“Ndoa ya Kidesturi” Katika Ghana
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA GHANA
NDOA—mamia ya maelfu huingia katika uhusiano huu kila mwaka kotekote ulimwenguni. Wao kwa kawaida hufanya hivyo kulingana na desturi ya ndoa iliyopo mahali wanapoishi.
Katika Ghana namna ya kawaida sana ya ndoa ni ile iitwayo ndoa ya kidesturi. Hii huhusisha familia ya bwana-arusi kulipa mahari kwa familia ya bibi-arusi. Ndoa ya kidesturi huzoewa na watu katika sehemu kubwa ya Afrika na katika mahali kama vile Hong Kong, Papua New Guinea, na Visiwa vya Solomon na vilevile miongoni mwa Wahindi wa Goajiro katika kaskazini-mashariki mwa Kolombia na kaskazini-magharibi mwa Venezuela, kutaja mahali pachache tu.
Kulipwa kwa mahari kulikuwa desturi katika nyakati za Biblia. (Mwanzo 34:11, 12; 1 Samweli 18:25) Ufahamu katika nyakati za kale na leo ni kwamba mahari ni fidia kwa wazazi wa msichana kwa sababu ya wao kupoteza utumishi wake na kwa wakati, nishati, na mali zilizotumiwa katika elimu na kutunzwa kwake kabla ya ndoa.
Daraka la Kimzazi
Katika nyakati za kale za Ghana, kupeana miadi ya kijinsia na kutafuta uchumba hakukuwapo miongoni mwa vijana. Wazazi walifanya mkataba wa ndoa kwa ajili ya watoto wao waliokua baada ya kuchunguza sana wanaume vijana na wanawake wawezao kufunga ndoa katika jumuiya. Wazazi fulani katika Ghana bado wanafanya hivyo.
Wazazi wa mvulana hufikiria mambo kama vile utu wa msichana; sifa zake na zile za familia yake; maradhi ya kurithiwa ambayo huenda yalipata familia hiyo kwa kuendelea; na kwa habari ya Mashahidi wa Yehova, hali yake ya kiroho. Wakiridhika, wazazi hao huwaendea kirasmi wazazi wa msichana na kuposa.
Wazazi wa msichana sasa huchunguza malezi ya mvulana na familia yake. Zaidi ya mambo yaliyotajwa hapo juu, wao hufikiria uwezo wa mvulana wa kumtegemeza mke—je, anafanya kazi au hajaajiriwa? Wazazi wa msichana wakiridhika, basi wanawafahamisha wazazi wa mvulana, na wazazi hao wanapanga pamoja mambo ya ndoa, baada ya mvulana na msichana kukubali.
Kwa nini wazazi fulani bado huona likiwa daraka lao kutafutia watoto wao waliokomaa wenzi? Mwanamke mmoja katika India ambaye wazazi wake walipanga ndoa yake alitaarifu hivi: “Kijana anaweza kustahilije kufanya uamuzi ulio mzito jinsi hiyo? Ni jambo bora zaidi kuwaachia wale ambao umri wao na uzoefu unawastahilisha kujua chaguo la hekima zaidi.” Maelezo yake pia yaonyesha maoni ya Waafrika wengi.
Hata hivyo, hali zinabadilika katika Ghana. Kupeana miadi ya kijinsia na kutafuta uchumba kunaanza kupendwa sana na wengi. Katika hatua ifaayo wakati wa uchumba, wenzi hao huwafahamisha wazazi kuhusu makusudio yao. Baada ya mawasiliano kati ya wazazi wao na baada ya wazazi kuridhika kwamba wanafaana, familia hizo hufanya sherehe rasmi ijulikanayo sana katika lugha kadhaa za Ghana kuwa kubisha mlango, mlango wa ndoa.
Sherehe ya Kubisha Mlango
Wazazi wa wenzi hao huwafahamisha washiriki wa familia juu ya tarehe na kusudi la huo mkutano. Neno “washiriki wa familia” hurejezea familia iliyopanuka ya Kiafrika ambayo hutia ndani wajomba, shangazi, binamu, wazazi-wakuu wa wenzi hao. Katika siku iliyopangwa, wawakilishi kutoka familia zote mbili hukusanyika kwa ajili ya sherehe hiyo. Bwana-arusi anaweza kuchagua kuwapo au kutowapo. Lifuatalo ni simulizi fupi sana la kile kilichotendeka kwenye sherehe moja ya kubisha mlango.
Mwakilishi wa Msichana (MM): [Akizungumza na wawakilishi wa bwana-arusi] Twajua sababu yenu ya kuja, lakini desturi inadai kwamba tuulize, Ni nini kinachowaleta hapa?
Mwakilishi wa Mvulana (MMV): Mwana wetu Kwasi alikuwa akipita karibu na nyumba yenu akaona ua maridadi naye ataka ruhusa yenu ya kulichuma.
MM: [Akijifanya hajui kinachomaanishwa] Hakuna ua katika nyumba hii. Mnaweza kujihakikishia hilo wenyewe.
MMV: Mwana wetu hajakosea. Twasisitiza kwamba kuna ua hilo maridadi katika nyumba hii. Jina la ua hilo ni Afi.
MM: Basi ni ua la kibinadamu. Naam, Afi huishi hapa.
MMV: Twataka kubisha mlango na kuomba mkono wa Afi katika ndoa kwa mwana wetu Kwasi.
Familia ya mvulana sasa yatoa bidhaa, kama vile vinywaji tofauti-tofauti na fedha. Ikitegemea kabila, kuna tofauti ndogo-ndogo katika wingi na bidhaa zinazotolewa. Sherehe hiyo inakaribia kufanana na uchumba wa mtindo wa Kimagharibi, na katika visa fulani pete ya uchumba huvishwa ili kuonyesha mapatano.
Sasa mwakilishi wa bibi-arusi amwuliza bibi-arusi mbele ya watazamaji wote ikiwa bidhaa zilizoletwa zapasa kukubaliwa. Kwa jibu lake la kukubali, wote waliopo ni mashahidi wa kujionea utayari wake wa kuolewa. Tarehe ifaayo familia zote mbili hukubaliwa kwa ajili ya sherehe ya ndoa. Viburudisho vyamalizia sherehe hiyo.
Sherehe ya Ndoa
Idadi ya watu ambao hukusanyika kwenye nyumba ya msichana au nyumba ya mwakilishi aliyechaguliwa kwa ajili ya kulipwa kwa mahari, tukio ambalo hufanyiza ndoa, kwa kawaida huwa kubwa kuliko idadi ya walioko katika sherehe ya kubisha mlango. Hii ni kwa sababu marafiki wengi sasa wapo.
Mazingira ni yenye shangwe. Wanaume na wanawake vijana walio waseja wana hamu ya kuona kile ambacho kimeletwa kwa bibi-arusi. Lakini mazingira hayo yenye furaha hupata mkazo wakati familia ya bibi-arusi ilalamikapo kwamba bidhaa za mahari hazijakamilika. Baadhi ya watazamaji huwa na wasiwasi wa litakalotokea wakati familia ya bibi-arusi ionekanapo kuwa ngumu. Msemaji wa bwana-arusi hubishana kwa ustadi ili aonewe huruma na familia ya bibi-arusi. Hali hutulia wakati familia ya msichana inapokubali. Kisha mazingira yabadilika tena. Sasa mazingira ni ya kusherehekea, na vitafuno tofauti-tofauti vyaandaliwa.
Ili kuanza sherehe ya ndoa, msemaji wa bibi-arusi awatuliza waliokusanyika na kuwakaribisha wote. Awauliza wawakilishi wa bwana-arusi kuhusu utume wao. Msemaji wa bwana-arusi ataja sababu yao ya kuja, akikumbusha waliokusanyika kwamba tayari mlango ulibishwa na kwamba kuna ruhusa ya kuingia.
Kisha kila msemaji wa familia awajulisha waliokusanyika washiriki wa karibu wa familia, kutia ndani yule anayepeana mkono wa msichana na vilevile yule anayetegemeza mvulana kuhusiana na ndoa hiyo. Sherehe yaendelea.
MM: [Akiwazungumzia wawakilishi wa bwana-arusi] Tafadhalini toeni bidhaa za ndoa tulizowaomba.
Msemaji wa bibi-arusi ataja bidhaa moja-moja za mahari ili wote wahakikishe kwamba zipo. Wawakilishi wa bwana-arusi wakihisi kwamba familia ya bibi-arusi imepandisha madai, wao wanatatua suala hilo faraghani kabla ya siku ya ndoa. Hata hivyo, familia ya bwana-arusi huja kwenye sherehe hiyo wakiwa tayari kupigania kupunguzwa kwa ziada zozote ikiwa familia ya bibi-arusi yathibitika kuwa ngumu. Mahali popote anapoishi mtu, mahari ya msingi—iwe ya juu au ya chini—ni lazima ilipwe yote.
Familia fulani hudai zipewe vitu kama vile, vinywaji, nguo, mikufu, vipuli, na vitu vingine vya mabibi. Katika kaskazini mwa Ghana, mahari yaweza kutia ndani chumvi, njugu aina ya kola, kanga (ndege), kondoo, na hata ng’ombe. Kuna sehemu ya mahari ya fedha taslimu isiyoepukika.
Makubaliano yanapokuwa yakiendelea, bibi-arusi hayupo lakini yuko karibu, akitazama. Bwana-arusi aweza kuchagua kuwapo au kutowapo. Hivyo, mtu anayeishi mbali sana aweza kuwapa wazazi wake idhini ya kufanya mkataba wa ndoa kwa niaba yake. Hata hivyo, kwa pindi inayofafanuliwa hapa, bwana-arusi yupo. Sasa ni zamu ya familia yake kufanya madai.
MMV: Tumetimiza yote tuliyotakikana kutimiza, lakini hatujamwona binti-mkwe wetu.
Sherehe ya ndoa si shughuli yenye uzito sana; pia ni pindi ya kufurahi. Familia ya msichana sasa yaitikia madai ya familia ya mvulana ya kumwona bibi-arusi.
MM: Twatamani kwamba bibi-arusi angekuwa hapa. Kwa kuhuzunisha, amesafiri kwenda ng’ambo na hatuna pasipoti au viza za kusafiri kwenda kumleta.
Kila mtu ajua kinachomaanishwa na hilo. Mara moja, familia ya bwana-arusi yatoa kiasi fulani cha fedha—kiasi chochote awezacho kutoa bwana-arusi—na ghafula! pasipoti na viza za kuwaziwa ziko tayari. Na bibi-arusi amerudi kutoka safari yake ya kuwaziwa!
Ili kuongezea raha, makabila fulani hupanga kwamba marafiki fulani wajifanye kuwa bibi-arusi. Kila anayejifanya kuwa bibi-arusi anakataliwa na umati hadi, huku wakipiga makofi mazito, bibi-arusi wa kweli anatolewa. Kisha anaalikwa na msemaji wake atazame bidhaa kadhaa za mahari yake. Anaulizwa ikiwa kile ambacho bwana-arusi ameleta chapaswa kukubaliwa. Kuna kimya huku kila mtu akingoja jibu kwa wasiwasi. Wasichana fulani ni waoga na wengine wajasiri, lakini sikuzote jibu huwa ndiyo, likifuatwa na makofi mazito.
Bwana-arusi akiwapo, familia ya bibi-arusi hutaka imjue. Raha inaendelea bila kukomeshwa kukipangwa mmoja wa rafiki zake ajifanye kuwa bwana-arusi. Akijichukua kwa kujisikia, rafiki yake asimama, lakini mara moja kila mtu apaaza sauti za kumkataa.
Wazazi wa bibi-arusi tena wadai kumwona mwana-mkwe wao. Bwana-arusi wa kweli sasa asimama, akitabasamu kwa furaha. Familia ya bibi-arusi yamruhusu msichana ajiunge na mume wake, ambaye hutia pete kwenye kidole chake ikiwa pete ilikuwa sehemu ya mahari. Pete ni wazo la kutoka Magharibi. Naye pia, atia pete kwenye kidole cha bwana-arusi. Pongezi na shangwe zajaa. Kwa ajili ya kufaa kwa hali na kupunguza gharama, watu fulani sasa huunganisha sherehe ya kubisha mlango pamoja na kufunga ndoa katika siku moja.
Washiriki wazoefu wa familia zote mbili na wengine sasa wawapatia mashauri maarusi hao wapya juu ya jinsi ya kufanya ndoa yao ifanikiwe hadi kifo kitakapowatenganisha. Ili kumalizia siku kwa njia yenye kupendeza viburudisho vyaandaliwa.
Sherehe ya ndoa imekwisha! Katika Ghana, tangu siku hiyo na kuendelea, wenzi hao huonwa na jumuiya kuwa wameoana kisheria. Ikiwa kwa sababu fulani washiriki wowote wakuu wa familia hawakuweza kuhudhuria sherehe hiyo, wao hupelekewa baadhi ya vinywaji vilivyotolewa ili kuhakikisha kukamilishwa kwa sherehe ya ndoa. Ikiwa bwana na bibi-arusi ni Mashahidi wa Yehova, katika visa fulani, Mashahidi hao hupanga hotuba ya Biblia itolewe, pamoja na viburudisho baada ya hapo.
Katika Ghana wenzi fulani huwa na sherehe ya arusi ya mtindo wa Magharibi, iitwayo hapa ndoa ya kiserikali, au ndoa kwa agizo la mamlaka. Hiyo yaweza kufanyiwa mkataba kwa idhini au bila idhini ya wazazi mradi wenzi hao wamefikia umri kisheria. Katika ndoa ya kidesturi idhini ya wazazi ni jambo la lazima.
Katika ndoa ya kiserikali wenzi wa ndoa hutoa nadhiri za ndoa. Lakini nadhiri hazipo katika ndoa za kidesturi. Serikali hutaka kwamba ndoa zote za kidesturi zisajiliwe, na Mashahidi wa Yehova hutii hilo. (Warumi 13:1) Kisha cheti cha usajili chatolewa.
Tangu nyakati za kale hadi Gold Coast, sasa Ghana, ilipokuja kuwa koloni ya Uingereza, ndoa ya kidesturi ndiyo iliyokuwa namna pekee ya ndoa katika nchi hiyo. Ndipo Waingereza wakajulisha ndoa ya mtindo wa Magharibi kwa wakazi wao walioishi hapa. Wenyeji wa bara hili pia waliruhusiwa kufanyia mkataba ndoa ya aina hii, na kwa miaka mingi sasa, ndoa ya mtindo wa Magharibi na ndoa ya kidesturi zimeendelea pamoja. Katika Ghana zote zinakubaliwa kisheria, hivyo zakubalika kwa Mashahidi wa Yehova. Ni juu ya watu mmoja-mmoja kuchagua ni aina ipi wanayotaka.
Katika nchi fulani za Afrika, ndoa za kidesturi huhitaji kusajiliwa kabla ya wenzi hao kuonwa kuwa wameoana kisheria. Hata hivyo, katika Ghana, ndoa ya kidesturi iliyofafanuliwa hapo juu ni halali kisheria bila kusajiliwa, wenzi wakionwa kuwa wameoana kisheria wakati sherehe ya ndoa ya kidesturi inapokamilishwa. Baadaye, ndoa ya kidesturi husajiliwa kwa kusudi la rekodi pekee.
Kwa kweli ndoa ni zawadi yenye upendo ya Mungu kwa wanadamu, zawadi ya kipekee ambayo hata malaika hawakupewa. (Luka 20:34-36) Ni uhusiano wenye thamani sana unaostahili kuhifadhiwa kwa utukufu wa Mwanzilishi wayo, Yehova Mungu.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Pete zikibadilishanwa