Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 11/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maandiko Matakatifu Katika Lugha 2,123
  • Nyangumi Mwenye Sumu
  • Madhara Makubwa ya Uchezaji Kamari
  • Wakatoliki Wasiopaswa Kuguswa?
  • Vyeo vya Kubuniwa
  • Uwezo wa Watoto
  • Ulozi Wakubaliwa na Serikali
  • Upunguzaji Silaha Ulio Ghali
  • Vitambaa vya Vyombo Vyaweza Kukufanya Uwe Mgonjwa
  • Upasuaji wa Moyo kwa Kutumia Vidio
  • Pigo la Kifua Kikuu
  • Shangwe ya Ushindi na Huzuni
    Amkeni!—1997
  • Kinga Mpya Dhidi ya Kifua Kikuu
    Amkeni!—1999
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2001
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 11/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Maandiko Matakatifu Katika Lugha 2,123

Hannah Kickel-Andrae, katibu wa kushughulika na waandishi wa habari wa German Bible Society, hivi majuzi alitangaza kwamba Maandiko Matakatifu yapatikana katika lugha 2,100, kulingana na gazeti Wetterauer Zeitung. Inakadiriwa kwamba wanadamu husema lugha na lahaja 6,000 hivi. Hilo lamaanisha kwamba angalau sehemu za Neno la Mungu zapatikana katika zaidi ya thuluthi ya lugha zote zisemwazo. Kulingana na gazeti Bibelreport, Biblia nzima sasa imechapishwa kwa lugha 349. “Agano Jipya” lapatikana katika lugha za ziada 841, na visehemu vinginevyo vya Biblia katika 933, kwa jumla ya lugha 2,123. Vikundi vingi vya utafsiri huhitaji miaka minne hivi kutafsiri “Agano Jipya” na miaka minane hivi kwa “Agano la Kale.” Kazi inaendelea kwa miradi mingine 600 ya kutafsiri.

Nyangumi Mwenye Sumu

Gazeti International Herald Tribune husimulia kwamba nyangumi aina ya sperm aliyepatikana akiwa amekufa katika njia zenye shughuli nyingi za meli kwenye pwani ya kaskazini ya Denmark alikuwa na “zebaki [nyingi mno] na kadmiamu hivi kwamba ilikuwa lazima matumbo yazikwe mahali maalum pa kutupia taka iwezayo kudhuru.” Chanzo cha metali hizi zenye sumu hakijulikani bado. Gazeti Time, katika kuzungumzia kisa hichohicho, liliongeza kwamba ingawa wengine huona hilo kuwa ishara ya uchafuzi mbaya wa bahari, wanazuolojia hutaja visababishi vya kiasili. Mtaalamu wa nyangumi Carl Kinze, wa Copenhagen Zoological Museum, ataja kwamba nyangumi aina ya sperm hula hasa pweza, ambao baadhi yao kiasili wana viwango vya juu vya kadmiamu.

Madhara Makubwa ya Uchezaji Kamari

Katika jimbo la Australia la New South Wales, uchunguzi wenye kudhaminiwa na serikali ulifunua takwimu zenye kushtua kuhusu athari za uchezaji kamari. Kulingana na The Sunday Telegraph, karibu asilimia 40 ya wale waliochunguzwa walisema kwamba wao hucheza kamari kila juma. Kati yao, zaidi ya 2 kati ya 10 walikiri kwamba wao hutumia zaidi ya dola 100 kwa juma katika zoea hilo. “Wanaume vijana waseja ambao walipendelea mashine za kuchezea kamari au kuchezea kamari mashindano ya mbio” walikuwa kikundi kiwezacho kusitawisha matatizo ya uchezaji kamari zaidi kuliko vyote. Vikundi vingine vilivyo hatarini sana vilitia ndani “watu ambao huchuma chini ya dola 20,000 kwa mwaka na waliostaafu au wasio na kazi ya kuajiriwa.” Isitoshe, uchunguzi huo ulifunua kwamba “karibu asilimia 15 ya familia za NSW [New South Wales] zimepatwa na magumu kwa sababu ya uchezaji kamari wa kupita kiasi.” Kwa kuongezea, inakadiriwa kwamba “waraibu wa kucheza kamari wanagharimu NSW dola milioni 50 kila mwaka katika gharama za utokezaji uliopotezwa, ufilisi na za talaka.”

Wakatoliki Wasiopaswa Kuguswa?

Kwa kipindi cha karne nyingi katika India, wengi wale waliozaliwa katika kikundi cha wale waitwao eti wasiopaswa kuguswa wamekuwa wageuzwa Wakatoliki katika matumaini ya kutoroka mfumo wa Kihindu wa kugawanya watu katika vikundi. “Lakini hilo halikumaanisha kwamba waliweza kuepuka hadhi zao za hali ya chini,” lasema gazeti la habari la Paris Le Monde. Wakatoliki wa India wa kikundi cha hali ya juu wameendelea kutendea Wakatoliki wa hali ya chini kama wasiopaswa kuguswa. “Likiwa tokeo,” lasema Le Monde, “wakati Wakatoliki wa vikundi vya hali ya chini na hali ya juu waendapo kanisani kusali, wao huketi katika viti tofauti.”

Vyeo vya Kubuniwa

Katika Marekani, vyeo “mwanalishe,” “tabibu,” na “mtaalamu wa ulaji” mara nyingi hutumiwa na watu wanaojisifu, wasio na sifa za ustahili. Kulingana na Tufts University Diet & Nutrition Letter, katika majimbo mengi “mtu yeyote, haidhuru ana elimu gani, aweza kudai kuwa mwanalishe bila hofu ya matokeo ya kisheria.” Hivi majuzi, watafiti walichunguza vitabu vya orodha za nambari za simu katika majimbo 32 na kutambua kwamba “kiasi kisichozidi nusu ya waitwao eti wataalamu waliokuwa chini ya vichwa ‘wanalishe’ na ‘matabibu’ ndio vyanzo vyenye kutegemeka vya habari ifaayo ya lishe inayotegemea sayansi.” Katika kurasa za manjano (orodha za simu za kibiashara), asilimia 70 hivi ya “Ph.D.” za wanalishe zilizoorodheshwa zilipatikana kuwa zina digrii za kubuniwa au hutoa habari yenye kulaghai.

Uwezo wa Watoto

“Watoto wa Brazili ndio wenye kudhibiti nyumbani, ndio wenye uvutano juu ya uamuzi wa wazazi wao, na hutumia karibu dola bilioni 50 (za Marekani) kwa mwaka,” laripoti gazeti Veja. “Watoto hujichagulia programu za televisheni kwa sababu watu wazima wana shughuli nyingi na mambo mengine. Wao huenda kupiga kambi na shule bila usimamizi wa baba au mama. . . . Wao huachwa karamuni na kulala katika nyumba za marafiki.” Leo, wazazi wengi “hupendelea watoto wenye kujiamini na wenye kujitegemea, hata ikiwa hawatii sana kama watoto wa vizazi vya hapo awali.” Lakini kulingana na mtaalamu wa afya ya akili Alberto Pereira Lima Filho, “kuacha fungu lao wakiwa waelimishaji, [wazazi] hawawezi kuandaa mipaka ya wazi kwa watoto wao.” Huenda isishangaze kwamba uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba “asilimia 40 ya watoto huvutiwa na wachezaji wa mpira zaidi kuliko na wazazi wao.”

Ulozi Wakubaliwa na Serikali

Nchi ya Afrika Magharibi ya Benin imepatia “utambuzi rasmi” “zoea la ulozi,” laripoti gazeti The Guardian la Nigeria. Kulingana na gazeti hilo la habari, ilikuwa “mara ya kwanza kwa serikali yoyote” kupatia hadhi rasmi “dini ya kidesturi ya Afrika.” Utambuzi huo wamaanisha kwamba wanaozoea ulozi wana haki ya kisheria kujenga mahekalu ambayo kwayo matoleo yanaweza kufanywa ili kuabudu na kutuliza roho wasioonekana. Inakadiriwa kwamba asilimia 70 ya watu katika Benin huzoea ulozi.

Upunguzaji Silaha Ulio Ghali

“Kati ya 1985 na 1994, matumizi ya kijeshi yalipungua ulimwenguni pote kwa asilimia 30 hivi, hadi dola za Marekani bilioni 800 ‘pekee,’” kulingana na watafiti Wajerumani. Bonn International Center for Conversion (BICC) kilitangaza mambo hayo ya hakika katika kitabu chao cha mwaka cha kwanza, chenye kichwa Conversion Survey 1996. Kati ya nchi 151, 82 zilipunguza matumizi yao ya kijeshi, huku 60 yakiongeza. Kulingana na gazeti la Ujerumani Focus, “tumaini la ‘faida za amani,’ yaani, kugawanywa tena kwa mabilioni ya dola kwa ajili ya misaada na programu za kijamii, tayari limekosa kutimizwa.” Wataalamu wa BICC walitaarifu hivi: “Kupunguzwa kwa vifaa vya kijeshi kumetokeza matumizi ambayo huondosha fedha ambazo ziliwekwa akiba katika sekta ya silaha.”

Vitambaa vya Vyombo Vyaweza Kukufanya Uwe Mgonjwa

Wanasayansi wamepata kiasi kikubwa cha bakteria katika vitambaa vya kupangusia vyombo na sifongo za jikoni zilizotumiwa. Kulingana na UC Berkeley Wellness Letter, uchunguzi wa hivi majuzi ulifunua kwamba kati ya vitambaa vyenye umajimaji 500 na sifongo zilizochunguzwa, “thuluthi mbili zilikuwa na bakteria ziwezazo kufanya watu wawe wagonjwa.” Robo yavyo “ilikuwa na salmonella au staphylococcus, visababishi viwili vikuu vya ugonjwa usababishwao na chakula,” katika Marekani. Wataalamu wapendekeza kwamba sifongo zibadilishwe kwa ukawaida na kwamba vitambaa vya kupangusa vyombo vioshwe mara nyingi. “Waweza kuweka vitambaa vya kupangusia vyombo na sifongo katika mashine ya kuoshea vyombo pamoja na vyombo vyako vichafu, au katika mashine ya kufua nguo,” lasema Wellness Letter. Baada ya kuguswa na nyama mbichi, nyuso za kukatia zapaswa kusafishwa kwa taulo za karatasi badala ya vitambaa na sifongo ziwezazo kutumiwa tena.

Upasuaji wa Moyo kwa Kutumia Vidio

Hospitali moja ya Paris hivi majuzi ilikuwa ya kwanza kimataifa kumfanyia mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 30 upasuaji wa moyo kwa kutumia vidio, laripoti gazeti la kila siku la Paris Le Monde. Upasuaji wa kawaida wa moyo huhitaji uwazi wa sentimeta 20 wa kifua kwenye kidari. Hata hivyo, ufundi huu mpya huhitaji tu mkato wa sentimeta nne, huku shimo jingine dogo likiwezesha kamera ya fumwale-maonzi imwongoze mpasuaji. Katika upasuaji huu kupotezwa kwa damu, mshtuko wa baada ya upasuaji, na hatari ya ambukizo zilipunguzwa sana. Mgonjwa huyo aliweza kuondoka hospitali kwa siku 12 tu baada ya upasuaji. Kila mwaka, watu milioni moja hivi hufanyiwa upasuaji wa moyo kwa njia ya kawaida ulimwenguni pote.

Pigo la Kifua Kikuu

“Thuluthi ya idadi ya watu ulimwenguni imeambukizwa TB [kifua kikuu],” na maradhi hayo yanatazamiwa kuua watu milioni 30 mwongo huu, laripoti The Times la London. Shirika la Afya Ulimwenguni hukazia kwamba tauni hiyo mpya, kama inavyoyaita maradhi hayo, itaenea zaidi na kuharibu kuliko UKIMWI, yaelekea ikiambukiza watu milioni 300 katika miaka kumi ijayo. Uhakika wa kwamba viini aina ya bacilli ni vyenye kupitishwa hewani humaanisha kwamba TB ni yenye kuenea sana. Tayari TB imeenea sana katika sehemu fulani za Urusi. Aina zenye kukinza dawa za hiyo bacillus zimetokea kwa sababu wagonjwa wengi wa TB hawajamaliza mfululizo wote wa miezi sita wa dawa za viuavijasumu, laripoti shirika la utulizaji wa kitiba la Uingereza. Likiwa tokeo, bacilli husitawisha kinga na kusalimika.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki