Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 10/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Tumbaku na Kazi
  • Majengo Marefu Zaidi Ulimwenguni
  • Je, Ni Kuokoa Ndege wa Baharini?
  • Mchochota wa Ini Aina ya C na Damu
  • Unapoacha Kuvuta Sigareti
  • Ngono na Jeuri Kutoka Kwenye Maktaba
  • Tohara ya Wanawake
  • Kufuata Nyuki
  • Televisheni Yahusianishwa na Kifafa
  • Muuaji Atambulishwa
  • Mamilioni ya Uhai Yakitokomea Moshini
    Amkeni!—1995
  • Sigareti—Je, Wewe Huzikataa?
    Amkeni!—1996
  • Je, Kuvuta Sigara Ni Dhambi?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Watetea Tumbaku Waanzisha Puto la Hewa-Joto
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 10/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Tumbaku na Kazi

“Upungufu wa fedha zinazotumiwa katika bidhaa za tumbaku utaimarisha kupatikana kwa kazi” katika maeneo fulani ya Marekani, yasema ripoti moja katika The Journal of the American Medical Association. Makadirio ya kompyuta yalitumiwa kuonyesha jinsi fedha ambazo awali zilitumiwa kwa tumbaku ziwezavyo kutumiwa kwa mambo mengine, kukiwa na ongezeko la jumla la kazi katika taifa zima. Ripoti hiyo pia yasema kwamba maeneo ya kukuza tumbaku hayangepoteza kazi nyingi kama ambavyo wenye biashara wa tumbaku wanavyokadiria. “Hangaiko la msingi kuhusu tumbaku lapaswa kuwa ukubwa wa madhara yayo kwa afya wala si athari yayo juu ya kazi,” yasema ripoti hiyo. Shirika la Kitiba la Marekani pia lilihimiza waweka rasilimali katika masoko ya hisa wauze hisa zao zilizo katika makampuni 13 ya tumbaku, kulingana na Los Angeles Times. Scott Ballin, wa Shirika la Moyo la Marekani, alisema: “Hatupaswi kuunga mkono makampuni ambayo huendelea kuuza maradhi na kifo katika nchi hii na ng’ambo.”

Majengo Marefu Zaidi Ulimwenguni

Kwa mara ya kwanza kwa muda unaozidi karne moja, jengo refu zaidi ulimwenguni halipatikani Marekani. Baraza la Majengo Marefu na Makazi ya Mijini, ambalo ni shirika la kimataifa la kuamua majengo marefu zaidi, lilitaja majengo ya Petronas Twin Towers katika Kuala Lumpur, Malasia, kuwa marefu zaidi. Jengo ambalo lilikuwa refu zaidi, lile Sears Tower katika Chicago, bado ndilo refu zaidi ikiwa minara ya televisheni inahesabiwa. Hata hivyo, baraza hilo liliamua kwamba minara hiyo si sehemu ya ujenzi wa jengo hilo. Ujenzi wa majengo marefu katika nchi kadhaa za Asia huonwa na waungaji mkono kuwa ishara ya ukuzi wenye kushangaza wa uchumi katika eneo hilo. Hata majengo ya Petronas Twin Towers yanaelekea kupoteza taji layo kwa jengo la World Financial Center, ambalo limeratibiwa kukamilishwa Shanghai, China, kufikia mwisho wa mwongo huu.

Je, Ni Kuokoa Ndege wa Baharini?

Mmwagiko mwingi wa mafuta unapotokea katika bahari iliyo karibu na bara, athari kwa wanyama yaweza kuwa yenye msiba. Nyakati nyingine mashirika—mengi yakiwa na wafanyakazi wengi wa kujitolea—huchukua hatua ya kufanya yote yawezayo. Jambo moja la kutangulizwa ni kusafisha ndege wa bahari waliojaa mafuta. Lakini hatua hiyo ni yenye matokeo na ya kudumu kwa kadiri gani? Utafiti wa kisasa waonyesha kwamba kati ya maelfu mengi yaliyosafishwa na kurudishwa kwenye makao yayo, wengi hufa kwa siku kumi. Kwa nini? Mbali na mshtuko wa kushikwa-shikwa na wanadamu, ndege hawa watakuwa wameingiza mwilini mafuta kadiri fulani wanapojaribu kusafisha manyoya yao kwa midomo yao, na hatimaye hayo yatawaua. Ili kukabili tatizo hilo, ndege wanaoshikwa Uingereza wanalishwa mchanganyiko wa udongo mweupe, makaa, na glukosi katika kujaribu kuondoa sumu hizo mwilini mwao. Na bado, ni ndege wachache sana wanaoishi kwa muda mrefu kuweza kutaga mayai, na usafishaji huo ni lazima uonwe kuwa “kazi ya kijuu-juu tu,” akata kauli mwanaekolojia mmoja aliyenukuliwa na The Sunday Times la London.

Mchochota wa Ini Aina ya C na Damu

Ripoti moja iliyotolewa na Mfumo wa Kitaifa wa Ufaransa wa Afya ya Umma yakata kauli kwamba “kati ya watu 500,000 na 600,000 katika Ufaransa wameambukizwa kirusi cha mchochota wa ini aina ya C.” Kulingana na gazeti la habari la Paris Le Monde, asilimia 60 ya maambukizo ya kirusi cha mchochota wa ini aina ya C hutokana na kutiwa damu mishipani au kwa kutumia dawa za kulevya kupitia sindano. Kwa kuongezea, watu fulani wameambukizwa wakati wa kutibiwa kupitia vifaa ambavyo havikufishwa viini ifaavyo. Mchochota wa ini aina ya C waweza kusababisha mnyauko au kansa ya ini.

Unapoacha Kuvuta Sigareti

Katika kipindi cha dakika 20 baada ya mtu kuacha kuvuta sigareti, mwili huanza kubadilika kuwa bora zaidi. Gazeti Reader’s Digest lilitangaza orodha ifuatayo ya mabadiliko yenye mafaa ambayo hutukia katika pindi tofauti-tofauti baada ya mvutaji wa sigareti kuacha kuvuta sigareti. Dakika 20: Msongo wa damu na mpwito hupunguka kufikia kawaida; halijoto ya mikono na miguu huongezeka kufikia kawaida. Muda wa saa nane: Kiwango cha kaboni monoksidi katika damu hupungua kufikia kawaida; kiwango cha oksijeni katika damu huongezeka kufikia kawaida. Muda wa saa 24: Uwezekano wa kupata maradhi ya moyo hupunguka. Muda wa saa 48: Miisho ya mishipa huanza kukua tena; uwezo wa kuonja ladha na wa kunusa huboreka; kutembea huwa rahisi zaidi. Majuma mawili hadi miezi mitatu: Mwenezo huboreka; utendaji wa pafu huboreka kwa asilimia 30. Mwezi mmoja hadi miezi tisa: Kukohoa, msongo wa mbweta, uchovu, na kukosa pumzi hupungua; cilia za pafu huanza kukua tena. Mwaka mmoja: Hatari ya kupatwa na maradhi ya moyo hupunguka kwa nusu kuliko katika mtu ambaye anavuta sigareti.

Ngono na Jeuri Kutoka Kwenye Maktaba

Baadhi ya maktaba katika Connecticut, Marekani, huruhusu watoto kuchukua sinema zinazoonyesha kufanya mapenzi na jeuri ya wazi, kulingana na The Advocate, la Stamford, Connecticut. Nyakati nyingine, watoto hufikia kwa urahisi kompyuta za maktaba ambazo zimeunganishwa kwa Internet. Hilo lazusha maswali zaidi kuhusu vitu ambavyo vijana waweza kuvifikia. Wazazi wengi walishtuka, lakini maofisa wa maktaba walisisitiza kwamba ni wazazi pekee walio na haki na madaraka ya kuchunga yale watoto wao huchukua katika maktaba. “Ni hali ngumu,” akasema mfanyakazi wa maktaba Renee Pease, akisema kwamba “hadithi nyingi za kubuniwa huenda zisiwafae watoto.”

Tohara ya Wanawake

Mwanamke mmoja mchanga Mwafrika aliyepata kimbilio Marekani amerudisha mawazo tena kwa tohara za wanawake, laripoti The New York Times. Mwanamke huyo alisema kwamba alikuwa akitoroka tohara ikiwa hali ya ndoa ya kulazimishwa. Katika nchi nyingi za Kiafrika, sehemu za uke wa wanawake hukatwa, ama wakiwa vitoto vichanga ama wakihitimu kuwa wanawake. Mara nyingi hilo hufanywa bila dawa ya nusukaputi au bila usafi kuzingatiwa. Mbali na madhara ya kihisia-moyo, matokeo yaweza kuwa ambukizo, kuvuja damu, utasa, na kifo. (Ona toleo la Amkeni! la Aprili 8, 1993, kurasa 20-24.) Kulingana na gazeti hilo la habari, inakadiriwa kwamba tokea wanawake milioni 80 hadi wanawake milioni 115 wamefanyiwa tohara. Hatua imechukuliwa Marekani ya kuipiga marufuku.

Kufuata Nyuki

Antena ndogo zaidi za rada ulimwenguni pote, zenye urefu wa milimeta 16, zimeshikanishwa kwa gundi kwenye migongo ya baadhi ya nyuki wa Uingereza. Antena hizo ni vyombo vinavyofanya iwezekane kufuata nyuki. Inatumainiwa kwamba majaribio yatatokeza hata antena ndogo zaidi, ambazo hatimaye zitashikanishwa kwa mbung’o wa Afrika ili kuchunguza miendo ya wadudu hao. Jambo hilo laweza kuboresha udhibiti wa ugonjwa wa malale ambao mbung’o hupitisha kwa watu. Antena hizo hazihitaji betri za kuzipa nguvu, kwa kuwa zina uwezo wa kupata nishati kutoka kwa ishara za kuzifuata. Na kwa manufaa mengine, wanasayansi wanatumaini kuboresha ujuzi wao wa tabia za nyuki, kwa lengo la kuweza kupata mizinga ya nyuki kwa urahisi zaidi.

Televisheni Yahusianishwa na Kifafa

Kuja kwa televisheni ya satelaiti katika India, yenye kutazamwa kwa muda wa saa 24 kwa siku, kunatokeza matatizo ya mishipa ya neva katika watoto. Dai hilo lilifanywa na mtaalamu mmoja mashuhuri wa mishipa ya neva katika mkutano wa All India Neurology Update—1996. Mkuu wa idara ya mishipa ya neva wa Chuo cha Kitiba cha Amritsar, Dakt. Ashok Uppal, alisema: “Watoto sasa hutazama televisheni kwa muda mrefu zaidi, jambo linalotokeza kile ambacho wataalamu wa mishipa ya neva wanakiita ‘kifafa chenye kutokezwa na picha au kifafa kinachosababishwa na televisheni.’” Dr. Uppal aliwashauri wazazi wapunguze muda wa watoto wao kutazama televisheni au kuwapumzisha kwa ukawaida wakitazama televisheni kwa vipindi virefu.

Muuaji Atambulishwa

Ingawa ni wanawake wachache wa Mexico ambao huvuta tumbaku, wengi wenye umri unaozidi miaka 40 huugua maradhi ya mapafu ambayo kwa kawaida huhusianishwa na kuvuta sigareti, laripoti karatasi ya habari Health InterAmerica. Kisababishi ni nini? “Kupika kwa majiko ya kutumia kuni,” watafiti walisema hivi majuzi. Kulingana na Peter Paré, ambaye ni profesa wa tiba, tatizo hilo halijakaziwa fikira kwa sababu “moshi wa kuni mara nyingi hauonwi kuwa wenye hatari kubwa kwa afya. Mara nyingi kifo husemwa kwamba kimesababishwa na moyo kukosa kufanya kazi, lakini tatizo lenyewe likiwa hasa ni kuwapo kwenye moshi mwingi kupita kiasi wa kuni.” Shirika la Afya Ulimwenguni lakadiria kwamba watu wapatao milioni 400 ulimwenguni pote wamo hatarini, hasa wanawake wa mashambani ambao hutumia majiko ya kuni katika majengo madogo ambayo hayapitishi hewa vizuri. Kujenga mabomba ya moshi kutasaidia, lakini kulingana na Dakt. Paré, “tatizo kubwa zaidi ni kusadikisha watu wabadili njia ambayo wameishi kwa karne nyingi.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki