1945-1995—Je, Ni Miaka 50 ya Maendeleo?
JE, UMEONA maendeleo yoyote katika ubora wa maisha yako kwa miaka 50 iliyopita?a Ebu fikiria tiba. Katika nchi nyingine, kama vile Uingereza, Kanada, Kuba, na Sweden, serikali kuanza kutunza raia, pamoja na mfumo wa matibabu ya kijamii, kulihakikisha kwamba hata hali ya kiuchumi ya mgonjwa iweje, madaktari na mahospitali yangepatikana kwa wote.
Hata mengine ya mataifa yanayositawi yameweza kuboresha viwango vya afya ya raia zao. JAMA (The Journal of the American Medical Association) lilitambua kwamba “baadhi ya wizara za afya za nchi zinazositawi zimefaulu katika kuandaa utunzi wa msingi wa afya kwa wote kwa gharama ambazo nchi zao zaweza kudumisha. . . . Maendeleo yenye kutokeza yamefanywa katika kupunguza vifo vya vitoto na vya utotoni katika China, Kosta Rika, Sri Lanka, na jimbo la India la Kerala.”
Maendeleo ya Kimwili
Kwa kulinganisha na hali ya kiuchumi katika 1945, watu wengi wako katika hali nzuri zaidi kwa habari ya vitu vya kimwili katika 1995. Wengi ambao miaka 50 iliyopita hawangeweza kugharimia vitu visivyo vya lazima maishani sasa wana magari, televisheni, video, plea ya diski-songamano, friji, simu zenye kubebeka, na bidhaa nyingine za maisha ya kisasa. Labda wewe ni mmoja wa mamilioni hao.
Kama vile watungaji wa mfululizo wa kitabu A History of Private Life waelezavyo, “kwa miaka thelathini baada ya Vita ya Ulimwengu 2 Ufaransa [pamoja na nchi nyingine za Ulaya magharibi] ilipata ukuzi thabiti wa kiuchumi, ambao, ingawa haukuondoa matabaka ya kijamii, ulileta utajiri mpya kwa matabaka yote ya kijamii. Wakiwa na nyumba ‘ifaayo,’ magari ya ‘kiasi,’ na televisheni, pamoja na baraka zilizoongezeka za kutunzwa na serikali na tiba ya kisasa, kila mmoja angeweza kufurahia, ikiwa si paradiso duniani, angalau maisha yenye kuvumilika.”
Hata hivyo, swali ni, Je, kuwa na mali nyingi za kimwili kunamaanisha kwamba watu wako katika hali nzuri zaidi katika kila hali? Je, kule kurundamana kwa faida za kimwili kwamaanisha moja kwa moja kwamba maisha ni bora ama salama? Mali zaidi kwa wengine bado kwaacha watu wengi maskini wakiwa hawana mahitaji ya lazima maishani. Hilo laongeza vishawishi vya kuiba, ubaradhuli, upujaji, na uhalifu mwingine wenye jeuri zaidi. Baadhi ya mafukara wameazimia kuwa mabwenyenye—kwa udi na uvumba. Kwa kielelezo, katika New York City, zaidi ya magari 100,000 huibiwa kila mwaka. Faida za kimwili hazihakikishi maisha yaliyo salama zaidi.
Kumekuwa na maendeleo katika nyanja nyinginezo, ingawa si sana kama vile wengine wangetaka.
Wanawake—Wakati Huo na Sasa
Vita ya Ulimwengu 2 ilichochea fungu jipya kwa baadhi ya wanawake. Wengi walizoea kutumika wakiwa akina mama na wake wa nyumbani, huku mume akiwa mtoa riziki. Vita ya ulimwengu ya pili ilibadili yote hayo. Wanaume walichukuliwa vitani, na ghafula wake zao wakajipata wakifanya kazi katika viwanda vya silaha ama katika kazi nyingine zilizoachwa na wanaume. Katika nyakati za hivi majuzi, baadhi ya wanawake wametumikia katika jeshi na kujifunza kuua. Mamilioni ya wanawake wakawa wachuma mshahara na kupata mwonjo wa mtindo-maisha tofauti wenye uhuru wa kifedha. Huo ulikuwa tu mwanzo wa mwanya ambao polepole uliwafungulia mlango “wanawake huru” wa leo. Katika pambano lao la usawa, wanawake wengine wanasema bado kuna mwendo mrefu ulio mbele katika nchi nyingi. Wao wasema kuna “dari ya kioo” ambayo huwazuia wasipande cheo katika kazi nyingi.
Uhamaji wa Halaiki Wasababisha Matatizo
Badiliko jingine kubwa kwa miaka 50 iliyopita ni kule kuacha maisha ya kijijini na kilimo katika jitihada ya kutafuta maisha yaliyo bora mjini. Kwa wengine tazamio hili limetimia. Lakini matokeo yamekuwa yapi kwa wengine wengi?
Kila mwaka mamilioni huhamia majiji ambayo tayari yana watu wengi kupita kiasi, ambapo makao hayatoshi na ni ghali. Tokeo moja ni nini? Mitaa ya vibanda ambayo huwa mahali pa kuzalishia maradhi, uhalifu, na mvurugo. Makao haya ya kujijengea, yaliyojengwa kwa masazo ya kadibodi, mbao, ama mabati, ni vibanda, barracas ama chabolas (Kihispania), ambamo tabaka la makabwela ulimwenguni hukaa. Makao haya machafu ya miji—favela katika Kireno na gecekondu katika Kituruki (kikimaanisha “nyumba zilizojengwa usiku”)—ni uhakika wa maisha ambao hauwezi kupuuzwa, iwe ni katika Afrika, India, Amerika Kusini, ama penginepo pote.
Wakati wa Sasa na Ujao wa Baadhi ya Nchi za Afrika
Ni jambo jipi linaloweza kusemwa kuhusu Afrika? Madaktari wawili waliandika katika JAMA wakiweka kichwa kikuu hivi: “Afrika Hatarini—Wakati Ujao Usio Dhahiri Lakini Wenye Matumaini.” Walitambua kwamba hali ya kisiasa na kijamii katika sehemu kubwa ya Afrika yatokeza uwezekano wa matatizo mengi. Waliandika hivi: “Kwa Afrika iliyoko Kusini mwa Sahara [eneo la nchi 45], miaka 20 iliyopita imetokeza maafa mengi. Hilo eneo limekumbwa na njaa, ukame, vita vya wenyewe kwa wenyewe, ufisadi wa kisiasa, UKIMWI, ongezeko kubwa la idadi ya watu, utokezaji wa chakula wenye kupungua, kuharibika kwa mazingira . . . Wastadi wanakubaliana katika matabiri yao kwamba kushuka zaidi kiuchumi, umaskini, na kuteseka ni mambo yasiyoepukika, angalau kwa kipindi kifupi cha wakati.” Makala hiyohiyo iliripoti kwamba nchi 32 kati ya nchi 40 zilizo maskini zaidi ulimwenguni ziko katika Afrika iliyoko Kusini mwa Sahara.
Sasa vipi kuhusu hali ya maadili ya sasa ulimwenguni? Makala ifuatayo itazungumzia kifupi “maendeleo” ya ulimwengu kwa upande huu.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa sababu ya kukosa nafasi, mazungumzo yetu hayatii ndani sehemu zote za maendeleo ama mabadiliko kwa muda wa nusu karne iliyopita.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 6]
Picha ya USAF
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 7]
Picha ya NASA