Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g01 11/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—2001
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuidhibiti Halijoto kwa Theluji
  • Aina Mpya ya Kifua Kikuu Inayoua
  • Je, Umri wa Miaka 49 Ni Umri Hatari?
  • Je, Tekinolojia Husababisha Usahaulifu?
  • “Tatizo Kubwa la Afya”
  • Kutojua Biblia
  • Maji ya Balungi na Dawa
  • Kumbukumbu Kama ya Ndovu
  • Kisababishi Kikuu cha Kifo
  • Jinsi ya Kuwa Mwenye Furaha
  • Shangwe ya Ushindi na Huzuni
    Amkeni!—1997
  • Kinga Mpya Dhidi ya Kifua Kikuu
    Amkeni!—1999
  • Kifua Kikuu Charudi kwa Pigo!
    Amkeni!—1996
  • Muungano Hatari
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2001
g01 11/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Kuidhibiti Halijoto kwa Theluji

Gazeti la Asahi Evening News la Japani linaripoti kwamba theluji inatumiwa kama chanzo kipya cha nishati katika majira ya kiangazi. Jiji la Bibai huko Hokkaido, katika sehemu ya kaskazini ya Japani, lina majira mafupi ya kiangazi yenye joto kali na majira ya baridi kali yenye theluji nyingi. Badala ya kuondoa theluji, wafanyakazi wanaihifadhi ghalani. Kisha, wakati wa kiangazi, “hewa hupitishwa katika chumba kikubwa kilichojaa theluji, nayo inakuwa baridi kama hewa ya friji,” gazeti hilo linasema. Hewa hiyo baridi hutumiwa kupunguza halijoto katika majengo yenye mifumo hiyo ya kudhibiti halijoto. Faida nyingine ya ghala hizo zenye kujaa theluji ni kwamba kuna unyevunyevu mwingi humo unaosaidia kusafisha hewa kwa kuondoa vumbi na harufu mbaya.

Aina Mpya ya Kifua Kikuu Inayoua

Gazeti la Star la Johannesburg linasema kwamba, ‘Aina mpya ya kifua kikuu inayoenea na inayokinza dawa nyingi (MDRTB), inaweza kumaliza familia nzimanzima. Katika miaka michache ijayo watu wa [Afrika Kusini] wataambukizwa ugonjwa huo kuliko ugonjwa wa kawaida wa kifua-kikuu.’ Kulingana na Shirika la Taifa la Kifua-Kikuu la Afrika Kusini, wagonjwa wa kifua kikuu wanaweza kupata ugonjwa wa MDRTB wakiacha kutumia dawa mapema au wasipotumia dawa jinsi inavyotakiwa. Kisha watu ambao hawakuugua kifua kikuu hapo awali wanaweza kuambukizwa ugonjwa huo mpya hatari. Gharama ya kutibu ugonjwa huo mpya ni mara 20 ya gharama ya kutibu ugonjwa wa kawaida wa kifua kikuu—na nusu ya wagonjwa wanakufa. Ripoti hiyo inasema kwamba tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu huko Afrika Kusini “linaenea kwa haraka hata ingawa watu hutibiwa kifua kikuu bila malipo.” Theluthi mbili za watu wana bakteria ya ugonjwa wa kifua kikuu mwilini, na watu hao wanaweza kupata ugonjwa huo wakiambukizwa virusi vya UKIMWI.

Je, Umri wa Miaka 49 Ni Umri Hatari?

Gazeti la Asahi Shimbun laonya hivi: ‘Mjihadhari, enyi wanaume wenye umri wa miaka 49.’ Wanaume wengi wa umri huo hukamatwa huko Japani kwa sababu ya uuaji au jaribio la kuua. Wengi wanaojeruhi wengine pia ni wanaume wenye umri wa miaka 49. Umri hatari unaofuata ni umri wa miaka 47, kisha umri wa miaka 48 halafu umri wa miaka 45. Kwa nini umri huo hasa? Daktari mmoja wa magonjwa ya akili huko Tokyo alisema kwamba maisha ya wanaume wanaokaribia miaka yao ya 50 yanabadilika. Daktari huyo alisema hivi: “Watoto wao wanaanza kujitegemea, inawabidi kutunza wazazi wao wazee, na uhusiano wao pamoja na wake zao huharibika. Uwezo wao wa kudhibiti tamaa hupungua, na baadhi yao wanatenda bila kufikiri hata wanapoweza kuona hatari iliyopo.” Kulingana na gazeti hilo, mikopo ya nyumba, karo za shule, matatizo kazini, kufutwa kazi, na kazi zisizo za kutegemeka, hufanya maisha ya wanaume walio katika miaka ya mwishomwisho ya 40 yawe magumu pia.

Je, Tekinolojia Husababisha Usahaulifu?

Gazeti la The Sunday Times la London laripoti kwamba baadhi ya madaktari huko Japani, Marekani, na Uingereza wanasema kwamba hali ya usahaulifu miongoni mwa vijana inasababishwa na tekinolojia ya kompyuta. Wanasema kwamba vitu kama vile kompyuta za mkono, kompyuta za magari zenye ramani na maagizo ya jinsi ya kufika mahali fulani, vimesababisha hali hiyo. Madaktari hao wanasema kwamba vifaa vya kisasa vimefanya watu wasitumie ubongo kuelewa mambo. Kwa hiyo, wafanyakazi, kutia ndani wale walio katika umri wao wa miaka ya 20 na 30, wameshindwa kukumbuka majina, maneno yaliyoandikwa, na miadi. Dakt. David Cantor wa Taasisi ya Matibabu ya Magonjwa ya Akili huko Atlanta, Georgia, Marekani, alisema hivi: “Wataalamu wengi wanadhani kwamba watu fulani husikia habari nyingi sana hivi kwamba wanashindwa kuzielewa . . . Watu hao wanasahau mambo kwa kuwa hawakuyaelewa kamwe walipoyasikia.” Dakt. Takashi Tsukiyama wa Tokyo anaonelea kwamba matatizo hayo ‘hayasababishwi na uzee bali yanasababishwa na mambo kama kutotumia ubongo vya kutosha.’

“Tatizo Kubwa la Afya”

Kulingana na takwimu za serikali, kujiua ni kisababishi kikuu cha nane cha vifo huko Marekani. Wamarekani zaidi ya 30,000 hujiua kila mwaka, na kila mwaka Wamarekani zaidi ya 650,000 hujaribu kujiua. Shirika la habari la Reuters lasema kwamba kwa kila watu wawili wanaouawa, watu watatu hujiua. Mashirika mbalimbali ya umma na yasiyo ya umma, huona kujiua kuwa “tatizo kubwa la afya.” David Satcher, afisa mkuu wa tiba huko Marekani, alisema hivi: “Karibu kila mtu huathiriwa na msiba wa kujiua.” Shirika la Reuters lilisema kwamba baadhi ya visababishi vya kujiua ni “kushuka moyo, kukata tamaa, kutokuwa na tumaini, ulevi, na kutumia dawa za kulevya.”

Kutojua Biblia

Ijapokuwa Biblia imeheshimiwa kidesturi huko Marekani, uchunguzi mmoja wa hivi majuzi ulionyesha kuwa ni asilimia 16 tu ya wafuasi wa Jumuiya ya Wakristo huko wanaosoma Biblia kila siku. Gazeti la The Sun Herald la Biloxi, Mississippi, Marekani, liliripoti kwamba uchunguzi mwingine ulionyesha kuwa ni watu 2 tu kati ya watu 10 waliojua jina la yule mtu aliyetoa Mahubiri ya Mlimani. Isitoshe, wale walioulizwa walijua tu amri tatu au nne kati ya zile Amri Kumi.

Maji ya Balungi na Dawa

Jarida la UC Berkeley Wellness Letter laripoti kuwa kunywa maji ya balungi pamoja na dawa kunaweza kuzidisha “athari mbaya za dawa, na nyakati nyingine [kusababisha] madhara mabaya sana.” Dawa zinazohusika hasa ni dawa za kupunguza kolesteroli, dawa fulani za kupunguza msukumo mkubwa wa damu na dawa fulani za kutuliza wasiwasi. Hata hivyo, si watu wote wanaoathiriwa na mchanganyiko huo, wala si maji yote ya balungi yanayosababisha tatizo hilo. “Ikiwa wewe hunywa maji ya balungi na vilevile dawa, uliza mwuzaji wa dawa juu ya athari zinazoweza kutokea,” jarida hilo lasema.

Kumbukumbu Kama ya Ndovu

Wachunguzi wanaofanya kazi katika Mbuga ya Wanyama ya Amboseli nchini Kenya wamegundua kuwa kumbukumbu ya ndovu-jike mzee zaidi ni mojawapo ya mambo yanayosaidia sana kundi la ndovu kuepuka hatari na kuendelea kuishi. Gazeti la Science News laripoti: “Ndovu-jike wazee ambao ni viongozi wa makundi, wenye umri wa angalau miaka 55, wanajua kuwatofautisha marafiki na wageni vizuri zaidi kuliko . . . ndovu wenye umri wa miaka 35.” Kwa sababu wanakumbuka milio ya mawasiliano, au mingurumo ya sauti ya chini, ndovu-jike wazee wanaoongoza makundi yao wanaweza kukusanya kundi na kulipanga kukinza hatari wanapotambua milio isiyo ya kirafiki. Ripoti hiyo yasema kwamba “ndovu-jike anaweza kutambua milio 100 hivi ya ndovu-jike wenzake.” Kwa hiyo, ujuzi mwingi unaosaidia kundi zima hupotea wawindaji-haramu wanapoua ndovu-jike mzee.

Kisababishi Kikuu cha Kifo

Gazeti la Le Figaro la Ufaransa laripoti kwamba “kileo husababisha vifo vya vijana 55,000 kila mwaka.” Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kileo ndicho kisababishi kikuu cha vifo vya wanaume wenye umri wa miaka 15-29 huko Ulaya, nacho chahusika katika asilimia 25 ya vifo vyote. Vifo hivyo husababishwa na “ulevi, aksidenti za barabarani, kujiua, na kuuawa,” gazeti hilo lasema. Hali ni mbaya sana katika baadhi ya nchi za Ulaya Mashariki, ambako “theluthi moja ya wanaume vijana watakufa hivi karibuni kwa sababu ya ulevi.” Kwenye kongamano huko Stockholm, Sweden, Dakt. Gro Harlem Brundtland, mkurugenzi mkuu wa WHO, alishutumu watengenezaji wa vileo wanaotangaza bidhaa zao kwa nguvu. Matangazo hayo ‘yanapotosha maoni’ ya vijana kuhusu kileo.

Jinsi ya Kuwa Mwenye Furaha

Kulingana na uchunguzi mpya uliofanywa na madaktari wa magonjwa ya akili, “maisha yenye furaha hayatokani na kuwa na fedha nyingi katika benki. Yamkini watu walio tajiri, mashuhuri, na wenye cheo, wanashindwa hasa kupata uradhi.” Kennon Sheldon wa Chuo Kikuu cha Missouri-Columbia, huko Marekani, asema: “Katika tamaduni za Magharibi, matangazo mengi ya biashara hutilia mkazo urembo, umashuhuri na utajiri. Huenda jambo hilo likafanya biashara ifanikiwe, lakini haliwaletei wale wanaodanganywa furaha.” Kama ilivyoripotiwa katika gazeti The Independent la London, wanafunzi zaidi ya 700 walio chuoni walisema kuwa, “kujistahi” na “kuwa na uhusiano wa karibu na wengine” huchangia furaha yao kuliko jambo jingine lolote. Wachache sana walitaja fedha kuwa jambo lenye kuchangia furaha. Watu hawaamini tena kuwa ‘fedha zinaweza kununua furaha,’ gazeti hilo lasema.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki