Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 7/8 kur. 9-11
  • Habu—Nyoka wa Kuepukwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Habu—Nyoka wa Kuepukwa
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ubuni Wenye Kutisha Ajabu
  • Kuepuka Shambulio Lake
  • Namna Gani Ukiumwa?
  • Habu wa Kuuzwa
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1997
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1997
  • Je, Ungependa Kukutana na Fira?
    Amkeni!—1996
  • Hatari!—Nina Sumu
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 7/8 kur. 9-11

Habu—Nyoka wa Kuepukwa

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA OKINAWA

ILIKUWA jioni moja yenye unyevu bila upepo wowote. Mvua ilikuwa imeacha tu kunyesha, na kila mtu alikuwa akijipepea polepole, ili kujaribu kuondoa joto. Kwa ghafula, makelele yakasikika: “Habu!” “Kuna habu!” Makelele hayo yakashtusha wanakijiji. Watu wazima wakachukua fimbo na kuondoka mbio; watoto wenye udadisi nao wakawafuata mbio. Alikuwa wapi? Kila mtu alitaka kujua. Mtu anaweza kufa akiumwa na nyoka huyo mwenye urefu wa karibu meta mbili. Wanakijiji walihisi wametulia wakati wale wenye umri mkubwa zaidi walipopiga kichwa cha nyoka huyo kwa fimbo zilizo ndefu mpaka akapoteza fahamu. Kisha akawekwa haraka-haraka ndani ya mfuko ili auzwe akiwa hai.

Katika Visiwa vya Ryukyu, ambavyo viko katika Bahari ya China Mashariki, kila mtu kutoka mtoto hadi babu huepuka habu—yule nyoka mwenye kichwa kama mkuki na madoa-doa manjano—ambaye ni vipiri mwenye matundu ya “kunusa” apatikanaye katika baadhi ya visiwa hivyo. Sasa ebu tumchunguze kwa ukaribu zaidi nyoka huyo mwenye kuogofya. Lakini kumbuka kumwepuka ni kukaa mbali sikuzote!

Ubuni Wenye Kutisha Ajabu

Kuna aina mbalimbali za habu. Aina moja ina madoa ya kijani-hudhurungi yanayomfanya ajifiche vyema sana katika nyasi na majani ya mti yanayooza. Wengine wana rangi nyeusi zaidi ambayo inapatana sana utendaji wa habu wa wakati wa usiku na mwelekeo wake wa kujificha katika sehemu zenye giza.

Kiumbe huyo ana uwezo mbalimbali ambao sisi hatuna, ingawa haoni vizuri sana vitu vya mbali. Amepewa matundu, kila moja likiwa kila upande wa kichwa chake. Hayo ni mashimo yaliyoko kati ya mianzi ya pua na macho ambayo huhisi joto haraka sana. Hayo matundu mawili humsaidia “kuona” mnururisho usioonekana ambao wanadamu huhisi kama joto. Akiwa na hayo, habu aweza kulenga kabisa panya mdogo mwenye joto, hata katika giza tititi.

Huenda umeona nyoka akitoa-toa ulimi wake nje. Ulimi wake hutumika ukiwa pua ya pili ya ajabu. Kwa kutoa-toa ulimi hivyo habu huchukua kemikali zilizo hewani na kisha afinya ulimi kwenye kiungo fulani chenye kuitikia kemikali katika sehemu ya juu ya kinywa chake. Pua hiyo ya pili inapofanya kazi, habu hupata habari nyingi za kemikali kutoka hewani.

“Habu huendelea kutoa-toa ulimi wake mara nyingi sana baada ya kufanya shambulio,” wakasema watafiti R. M. Waters na G. M. Burghardt wa Chuo Kikuu cha Tennessee. Kwa nini habu hutafuta kichocheo cha kemikali hewani baada ya kufanya shambulio? Kwa kuwa kuna hatari ya kushambuliwa na windo lisilo na tumaini, habu, baada ya kuuma na kuingiza sumu, mara nyingi huliacha hilo windo. Kisha, sumu inapoanza kuathiri windo hilo, huyo vipiri hulitafuta kwa “kunusa” akitumia ulimi wake.

Akiwa amelipata windo hilo ambalo sasa halijiwezi, liwe ni panya, kifaranga, au ndege, basi habu hulimeza lote—kichwa, miguu, mkia, manyoya, na kila kitu. Utaya wake wa chini hujifungua upande wa nyuma, ukifanya mfupa wa utaya ujitenganishe ili windo kubwa sana liweze kumezwa. Paka mzima alipatikana tumboni mwa habu mmoja ambaye amewekwa kwenye maonyesho katika mojayapo vituo vya utafiti vya habu katika Okinawa.

Namna gani habu akipoteza jino lake lililo kama sirinji anaposhambulia kitu? Jino jipya litamea mahali palo. Kwani, baadhi ya habu wameonekana na meno mawili kila upande wa vinywa vyao! Isitoshe, hata habu akipoteza meno yake, hawezi kufa njaa. Habu mmoja alirekodiwa kuishi kwa miaka mitatu kwa kunywa maji pekee.

Kuepuka Shambulio Lake

Ingawa koboko wa Asia ya Kusini-Mashariki na songwe wa Afrika huingiza sumu ya neva, habu huingiza sumu kali ya mvujo wa damu. Hiyo huitwa sumu ya mvujo wa damu kwa sababu sumu hiyo husababisha mvujo kwa kuharibu mishipa ya damu. Sumu hiyo husababisha maumivu makali kana kwamba unachomwa na moto na kufura, nayo yaweza kuua.

Wengine hufikiri kwamba nyoka huyo huruka kutoka mafichoni na kukimbiza wanadamu, lakini si hivyo. Habu hapendi kuuma watu. Ila tu ukimkanyaga habu bila kujua au kuingia katika eneo lake ndipo tu huenda akakushambulia. Wengi wa wale ambao wameumwa na habu ni wale ambao walikuwa katika maeneo ambamo habu alikuwa akitafuta mawindo, kama vile katika mashamba ya mboga au ya miwa. Wenyeji wa kisiwa hicho hawatembei kamwe katika nyasi ndefu bila kukinga vizuri miguu, nao hubeba tochi wakati wa usiku. Habu hutenda hasa wakati wa usiku. Na usisahau kwamba nyoka hawa wanajua sana kupanda miti, jambo ambalo huwawezesha kupoza joto wakati wa kiangazi na vilevile kuwa karibu na ndege wasiotahadhari. Basi chunga kichwa chako, na vilevile hatua zako, unapokuwa karibu na makao yao!

Njia bora zaidi ya kushughulika na vipiri huyo kwanza kabisa ni kutomkaribisha. Ziba mashimo yote katika msingi wa nyumba na kuta za nje. Ondoa nyasi ndefu katika ua wako. Yaani, usimpe habu mahali pa kujificha.

Namna Gani Ukiumwa?

Ni nini kinachoweza kutokea iwapo ungekutana na mmojawapo nyoka hawa wenye sumu? Labda habu atajikunja, nusu ya mbele ya mwili wake ikiwa na umbo la S. Ndiye huyo yuaja! Thuluthi-mbili za mwili wake warushwa mbele kukuelekea, taya zikiwa wazi, meno yakikufikia kwanza.

Usishikwe na hofu. Chunguza uone kama kwa hakika ni habu aliyekushambulia. Umo la habu laweza kutambulishwa kwa madoa mawili mekundu-mekundu, yaliyoachana kwa karibu sentimeta mbili, ambapo meno yaliingia katika ngozi yako. Baadhi ya habu waweza kuwa na meno matatu au manne, jambo linaloongeza idadi ya madoa mekundu-mekundu. Upesi, hisi ya kuchomwa, kana kwamba mtu ameweka mkono wako katika moto, huongezeka. Unaweza kufanya nini? Omba msaada. Kisha nyonya sumu na kuitema chini. “Nyonya damu kwa kurudia-rudia kwa angalau mara kumi,” chasema Handbook for the Control of Habu, or Venomous Snakes in the Ryukyu Islands. Nenda hospitali ambayo ina dawa ya sumu ya habu. Lakini usikimbie kamwe. Kukimbia kutafanya sumu ienee upesi mwilini, jambo linaloongeza madhara na kupunguza hali yako ya kupata nafuu. Ikiwa huwezi kufika hospitali kwa muda usiopungua dakika 30, funga mpira mkono au mguu ulioumwa katika mahali ambapo ni karibu zaidi na moyo ili kukawiza mweneo wa sumu. Hata hivyo usikaze mpira huo sana kwa sababu ni lazima mpwito wa moyo udumishwe. Punguza mkazo kila dakika kumi ili kuruhusu mzunguko wa damu.

Masatoshi Nozaki na Seiki Katsuren, wa idara ya utafiti wa habu katika taasisi ya Okinawa Prefectural Institute of Health and Environment, waliambia Amkeni! kwamba wanadamu, hata baada ya kuumwa, hawasitawishi kinga ya kudumu kwa sumu ya habu. Nyakati zilizopita, mara nyingi kuumwa kulitokeza kukatwa kwa kiungo, lakini leo ni watu wachache sana wanaopoteza kiungo, achilia mbali kufa, kwa kuumwa na habu. Kwa sababu ya dawa zenye kutumika vizuri na mbinu za kutibu, sasa asilimia 95 ya wale wanaoumwa hupona. Ni wale tu wasiotafuta msaada wa kitiba au wale walio mbali sana na tiba ndio wawezao kupatwa na majeraha mabaya sana.

Habu wa Kuuzwa

Habu wana maadui wachache kiasili. Paka wa nyumbani na mbwa wana mwelekeo wa kucheza naye. Nyoka mmoja asiye na sumu aitwaye akamata, vicheche fulani, nguruwe mwitu, na mwewe ni miongoni mwa wale wanaomla. Ingawa nguchiro waliletwa Visiwa vya Ryukyu ili kusaidia kudhibiti idadi ya habu, hawajafanikiwa katika kuwaondosha.

Adui wake wa kiasili aliye hatari zaidi ya wote ni binadamu. Kama tu wale wanakijiji waliotoka mbio wakipiga kelele za “Habu!” mara tu walipomsikia, kuna wengi wanaotamani kumshika habu mara tu aonekanapo. Japo hatari iliyoko, bei ya kati ya dola 80 na 100 (za Marekani) kwa habu mmoja ni kishawishi kikubwa sana kwa wengi.

Habu hutumiwaje? Pombe ya habu na poda yake iliyokaushwa, ambazo hutumiwa kwa ajili ya afya, hutengenezwa kutokana naye. Wengi hutumiwa wakiwa hai katika maonyesho ya kuvutia watalii. Bila shaka ngozi yake ni nzuri kwa kutengeneza vibeti na mishipi, na sumu yake hutumiwa kutengeneza dawa ya sumu ya nyoka. Hata awe anatumiwa kivipi, shauri ni lilelile, kaa mbali na habu!

[Picha katika ukurasa wa 10]

“Habu” akiwa na meno kama sirinji. Utaya wake wa chini hujifungua ili ameze windo kubwa sana

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki