Kuutazama Ulimwengu
Gharama Kubwa ya Wivi wa Magari
Kulingana na tarakimu za majuzi zilizotolewa na Statistics Canada, magari 146,846 yaliibwa katika Kanada katika mwaka 1992, rekodi ya juu zaidi. Hii ilijumlika kuwa uwiano wa wivi wa magari 8.4 kwa kila magari 1,000, ilihali uwiano wa Marekani ulikuwa karibu 8.3, likasema gazeti The Vancouver Sun. Ni mara chache sana magari yaliyoibwa yalirudishwa katika hali yayo ya mwanzoni, na ripoti hiyo ilieleza kwamba “hasara kutokana na wivi wa magari, vitu kutoka kwenye magari, na kutokana na uharabu wa magari ulijumlika kuwa dola bilioni 1.6 katika 1992.” Hasara hizi zakadiriwa kuwa mara 30 juu zaidi kuliko zile zipatikanazo kutokana na ulaghai na wivi wa kadi-mkopo na yapata mara 500 zaidi kuliko kinachopotea kupitia wivi wa benki. Wivi wa gari ili kulifurahia kwa muda mfupi kulitajwa kuwa sababu ya kawaida zaidi kwa wivi wa magari. “Vijana wenye umri wa miaka 12 hadi 17 walikuwa karibu nusu ya wale walioshtakiwa na wivi wa magari,” likaongeza Sun.
Mlaji wa Mfulululizo
Mwanamume mmoja kutoka New York amekuwa ndani na nje ya gereza kwa zaidi ya mara 31 kwa kosa lilelile: kuiba mlo. Mwanamume huyo mwenye miaka 36 ataingia mkahawani, aagize kinywaji cha kileo kiamshacho hamu ya kula na mlo mzuri, na kumalizia kwa kahawa isiyotiwa maziwa. Risiti ya malipo iletwapo, amwarifu mtumishi wa mkahawa kwamba hana fedha na angojea kufungwa. Kwa nini yeye hufanya hivyo? “Maisha ni magumu nje ya gereza,” mwanamume huyo asiye na makao asema. Kuna utaratibu gerezani, mwala kwa wakati, na chakula ni kizuri, yeye ajadili. Kando na hilo, yeye hataki kunyang’anya au kuumiza watu; yeye ataka tu kula vizuri na kuwa na kitanda safi na mahali pa kulala penye utulivu. Kwa hiyo yeye nyakati zote hukiri kosa mahakamani na hutafuta kifungo kamili. Kumshughulikia kinyumba gerezani hugharimu walipaji kodi dola 162 kwa siku. Kwa hakika, mlo wake wa hivi majuzi wa dola 51.31 uliwagharimu dola 14,580 ili kumweka gerezani kwa kifungo chake cha siku 90. Amegharimisha New York zaidi ya dola 250,000 kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. “Wanasheria wa Misaada ya Kisheria,” lasema The New York Times, ‘wameona idadi ndogo lakini inayokua ya watu wanaotenda uhalifu mdogo wakiwa na nia ya kwenda gerezani’ kwa ajili ya “ukimbizi kutoka umaskini au njaa.”
Muulize Daktari Wako wa Meno
Kisio la hivi majuzi juu ya uwezekano wa kuambukiza virusi ya UKIMWI kupitia taratibu za kutibu meno lafanya watu wawe na hofu. Uchunguzi uliofanywa na Shirika la American Dental Hygienists ulifunua kwamba asilimia 83 ya wagonjwa wa meno wana wasiwasi wa kupata maradhi ya kuambukiza wanapokuwa wakipokea utunzi wa meno. Kulingana na gazeti American Health, wagonjwa wanapaswa kuhakikisha kwamba wafanyakazi wa kutibu meno huvaa si tu glovu na vifunika uso bali kwamba wanavibadili kabla ya kutibu mgonjwa anayefuata. Vifaa vinavyoweza kutumika mara nyingine vyapaswa kufishwa vijidudu vyote vya ugonjwa kwa moto baada ya mgonjwa. American Health laeleza kwamba “ufundi wa kufisha vijidudu vyote vya ugonjwa kwa baridi, kama vile kusafisha vifaa kwa alkoholi, hakutoshi.” Gazeti hilo laongeza kwamba “ikiwa daktari wako wa meno hataki kujibu maswali yako, tafuta daktari mwingine wa meno.”
Wasafiri Waliochafuliwa
Kati ya asilimia 20 hadi 50 ya watu bilioni nne wanaosafiri kila mwaka wanaathiriwa na kuhara, kwa kawaida kwa sababu ya chakula au maji yaliyochafuliwa, lakadiria WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni). Uchovu wa safari, au badiliko la ulaji na tabia-anga zaweza kuchangia tatizo hilo kwa kudhoofisha kinga ya wasafiri. Ili kupunguza uwezekano wa kuhara, WHO lapendekeza yafuatayo: Hakikisha kwamba chakula kimepikwa kabisa na kingali moto kinapoandaliwa. Ikiwa maji ya kunywa huenda yasiwe salama, yachemshe au uue viini kwa tembe zinazotegemeka zipatikanazo katika maduka ya dawa. Epuka vyakula vibichi isipokuwa matunda au mboga ambazo zaweza kuambuliwa au kutolewa maganda. “Kumbuka ule msemo,” lasema WHO, “Kipike, kiambue au kiache.”
Ukiukaji-Sheria wa Katoliki
Kulingana na The New York Times, Papa John Paul 2 anawahimiza Wakatoliki watubie ukiukaji-sheria wao walioutenda dhidi ya ubinadamu kwa miaka 2,000 iliyopita. Papa alisema kwamba kanisa lapasa “kufahamu kikamili juu ya utendaji-dhambi wa watoto walo.” Kwa wazi ukiukaji-sheria huu unahusianishwa na lile fungu waliloshiriki Wakatoliki wakati wa Kuhukumu Wazushi kwa Kihispania kwenye kuogofya na lile Teketezo la Umati la Kinazi. Times laeleza kwamba “suala la ufuniko kwa makosa ya Wakatoliki ni lenye kutatanisha kwa kuwa hudokeza uelekeo wa kukosea katika ufafanuzi wa kanisa wa kweli yalo.” Gazeti hilo liliongezea kwamba makadinali fulani walihisi kwamba “ilikuwa muhimu zaidi kuchunguza kuzorota kwa kisasa kwa maadili.”
Bunduki Marekani
Kulingana na ripoti ya hivi majuzi, kuna yapata bastola milioni 200 zinazozunguka miongoni mwa umma katika Marekani. Kwa wastani, mtu fulani anapigwa risasi kila dakika mbili. Kila dakika 14 mtu fulani hufa kutokana na mpigo wa bunduki. Kila saa sita mtoto au tineja ajiua kwa bastola. Ripoti hiyo yataarifu kwamba katika siku yoyote, watoto Wamarekani huleta shuleni yapata bastola 270,000. Gazeti Redbook laeleza kwamba “kati ya 1979 na 1991, karibu watoto 50,000 waliuawa kwa bunduki—kwa kukadiria ni sawa na idadi ya Wamarekani wote waliouawa katika Vita ya Vietnam.”
Waume na Wake wa India Chini ya Matatizo Yenye Kuendelea
Katika India, ndoa “iko chini ya matatizo yenye kuendelea katika kile kinachogeuka kwa haraka mno kuwa jamii ya ‘mimi kwanza,’” lataarifu gazeti India Today. Waume na wake wengi zaidi walio wachanga wanaenda mahakamani kumalizia magombano yao. Daktari mshauri Narayana Reddy aripoti kwamba “idadi ya watu wanaomjia kwa ajili ya ushauri wa kitaalamu katika miaka michache ya kwanza ya ndoa imerudufika katika miaka mitano iliyopita,” kulingana na India Today. Baadhi ya waume na wake wametafuta usaidizi wa kitaalamu siku kadhaa baada ya arusi yao. Kwa sehemu kubwa, hakuna chochote kipya kuhusu visababishi vya vurugu miongoni mwa ndoa za Wahindi: uzinzi, uraibu wa alkoholi, mabishano ya kifedha na mali, magumu na wakwe, na masuala ya kingono. Mkazo “umekuja kuwa mgeni aliye kote, asiyeonekana na mwovu katika nyumba ya Mhindi.”
Redio Ifukuzayo Mbu
Inadaiwa kwamba kituo fulani cha redio katika Poland kimeanzisha mbinu fulani ya kukabiliana na mdudu huyo wa miaka na miaka mbu. Gazeti la mambo ya asili la Kifaransa Terre Sauvage laripoti kwamba wakati wa kipindi cha kuangua cha mbu katika Poland, maelfu ya wasikilizaji wa redio waliweza kupigana na wadudu hawa wenye kukasirisha bila kutumia dawa za kufukuza wadudu. Wao walibadili tu redio zao katika stesheni inayoitwa Radio Zet. Kulingana na Terre Sauvage, stesheni hiyo hutoa mawimbi ya redio kwa kuendelea ambayo, yakiwa hayawezi kusikiwa na binadamu, yangeweza kusikiwa na mbu. Utoaji huo ulikuwa mwigizo wa elektroniki wa sauti zilizo na udukizi-wimbi wa juu zinazotolewa na popo wanaokula mbu—wa kutosha kuwafukuza mbu wowote waliosikia.
Wengi Zaidi Wanazeeka
Familia ya kibinadamu inazidi kuzeeka. World Health, jarida la Shirika la Afya Ulimwenguni, laeleza kwamba “kila mwezi, jumla ya wakati huu ya ulimwenguni ya watu milioni 360 walio na miaka 65 na zaidi inaongezeka kwa watu 800 000.” Kwa kipindi cha miaka 30 ijayo, idadi ya wazee-wazee inatarajiwa kufikia kadirio la milioni 850. Ulaya na Amerika Kaskazini zapatwa na ukuzi unaotazamisha katika asilimia ya watu wazee zaidi kwa sababu ya “uzaaji wa chini wenye kuendelea na matazamio ya kuishi yanayoongezeka” katika nchi hizo, lasema World Health. Gazeti hilo laeleza kwamba “Sweden sasa ina idadi ya watu ‘wazee zaidi’ ulimwenguni, ikiwa na zaidi ya asilimia 18 ya wananchi wayo wakiwa na umri wa miaka 65 au zaidi.”
Chakula na Afya Katika Uingereza
“Waingereza wako miongoni mwa wale wasio na afya zaidi wa Wanaulaya wote,” ladai gazeti la Uingereza The Economist. Uchunguzi wa hivi majuzi ulifunua kwamba karibu nusu ya idadi ya watu wazima katika Uingereza ni “wenye uzito kupita kiasi au wanene kupita kiasi kiklinikali—jambo ambalo laweza kueleza kwa nini Waingereza baada ya Wacheki, ni wenye uelekeo wa kupatwa na mshiko wa moyo kuliko taifa jinginelo lote,” lasema The Economist. Kamati ya serikali ya Mambo ya Kitiba ya Sera ya Chakula imefanya mapendekezo kadhaa ili kuboresha hali hiyo. Madokezo yayo yalitia ndani kula zaidi “samaki, mkate, mboga na viazi” na kupunguza ulaji wa chumvi, sukari, na mafuta.
Kumalizika kwa Ozoni
OMM (Shirika la Kimeterolojia Ulimwenguni) katika Geneva, Uswisi, latabiri kwamba ijapokuwa jitihada za kupunguza uharibifu kwenye tabaka la ozoni la dunia, kumalizika kwa tabaka lenye kukinga kutaendelea kuongezeka kasi angalau hadi mwishoni mwa karne ya 20. Kulingana na utumishi wa habari France-Presse, mikataa ya OMM inategemea uchungulizi wa wanasayansi 266 kwa kipindi cha miaka minne iliyopita katika nchi 29 tofauti. Hatua zilizochukuliwa kufikia sasa ili kupunguza utokaji wa kiviwanda unaoharibu ozoni yaonekana zinaanza kuwa na matokeo yaliyotamaniwa. Lakini ripoti ya OMM ilifunua kwamba kuna “udidimiaji wa kitufe na wenye kuendelea” katika ushikamanifu wa utabakastrato wa ozoni wa dunia na kuonya kwamba kipindi chenye hatari zaidi “bado kiko mbele yetu.”