuhisi mnyeo wa juujuu tu, na mchomo mwingi au mwasho unaoendelea kuwa mbaya, maumivu makali huwa ni matatizo yaliyo kawaida ya wauguao malengelenge.
Kwa karibu juma moja hivi tangu mwanzo wa dalili za ugonjwa, ukanda mwembamba wa vipele vyekundu vyenye kuwasha hutokea kando kando ya mfumo wa mishipa ya kuhisi ulioshambuliwa na virusi, kwa kawaida juu ya kiuno na upande mmoja wa mwili. Mahali hasa pa kuvipata ni kwenye kidari, mgongo wa chini, kifuani, shingoni, kipajini, ama macho, ikitegemea kifundo cha mishipa kilichoathiriwa. Mara harara husitawi kuwa vikundi vya vilengelenge, au michibuko yenye umajimaji, ionekanayo kama harara ya ngozi iliyosababishwa na mmea fulani wenye sumu. Kufikia siku kumi hivi, haya huwa na kovu na huanza kuumbuka, katika visa vingi yakiacha jeraha na maumivu yabakiyo yakiwa kikumbusha cha kabiliano la mmoja la malengelenge.
Visababishi, Mweneo, na Makisio ya Ugonjwa
Mmoja anapataje malengelenge? Uwezekano ni kwamba mgonjwa hujiambukiza mwenyewe. Watafiti wa kitiba wamevumbua wakiwa na uhakika usio kamili kwamba virusi ya herpes (varicella zoster) ambayo husababisha malengelenge ni ileile yenye kuenezwa kwa kugusana ile isababishayo tetekuwanga. Hili laelewesha kwa nini mmoja aliye na malengelenge anaweza kuambukiza mwingine (kwa ujumla watoto) tetekuwanga. Hata hivyo, ili kupata malengelenge, mmoja ni lazima kwanza awe alikuwa na tetekuwanga.
Baada ya kuwa na tetekuwanga, kwa kawaida mapema utotoni, mfumo wa kinga hauondoi kabisa kutoka mwilini virusi ya varicella-zoster. Husafiri katika kituo kilicho pekee cha mishipa (watafiti wahisi eneo hili kuwa uti au fuvu), na hapo hukaa bila kutenda mpaka wakati itakapopata kwamba hali zafaa kwa ajili ya kushambulia tena, mara nyingi huwa ni miaka mingi baadaye wakati mfumo wa kinga za mwili unapoelekea kuwa dhaifu kidogo.
Ingawa asilimia 10 hadi 20 ya idadi ya watu kwa ujumla hupata malengelenge wakati fulani maishani mwao, wale walio na uwezekano kupatwa ni wale walio na umri wa zaidi ya miaka 50. Watafiti wakadiria kwamba nusu ya wale wanaofikia umri wa 85 wamekuwa na maradhi hayo. Wanaume kwa wanawake wanaathiriwa karibu kwa usawa. Maradhi hayo yaweza kutokea tena, lakini yafariji kujua kwamba karibu asilimia 2 hadi 4 ndiyo hupata shambulio la pili.
Shambulio la malengelenge mara nyingi huja baada ya kipindi cha ugonjwa mkali, mkazo usio wa kawaida, uchovu wa muda mrefu, na magumu mengine katika maisha ya mmoja. Huenda lifuatie matibabu ya tibakemili, mnururisho, ama taratibu nyingine ambazo huhatarisha ama hudhoofisha mfumo wa kinga wa mwili. Hili shambulio la pili la virusi vya tetekuwanga hutokeza, si kutukia tena kwa tetekuwanga, bali malengelenge, ambayo yana baadhi ya tabia za ujumla za tetekuwanga. Tabia hizi hutia ndani zile hatua za harara, vilengelenge, na makovu, na bado malengelenge ni maradhi yaliyo tofauti.
Malengelenge ni mabaya kiasi gani, nalo shambulio hudumu kwa muda mrefu kiasi gani? Ingawa malengelenge ni yenye kutaabisha mno, maradhi hayo hayahatarishi uhai sana. Lakini mara ukiyapata, jitayarishe kuvumilia majuma kadhaa ya maumivu yenye kuendelea kadiri mwili unavyobuni kinga ili kushughulika na shambulizi la ghafula la ambukizo la kiviini. Kipindi cha maradhi hutofautiana kutoka siku saba hadi kumi katika visa vilivyo vingi, ingawa majeraha yaweza kuchukua majuma manne ili kupona. Ni kawaida kwa wagonjwa wa malengelenge kuwa na maumivu ya mishipa kwa majuma kadhaa, yaitwayo postherpetic neuralgia, kwa majuma kadhaa nyakati nyingine hata miezi, baada ya vilengelenge kuwa vimepotea.
Ikiwa ambukizo laenea jichoni, hili laweza kuathiri mwono wa jicho vibaya sana na laweza kusababisha upofu. Kwa hivyo inashauriwa umwone tabibu wa macho mara moja ikiwa eneo lililoathiriwa ni kwenye uso. Matibabu ya mapema mara nyingi yaweza kuzuia matatizo mazito ya macho.
Matibabu
Ni nini laweza kufanywa ili kutibu malengelenge kwa matokeo? Ingawa tiba nyingi zimekuwa zikijaribiwa tangu nyakati za kale hadi za leo, jibu la unyoofu ni kwamba sayansi ya kitiba bado haijapata matibabu ambayo hufanya vizuri zaidi ya kupunguza athari na kudhibiti maumivu mpaka maradhi yamalize mkondo wayo.
Uchunguzi wa majuzi wa kutumia madawa na kukinga viini katika kutibu maambukizo mbalimbali ya herpes umetokeza matokeo yenye kutoa tumaini katika kutibu malengelenge. Kwa kielelezo, ingawa kwa kukubali acyclovir si tiba, hupunguza kurudufika kwa virusi na huelekea kupunguza maumivu na kipindi cha maradhi hayo katika baadhi ya wagonjwa. Watafiti wasema kwamba kwa matokeo bora zaidi, matibabu yanapasa kuanza mapema.
Katika uchunguzi kwenye Chuo Kikuu Cha Colorado Cha Shule ya Madawa, wagonjwa wenye malengelenge wanaopokea kufikia miligramu 800 za acyclovir kwa kunywa mara tano kila siku kwa siku kumi walipata kwamba ufanyizwaji wa vipele, makovu, na maumivu ulikuwa mdogo kuliko wale waliopokea dawa za kutuliza maumivu. Watafiti wamegawanyika kuhusu kama acyclovir pia hutumika kupunguza ukali wa postherpetic neuralgia. Vidarabine, dawa nyingine ya kukumbana na viini, imekuwa na mafanikio katika kutibu malengelenge. Utafiti waendelea kufanywa juu ya chanjo, lakini hili lingali katika hatua za majaribio.
Wengi ambao wamekwisha kuwa na malengelenge wasema kwamba maumivu yangekuwa yenye kuvumilika ikiwa hayangekuwa yenye kuendelea. Usiku na mchana huendelea, yakichosha akili pamoja na mwili wa mgonjwa.
Wakati wa hizo siku kiwango cha mgonjwa cha maumivu kinapokuwa juu, huenda madaktari wafikirie kumpa dawa zivizazo maumivu kwa siku chache, ingawa hizi huelekea kuwa na athari za kando zisizopendeza. Ikiwa mgonjwa anaweza kuvumilia, kutumia kitambaa chenye maji baridi kwaweza kutuliza. Krimu inayopakwa ngozini yenye asilimia 1 ya silver sulfadiazine ikitumiwa mara kadhaa kwa siku imekuwa yenye kusaidia kwa wengine. Yaache malengelenge usiyaguse; ama kuyafunika kwa bendeji.
Vidonda hivyo polepole vitapona, lakini kwa wengi wanaougua maumivu hayapungui kwa kuwa malengelenge yanashambulia mara ya pili. Postherpetic neuralgia huanza kuathiri mwili, ambayo hasa hulemaza nguvu kwa walio wazee-wazee na kwa wagonjwa walio na athari za kando kwa madawa. Kuvumilia maumivu haya yatekenyayo na kuuma ni vigumu. Steroidikoteksi imejaribiwa, lakini tarakimu za kikemikali hazijafikia mkataa kuhusu uwezo na usalama wa madawa haya yenye nguvu. Matabibu nyakati nyingine hupendekeza antidepressant amitriptyline kunapokuwa na maumivu ya muda mrefu, lakini hii pia yaweza kukuza tatizo, inapotumiwa kwa muda mrefu.
Kwa kushangaza, matokeo yenye kutumainika katika kudhibiti maumivu yamefikiwa na dawa ya kupaka iliyo na capsaicin, ambayo hutokana na pilipili hoho itumiwayo kutengeneza unga wa pilipili hoho. Lakini hii haiwezi kutumiwa hadi michibuko ipone juu. Kwa kung’ang’ana na kisa kikali cha malengelenge, Jean, aliyetajwa mwanzoni, alipata kitulizo kwa kuvaa kivao cha TENS (Transcutaneous Electrical Nerve Stimulation) usiku na mchana kwa majuma kadhaa. Mipwito midogo ya kiumeme ilifunika maumivu ya kindani na kumpa uhuru wa kutembea.
Orodha ya tiba za nyumbani ni ndefu, nyingi zazo zikihusisha mlo fulani wenye kujenga mwili (wenye ajinini kidogo) na kutia ndani vijazio, kama vile vitamini B na C na L-lysine. Wengine hudai kunufaika kutokana na kupaka siki iliyotengenezwa kutoka kwa tofaa, wengine hutumia vitamini E ili kusaidia kupona kwa majeraha ya ngozi.
Uwezekano ni kwamba ukipata malengelenge, haitachukua muda mrefu kabla ya marafiki wa mbali na karibu kukutumia bila kuulizwa tiba zao wazipendazo za kutengenezewa nyumbani. Baadhi ya madokezo huenda yasaidie, mengi huenda yasifae. Pengine yatakuletea tabasamu miongoni mwa maumivu yako. Angalau marafiki wako wanakujali, na kujua hili huenda kuwe na manufaa kuliko tiba zao.
Hivyo katika kukabiliana na malengelenge, mgonjwa na daktari wake huenda wafanye mambo fulani ili kupunguza ukali wa shambulio na maumivu. Lakini ikiwa tabibu wako asema, “Yaonekana kama una shambulio la malengelenge,” huenda aseme tu ni bora zaidi kujaribu kuzoea kwa saburi na uvumilivu wakati kinga ambazo Muumba wetu aliziweka ndani ya miili ziletapo maradhi hayo chini ya udhibiti.