Msiba Unapopiga
KARNE ya 20 imetiwa alama na misiba mikubwa, na mingi yayo imesababishwa na mwanadamu. Ingawa hivyo, baadhi yayo sivyo. Akitabiri kuhusu siku zetu, Yesu Kristo alisema hivi: “Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali.” (Mathayo 24:7) Kweli, mwanadamu ndiye wa kulaumiwa kwa vita na upungufu wa chakula, lakini yeye hana daraka kuhusu matetemeko ya dunia. Katika njia inayofanana na hiyo, huku baadhi ya misiba ya mafuriko ikisababishwa na utendaji wa mwanadamu, yeye hawezi kulaumiwa kwa sababu ya matetemeko ya dunia. Wala vimbunga wala milipuko ya volkeno si kosa la mwanadamu.
Hata kisababishi kiwe kipi, misiba ya asili huonyesha udogo wa mwanadamu, kutoweza kwake akabilipo kani za asili zenye kutisha. Dunia hii, makao yetu, kwa kawaida huhisi ikiwa salama na thabiti sana. Lakini inapotikiswa na tetemeko la dunia, kufurikishwa kwa maji yanayofurika, ama kuyumbishwa na pepo kali ambazo huikumba kana kwamba ni kani za milipuko, hisia hiyo ya usalama hutoweka.
Misiba ya asili imesababisha uharibifu mkubwa na hasara kubwa ya uhai wakati wa hii karne ya 20. Je, hili lingeweza kuwa liliepukwa? Je, kuna lolote liwezalo kufanywa ili kupunguza hayo madhara yenye maafa? Tukiwa mmoja-mmoja, ni nini tunaloweza kufanya ili kujilinda? Je, tumebaki bila tumaini kabisa wakati msiba unapopiga? Je, jamii ya kibinadamu sikuzote itazidi kupatwa na mabaya yasiyoistahili kwa njia hii? Makala zifuatazo zitazungumzia maswali haya.