Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 9/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uhuru wa Dini Waimarishwa
  • Uatheisti Waendelea
  • Nipitishie Hao Wadudu, Tafadhali!
  • Komesha Kuungua Nishati!
  • Epuka Usumishaji wa Utotoni
  • Kusoma—Je, Ni “Kifo cha Polepole”?
  • Simu za Kuomba Msaada
  • Vipepeo Wasafiri
  • Maonyo ya Mavazi Mapya
  • Uhalifu na Matineja wa Urusi
  • Ushindi wa Wachache Katika Bara la Usawa
    Amkeni!—1995
  • Kuungua Nishati—Waweza Kuikabilije Hali?
    Amkeni!—1995
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1999
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 9/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Uhuru wa Dini Waimarishwa

Mnamo Machi 8, 1996, Mahakama Kuu Zaidi ya Japani ilitoa uamuzi kwamba Chuo Cha Manispaa cha Ufundi wa Kiviwanda cha Kobe kilivunja sheria kwa kumwondosha shuleni Kunihito Kobayashi, mmoja wa Mashahidi wa Yehova, kwa sababu ya kukataa kwake kushiriki katika mazoezi ya mbinu za kupigana, laripoti The Daily Yomiuri la Tokyo. Kwa kufanya hivyo, mahakama kuu zaidi ya Japani ilikataa rufani iliyofanywa na chuo hicho na kuanzisha kielelezo kwa ajili ya kesi zijazo. (Tafadhali ona toleo la Amkeni! la Oktoba 8, 1995 kwa habari za kina.) Mahakama hiyo ilitambua kwamba sababu za mwanafunzi huyo za kukataa kushiriki katika mazoezi ya kendo ya mbinu za kupigana “zilikuwa za maana na zilihusiana kwa ukaribu na kiini” cha imani yake. Mahakama hiyo ilimtaja Kobayashi kuwa “mwanafunzi mwenye kutokeza” na kutaarifu kwamba shule hiyo ingalimpa elimu ya badala ya kimwili badala ya kendo.

Uatheisti Waendelea

Kadinali Joachim Meisner aona katika Ujerumani “msukumo wenye nguvu kuelekea uatheisti.” Huenda Ukomunisti ulishindwa kiuchumi, lakini yaonekana unasitawi kinadharia, aonelea Meisner. Yeye asema: “Mwelekeo huu yaonekana unaenea kutoka majimbo mapya [yaliyokuwa ya Kikomunisti] hadi kwenye majimbo ya zamani [ya magharibi].” Kulingana na gazeti la habari Weser Kurier, asilimia 70 hivi ya wakazi milioni 16 wa ile iliyokuwa Ujerumani Mashariki si wa kanisa lolote. Ripoti hiyo yaendelea hivi: “Ikiwa kanisa halina ujasiri wa kuchukua hatua nzito katika kutangaza kweli iliyofunuliwa kwalo, basi hilo ni bure.”

Nipitishie Hao Wadudu, Tafadhali!

Watu wengi, ingawa kwa wazi si wote, huenda wakaona taraja la kutibu magonjwa kwa kula wadudu kuwa lenye kuchukiza. Hata hivyo, kulingana na gazeti Asiaweek, wazo hilo si jambo jipya. Katika Singapore, Imperial Herbal Restaurant huandaa vyakula vilivyo na vichanganyiko kama vile sisimizi na nge, wadudu hao wakiwa na sifa si ya kuwa wenye lishe tu bali pia ya kuponya. Mwenye mkahawa huo, Bi. Tee Eng Wang-Lee, asema kwamba sisimizi ni wazuri kwa kutibu baridi-yabisi, huku sumu ya nge yasemekana kuwa hutuliza mishipa ya fahamu na kutuliza tukuta (maumivu makali ya kichwa). Dawa nyinginezo zitokanazo na wadudu hutia ndani mabuu yaliyokaushwa ili kutuliza maumivu; mabuu ya mdudu aitwaye chikada ili kupambana na kujaa hewa tumboni, vidonda vya ngozi, na surua; na kiota kilichokaushwa cha manyigu ili kuua vimelea. Viumbe hivi huonjaje? Sisimizi wana ladha kali-kali kama siki, nao nge ni wenye kutafunika-tafunika. Bi. Wang-Lee ataja: “Ni lazima watu wajaribu mara kadhaa ili wapende ladha hiyo.”

Komesha Kuungua Nishati!

Mkazo wa aina zote unaongezeka, na Ellen McGrath, mwanasaikolojia anayeandika katika gazeti la Marekani Health, aandaa mikakati michache ya kuzuia mkazo usiongoze kwenye kuungua nishati maishani mwako.

▪ Pata pumziko, pumziko lolote: Tembea kwa dakika kumi au upumue kwa kina sana kwa utulivu kwa dakika tano. Weka kando dakika 15 ili kusoma na kuwaza mwanzoni na mwishoni mwa kila siku.

▪ Dhibiti maisha yako: Weka karibu nawe vitu vinavyokufanya utabasamu—picha, maua, au vikumbusho. Chukua hatua ya kupanga ratiba yako na kupanga wakati usio na mkazo mwingi ili ufanye mambo muhimu.

▪ Kula vizuri: Usifanye kazi hadi unapokuwa na njaa kali, wala usiridhike na kitafuno kisicho na lishe bora ili kutuliza njaa yako—hata uwe na shughuli nyingi namna gani. Milo ya mara kwa mara iliyo hasa na matunda na mboga itakusaidia kuepuka uchovu.

▪ Fanya mazoezi: Mazoezi yenye nguvu hupunguza mkazo na kuongeza hisi ya uradhi na ya udhibiti. Yafanye kwa njia ya kufurahisha!

Epuka Usumishaji wa Utotoni

Watoto wachanga wako hatarini mwa kusumishwa nyumbani mwao wenyewe kwa kula hata tembe moja tu ya dawa isiyokusudiwa kuwa yao, lasema gazeti FDA Consumer. Kumeza dawa, kemikali za nyumbani, na vinywaji vya kialkoholi kwaweza kusababisha ugonjwa na hata kifo kwa mtoto mdogo. Kwa hivyo, bidhaa hizi zapasa kuwekwa mahali ambapo watoto hawawezi kuzifikia na kuziona. Kumeza viongezi vya chuma kupita kiasi, kutia ndani vitamini za watoto, ndiyo mahangaiko ya kipekee. “Kwa sababu [vitamini za watoto] huuzwa zikifanana na peremende au vibonzo, hufanana na peremende wala haionekani kama dawa,” aeleza Dakt. George Rodgers wa Kitovu cha Kimkoa cha Usumishaji cha Kentucky, Marekani. Mtoto akiwa na dalili zisizo za kawaida, kama vile kusogea-sogea kwa macho kusiko kwa kawaida au kusinzia kupita kiasi, au ikiwa chupa ya dawa yapatikana ikiwa wazi, mwite daktari au kitovu cha udhibiti wa sumu mara moja na ufuate maagizo yao kabisa, wanashauri wataalamu.

Kusoma—Je, Ni “Kifo cha Polepole”?

Kulingana na uchunguzi uliofanywa katika Italia kwa ajili ya Association of Small Publishing Houses, mwaka uliopita asilimia 80 ya Waitalia “hawakufungua kitabu kamwe, au ikiwa walifungua, hawakumbuki hata kichwa cha kitabu hicho au jina la mwandikaji.” Kidesturi, mwenendo, vitendo, na maisha ya Waitalia huathiriwa sana na vitu vya kuonekana, kutia ndani televisheni, kuliko na habari ya kusoma, lakataja gazeti la habari la Roma La Repubblica. “Waitalia hawasomi, nao hawatambui kwamba wanakosa chochote cha maana,” gazeti hilo likataarifu. Uchunguzi huo pia ulionyesha kwamba Waitalia wengi huhusianisha usomaji wa vitabu na “kutoweza kuanzisha mahusiano ya kibinadamu ‘machangamfu’” na pamoja na “ukosefu wa shauku.” Wasiosoma “wana uhakika kwamba kusoma ni kupoteza wakati tu,” kwamba hilo ‘ni jambo la wazee,’ au hata kwamba “huleta ‘kifo cha polepole.’”

Simu za Kuomba Msaada

Laini ya simu ambayo vijana wenye kutaabika waweza kupiga bila malipo katika Kanada hupata simu 4,000 kila siku, hilo likifunua “kukata tumaini kubaya sana kuliko wakati mwingineo,” likaripoti gazeti la habari The Globe and Mail. Christine Simmons-Physick, mkurugenzi wa huduma za ushauri wa hiyo programu, alitaarifu: “Mabadiliko [ya kiuchumi] yanayoendelea ulimwenguni yanasababisha ukosefu wa uhakika katika watu wazima na hili linaathiri watoto.” Karibu nusu ya simu zipokewazo huhusu mahusiano ya kibinadamu, na asilimia 78 hutoka kwa wasichana, ambao huona ikiwa rahisi zaidi kuomba msaada kuliko wavulana. Vijana hupiga simu kwa sababu hilo huwapatia fursa ya matatizo yao kusikiwa na mtu mzima kwa uzito, akaonelea Simmons-Physick. Wazazi na watu wengine wazima mara nyingi “huelekea kupuuza matatizo ya watoto kuwa ya kupita tu kulingana na umri—wanasema kwamba wanapozidi kukua, matatizo hayo yataacha kuwapata,” yeye asema, akiongeza: “Ukionyesha mtazamo huo, waweza kuwa na hakika kwamba hawatakuja kwako tena ili kuomba msaada.”

Vipepeo Wasafiri

Kila mwezi wa Machi vipepeo wengi mno aina ya monarch husafiri kuvuka kilometa 800 za bahari iliyo wazi, wakihama kutoka Mexico hadi sehemu ndogo ya pwani Louisiana, Marekani. Kisha vipepeo hao huelekea kaskazini, wengine mbali sana kufikia Kanada. Mwezi wa Oktoba ujao watoto wao wa vizazi vitano baada yao hurudi Mexico kupitia njia iyohiyo. Lakini wakiwa na ubongo mdogo mno, ukubwa wa kichwa cha pini, wao wanajuaje wapuruke kuelekea wapi? Hilo bado ni fumbo. Jarida Enterprise-Record la Chico, California, laripoti kwamba mtafiti wa vipepeo Dakt. Gary Noel Ross huamini kwamba wadudu hao huenda wanaongozwa na usumaku. Swali lenye kutatanisha ni, Plani ya kuruka ya safari ya kurudi Mexico hupitishwaje kwa vizazi vitano? “Utata wa yote haya unapita ufahamu,” akasema Dakt. Ross.

Maonyo ya Mavazi Mapya

Maonyo kuhusu hatari za kemikali zitumiwazo katika kutengeneza nguo yanatangazwa katika Ufaransa, Uingereza, na Thailand, laripoti gazeti Asiaweek. Fomaldehidi, kihifadhi chenye nguvu kitumiwacho katika rangi, hupatikana katika vitambaa vingi, nayo husemekana kuwa husababisha matatizo ya ngozi, macho, na ya upumuaji. Wafanyakazi katika viwanda vya kutengeneza vitambaa wanaweza kuwa hatarini viwanda vyao visipokuwa vikavu na vyenye mfumo wa hewa safi, kulingana na ripoti hiyo, nao wateja wapaswa kuosha nguo yoyote mpya kabla ya kuivaa, ili kuepuka kuathiriwa vibaya.

Uhalifu na Matineja wa Urusi

Katika St. Petersburg, Urusi, “uhalifu wa vijana unakuwa mbaya zaidi na wa makusudi,” laripoti The St. Petersburg Press. Kwa kielelezo kwenye shule moja ya jiji katika 1995, mvulana mmoja mwenye umri wa miaka 13 alifungwa na kupigwa hadi kifo baada tu ya kumaliza mitihani yake ya mwisho wa mwaka. Hangaiko kwa upande wa wazazi na walimu kuhusu uhalifu wenye jeuri wa shuleni lilitokeza masomo ya kipekee kwa ajili ya watoto wa shule juu ya “Mambo ya Msingi ya Kusalimika,” kutia ndani “Mambo ya Msingi ya Kitiba” kwa wasichana. Kwenye semina ya walimu wa masomo hayo, ilifunuliwa kwamba asilimia 25 ya wasichana wa shule za sekondari jijini hufikiri kwamba ukahaba ni sehemu muhimu ya maisha ya Urusi. Isitoshe, idadi ya utoaji-mimba miongoni mwa wasichana wenye umri wa miaka 17 na chini yaaminika kuwa ilirudufika kwa miaka mitano iliyopita, kulingana na Populi, gazeti la Hazina ya Umoja wa Mataifa ya Idadi ya Watu.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki