Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kuwa na Raha Nina umri wa miaka 12, na nilifurahia sana makala “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Vijana Wengine Hupata Raha Yote?” (Julai 22, 1996) Nilikuwa nikijiuliza swali hilohilo. Katika shule yetu unaweza kupeleka jina ili uende kwenye karamu, dansi, na utendaji mwingine mwingi. Mara nyingi nimetaka kwenda. Lakini makala hiyo ilinisaidia kufahamu kwamba nina daraka mbele ya Yehova kwa machaguo niyafanyayo. Kwa hiyo nitadumu na marafiki wangu wa Kikristo.
A. S., Marekani
Kumekuwa na nyakati ambazo nimehisi kama Asafu [mwandikaji wa Biblia], kama tu mlivyojadili katika makala hiyo. Makala hiyo ilinipa nguvu zaidi nilizohitaji ili kukabiliana na shule.
A. S., Japani
Ni kweli kwamba baadhi ya vijana huhisi hawashirikishwi au kunyimwa kwa sababu “hawaruhusiwi” kushiriki katika karamu za kilimwengu. Lakini si wote wa watoto wa Mashahidi wa Yehova huhisi hivyo! Mimi binafsi huchukizwa na mambo mengi ambayo huendelea katika karamu za kilimwengu, na marafiki wangu wa Kikristo pia huhisi hivyo hivyo. Sisi—na bila shaka wengine wengi—hatuhisi tumenyimwa chochote!
C. H., Marekani
Brewery Gulch Ninawaandikia kuwaeleza jinsi nilivyofurahia ile makala “Maua ya Kiroho Yalikua Katika Brewery Gulch.” (Julai 22, 1996) Ilinikumbusha mambo mazuri ajabu ya miezi 21 niliyotumia huko miaka kadhaa iliyopita. Niliondoka nyumbani kwa mara ya kwanza. Baadhi ya familia mlizotaja katika makala hiyo—akina Smith, Griffin, na Pugh—walikuwa kama mama, baba, shangazi, na wajomba kwangu. Walinisaidia kukomaa kiroho nikiwa Mkristo. Kusoma makala hiyo kulinifanya nitamani kurudi huko kuwa nao. Nawakumbuka wote kwa upendo mwingi sana na kuwathamini.
P. A., Marekani
Majani ya Muhogo Asanteni kwa makala “Majani ya Muhogo—Chakula cha Kila Siku cha Mamilioni.” (Julai 8, 1996) Katika Afrika muhogo hustahiwa sana kwa sababu umekuwa chakula chetu kikuu kwa karne nyingi. Hata hivyo, katika Nigeria hatujui mambo mengi kuhusu majani yao kwa kuwa ni mizizi yao ambayo hutuandalia milo tuipendayo sana, kama vile gari na foo-foo. Ilipendeza kujua kwamba katika sehemu nyinginezo za ulimwengu, majani ya muhogo hayatumiwi tu kwa tiba bali pia kwa milo mitamu. Shukrani zimwendee Yehova kwa kuumba muhogo!
J. S. E., Nigeria
Vipaumbele Vilivyobadilishwa Ni lazima niwaeleze jinsi nilivyotiwa moyo na makala “Sababu Iliyofanya Abadili Vipaumbele Vyake.” (Julai 22, 1996) Nimetumikia nikiwa mweneza-evanjeli wa wakati wote kwa miaka 13, na si rahisi sikuzote kuweka vipaumbele katika ulimwengu wetu unaozidi kuwa na mkazo. Kila mwaka, kudumu katika huduma ya wakati wote huzidi kuwa kugumu. Kufikiria kwamba Jeremy aliacha kazi yenye kuthawabisha akiwa msimamizi wa hifadhi ya asili ili kuwa mhudumu wa wakati wote kulinithibitishia kwamba kutanguliza huduma maishani kunastahili jitihada hiyo.
N. C., Marekani
Dirisha Lafunua Tumbo la Uzazi Hivi majuzi niligundua kwamba nina mimba. Kwa sababu ya tiba fulani ambayo haikufanywa vizuri, kulikuwa na hatari kwamba mtoto wangu angezaliwa na kasoro fulani-fulani. Makala yenu “Dirisha Lafunua Tumbo la Uzazi” (Agosti 8, 1996) ilinisaidia kuamua nisitoe mimba. Nilipokea gazeti hilo juma moja kabla ya kugundua kwamba nina mimba.
M. C., Marekani
Dyslexia Asanteni sana kwa makala yenu “Kushinda Fadhaiko la Dyslexia.” (Agosti 8, 1996) Maishani mwangu mwote nilijua kwamba kulikuwa na kasoro, lakini sikujua ni nini. Hivi majuzi iligunduliwa kuwa nina ugonjwa wa dyslexia na mtaalamu wa Kasoro ya Upungufu wa Makini. Sasa najifunza kutumia vidole kuwa msaada katika kusoma.
P. C., Marekani