Kuutazama Ulimwengu
Mambo Mapya Kuhusu Ulimwengu Wote Mzima
Uvumbuzi mwingi wa majuzi unafanya wanasayansi wa anga za nje wafikirie tena nadharia nyingi, kulingana na The New York Times. Kwa mfano, waastronomia wenye kuchunguza mbali sana katika mbingu wakitumia Darubiniupeo ya Angani ya Hubble wamefikia mkataa wa kwamba kuna galaksi zikadiriwazo kuwa kati ya bilioni 40 na 50 katika ulimwengu wote mzima wetu. Hilo latofautiana na makadirio ya awali ya bilioni 100. Siku moja baada ya kutangaza jambo hilo, wanasayansi wa Shirika la Anga la Marekani walitoa ripoti zaidi kwamba walikuwa wametambua angalau nusu ya “mata iliyokuwa imekosekana” ya ulimwengu wote mzima, masi isiyojulikana inayotoa nguvu ya uvutano ambayo inashikilia galaksi zote pamoja. Wanasayansi wasema kwamba kiasi kikubwa cha mata hiyo isiyoonekana chaweza kuwa kimefanyizwa na idadi kubwa za nyota ambazo zimeungua ziitwazo white dwarfs. Kwa kuongezea, nadharia zinazohusu sayari Sumbula zinapingwa na habari zinazotoka katika chombo cha anga cha Galileo. “Sikuzote kuna hisia ya unyenyekevu wakati ambapo habari huja kwa mara ya kwanza,” akasema mwanasayansi mkuu wa mradi huo Dakt. Torrence Johnson. “Matokeo ya habari hizo mara nyingi hayapatani na nadharia zetu.”
Ongezeko la Utekaji-Nyara
Katika mwaka mmoja wa majuzi, wahalifu katika Rio de Janeiro, Brazili, walipata dola bilioni 1.2 (za Marekani) kutokana na biashara inayositawi ya utekaji-nyara, laripoti Jornal da Tarde, jambo linalofanya utekaji-nyara kuwa chanzo kikuu cha mapato kwa magenge ya kufanya uhalifu katika jiji hilo. Utekaji-nyara umekuwa wenye kutatanisha hata zaidi. Kuna ule uitwao “umeme,” au wa muda mfupi, utekaji-nyara wa watu wenye mapato ya kiasi, “ambao mara nyingi hulazimika kulipa fidia polepole,” na mpango wa hali ya juu sana na wenye kuratibiwa vizuri wa kuteka nyara matajiri. Katika nchi nyinginezo utekaji-nyara unaongezeka pia. Gazeti Asiaweek lasema kwamba wataalamu wa Filipino wapendekeza hivi, miongoni mwa mambo mengine: Usisafiri peke yako, hasa baada ya giza kuingia. Sikuzote mwambie rafiki unayemtumaini mahali ambapo utakuwa. Egesha gari lako katika maeneo salama yenye taa. Usiache watoto wakiwa peke yao.
Tahadhari ya Vitamini-A
Kulingana na uchunguzi mmoja wa wanawake waja wazito 22,000, ambao ulitangazwa katika The New England Journal of Medicine, mama waja wazito wapaswa kujihadhari wasile vitamini-A kupita kiasi. Ingawa kiasi fulani cha vitamini-A ni muhimu kwa afya na ukuzi wa kiinitete cha kibinadamu, ilipatikana kwamba inaweza kusababisha madhara inapopita kiasi. Kiasi cha vitamini-A kinachopendekezwa kutumiwa kila siku na wanawake waja wazito ni vipimo 4,000 vya kimataifa, yasema Tufts University Diet & Nutrition Letter, lakini wanawake wanaotumia zaidi ya vipimo 10,000 kwa siku “wamo hatarini zaidi ya mara mbili na nusu ya kuzaa mtoto mwenye kulemaa kuliko wanawake wasiotumia vitamini-A kupita kiasi.” Kwa sababu mwili huweka akiba ya vitamini-A, hata kutumia vitamini-A nyingi kabla ya kushika mimba kwaweza kuhatarisha mtoto. Ilipatikana kwamba beta-karotini, tokeo la mmea ambalo hugeuzwa nusu kuwa vitamini-A mwilini, si hatari.
Mbao Yenye Kukinza Visumbufu
Hekalu moja la mbao lililoko Nara, Japani, limekuwapo kwa miaka 1,200 bila kuharibiwa na wanyama wenye kuguguna, mchwa, au vijiumbe, laripoti gazeti New Scientist. Wawakilishi wa Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Seoul katika Korea na wanasayansi wawili Wajapani walienda kujifunza ni nini kinachofanya hekalu hilo likirihiwe sana na visumbufu. Walipopima aina hiyo ya mteashuri iliyotumiwa kujenga jengo hilo la kale, waligundua kwamba ulikuwa na kemikali fulani inayokirihiwa sana na wanyama wenye kuguguna hivi kwamba hawawezi kuuma chochote kilichopakwa kemikali hizo. Viwanda vya Japani vya mbao hutengeneza karibu tani 4,000 za mavumbi kutokana na mteashuri kila mwaka, na inatumainiwa kwamba vitu vinavyotengenezwa kwa mavumbi hayo vyaweza kuchukua mahali pa baadhi ya sumu zinazotengenezwa kudhibiti visumbufu.
Ombi la Kutaka Giza
Waastronomia katika Ufaransa wanapigania giza zaidi. Kiasi kikubwa sana cha nuru isiyofaa majijini kinafanya isiwezekane kuona vizuri sana mbingu zenye nyota. Kulingana na gazeti Le Point, waastronomia walikuwa wakiwasihi sana wenye mamlaka wa jiji kuzipa taa za barabarani viakisi vyenye kuelekeza taa hizo chini na kutaka kwamba taa za matangazo ya biashara na za majengo ya ofisi, na vilevile taa za wonyesho za leza, zizimwe saa tano za usiku. Michel Bonavitacola, msimamizi wa Kituo cha Kulinda Anga ya Usiku, alibisha hivi: “Leo hakuna hata mtoto mmoja kati ya mia moja awezaye kusema kwamba amepata kuona nyota za Njia ya Kimaziwa. Ilhali tamasha hii, ambayo ni maridadi sana na ya bure kutazama, hutusaidia kufahamu mahali petu hasa katika ulimwengu wote mzima.”
Wazazi Wasiofahamu
Kuhusu kuelimisha watoto wao, wazazi wengi sana wasema kwamba “mafanikio” na “uhuru” ndiyo mambo ya kutangulizwa zaidi, nao wanahisi ni juu ya watoto kuchagua maadili yao wenyewe, kulingana na uchunguzi mmoja ulioripotiwa katika gazeti la Ufaransa L’Express. Walipoulizwa ikiwa mradi wa elimu ni kufundisha maadili yafaayo, asilimia 70 ya wazazi wenye watoto walio na umri kati ya miaka 6 na 12 walijibu la. Asilimia 60 ya wazazi na walimu waliohojiwa huona watoto kuwa hawajajiandaa vyema kwa wakati ujao na kwa kushangaza wao bado waamini kwamba hao watoto watakuwa wenye mafaa sana kwa jamii, likasema gazeti hilo. Uchunguzi huo wathibitisha hofu za wataalamu wengine, lasema L’Express, kwamba “wazazi leo hawajui kamwe daraka lao wala wajibu wao.”
Onyo Juu ya Chakula Kisicho na Mafuta Mengi
Uchunguzi wa mapendezi ya wanunuzi wafunua kwamba viongezo vinavyotumiwa mahali pa mafuta katika vyakula vingi visivyo na mafuta mengi havina muundo wa mtindi kama mafuta halisi, laripoti Globe and Mail la Kanada, na hilo laweza kufanya watu wale vyakula hivyo zaidi au kuongeza vyakula vingine zaidi ili kupata ladha. Viongezo ambavyo hutumiwa kuchukua mahali pa mafuta, kama vile sukari, chumvi, na ladha za kutengenezwa, mara nyingi hazifai lishe, kulingana na Dakt. David Jenkins, profesa wa sayansi na fisiolojia ya lishe kwenye Chuo Kikuu cha Toronto. Dakt. Jenkins ashauri hivi: “Watu wakiamua kwamba mojayapo njia za kupunguza mafuta mwilini ni kwa kula chakula kisicho na mafuta mengi, ni sawa, maadamu chakula hicho ni chenye lishe kiafya.” Yeye apendekeza kwamba mboga, matunda, nafaka, na vilevile njugu zisizo na mafuta mengi na vitu vinavyotokana na soya, ni vibadala vizuri.
Mapenzi na Chokoleti
Katika nchi nyingi mwanamume aweza kumpa mwanamke chokoleti ikiwa wonyesho wa kwamba anampenda. Kwa kupendeza, hisia zenye kuamka zitokezwazo na kula chokoleti na hisia ya kushikwa na mapenzi huenda zikawa na uhusiano fulani—kutokezwa kwingi kwa hormoni iitwayo phenylethylamine katika ubongo. Kulingana na The Medical Post la Toronto, Kanada, Peter Godfrey, mtafiti mmoja wa Australia, amegundua “molekuli ya mapenzi,” kama ambavyo imeitwa. Wakiwa na habari hii mpya, wanasayansi wanatumaini kujifunza zaidi kuhusu jinsi hisia-moyo huchochewa katika ubongo. Isitoshe, likasema Post, hilo “laweza kueleza ni kwa nini wengine hupenda chokoleti sana.”
Daraja la Skye
Daraja kubwa zaidi kati ya madaraja yenye egemeo moja, lenye umbali wa kilometa 2.4, lilifunguliwa majuzi katika Scotland, laripoti The Times la London. Daraja hilo huunganisha Kisiwa cha Skye cha Scotland chenye wakazi 9,000 na pwani ya magharibi ya Scotland. Ili kusherehekea kuzinduliwa kwa daraja hilo, bendi ya kupiga begipaipu na andamano la magari ya zamani ziliongoza msafara wa wasafiri—wote walialikwa kuvuka bila malipo siku hiyo. Daraja hilo lachukua mahali pa utumishi wa feri ambayo imevukisha magari na abiria kwenda na kutoka kisiwa hicho kwa miaka 23 ambayo imepita. Kulingana na The Times, katibu wa Scotland alisema kwamba sasa inawezekana kwa wenye magari kusafiri kutoka Roma hadi Uig, katika kaskazini-magharibi mwa Skye, bila kuondoka ndani ya magari yao.
Maumivu ya Koo Yatokezwayo na Kompyuta
Watumiaji wa kompyuta wanaotafuta njia za kuondoa maumivu ya viganja na mikono kwa kutumia mfumo wa kutumia sauti inayotambulika na kompyuta wanakabili kile ambacho wengine wanaona kuwa tatizo kubwa hata zaidi—mkwaruzo wa kudumu wa sauti na hata kupoteza sauti kabisa, laripoti gazeti la habari The Globe and Mail la Kanada. Kwa kuwa ni lazima kila neno lisemwe wazi na kwa uzito na mkazo uleule ili lieleweke na kompyuta, watumiaji hawapumui kwa njia ya kawaida, na nyuzi za sauti huelekea kupoteza hali yayo ya kunyumbuka. Dakt. Simon McGrail wa Chuo Kikuu cha Toronto aliliambia Globe kwamba vidonda vyaweza kutokea katika nyuzi za sauti zinapojigonganisha kila wakati, au nyuzi zenyewe zichoke. Ili kudumisha nyuzi za sauti zikiwa zenye afya, wataalamu wa sauti wapendekeza kwamba watumiaji wapunguze muda wanaotumia kwenye kompyuta kama hizo, wapumzike mara kwa mara, wanywe maji mengi, na kuepuka alkoholi, kafeni, na dawa ambazo hukausha nyuzi za sauti.