Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Dalili za Kabla ya Hedhi Lazima nieleze shukrani zangu za unyoofu kwenu kwa kuchapisha ile makala “Dalili za Kabla ya Hedhi—Ni Ngano au Uhalisi?” (Agosti 8, 1995) Nimekuwa nikisali kwa ajili ya makala kama hiyo, kwa kuwa sikuwa naelewa kwa nini nilikuwa na hisia mbaya hivyo kila mwezi. Nilipoisoma hiyo makala, nilitulizwa; sasa natambua kwamba tatizo langu si kwa sababu ya udhaifu wa kiroho.
Y. E., Jamaika
Nimeteseka kutokana na dalili za kabla ya hedhi kwa muda mrefu niwezavyo kukumbuka, lakini nilizipuuza sikuzote nikiziona kuwa jambo ninalopaswa kukabiliana nalo. Makala hii ilinisaidia kutambua kwamba dalili za kabla ya hedhi ni tatizo halisi, linalohitaji kuzungumzwa.
Y. M., Uingereza
Kwa karibu miaka 12, dalili zangu za kabla ya hedhi zimesababisha mkazo mwingi kwa mtoto wangu na mume wangu. Makala hii ilieleza dalili zangu vizuri sana! Jambo lililonifurahisha ni itikio la mume wangu asiye Shahidi, ambaye sikuzote huchambua Amkeni! Alionyesha kupendezwa sana katika makala hiyo na kusema, ‘Nafurahi tuna makala hii.’
K. O., Japani
Uzinzi Asanteni sana kwa ile makala “Maoni ya Biblia: Uzinzi—Kusamehe au Kutosamehe?” (Agosti 8, 1995) Baada ya miaka ya kutendwa vibaya, nilimtaliki mume wangu Kimaandiko. Hata hivyo, watu fulani walinifanya nihisi kuwa mwenye hatia kwa kufanya hivyo, na ilinilazimu kushindana na hisia hii kwa miaka mingi. Hata nilifikiria Yehova alikuwa ameniacha. Hata hivyo, makala hii ilizungumzia hisia zangu nyingi, nayo imenitia moyo sana.
A. K., Jamhuri ya Cheki
Vinyago vya Kufunika Uso vya Afrika Ile makala yenu “Maana ya Kinyago cha Kufunika Uso” (Agosti 8, 1995) ilikuwa yenye kuelimisha sana. Ndani yayo mlisema kwamba Wakristo wa kweli hawawezi kuwa na vifuniko vya uso kama hivyo. Lakini vipi vinyago vya kufunika uso vinavyotengenezwa kama vikumbusho au vile ambavyo havijatumiwa kamwe kwa makusudi ya kidini?
J. A., Marekani
Makala yetu ilishughulika hasa na vinyago vya kufunika uso ambavyo vilitengenezwa kwa makusudi ya dini bandia. Tulionyesha kwamba “kuna tofauti kubwa kati ya vinyago vya kufunika uso vitumiwavyo katika ibada na visanamu vilivyochongwa kwa ajili ya biashara ya watalii.” Katika nchi za Magharibi, vinyago vya kufunika uso vya kibiashara huenda visiwe na vyanzo vya kidini hata kidogo lakini huenda kwa ujumla vikaonwa kuwa sanaa ya mapambo. Kwa hiyo kila Mkristo mmoja-mmoja atafanya uamuzi wa kibinafsi kama ataweka vinyago vya kufunika uso, akikumbuka jinsi huenda kufanya hivyo kukaathiri dhamiri za wengine. (1 Wakorintho 10:29)—MHARIRI.
Kifaru Nilitaka kueleza uthamini na upendezi kwa uwezo wenu wa kufanya habari isiyo ya maana iwe ya kupendeza—hata kwa mtu kama mimi ambaye sikuwa nikisoma kwa ajili ya starehe. Nimemaliza tu kusoma “Yule Mnyama Mwenye Hizo Pembe Zenye Bei.” (Agosti 8, 1995) Mara nyingi mimi huanza kusoma makala kama hizi kwa sababu tu nahisi nawajibika kuzisoma. Hata hivyo, mwishowe, sikuzote mimi hushangazwa na jinsi zinavyofurahisha kuzisoma!
J. M., Marekani
Masimulizi ya Celeste Jones Nimekuwa nikisoma magazeti yenu kwa miaka 17. Baada ya kusoma yaliyoonwa ya Celeste Jones katika ile makala “Jinsi Nilivyonufaika Kutokana na Utunzaji wa Mungu” (Juni 22, 1995), ilinilazimu kuandika nieleze uthamini wangu.
M. M., Kolombia
Celeste Jones alikufa Oktoba 27, 1995. Kabla ya kifo chake alipokea barua nyingi kutoka kwa wasomaji ulimwenguni pote waliokuwa wakimshukuru kwa kushiriki nao mambo yake yaliyoonwa.—MHARIRI.