Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 9/8 kur. 4-7
  • Walitoka Wapi?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Walitoka Wapi?
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Wenyeji wa Amerika —Asili na Itikadi Zao
  • Kuelewa Falsafa za Wenyeji wa Amerika
  • Jinsi Ulimwengu Wao Ulivyopotea
    Amkeni!—1996
  • Wazaliwa wa Amerika na Biblia
    Amkeni!—1999
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1997
  • Wakati Wao Ujao Una Nini?
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 9/8 kur. 4-7

Walitoka Wapi?

“TULIJIITAJE kabla ya Columbus kuja? . . . Katika kila kabila, hata leo, ukitafsiri neno ambalo tulijiita katika kila kabila, bila kujua makabila mengine yamejiitaje, mara nyingi jina hilo lilimaanisha jambo lilelile. Katika lugha yetu [Kinarrangansett] tulijiita Ninuog, au watu [katika Kinavajo, Diné], yaani wanadamu. Ndivyo tulivyojiita. Hivyo wakoloni [watu wa Ulaya] walipofika hapa, tulijijua, lakini hatukujua wao ni nani. Basi tukawaita Awaunageesuck, au watu wasiojulikana, kwa sababu ni wao ambao hawakujulikana, ni wao ambao sisi hatukuwajua, lakini sisi tulijuana. Na ni sisi tuliokuwa wanadamu.”—Oki Mrefu, wa kabila la Narragansett.

Kuna nadharia nyingi kuhusu asili ya Wenyeji wa Amerika.a Joseph Smith, mwanzilishi wa Wamormon, alikuwa mmojawapo watu kadhaa, kutia ndani mfuasi wa Quaker William Penn, walioamini kwamba Wahindi walikuwa Waebrania, wazao wa yale yaitwayo makabila kumi yaliyopotea ya Israeli. Leo, ufafanuzi unaokubaliwa na wengi wa waanthropolojia ni kwamba ama kwa kupitia ardhi inayounganisha Asia na Amerika au kwa mashua, makabila ya Asia yaliingia katika eneo linaloitwa sasa Alaska, Kanada, na Marekani. Hata uchunguzi wa DNA (kanuni za kuongoza urithi) waonekana kuunga mkono wazo hilo.

Wenyeji wa Amerika —Asili na Itikadi Zao

Wahariri ambao ni Wenyeji wa Amerika Tom Hill (wa kabila la Seneca) na Richard Hill, Sr., (wa kabila la Tuscarora) waandika katika kitabu chao Creation’s Journey—Native American Identity and Belief: “Wenyeji wengi wa Amerika huamini kimapokeo kwamba wao waliumbwa kutokana na dunia yenyewe, kutokana na maji, au kutokana na nyota. Kwa upande mwingine, waakiolojia wana nadharia ya ardhi kubwa iliyovuka Mlangobahari wa Bering, ambayo kuipitia, Waasia walihamia nchi za Amerika; Waasia hao, nadharia hiyo yasisitiza, walikuwa wazazi wa kale wa wenyeji wa Kizio cha Magharibi.” Baadhi ya wenyeji wa Amerika huelekea kutilia shaka nadharia ya mzungu ya Mlangobahari wa Bering. Wao hupendelea kuamini hekaya zao na masimulizi yao. Wao hujiona kuwa wakazi wa asili badala ya kuwa wavumbuzi waliohamia huko kutoka Asia.

Katika kitabu chake An Indian Winter, Russell Freedman aeleza hivi: “Kulingana na itikadi ya Wamandan [kabila lililokuwa karibu na sehemu za juu za Mto Missouri], Mtu wa Kwanza alikuwa roho mwenye nguvu sana, kiumbe cha kimungu. Alikuwa ameumbwa zamani sana na Bwana wa Uhai, muumba wa vitu vyote, atende akiwa mpatanishi kati ya wanadamu wa kawaida na miungu mingi, au roho, zilizokuwa zikiishi mbinguni.” Itikadi ya Wamandan hata ilitia ndani hekaya ya furiko. “Pindi moja, furiko kubwa lilipojaza ulimwengu, Mtu wa Kwanza aliokoa watu kwa kuwafundisha kujenga mnara wa ulinzi, au ‘safina,’ ambao ungeinuka juu sana kupita maji ya furiko. Kwa heshima yake, kila kijiji cha Wamandan kilikuwa na kifananishi kidogo cha mnara huo wa kihekaya—nguzo ya mwerezi yenye kimo cha karibu futi tano, iliyozingirwa na ua wa mbao.”

Wamandan walikuwa na mfano wa kidini pia “ufito mrefu uliofunikwa kwa manyoya nao ulikuwa na kichwa chenye kuogofya cha mbao, kilichopakwa rangi nyeusi.” Huo uliwakilisha nani? “Mfano huo uliwakilisha Ochkih-Haddä, roho mwovu ambaye alikuwa na uvutano mkubwa sana juu ya wanadamu lakini ambaye hakuwa na nguvu kama Bwana wa Uhai au Mtu wa Kwanza.” Kwa Wahindi wa Nyanda, “kuamini viumbe vya roho kulikuwa sehemu ya maisha isiyobishaniwa. . . . Hakuna uamuzi mkubwa ambao ungeweza kufanywa, hakuna mradi ambao ungeweza kuanzishwa, bila kwanza kutafuta msaada na kibali cha viumbe vitakatifu ambavyo viliongoza mambo ya wanadamu.”

Katika kitabu chake The Mythology of North America, John Bierhorst aeleza: “Kabla ya mbari kuwapo, ilisemwa kwamba Waosage walienda huku na huku katika hali iitwayo ganítha (bila sheria au utaratibu). Maoni ya kimapokeo yalisema kwamba katika siku hizo za awali watu fulani wenye kufikiri walioitwa Wazee Wadogo . . . walifanyiza nadharia kwamba nguvu fulani yenye ukimya ya uumbaji hujaza anga na dunia na kufanya nyota, mwezi, na jua lisonge katika utaratibu kamili. Waliiita nguvu hiyo Wakónda (nguvu isiyofahamika) au Eáwawonaka (msababishi wa kuwapo kwetu).” Wazo kama hilo lashirikiwa na Wazuni, Wasioux, na Walakota katika Magharibi. Wawinnebago pia wana ngano ihusuyo “Mfanyi wa Dunia.” Hilo simulizi lasema: “Alitaka nuru nayo nuru ikaja. . . . Kisha tena akafikiri na kutaka dunia, na dunia hii ikawapo.”

Kwa wanafunzi wa Biblia, ni jambo la kupendeza kuona baadhi ya ulinganifu uliopo kati ya itikadi za Wenyeji wa Amerika na mafundisho yanayoonyeshwa katika Biblia, hasa kwa habari ya Roho Mkuu, “msababishi wa kuwapo kwetu,” jambo ambalo linatukumbusha maana ya jina la kimungu, Yehova, “Yeye Husababisha Iwe.” Ulinganifu mwingine hutia ndani Furiko na roho mwovu aitwaye Shetani katika Biblia.—Mwanzo 1:1-5; 6:17; Ufunuo 12:9.

Kuelewa Falsafa za Wenyeji wa Amerika

Wale waandikaji ambao ni Wenyeji wa Amerika Tom Hill na Richard Hill wafafanua zawadi tano ambazo wao wasema Wenyeji wa Amerika wamepokea kutoka kwa wazazi wao wa kale. “Zawadi ya kwanza . . . ni ushikamano wetu mkubwa kwa ardhi.” Kwa kufikiria historia yao kabla ya na baada ya kufika kwa watu wa Ulaya, ni nani awezaye kukanusha jambo hilo? Ardhi yao, ambayo mara nyingi ilionwa kuwa takatifu na Wenyeji wa Amerika, ilichukuliwa hatua kwa hatua kwa kutumia nguvu, madanganyo, au mikataba ambayo haikutimizwa.

“Zawadi ya pili ni uwezo na roho ambayo wanyama wanashiriki na watu wetu.” Staha ya Wenyeji wa Amerika kuelekea wanyama imeonyeshwa katika njia nyingi. Wao waliwinda kwa ajili ya chakula, nguo, na vibanda vyao pekee. Haikuwa wenyeji ambao karibu wamalize kabisa nyati-singa bali ni mzungu mwenye tamaa ya kumwaga damu na pupa isiyofikiria matokeo.

“Zawadi ya tatu ni viumbe wa roho, ambao ni watu wetu wa ukoo wanaoishi na kuwasiliana nasi kupitia sanamu zao tunazofanyiza.” Hili ni jambo la kawaida kwa dini nyingi ulimwenguni pote—kuokoka kwa roho au nafsi baada ya kifo.b

“Ya nne ni kujua sisi ni nani, jambo linaloonyeshwa na kuendelezwa katika mapokeo yetu ya kabila.” Leo jambo hilo laweza kuonekana katika sherehe za kikabila, ambako watu hukusanyikia kujadili mambo ya kabila, au kwenye makusanyiko ya kijamii, ambako watu hucheza dansi na muziki wa kikabila. Mavazi ya Wahindi, kupigwa kwa ngoma kwa mtindo fulani, michezo ya ngoma, kukutana tena kwa familia na mbari—zote zaonyesha pokeo la kikabila.

“Zawadi ya mwisho ni uwezo wa kubuni—itikadi zetu hufanywa kuonekana kihalisi kupitia kufanyiza vitu vya asili kuwa vitu vya imani na fahari.” Iwe ni kutengeneza vikapu, ufumaji, kufinyanga na kuchora vyombo vya udongo, kutengeneza vito na mapambo, au utendaji mwingine wowote wa sanaa, unahusika na pokeo lao na utamaduni wao wa miaka mingi.

Kuna makabila mengi sana hivi kwamba ingehitajika vitabu vingi kueleza itikadi zayo na matendo yayo yote ya kimapokeo. Sasa kile kinachotupendeza ni, Kuja kwa mamilioni ya watu wa Ulaya, wengi wakiitwa eti Wakristo, kuliathirije Wenyeji wa Amerika?

[Maelezo ya Chini]

a Neno “Wahindi wa Amerika” kwa wazi latia ndani yale makabila yanayoishi Kanada. Wengi huamini kwamba wahamiaji wa mapema kutoka Asia walisafiri kupitia kaskazini-magharibi mwa Kanada wakiwa njiani kuelekea sehemu zenye joto zaidi.

b Biblia haiungi mkono itikadi katika nafsi isiyoweza kufa au roho iokokayo kifo. (Ona Mwanzo 2:7; Ezekieli 18:4, 20.) Kwa habari zaidi, ona kitabu Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu, kurasa 52-56, 75, na faharisi yacho chini ya kichwa “Nafsi isiyoweza kufa, imani katika.” Kitabu hiki kimetangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki