Pupa—Inatuathirije?
PUPA inaharibu maisha ya mamilioni ya watu. Inafanya wenye pupa wasiwe na ubinadamu na kutokeza maumivu na huzuni kwa wahasiriwa. Huenda unahisi athari za pupa maishani mwako. Hata wizi wa kawaida wa madukani huongeza bei za vitu unavyonunua. Ikiwa unapata mshahara mdogo na gharama za vitu vya lazima maishani zinakushinda, huenda wewe ni mhasiriwa wa pupa ya mtu mwingine.
Wenye Njaa na Wanaokufa
Kujifikiria kwa pupa kwenye kuenea taifani hudhoofisha jitihada za serikali za kusaidia maskini ifaavyo. Huko nyuma katika 1952, mwanasayansi aliye mtaalamu wa lishe Sir John Boyd Orr alisema: “Serikali ziko tayari kuunganisha watu na mali kwa ajili ya vita ya ulimwengu lakini zile Mamlaka Kubwa haziko tayari kuungana ili kuondoa njaa na umaskini ulimwenguni.”—Food Poverty & Power, cha Anne Buchanan.
Bila shaka kiasi kidogo cha msaada huandaliwa. Lakini, ni nini hali ya maisha ya walio maskini, wanaopuuzwa na ambao pia wana idadi kubwa zaidi duniani? Ripoti moja ya majuzi ilisema kwamba licha ya ongezeko la mazao ya chakula katika maeneo fulani, “njaa na utapiamlo zingali zinakumba wengi wa walio maskini wa ulimwengu . . . Sehemu moja kwa tano [zaidi ya bilioni moja] ya watu wa ulimwengu hulala njaa kila siku.” Ripoti hiyo yaendelea kusema: “Kwa kuongezea, watu bilioni 2 ‘hupungukiwa lishe’ kwa sababu ya . . . kukosa [mlo] kamili ambako hutokeza matatizo makubwa ya afya.” (Developed to Death—Rethinking Third World Development) Hakika tarakimu hizo zapaswa kuwa mambo makuu ya habari!
Waliotumikishwa
Wakuu wa uhalifu hujitajirisha kwa hasara ya wahasiriwa wa uhalifu na kwa hasara ya umma kwa ujumla. Dawa za kulevya, ujeuri, umalaya, na kutumiwa vibaya kiuchumi kumetumikisha mamilioni ya watu. Pia, Gordon Thomas asema katika kitabu chake Enslaved: “Kulingana na Shirika la Kupinga Utumwa, kuna watumwa wapatao milioni 200 ulimwenguni. Wapatao milioni 100 kati yao ni watoto.” Sababu ya msingi ni nini? Ripoti hiyo yaeleza: “Tamaa ya kutia watu utumwani inadumu kuwa sifa isiyopendeza ya asili ya binadamu . . . [Utumwa] ni tokeo la tamaa, pupa, na kupenda mamlaka.”
Wenye nguvu huwanyang’anya walio dhaifu na kuua wengi. “Kati ya Wahindi milioni mbili waliokuwa wakiishi Brazili wakati wazungu walipofika kwa mara ya kwanza, labda ni 200,000 pekee wanaobaki sasa.” (The Naked Savage) Kwa nini? Sababu ya msingi ni pupa.
Pengo Linalozidi Kukua Kati ya Matajiri na Maskini
Gazeti The New York Times liliripoti kwamba James Gustave Speth, mmoja wa wasimamizi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo, alisema kwamba “mabwanyenye wanaoibuka duniani . . . wanarundika mali nyingi na mamlaka, huku nusu ya wanadamu wakibaki maskini hohehahe.” Pengo hilo hatari kati ya matajiri na maskini linakuwa bayana kwa maneno yake: “Zaidi ya nusu ya watu duniani wangali wanachuma kiasi kisichozidi dola 2 kwa siku—watu zaidi ya bilioni 3.” Aliongezea: “Kwa walio maskini katika ulimwengu huu wa matabaka mawili, hali hiyo inazusha kukata tamaa, hasira, na mfadhaiko.”
Kukata tamaa huku kunazidishwa na jambo la kwamba matajiri hawaonekani kama wana dhamiri wala huruma yoyote kwa hali ya umaskini wa wengi.
Wahasiriwa wa pupa wapo kila mahali. Kwa mfano, ona macho yenye maogofyo ya wakimbizi walionaswa kati ya vikundi vyenye kung’ang’ania mamlaka katika Bosnia, Rwanda, na Liberia. Ona kukata tamaa katika nyuso za wale wanaokumbwa na njaa katika ulimwengu wenye chakula tele. Ni nini kinachosababisha hayo yote? Pupa—katika njia moja au nyingine!
Unaweza kuishije ukiwa umezingirwa na wanyafuzi wenye pupa katika mazingira hayo makali? Makala mbili zifuatazo zitajibu swali hilo.