Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 5/8 kur. 15-19
  • Kuvinjari kwa Usalama Ulimwengu Ulio Chini ya Mawimbi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuvinjari kwa Usalama Ulimwengu Ulio Chini ya Mawimbi
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mbinu Mbili za Kuvinjari
  • Lakini Ni Salama Kweli?
  • Vifaa Utakavyohitaji
  • Madokezo Yenye Kusaidia kwa Kutumia Kipumulio
  • Furahia Uogeleaji Wako wa Kinyambizi
  • Vipi Kuhusu Kuruka Mtumbwi?
  • Staha kwa Bahari na Viumbe Vyayo
  • Mandhari Nyingi Zenye Kuthawabisha
  • Maana ya Kinyago cha Kufunika Uso
    Amkeni!—1995
  • Maajabu ya Bahari Nyekundu Chini ya Mawimbi
    Amkeni!—1994
  • Matumbawe—Yamo Hatarini na Yanakufa
    Amkeni!—1996
  • Mbinu za Ndege za Kuvua Samaki
    Amkeni!—2011
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 5/8 kur. 15-19

Kuvinjari kwa Usalama Ulimwengu Ulio Chini ya Mawimbi

Na mleta-habari wa Amkeni! katika Australia

KUNA ulimwengu wenye kusisimua ambao kwa kulinganishwa ni watu wachache wamepata kuuona kwa macho yao. Umetanda chini tu ya uso wa bahari. Ni ule ulimwengu ulio chini ya mawimbi, tayari kwako kuuvinjari. ‘Ziara kama hiyo ni salama kadiri gani?’ huenda ukauliza. ‘Je, nahitaji kuwa mwogeleaji mahiri kabla sijaweza kuzuru huu ulimwengu wenye kusisimua wa chini ya maji? Na je, naondolewa ikiwa siwezi kuogelea kabisa?’

Mbinu Mbili za Kuvinjari

Njia mbili za msingi za kuvinjari ulimwengu wa chini ya maji huwa maarufu—kuogelea kinyambizi na kuruka mtumbwi.a

Kipumulio ni kidude fulani kilicho na neli iliyobeteshwa ambayo huingia kwenye mdomo wa mwogeleaji na hutokea juu ya maji anapoogelea kifudifudi kwenye maji na uso wake ukiwa umezamishwa nusu ndani ya maji. Humwezesha mwogeleaji kupumua, bila kuinua kichwa chake kutoka majini kwa ajili ya hewa. Kisetiri fulani hulinda macho yake.

Mtumbwi, kwa upande ule mwingine, hurejezea kifaa kilicho na silinda moja ama nyingi zilizo na hewa iliyobanishwa na kushikilishwa kwenye kifaa fulani cha kupumulia. Kwa hivyo, bila shaka kuruka mtumbwi ni kwa ajili ya wale wanaopendezwa kuabiri ndani zaidi ya maji, ni tata mno zaidi, na yaweza kuwa ghali zaidi.

Tafrija sahili na isiyo ghali mno ya kuogelea kinyambizi itakuwezesha kuona upendezi mkubwa wa ulimwengu wa chini ya maji hata kutoka usoni pa maji. Hivi ndivyo mwogelea kinyambizi mmoja alieleza ono lake la kwanza: “Bado nakumbuka kwa uwazi wakati wa kwanza nilipoogelea kinyambizi kupitia umati mkubwa wa maelfu ya samaki wadogo, nilipokuwa kijana wa miaka 14 tu. Samaki walionekana kufanyiza mlango-bahari wa uhai kwa ajili yangu kadiri nilivyopita. Miili yao ya kifedha iliakisa jua, ikitokeza urembo fulani. Nilikuwa katika upeo wa usisimukaji. Na kwa jinsi hiyo nikaanza upendezi wa maisha katika kuogelea kinyambizi.”

Lakini Ni Salama Kweli?

Shabiki fulani ambaye amefurahia kwa usalama kuogelea kinyambizi kwa zaidi ya miaka 20 adokeza kwamba ni hatari zaidi kuendesha gari kuelekea bichi kuliko kuogelea kinyambizi! Unapokuwa majini, usalama hutegemea zaidi mtu kuliko utendaji huo. Ikiwa wewe si mwogeleaji mahiri, haupaswi kuendelea kupita maji yaliyo matulivu, machache, na hupaswi kamwe kwenda kupita kimo chako. Kwa hakika, kunaweza kuwa na mengi ya kuona katika meta moja tu ya maji. Kadiri unavyopata ustadi na uhakika, utaweza kwenda kwa usalama ndani ya maji mengi zaidi, lakini hata wakati huo sikuzote unapaswa kuwa na mwandamani mwenye uwezo. Wapiga mbizi wengi wenye uzoefu wameamua kamwe kutosafiri mbali na ufuo ama ndani ya maji mengi wakiwa peke yao. Fauka ya sababu ya usalama, inaburudisha na kufurahisha kushiriki ono la kuogelea kinyambizi na mwandamani.

Ni kweli kwamba kupumua kupitia kipumulio uso wako ukiwa ndani ya maji huenda kukuchukue muda kuzoea, lakini ukistahimili, utapata kwamba si tatizo kwa kweli. Wengine wanaoanza hufanya mazoezi katika vidimbwi vya kuogelea ama katika vibwawa kwenye ufuo wa bahari mahali ambapo hakuna mawimbi. Hata wengine hufanya mazoezi katika hodhi.

Vifaa Utakavyohitaji

Vifaa utakavyohitaji kwa ajili ya kuogelea kinyambizi kwa kulinganishwa ni sahili na si ghali: kisetiri cha uso, viatu-pezi viwili vya kuogelea, na kipumulio chenyewe. Bila shaka, ikiwa umepanga kupiga mbizi wakati wa majira ya baridi ama katika maji yaliyo baridi mno kwa uogeleaji wa kawaida, huenda ukahitaji vazi la baridi, na hili litaongeza gharama kwa kiasi. Acheni tufikirie tu vifaa vitatu vya msingi vihitajiwavyo ili kuanza.

Kisetiri chapaswa kutoshea vizuri, kisichoruhusu maji, kinachokufanya uhisi umestareheka. Na ni lazima pia kiwe na uwiano, yaani, mifululizo ya mibonyeo inayokuruhusu kulifinya pua lako kutoka nje ya kisetiri. Sababu ya jambo hili itaelezwa baadaye. Kisetiri chapasa kuwa na mwono mzuri kwa macho, na chapaswa kuwa cha ujazo wa chini, ikimaanisha kwamba kioo chapasa kuwa karibu na uso wako, kikipunguza kiasi cha hewa iliyo ndani. Visetiri vilivyo vizuri zaidi hutengenezwa kwa silikoni. Hata inawezekana siku za leo kupata kilichorekebishwa kwa ajili ya macho ya wale walio na tatizo la mwono wa karibu.

Baada ya hapo ni viatu-pezi, kimoja kwa kila mguu. Kwa kawaida hutengenezwa na mpira na ni vidude vifananavyo na kafi ambavyo huvaliwa miguuni ili kukupa mwendo unapoogelea. Kuna aina mbili za kuchagua kutokana nazo: aina ya mguu mzima na ubuni wa kisigino kikiwa wazi. Ikiwa unahitaji viatu kwa sababu ya kutembea kupitia miamba yenye kiganzimwamba ama sakafu za marijani zenye maji kidogo kabla ya kufikia maji mengi, basi utahitaji ile aina yenye kisigino wazi. Hili hukusaidia kuweka viatu-pezi kwenye valio lako la mguuni na kuanza kuogelea. Kipezi cha mguu mzima hutoshea kamili ndani ya mguu wako na chaweza kutumiwa ikiwa hakuna viatu vinahitajiwa zaidi ya viatu-pezi.

Hatimaye, kipumulio chenyewe. Kipumulio sahili chenye muundo wa J ni bora zaidi, hasa kwa wale wanaoanza, kwani jambo lililo la maana zaidi ni kupumua kwa usahili. Kitabu kimoja cha kupiga mbizi chadokeza kwamba aina yenye kukubalika zaidi yapasa kuwa na shimo la angalau kipenyo cha sentimeta 2 na urefu wa sentimeta 30 hadi 35.

Madokezo Yenye Kusaidia kwa Kutumia Kipumulio

Kama ilivyoelezwa tayari, kipumulio hukuruhusu kupumua wakati ungali unaogelea kwenye uso wa maji bila kuinua kichwa. Vipi kuhusu kupiga mbizi chini kidogo ya maji? Hili pia lawezekana, lakini kwanza utahitaji kupumua ndani kikamili, na kwa uzito. Bila shaka, maji yataingia ndani ya kipumulio mara uingiapo chini ya uso wa maji. Huenda umeona kwamba wakati mpiga mbizi anapozuka kwenye uso wa maji, mara nyingi mruko wa maji hutoka kwa nguvu kutoka kwenye kipumulio chake. Hii huitwa mbinu ya kulipua ya kuondoa maji nje. Hii ni rahisi sana kujifunza lakini huhitaji kutoa pumzi kwa kishindo, hivyo ni lazima uzuke kwenye uso wa maji na hewa ya kutosha ikiwa ingali katika mapafu yako ikiwa utaondoa maji kutoka kipumulio kwa njia yenye mafanikio.

Wengine huifikiria ile mbinu ya uondoaji kuwa bora, lakini huchukua mazoezi zaidi kidogo. Mbinu hii hufanyaje kazi? Kadiri unapoelekea uso wa maji baada ya upigaji mbizi wako, tazama kuelekea juu. Ncha ya kipumulio chako yapasa sasa kuwa inaelekea chini. Kichwa chako kikiwa katika kikao hiki, itakuchukua tu kutoa pumzi kwa kishindo kidogo ili kuondoa maji ambayo yamejaza kipumulio chako. Weka kichwa chako katika kikao hiki mpaka uso wako uwe karibu kutokea kwenye uso wa maji. Katika pindi hiyo, pindua kichwa chako kuelekea chini na upumue nje. Kipumulio kilichoondolewa maji kitabaki kikiwa wazi, na utapata kwamba unaweza kupumua bila jitihada nyingi.

Usigutushwe pindi kwa pindi ukitapata maji ndani ya kipumulio kutokana na mawimbi fulani yanayopita hata unapokuwa ungali kwenye uso wa maji. Ikiwa hili litatukia, kwa usahili toa pumuo imara la hewa, na kipumulio chako kitatoka maji yote yaliyoko.

Furahia Uogeleaji Wako wa Kinyambizi

Ukiwa ungali kwenye uso wa maji, jaribu kujifunza kupumua kwa udumifu—pumua ndani kwa uzito, kisha nje kwa uthabiti. Mapafu yako yatahisi manufaa ya hili. Kumbuka kwamba siri ya kuogelea kinyambizi kwenye kufurahisha ni, si umbali au ukasi uogeleao, bali kiasi unachoona na kuvinjari kadiri uendeleavyo. Unapotaka kupiga mbizi chini ya maji, jifunze kustarehe na kuhifadhi oksijeni nyingi uwezavyo, kwani utakuwa unaweza kukaa kwa muda mrefu zaidi. Lakini usijaribu kuweka viwango vya ustahimilivu!

Unapopita polepole, acha mikono yako ipembelee kwa ustarehe kando yako. Tumia viatu-pezi vyako tu, ukiwa na mipigo ya maji, mirefu, imara, ukiyaweka magoti yako yakiwa yamekunjwa kidogo. Mwanzoni, itakubidi kuwa makini ili kufanya hili bila jitihada nyingi na kwa urahisi, lakini baada ya wakati mfupi, itakuja kuwa kawaida. Lakini ufanyeje ikiwa kisetiri chako kinakuwa na ukungu? Njia iliyo sahili ya kuzuia hili ni kupaka mate kidogo kwenye kioo kabla ya kuvalia kisetiri. Suza mate hayo baada ya muda fulani, na utapata kwamba kioo kitabaki kikiwa safi kwa muda mrefu sana.

Nyakati nyingine huenda uhisi umivu katika sehemu ya sikio lako la kati wakati wa kupiga mbizi. Hili huitwa mfinyizo wa sikio-kati. Jambo hili husababishwa na utofautiano wa kanieneo kuvuka kiwambo chako cha sikio. Kwa kawaida, huanza baada ya kuwa umeshuka meta moja hadi mbili. Usipuuze umivu hili na kuendelea kushuka, ukitumaini kwamba litakuwa nafuu. Litazidi kuwa baya zaidi kadiri ushukavyo, na ungeweza hata kupasua kiwambo cha sikio. Jarida la wapiga mbizi Padi Diver Manual lapendekeza kwamba kanieneo iwianishwe kila meta kabla ya umivu lolote kuhisiwa. Hili hufanywa kwa kufinya pua lako na kwa wanana upenge. Hii ndiyo sababu kiwianishi huhitaji kuwa ndani ya kisetiri, ili kwamba unaweza kufinya pua lako kisetiri kikiwa kingali kimenata usoni. Kwa uzoefu, taratibu hii huja kuwa rahisi, sawa na uasilia. Mara umivu linapohisiwa, ni bora zaidi kuzuka kutoka majini, kwani baada ya umivu kuanza, jitihada nyendelevu ili kuwianisha hazitafua dafu.

Kama aina ya tafrija, kuogelea kinyambizi kunajenga, kunaelimisha, na kusisimua. Kwa karibu kila rika, ni njia fulani murua zaidi ya kuunganisha mazoezi, hewa safi, na mng’ao wa jua. Kujifunza tu kufahamu na kutambulisha majina ya idadi ndogo ya viumbe wa chini ya bahari hufanya kuogelea kinyambizi kuwa jambo lenye kupendeza na lenye kusisimua kwa wale wenye mwelekeo huo. Hata hivyo, kwa wengi, kama Tony, akiwa amerudi tu kutoka kuogelea kinyambizi katika Fiji, ule upendezi mtupu wa “kuwa katika ulimwengu mwingine wenye rangi zenye kutwetesha” hili ndilo hufanya kuogelea kinyambizi kustahiki na kupendeze. Rafiki yake Lena akubali hivi: “Nilisisimuliwa sana na urembo ulionizunguka kwamba nilisahau nilipokuwa!”

Vipi Kuhusu Kuruka Mtumbwi?

Kwa wale ambao ni waogeleaji wazuri na wamenaswa na maajabu ya maji mengi ama labda wataka kupiga picha chini ya maji, kuruka mtumbwi ni hatua inayofuata. Ukijiweka katika hali nzuri ya afya, kutunza vizuri vifaa vyako, na kufuata kanuni za msingi, huenda uingie ndani ya maji ukiwa na usadikisho. Hata hivyo, usithubutu kwenda kuruka mtumbwi bila kwanza kujifunza mifululizo ya mitaala na ikihitajika, pata leseni kupitia kwa mfunzi anayestahika. Hata wakati huo, hupaswi kupita mipaka ya kilindi ambayo leseni yako inaruhusu. Na sikuzote upige mbizi ukiwa na mwandamani. Katika nchi nyingine, kama vile Australia, sheria hutaka kwamba upite mtihani fulani wa kitiba wa kupiga mbizi kabla ya kuanza mtaala huo.

Vifaa vya kuruka mtumbwi vyaweza kuwa ghali mno. Kuongezea vifaa vinavyotumika kwa ajili ya uogeleaji wa kinyambizi—kisetiri cha usoni, viatu-pezi, na kipumulio—kwa kawaida utahitaji vazi la baridi, isipokuwa katika maji ya kitropiki yenye ujoto. Pia utahitaji kidude cha kudhibiti ueleaji, mshipi wa uzani, kisu, kifaa cha kupumua (kikiwa na ziada kwa ajili ya mwandamani wako ikiwa atapata matatizo ya ugavi wa hewa yake), na mtungi wa hewa. Pia ni lazima uwe na zana muhimu, kama vile saa ya kupiga mbizi, kipima-kina, na kipima-kanieneo kiwezacho kuzama kwa ajili ya mtungi wako wa hewa ili kwamba ujue kiasi cha hewa ulicho nacho. Katika maeneo maarufu ya kupiga mbizi, kifaa hiki chaweza kukodishwa bila shida, jambo ambalo kwa ukawaida mara nyingi huthibitika afadhali kiuchumi kuliko kununua chako ikiwa hupigi mbizi kila wakati.

Staha kwa Bahari na Viumbe Vyayo

“Nilikuwa nikiogelea kinyambizi kwenye miamba fulani karibu na Caloundra kwenye Queensland Sunshine Coast, nikitazama samakikipepeo mwenye urangi kutoka umbali wa karibu meta mbili,” akumbuka shabiki wa kuogelea kinyambizi Peter. “Kisha, mara, fumo lenye umetometo likatokea kwa ghafula na kutua kwa mshindo mkubwa. Samaki mdogo huyo aling’ang’ana bila kufaulu—alitundikwa kupitia shavu kwenye mwamba. Kijana aliyehusika alikiri kwamba aliua samaki huyo maridadi tu kwa ajili ya zoezi la ulengaji shabaha! Alikuwa mdogo mno kuliwa.” Kwa kusikitisha, vitendo kama hivyo vya kutofikiria vinaongezeka kotekote ulimwenguni.

Uchafuzi pia umeacha alama yawo. Maeneo maarufu mara nyingi huja kushabihi majaa ya takataka, yakiwa yamejazwa na mifuko ya plastiki na mikebe ya vinywaji vilivyotumika. Hata vichafuzi vya kikemikali vimekuwa tatizo lenye kuongezeka katika mabara mengine. Kadiri uchafu na takataka zinavyoongezeka, samaki huhamia kwingine, nayo marijani hufa.

Ni zoea zuri sikuzote kuvaa glovu unaporuka mtumbwi. Hata hivyo, inastahiki kutahadhari kuhusu kile unachoshika. Kwa kielelezo, ile nyamizibahari huwa na miiba iliyo kama sindano iwezayo kupenya mikono iliyo mitupu. Na yule kipepeo chewa mwenye uvutio, ingawa mdogo, huonekana kutoa onyo, ‘Usije karibu sana. Hili ni eneo langu!’ anapoyumbisha ile milia yake myekundu na myeupe kwa madaha. Kwa hadaa miongoni mwa virinda vyake akiwa na miiba mirefu iliyo kama sindano ikiwa na ute wenye sumu. Kugusana nayo tu kunaweza kuwa kwenye maumivu.

Viumbe wengine ni vigumu kuwaona. Kwa kielelezo, gugundefumo wa baharini, ni aina ya kujibadili rangi. Huonekana kama tu kipande cha majani, akitatanisha na kutia kiwi mwono wa mpiga mbizi. Kinyume, rangi kamili, na zenye kuonekana za samaki-tawi, koauchibahari, kwa hakika zavuta umakini wako. Lakini je, hili ni donge lenye kushawishi? Wanaoelekea kuwa wanyafuaji hujifunza tofauti, kwani yeye hujikinga na kemikali fulani zenye kunyarafisha.

Mandhari Nyingi Zenye Kuthawabisha

Kwa wote, mwogelea kinyambizi na mruka mtumbwi, bahari kuu kwa hakika imejawa na uhai. Mawe ya marijani huwa ni taswira ya viumbe visivyohesabika na rangi ambazo zaweza kuonwa kwa kuogelea kidogo tu kuelekea baharini. “Ule usisimukaji wa kuwa umezungukwa na samaki wenye urangi wa maumbo na saizi zote, wengine wakijilisha mkononi mwako, ni vigumu kulinganika na chochote. Ni ono lenye kugusa moyo mno,” akasema mpiga mbizi mmoja. Kisha akaongezea hivi: “Kuwa pale kama mmoja wao, ukiwa umeelea bila udhibiti mkubwa wa nguvu za uvutano, inasisimua sana.”

Hivyo basi, ukipata nafasi wakati wowote ya kuogelea kinyambizi ama kuruka mtumbwi, kumbuka kwamba kunaweza kufanywa kwa njia salama zaidi ukichukua tahadhari sahili zinazopendekezwa na wapiga mbizi wazoefu. Labda siku moja huenda ufurahie ono hili lenye kuthawabisha la kuvinjari urembo wa ulimwengu ulio chini ya mawimbi.

[Maelezo ya Chini]

a “Kuruka mtumbwi” humaanisha kuogelea chini ya maji ukiwa na “vifaa kamili vya kupumua.” Bendera ya kimataifa kwa sasa inayoashiria kuwapo kwa waruka mtumbwi ni bendera ya mfanyizo wa samawati-nyeupe. Na nchi nyingine bado zatumia bendera nyekundu ikiwa na mlia mweupe, kama ionyeshwavyo hapo juu.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Kipepeo chewa

[Picha katika ukurasa wa 17]

Heroe ulimi

[Picha katika ukurasa wa 17]

Tangi samawati

[Picha katika ukurasa wa 17]

Samaki-tawi kwenye marijani

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Kwa hisani ya Australian International Public Affairs

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki