Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Wamormon Sikuamini macho yangu niliposoma makala “Kanisa la Mormon—Je, Ni Urejesho wa Mambo Yote?” (Novemba 8, 1995) Mnajiita Wakristo wa kweli kwa sababu ya kukataa kujihusisha katika vita. Lakini mimi nawaonea fahari Wamormon ambao walipigana katika Vita ya Ulimwengu 2 na kuwasaidia Wayahudi, ambao walikuwa wakinyanyaswa na Hitler. Mashahidi wa Yehova walikuwa wakifanya nini wakati huo mbali na kuketi tu na kutazama Wayahudi milioni sita wakifa?
G. D., Ujerumani
Ni kweli kwamba Wamormon katika Marekani na Uingereza walipigana dhidi ya Unazi. Lakini si katika Ujerumani yenyewe. Kitabu “The Nazi State and the New Religions,” kilichoandikwa na mwanahistoria Christine King, kaimu mkuu wa Chuo Kikuu cha Staffordshire katika Uingereza, charipoti hivi: “Wamormon walijiunga na huduma za kijeshi na kulikuwa na Wamormon mia sita katika jeshi la Ujerumani kufikia 1940. . . . Wamormon waliendelea kukazia ‘miradi sambamba’ ya Umormon na Usoshalisti wa Kitaifa. . . . Viongozi fulani Wamormon walianza kuagiza makutaniko yao kuhusiana na kanuni za Usoshalisti wa Kitaifa, wakisali kwa Führer, wakisema kwamba ‘aliagizwa kimungu.’ . . . Kuna visa viwili tu vilivyoripotiwa vya Wamormon wakikinza Wanazi.” Hata hivyo, wakiwa kikundi Mashahidi wa Yehova walikataa kutegemeza utawala wa Nazi. Hivyo, wakawa shabaha ya mnyanyaso mkali kutoka kwa serikali ya Hitler. Maelfu yalifungwa gerezani katika kambi za mateso na wengi walikufa huko. Ona toleo letu la Agosti 22, 1995.—Mhariri.
Mchanganyo wa Picha Ule mfululizo “Ubuni wa Sayansi—Je, Ni Mchungulio wa Wakati Ujao Wetu?” (Desemba 8, 1995) ulikuwa wenye kufurahisha sana. Hata hivyo, ile picha ya Jules Verne kwenye ukurasa 3 yaelekea ni ile ya William Morris, msanii na mwandikaji wa karne ya 19.
R. G., Marekani
Wasomaji kadhaa waligundua kosa hilo. Kosa la uandishi lilifanywa, na picha yetu ya faili ya William Morris ikabandikwa jina jingine kwa makosa. Twaomba radhi kwa mchanganyo huo.—Mhariri.
Ulimwengu Wote Mzima Wenye Kutisha Baada ya kusoma mfululizo wenu “Ulimwengu Wote Mzima Wenye Kutisha—Ulitoka Wapi?” (Januari 22, 1996), nilipata ufahamu wa wazi zaidi wa wazo la wakati huu la kisayansi juu ya ulimwengu wote mzima. Utoaji wenu ulikaziwa na utumizi wenye ustadi wa habari, vyanzo, na marejezo mengi. Nikiwa mwalimu, nitatumia vizuri habari mliyotoa.
M. P., Marekani
Nimesoma mara nyingi makala kama hizo katika magazeti mengineyo, lakini sikuzote yalikosa kumpatia sifa Mbuni wa maajabu hayo. Makala zenu ziliandaa kilichohitajika kujazia utupu huo.
P. B., Italia
Habari hiyo haikuwa ya hakika tu bali ilikuwa yenye kuimarisha imani. Ilijenga uthamini wetu kwa Mungu wetu—Mwanzilishi wa ulimwengu wote mzima wetu wenye kutisha na wa ajabu!
C. S., Ugiriki
Ilisisimua kwelikweli kusoma makala hizo. Nina umri wa miaka 14, nami sikuzote nimevutiwa sana na ulimwengu wote mzima. Makala hizi zilinifanya nitambue hali duni ya wanadamu wakilinganishwa na utata wa uumbaji huu.
M. D., Ureno
Nilisoma makala hizo kwa upendezi upitao wa kawaida. Nafurahi kwamba Amkeni! hushughulikia habari kama hizo. Ilinipa ufahamu wenye kina zaidi kuhusu mafumbo ya ulimwengu wote mzima, hasa habari iliyohusu uthibitisho wa “utupu-tupu” ambao una ukubwa wa miaka nuru [milioni 100], ukiwa na galaksi nyingi upande wa nje na utupu ndani. Hilo latokeza tatizo kwa nadharia ya kisasa ya mshindo mkubwa! Nashangazwa na jinsi tujuavyo machache kuhusu ulimwengu wote mzima.
D. K., Jamhuri ya Cheki