Kuutazama Ulimwengu
Wapiganaji wa Kuvizia Walio Watoto
Watoto wamekuwa wa kawaida katika majeshi ya kuvizia kotekote duniani. Kulingana na International Herald Tribune, watoto hujifunza jinsi ya kuua upesi sana, nayo maoni yao juu ya lililo sawa na lililo ovu si yenye nguvu kama ilivyo tamaa yao ya kutaka kukubaliwa na kikundi kiwacho chote cha kijeshi ambacho wamejiunga nacho. “Katika Rwanda na sehemu nyinginezo, waliotenda baadhi ya mauaji yaliyokuwa mabaya sana walikuwa watoto,” akasema mnenaji wa Umoja wa Mataifa. “Wanataka kuwa washiriki wa kikundi fulani na kusifiwa, na kibali pekee cha marika chaweza kupatikana kwa kuwa wajasiri zaidi au wakatili kuliko watu wazima.” Katika pigano moja la Kiafrika, wavulana wenye umri wa miaka minane walizoezwa na kulazimishwa kufanya matendo maovu, kama vile kuwapiga risasi wazazi wao wenyewe na kukata koo zao. Wasichana waliotekwa nyara walilazimishwa kupika, kufanya kazi za usafi, na kufanya ngono pamoja na wanaume. “Makadirio ya idadi ya watoto walio vitani ni kati ya 50,000 na 200,000 katika mapigano 24,” lasema gazeti Newsweek.
Ulinzi wa Sikadi
Wanabotania walio wengi huona sikadi Encephalartos woodii kuwa mmea ulio adimu zaidi ulimwenguni. Hivyo Afrika Kusini ilipoamua kupeleka kipande cha mmea huu wa kitropiki ufananao na mtende kwenye Maonyesho ya Maua ya Chelsea ya London mwaka uliopita, walitahadhari kwa kuweka shinani mwao mikrochipu ya kuzuia wezi iliyofunikwa katika mafuta yenye kiuabakteria. Sikadi zote zinazosafirishwa katika Afrika Kusini sasa zinalindwa kwa njia hii, laripoti New Scientist. Ili kuzuia wezi wahifadhi wa vitu vya asili wa Afrika Kusini sasa wanalinda sikadi za mwituni kwa njia hiyohiyo, kwa msaada wa mfumo wa uchunguzaji wa sateliti.
Vifuniko vya Mashimo ya Maji Machafu Vikosekanavyo
Zaidi ya wakazi 200 wa Beijing walianguka kwenye mashimo katika 1994, liliripoti gazeti Economic Daily. Sababu ilikuwa nini? Wezi walikuwa wameiba vifuniko vya mashimo zaidi ya 2,000 kwenye barabara za mji mkuu wa China mwaka huo. Vingi vyavyo vilisemekana kuwa viliibiwa na wahamiaji, waitwao watu wa China wazururao. Wizi wa hivyo vifuniko umeongezeka katika mwongo uliopita kadiri wahamiaji wa mji huo walivyoongezeka. Hivyo vifuniko vya kilogramu 60 vyaweza kuuzwa kwa zaidi ya dola 12 za Kimarekani. Wakazi waumiao kwa kuanguka hutia ndani wanaokwenda kwa miguu na waendesha baiskeli na pikipiki.
Tafsiri Mpya za Biblia
“Kuna ongezeko kubwa la chapa mpya za Biblia katika Kiingereza cha kisasa kwenye maduka ya vitabu,” laandika U.S.News & World Report. Biblia zimechapishwa kwa ajili ya watoto, wachezaji, walio wazee-wazee, akina mama wanaokaa nyumbani, akina baba, na vikundi vingine. Moja yazo, Black Bible Chronicles, “hutumia semi za mitaani na drama ili kufanya masimulizi ya Biblia yawe yenye kupendeza matineja Waafrika-Waamerika.” Nyingine, The New Testament and Psalms: An Inclusive Version, hujaribu kutumia lugha isiyopendelea jinsia. Mungu anaitwa “Baba-Mama,” naye Mwana wa binadamu anaitwa “yule wa kibinadamu.” Ili kuepuka kuwaonea watumiao mikono ya kushoto, watafsiri wayo huita mkono wa kuume wa Mungu “mkono [wake] wenye uweza,” na kwa sababu ya ubaguzi wa rangi, giza halilinganishwi tena kamwe na uovu. Na ya tatu, New International Reader’s Version New Testament, yafafanuliwa na mtangazaji wayo kuwa “Biblia ya kwanza kabisa ambayo imepata kuandikwa kwa ajili ya watu wasio na elimu kabisa iliyo sokoni.” Makala hiyo yamaliza kwa kusema: “Kwa ujumla, sasa kuna zaidi ya tafsiri 450 za Biblia katika Kiingereza pekee. Kukiwa na chapa zote hizi mpya madukani, yaelekea Biblia haitaondolewa karibuni kuwa kitabu kiuzwacho zaidi ya kinginecho chote.”
Matatizo ya Majina
China, ikiwa na watu zaidi ya bilioni 1.2, inakumbwa na ukosefu wa majina ya pili. Kulingana na watafiti, ni majina ya pili 3,100 tu yanayotumiwa huko, yakilinganishwa na 12,000 hivi yaliyotumiwa wakati uliopita. Karibu watu milioni 350—sawa na idadi za watu wa Marekani na Japani zikiunganishwa—wanatumia majina ya pili matano yaliyo ya kawaida sana: Li, Wang, Zhang, Liu, na Chen. Kwa kuongezea, majina ya kwanza yaleyale pia hutumiwa na watu wengi. Kwa kielelezo, katika Tianjin, zaidi ya watu 2,300 wanatumia jina Zhang Li na kuliandika kwa kutumia herufi zilezile, na wengine wengi hutumia matamshi yayo hayo lakini wakiandika kwa kutumia herufi tofauti. Kwa sababu ya utatanishaji, watu kadhaa wameshikwa na polisi kimakosa, fedha katika benki zimetolewa kimakosa, na upasuaji kufanyiwa watu wasioustahili kwenye hospitali. Jamhuri ya Korea ina tatizo lilo hilo. Uchunguzi katika 1987 ulionyesha kwamba mtu 1 kati ya kila watu 5 huko ana jina la ziada Kim. Ndoa kati ya watu wenye majina ya pili yanayofanana zilikatazwa ili kuzuia watu wa ukoo kuoana. Hili lilisababisha maelfu ya wenzi kuishi pamoja bila kusajili ndoa zao, hivyo wakikosa kustahili kupata bima na mengineyo. Hata hivyo, mahakama ya juu zaidi ya hiyo nchi sasa imeamua kwamba ndoa za watu wenye majina sawa zitaonwa kuwa halali ikiwa wenzi hao kwanza waoana katika nchi nyingine.
Wanawake wa Rwanda Walaumiwa
Wanawake, pamoja na wanaume, lazima walaumiwe kwa uchinjaji wa angalau watu 500,000 Rwanda katika 1994, ladai shirika la London la Haki za Afrika. “Maelfu ya wanawake yaliuawa na wanawake wengine,” ripoti yao yasema. “Kadiri ambayo wanawake walishiriki katika mauaji haina kifani. Hilo halikutokea kiaksidenti. Waliopanga hayo maangamizi makubwa walitaka sana kuhusisha wengi zaidi iwezekanavyo—wanaume, wanawake na hata watoto wa miaka minane. Walikusudia kufanyiza taifa lenye siasa kali lililounganishwa kwa damu ya yale maangamizi ya jamii nzima-nzima.” Wengi wa wanawake waliohusika walikuwa katika nyadhifa zenye kutumainika—mawaziri, wakuu wa maeneo fulani, watawa, walimu, na wauguzi. Wengine walihusika moja kwa moja katika huo uchinjaji, wakitumia panga na bunduki, huku wengine wakitimiza fungu la kutegemeza kwa kuwachochea wauaji wa kiume, kwa kuwaruhusu nyumbani mwao na kwenye hospitali, na kwa kupora nyumba mbalimbali na kuvua nguo za maiti na kuchukua vitu vingine vyazo.
Visafishi vya Kiasili
Mimea fulani yenye maua huonyesha uwezo wa ajabu wa kusafisha na kuufanya upya mchanga wa jangwani uliochanganyika na mafuta kuwa mzuri, laripoti The Times la London. Wanasayansi wamegundua kuwa mahali ambapo mafuta hupungua asilimia 10 ya uzito wa mchanga, mimea hiyo yaweza kukua vizuri nayo mizizi yayo hubaki ikiwa misafi kabisa. Sababu ni nini? Mamilioni ya bakteria zinazoizingira mizizi ya hiyo mimea hula mafuta na kuyavunjavunja yawe yasiyo na madhara. Mimea hii hutoka katika mojawapo familia zilizo kubwa zaidi za mimea, Compositae, ambayo hutia ndani daisi, asta, na magugu mengine mengi. Wanasayansi hupendekeza kwamba mimea hiyo ipandwe ili iharakishe usafishaji wa jangwa katika Kuwait. Miaka minne baada ya vita na Iraki, karibu kilometa 50 za mraba za jangwa bado ni chafu.
Watumia Vichwa Vyao
“Wanawake wa Afrika hutembea kilometa nyingi wakibeba mitungi mizito ya maji au vyungu vya chakula kana kwamba hawabebi chochote,” lasema gazeti Discover. “Watafiti wamegundua kwamba wanawake hubeba mizigo mizito bila kutumia nguvu zozote za ziada.” Baadhi ya wanawake wa Kenya hubeba hata kufikia asilimia 20 ya uzito wao wenyewe bila jitihada ya ziada. Wao hufanyaje hilo? Kwa kubeba “mizigo yao kwa njia ifaayo zaidi kuliko watu wanaobeba mizigo mizito migongoni ambao hawajazoezwa kutumia vichwa vyao,” lajibu New Scientist. “Watafiti huamini kwamba siri iko katika ule mwendo wa wanawake wa kuyumba.” Tutembeapo, sisi huyumba tukipitisha sehemu fulani ya nguvu hizo hadi kwenye hatua ifuatayo. Kwa Wazungu, ufanisi wa kupitisha nguvu hizo hupungua kadiri mzigo unavyozidi kuwa mzito. Lakini kwa wanawake wa Afrika wanaobeba mizigo kwenye vichwa vyao, ufanisi huongezeka, hivi kwamba misuli yao haihitaji kufanya kazi yoyote ya ziada. Hata hivyo, mbinu hiyo huchukua miaka mingi kusitawisha.
“Ugonjwa wa Yerusalemu”
Huo ni “ugonjwa wa watalii, ambao kwa kuzidiwa na hisia zenye nguvu zinazotokezwa na kuwa katika Yerusalemu, wanasadiki kabisa kuwa wao ndio Mwokozi, au watu wengine wa kibiblia, au kwamba wamepewa ujumbe wa pekee au mamlaka na Mungu,” lasema gazeti Time. “Wengi wao wana historia ya matatizo ya kiakili.” Mwitalia mwenye ndevu nyingi, aliyepatikana akizurura katika vilima karibu na Bethlehemu akiwa amevalia magunia, adai kuwa ndiye Yesu. Mtu aliye uchi, abebaye upanga, anayekimbia-kimbia sehemu ya Mji wa Kale, asema kwamba ana utume wa kuwaponya vipofu. Mkanada mwenye maungo mapana asema kwamba yeye ndiye Samsoni na “kuthibitisha” hilo kwa kuvunja vyuma vya dirisha la wodi ya hospitali na kutoroka. Walio na ugonjwa huo kwa kawaida hupelekwa kwenye Hospitali ya Matatizo ya Akili ya Kfar Shaul ya Yerusalemu—si ili waponywe bali watulizwe ili warudi nyumbani wakatibiwe. Hiyo hospitali huwahudumia wagonjwa karibu 50 wa aina hiyo kwa mwaka, wengi wao wakiwa wametoka Ulaya Magharibi na Marekani.