Kuenea kwa Vijiumbe-Maradhi Vyenye Kufisha
Eloise pamoja na abiria wenzake walipewa kadi ya Notisi ya Tahadhari ya Afya baada ya kupanda ndege kutoka London hadi New York. Hiyo ilikuwa Mei 1995. Upande wa mbele wa hiyo kadi ulisomeka hivi:
“KWA Msafiri: Weka kadi hii katika pochi au kibeti chako kwa majuma 6. Ukiwa mgonjwa katika kipindi hicho, mpe tabibu wako kadi hii na umweleze juu ya safari yako ya hivi majuzi nje ya Marekani.
“Huenda ulipatwa na maradhi yenye kuambukiza kabla ya kufika Marekani, na kujua juu ya hilo huenda kukamsaidia tabibu wako katika kugundua ugonjwa.”
Wahudumiaji katika ndege pia walitoa magazeti ya habari ambayo yalifafanua mweneo wa Ebola, maradhi yasababishwayo na virusi ambayo yalikuwa yakiua watu wengi katika Zaire.
Eloise alisoma juu ya Ebola—maradhi mabaya mno yenye kufisha. Wagonjwa walioambukizwa kwanza walipatwa na homa, vidonda vya kooni, na kuumwa na kichwa, kukifuatiwa haraka na kutapika, maumivu ya fumbatio, na kuhara. Dalili hizi zilifuatiwa na kuvuja damu sana, kusikoweza kudhibitiwa, kwa ndani na nje. Katika visa 9 kati ya 10, kifo kilikuja haraka.
Miezi kadhaa mapema, kulikuwa kumekuwa na ripoti za maradhi yasiyojulikana yenye kufisha: kwa kielelezo, tauni katika India. Mahali penginepo watu walikuwa wamekufa mnamo saa chache kutokana na kile ambacho vyombo vya habari viliita “kiini kila-mnofu.”
Eloise aliipindua kadi upande ule mwingine mkononi mwake. Upande ule mwingine ulisomeka hivi:
“Kwa Tabibu: Mgonjwa anayetoa kadi hii amekuwa ng’ambo hivi majuzi, na yawezekana alipatwa na maradhi yenye kuambukiza ambayo hayaonekani kwa ukawaida Marekani. Ukishuku maradhi yenye kuambukiza yasiyo ya kawaida katika kisa hiki (kipindupindu, homa za kutokwa damu, malaria, homa-njano, n.k.), tafadhali yaripoti mara moja kwa Ofisa wa Afya wa jiji, wilaya, au Jimbo lako na pia (kupitia simu—itakayolipwa na unaowapigia) kwa Idara ya Kutenga Wagonjwa, Vitovu vya Kudhibiti Maradhi, Atlanta, Georgia . . .”
Hiyo kadi ilionyesha hangaiko lenye kuongezeka la kimataifa kuhusu kuenea kwa vijiumbe-maradhi—vimelea, bakteria, na virusi—ambavyo, baada ya kuanzisha maradhi sehemu moja duniani, vyaweza kuenea haraka kama moto wa msitu hadi kwenye sehemu nyinginezo. Tofauti na Eloise na abiria wenzake, vijiumbe-maradhi havibebi paspoti wala kuheshimu mipaka ya kitaifa. Ndani ya mtu aliyeambukizwa, hivyo husafiri bila kujulikana kwa uhuru wenye kushangaza.
Alipokuwa akiiweka kwa uangalifu kadi ya Notisi ya Tahadhari ya Afya katika kibeti chake, Eloise alijiuliza, ‘Maradhi haya yenye kuua yanatoka wapi? Kwa nini sayansi ya kitiba ya kisasa yaonekana kutoweza kuyashinda?’ Labda umejiuliza juu ya hilo pia.