Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 3/22 uku. 3
  • Msitu wa Mvua wa Amazon—Ulifunikwa na Hekaya

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Msitu wa Mvua wa Amazon—Ulifunikwa na Hekaya
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • ‘Wanawake Wapigana Kama Wanaume Kumi’
  • Mto Mkubwa wa Amazon Unawategemeza Mamilioni
    Amkeni!—2003
  • Huzuni kwa Msitu Huo wa Mvua
    Amkeni!—1997
  • Je, Wahindi wa Brazili Wanakabili Hatari ya Kutoweka?
    Amkeni!—2007
  • Kutafuta Masuluhisho
    Amkeni!—1997
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 3/22 uku. 3

Msitu wa Mvua wa Amazon—Ulifunikwa na Hekaya

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA BRAZILI

WAHINDI wa Irimarai wanaoishi kandokando ya Mto Napo wa Peru hawakuamini macho yao! Merikebu mbili zenye matanga-mraba, tofauti sana na mitumbwi yao wenyewe myembamba, zilikuwa zikija kuelekea kijiji chao. Waliona ndani ya merikebu hiyo mashujaa wa vita wenye ndevu—tofauti sana na kabila jinginelo lote walilopata kuona. Wakiwa wamepigwa na bumbuazi, Wahindi hao walikimbilia maficho na kutazama huku wageni hao wenye ngozi nyeupe wakishuka ufuoni, kula kwa pupa ugavi wa chakula wa kijiji chao, na kisha kwenda zao tena—wakiwa na wazo la kuweka historia ya kuwa wa kwanza kufanya safari ya kujasiria kuvuka msitu wote wa mvua, kutoka Milima Andes hadi Bahari Kuu ya Atlantiki.

Katika mwaka huo, 1542, kabila moja la Kihindi baada ya jingine lilipatwa na mishtuko kama hiyo huku wavumbuzi wa Ulaya, wenye kupunga pinde na bunduki aina ya harquebuses, wakipenya ndani zaidi ya msitu wa kitropiki wa Amerika Kusini.

Francisco de Orellana, nahodha Mhispania aliyesimamia washindi hao, baada ya muda akagundua kwamba habari za uporaji na ufyatuaji wa vikosi vyake zilikuwa zimefikia makabila ya Wahindi mbele ya merikebu zake mbili. Makabila ya Wahindi yaliyokuwa sehemu ya chini ya mto huo (karibu na jiji la Brazili la leo la Manaus) yalikuwa na mishale yayo tayari yakiwangoja washambulizi hao zaidi ya 50 hivi.

Na Wahindi hao walikuwa na shabaha kweli, akakiri mshiriki wa safari hiyo Gaspar de Carvajal. Alisema kutokana na aliyojionea, kwa kuwa mshale mmoja wa hao Wahindi ulitua katikati ya mbavu zake. “Kama si unene wa mavazi yangu,” akaandika ndugu-mtawa huyo aliyeumia kwa mwandiko wa kizembe, “huo ndio ungelikuwa mwisho wangu.”

‘Wanawake Wapigana Kama Wanaume Kumi’

Carvajal aliendelea kufafanua kani iliyokuwa ikiwachochea Wahindi hawa wajasiri. ‘Tuliona wanawake wakipigana mbele ya wanaume wakiwa viongozi wanawake. Wanawake hawa ni weupe na warefu, nywele zao ndefu zikiwa zimesukwa na kufungwa kuzunguka vichwa vyao. Wao ni kakawana na, wakiwa na pinde na mishale yao mikononi, kila mmoja wao anapigana kama wanaume kumi.’

Iwe kwamba wavumbuzi hao waliona wanawake mashujaa wa vita kihalisi au, kama chanzo kimoja kinavyosema, “ni mazigazi tu yasababishwayo na malaria” au la haijulikani. Lakini kulingana na angalau masimulizi fulani, kufikia wakati Orellana na Carvajal walifika mahali ambapo mto huo huingia baharini na kusafiri kuingia Bahari Kuu ya Atlantiki, waliamini kwamba walikuwa wamepata mwono wa haraka wa Kizio cha Magharibi wa ufafanuzi wa Waamazon, wanawake wakali walio mashujaa wa vita katika hekaya za Kigiriki.a

Ndugu-mtawa Carvajal alihifadhi hadithi ya Waamazon wa Amerika kwa vizazi vijavyo kwa kuitia katika simulizi lake la kujionea katika safari ya uvumbuzi ya Orellana ya muda wa miezi minane. Nahodha Orellana, kwa upande wake, alisafiri hadi Hispania, ambapo alitoa simulizi halisi la safari yake katika kile alichokiita kwa upendezi Río de las Amazonas, au Mto Amazon. Muda si muda, wafanyiza-ramani wa karne ya 16 walikuwa wakiandika jina jipya kuvuka ramani ya Amerika Kusini iliyokuwa katika hatua ya mapema ya uvumbuzi—Amazon. Kwa hiyo msitu wa Amazon ukafunikwa na hekaya, lakini sasa msitu huo unakumbwa na uhalisi wenye kuhuzunisha.

[Maelezo ya Chini]

a Neno “Waamazon” yaelekea hutokana na neno la Kigiriki a, limaanishalo “bila,” na ma·zosʹ, limaanishalo “matiti.” Kulingana na hekaya, Waamazon waliondoa titi la kulia ili waweze kutumia upinde na mshale kwa urahisi zaidi.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

Juu mandhari-nyuma: The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki