Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 8/8 kur. 16-17
  • Dirisha Lafunua Tumbo la Uzazi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Dirisha Lafunua Tumbo la Uzazi
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “Wasiogusika” Katika Tumbo la Uzazi?
  • Biblia Inasema Nini Kuhusu Kutoa Mimba?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2009
  • Matokeo Yenye Msiba ya Utoaji-Mimba
    Amkeni!—1993
  • Je, Utoaji-Mimba—Ndio Suluhisho?
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 8/8 kur. 16-17

Dirisha Lafunua Tumbo la Uzazi

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA

MAENDELEO ambayo yamefanywa katika kupimwa kwa mimba siku hizi yanawezesha madaktari kugundua kwa usahihi zaidi matatizo yoyote, ya kimwili au kiakili, ambayo mtoto asiyezaliwa aweza kuwa nayo. Vifaa vinavyotumiwa sana vyatia ndani ultrasound na amniocentesis.

Njia ya ultrasound ni ile isiyohusisha kuingizwa kwa chochote kwenye tumbo la uzazi bali hutumia mawimbi ya juu sana ya sauti ili kufanyiza kwenye kompyuta taswira ya mtoto mchanga aliye katika tumbo la uzazi. Njia ya amniocentesis huhusisha kuchukua kwa sindano umajimaji wa mimba, ule umajimaji ambao mtoto huelea kwao katika tumbo la uzazi, na kuupima ikiwa kuna dalili za kemikali zinazoonyesha kasoro za vijusu, kama vile ugonjwa wa Down’s syndrome.

Ikitupiwa jamii kama mwamba unaotupwa katika kidimbwi, aina hii ya tekinolojia ya kitiba, ikiambatana na utoaji-mimba wa kuteuliwa, inasababisha msukosuko mkubwa katika maadili ya kitiba.a Kwa ubaya, kanuni za ulimwengu si msingi thabiti wa kusuluhishia masuala ya maadili nazo huonekana kama kitu chenye kuelea majini katika mawimbi mazito kisichojua mahali ambapo kinaelekea.

Utoaji-mimba wa kuteuliwa, ukisaidiwa na tekinolojia, haujafikiwa na marekebisho ya sheria katika nchi fulani. Katika chunguzi 13 zilizofanywa Marekani katika kipindi cha miaka 15 cha majuzi, kwa kurudia-rudia asilimia 75 hadi 78 ya waliohojiwa wanaamini kwamba mwanamke mjamzito apaswa kuwa na haki kisheria ya kutoa mimba mtoto mchanga ambaye inaelekea sana ana dalili kubwa za kasoro mbaya sana. Katika nchi fulani “kutabiri kwamba mtoto asiyezaliwa hajiwezi” kwatosha kuruhusu utoaji-mimba ufanywe.

Hivi majuzi katika Australia, mama mmoja kwa mafanikio alishtaki daktari wake kwa ajili ya madhara kwa sababu mapema katika mimba yake, daktari huyo alikosa kugundua ugonjwa wa surua ya Ujerumani. Ugonjwa huo, unapokushika mapema katika mimba, waweza kutokeza ulemavu mbaya sana kwa mtoto asiyezaliwa. Huyo mama alidai kwamba kwa sababu daktari wake alikosa kuugundua ugonjwa huo hakuweza kutoa mimba hiyo.

Akitoa maelezo juu ya matokeo ya kisheria na kimaadili ya kesi hiyo, mtafiti wa mambo ya sheria Jennifer Fitzgerald katika makala moja katika Queensland Law Society Journal la Aprili 1995, alisema: “Si kwamba tu yeye [mwanamke mjamzito] ahitaji kuamua, ‘Je, nataka kuwa na mtoto?’, ni lazima pia aamue, ‘Nataka mtoto wa aina gani?’” Lakini ni kutojiweza kupi, auliza Fitzgerald, ambako ni msingi mzuri wa kutoa mimba kihalali? “Midomo iliyopasuka, kaakaa lililopasuka, kengeza, ugonjwa wa Down’s syndrome, nafasi kwenye uti wa mgongo?” Katika sehemu fulani za ulimwengu, ni jinsia ya mtoto inayotokeza utoaji-mimba, hasa kama ni wa kike!

“Wasiogusika” Katika Tumbo la Uzazi?

Jenomu (nyuzi-nyuzi katika chembe za uhai) za binadamu zinapoonekana wazi mbele za wanasayansi na vifaa vya kisasa kuwa kama hadubini ya kuchungulia tumbo la uzazi, yule asiyezaliwa ataendeleaje? Je, wale ambao wana kasoro ndogo-ndogo watateuliwa ili watolewe mimba? Hakika, mwendo wa miongo ya majuzi unapendelea utoaji-mimba zaidi, si chache. Wakikabiliwa na ongezeko la utoaji-mimba na ongezeko la mashtaka mahakamani—kama ile kesi iliyotajwa mapema—madaktari wanahangaika. Kwa kueleweka, hilo laweza kuwashurutisha wajikinge zaidi kitiba, kama vile kudai upimaji fulani ufanywe, si sana kwa ajili ya mama na mtoto bali ili kujikinga dhidi ya mashtaka. Fitzgerald aandika matokeo ni kwamba “idadi ya kupimwa kwa mimba yaelekea kuongezeka na, ndivyo ilivyo na utoaji-mimba wa kuteuliwa.” Aongezea kwamba hilo, litaingiza “mfumo wa ubaguzi ambamo ‘wasiogusika’ wawa ‘waondolewao.’”

Na vipi mama akizaa mtoto asiyejiweza licha ya kupata kila fursa—na hata kutiwa moyo—kumtoa mimba? “Labda wakati utakuja,” asema Fitzgerald, “wakati wazazi wataambiwa kwamba wao hawawezi kupata msaada wa serikali katika kutimiza mahitaji ya watoto wao wenye ulemavu kwa sababu wao walichagua kumzaa mtoto huyo ilhali walikuwa na fursa ya kumtoa.”

Jambo ambalo halipaswi kupuuzwa ni ujumbe ambao utoaji-mimba wa kuteuliwa utawapa watu wasiojiweza katika jumuiya zetu. Ikiwa jamii inamtoa mimba mtoto asiyezaliwa kwa sababu ya kasoro zake, je, hilo litafanya watu wasiojiweza kuhisi kwamba wao ni mzigo kwa wengine? Je, itafanya iwe vigumu kwao kukabiliana na hali ya kujishusha heshima ambayo huenda tayari wanayo?

Jambo la kwamba jamii ya kisasa ingetupilia mbali watoto wasiozaliwa kama wafanyakazi wanavyotupilia mbali sehemu mbovu za gari zinapotengenezwa lapatana kabisa na utu ambao Biblia hutaja watu wanaoishi katika “siku za mwisho” za ulimwengu huu mwovu wangekuwa nao. Ilitabiri kwamba kwa kiwango kikubwa sana, watu wangekuwa “wasiowapenda wa kwao.” (2 Timotheo 3:1-5) Neno la Kigiriki aʹstor·goi, lililotafsiriwa “wasiowapenda wa kwao,” larejezea kifungo cha asili kilicho kati ya washiriki wa familia, kama vile upendo wa mama kwa watoto wake.

‘Wakitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu,’ watu wa ulimwengu huu wasio na mwongozo kwa hakika ni tofauti na watu wafuatao Neno la Mungu lililo hakika. (Waefeso 4:14) Kama nanga ya nafsi, Biblia hutuweka imara na thabiti kiadili katika bahari iliyochafuka. (Linganisha Waebrania 6:19.) Hivyo, ingawa Wakristo watambua kwamba mimba yenye kasoro mbaya sana inaweza kutoka yenyewe, wazo lenyewe tu la kuchungulia tumbo la uzazi kuona ikiwa mtoto mchanga ni mwenye afya nzuri ili asitolewe ni chukizo sana kwao.b—Linganisha Kutoka 21:22, 23.

Jambo la kuimarisha azimio la Mkristo la kudumisha uaminifu-maadili ni ahadi ya Mungu ya wakati ambapo “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” (Isaya 33:24; 35:5, 6) Ndiyo, japo magumu ya sasa kwa mtoto asiyejiweza na dhabihu zinazofanywa na wale wanaowatunza, “itakuwa heri kwao wamchao Mungu.”—Mhubiri 8:12.

[Maelezo ya Chini]

a Utoaji-mimba wa kuteuliwa ni zoea la kutoa mimba kwa sababu huyo mtoto mchanga ana hali fulani ambazo mzazi (au wazazi) hataki.

b Bila shaka, hilo halimaanishi kwamba si sawa kwa Mkristo kwenda kupimwa kujua afya ya mtoto mchanga asiyezaliwa. Kunaweza kuwa na sababu kadhaa za kitiba zinazokubalika Kimaandiko zinazofanya tabibu apendekeze apimwe. Hata hivyo, kupimwa kwingine kwaweza kuhatarisha mtoto, na basi ni jambo la hekima kuongea na daktari kuhusu mambo hayo. Kwa sababu ya kupimwa huko, mtoto akipatikana ana kasoro mbaya sana, wazazi Wakristo katika nchi fulani waweza kukazwa watoe mimba hiyo. Lingekuwa jambo la hekima kujitayarisha kushikilia kanuni za Biblia.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki