Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 6/8 kur. 4-7
  • Ni Nini Huathiri Mtazamo Wako?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ni Nini Huathiri Mtazamo Wako?
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ponografia Yapotosha Ngono
  • Vitumbuizo Huonyesha Vibaya Ngono
  • Kubadilika kwa Hali Hubadili Mitazamo
  • Mafunzo ya Ngono Shuleni
  • Upendo na Uwajibikaji Ni Nini?
  • Mitazamo Inayobadilika Yazusha Maswali Mapya
    Amkeni!—1997
  • Ngono—Ni Shauri Gani Hasa Lihalofaa?
    Furaha​—Namna ya Kuipata
  • Ufahamu Katika Habari
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1983
  • Kwa Nini Ni Vigumu Sana Kwangu Kuacha Kufikiria Watu wa Jinsia Tofauti?
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 6/8 kur. 4-7

Ni Nini Huathiri Mtazamo Wako?

MIAKA ipatayo 2,700 iliyopita, mwandikaji aliyepuliziwa aliandika methali hii yenye kuchochea fikira: “Kwa mpumbavu kutenda maovu ni kama mchezo.” (Mithali 10:23) Ukweli wa jambo hili umeonekana hasa tangu mvuvumko wa ngono ovyoovyo. Kabla ya tisho la UKIMWI, mtazamo ulioenea ulikuwa kwamba ngono ni ‘mchezo wa raha’ na kwamba tamaa ya ngono ni lazima itoshelezwe ‘bila kujali matokeo.’ Je, mtazamo huo umebadilika? Sivyo hasa.

Leo, ashiki ya kingono bado hutokeza “waraibu wa mapenzi,” ‘watu wenye kufunga mfululizo wa ndoa,’ na “waoteaji wa kingono,” ambao hubisha kwamba maadili ni mambo ya mtu binafsi na kwamba kufanya ngono na watu tofauti-tofauti ni jambo la kawaida. (Ona sanduku “Mitindo-Maisha ya Kingono,” kwenye ukurasa wa 6.) Wao wadai kwamba ‘hakuna mtu anayeumizwa’ kwa kufanya ngono na mtu yeyote yule, maadamu ni watu wazima ambao wamekubaliana. Katika 1964, mwanasoshiolojia wa Chuo Kikuu cha Jimbo la Iowa, Ira Reiss alifafanua hali hiyo kuwa “uendekevu wenye mapenzi.”

Askofu wa Anglikana wa Edinburgh, Scotland, aonekana kuhisi hivyo, kwani alisema kwamba wanadamu waliumbwa ili wawe na wapenzi wengi. Katika hotuba juu ya ngono na Ukristo, yeye alisema: “Mungu alipotuumba alijua kwamba ametupatia tamaa ya kufanya ngono ili tupande mbegu zetu. Ametupatia urithi unaotufanya tufanye ngono ovyoovyo. Nafikiri ni vibaya kwa kanisa kushutumu watu ambao wamefuata silika zao.”

Je, hayo ni maoni mazuri? Kuna hasara gani ya kufanya ngono kiholela? Je, mahusiano ya muda mfupi-mfupi pamoja na wenzi tofauti-tofauti wa kingono yaweza kuridhisha na kuleta furaha?

Mweneo wa duniani pote wa maradhi yanayopitishwa kingono na uhalisi wa mamilioni ya mimba zinazopatikana nje ya ndoa, hasa miongoni mwa matineja, huthibitisha kwamba falsafa hiyo haifai. Kulingana na gazeti Newsweek, katika Marekani pekee, maradhi yanayopitishwa kingono huambukiza matineja wapatao milioni tatu kila mwaka. Isitoshe, wengi wa hao “watu wazima wanaokubaliana” waonekana kama hawana “shauku ya asili” au kuona wajibu wao kwa yule mtoto asiyezaliwa bado ambaye mara nyingi ndiye matokeo, nao upesi wao hujaribu kutoa mimba. (2 Timotheo 3:3) Jambo hilo hufanya mtoto asiyezaliwa bado apoteze uhai wake, anapoondolewa kikatili kutoka kwa mamake. Hasara kwa mama mchanga yaweza kuwa ni kushuka moyo sana na pia hatia ambayo inaweza kumlemea maisha yake yote.

Katika miaka ya katikati ya 1990 katika Uingereza pekee, gharama za kifedha kwa athari za mvuvumko wa ngono ovyoovyo zilikuwa za kiwango cha kushtusha cha dola bilioni 20 kila mwaka, kulingana na hesabu ya Dakt. Patrick Dixon. Katika kitabu chake The Rising Price of Love, Dakt. Dixon alifikia hesabu hiyo kwa kuhesabu gharama za kutibu maradhi yanayopitishwa kingono, kutia ndani UKIMWI; gharama za talaka; gharama kwa jumuiya ya mzazi mmoja kulea watoto; na gharama za tiba ya familia na mtoto. Kama ilivyoripotiwa katika The Globe and Mail, gazeti la kila siku la Kanada, Dakt. Dixon amalizia: “Mvuvumko wa mahusiano ya ngono ovyoovyo ambao ulituahidi uhuru umetia wengi utumwani, katika ulimwengu ulioharibiwa na ngono za kiholela, misiba, upweke, maumivu ya kihisia-moyo, ujeuri na kutendwa vibaya.”

Lakini ni kwa nini watu bado wana ashiki sana ya kingono, wanapendelea mahusiano ya muda mfupi-mfupi, na kusisitiza kufanya mapenzi kiholela bila kutaka kuwajibika? Kukiwa na matunda mabaya ya wazi kama hayo katika miongo mitatu ambayo imepita, ni nini kinachochochea ashiki hiyo yenye kusababisha uharibifu?

Ponografia Yapotosha Ngono

Ponografia imetajwa kuwa jambo moja linalochochea ashiki ya kingono. Mtu mmoja aliyekiri kuwa mraibu wa ngono aandika hivi katika gazeti The Toronto Star: “Niliacha sigareti miaka mitano iliyopita, kileo miaka miwili iliyopita, lakini maishani mwangu hakuna jambo ambalo limenishinda kuacha kuliko uraibu wangu wa ngono na ponografia.”

Pia amesadiki kwamba matineja ambao wanajihatarisha kwa kutazama kwa ukawaida ponografia husitawisha maoni mabaya juu ya mwenendo wa kingono. Wao huiga fantasia zao za kingono na kupata kwamba mahusiano halisi ni yenye kutatanisha na magumu. Hilo hutokeza upweke na matatizo mengine, ambalo tatizo kubwa ni kufanyiza vifungo vyenye kudumu vya upendo.

Vitumbuizo Huonyesha Vibaya Ngono

Mitindo-maisha ya kufanya ngono ovyoovyo na wenzi tofauti-tofauti, wawe wamefunga ndoa au la, imependelewa sana na kuonyeshwa waziwazi katika vitumbuizo. Maonyesho yenye kushusha hadhi ya mwenendo wa kingono usio na upendo yanayoonyeshwa kwenye televisheni huchochea ashiki ya kingono, yakifanya kizazi hiki kiwe na maoni yaliyopotoka juu ya mwenendo wa kingono wa kibinadamu. Vyombo vya vitumbuizo mara nyingi huhusianisha isivyofaa ngono ya nje ya ndoa na ukaribu wenye upendo. Mashabiki wa watu mashuhuri katika vitumbuizo hawaonekani kama wanaweza kutambua tofauti zilizopo kati ya kuwaka tamaa kingono na upendo, kati ya mahusiano ya muda mfupi-mfupi wa kimapenzi na uwajibikaji wa muda mrefu, au kati ya fantasia na uhalisi.

Vilevile, mara nyingi zaidi matangazo ya biashara yameonyesha vibaya ngono yanapotangaza bidhaa. Ngono imekuwa “chombo cha kunasa akili kwenye bidhaa inayotangazwa,” akasema mwanatiba wa ngono. Watangazaji wa kibiashara wametumia vibaya ngono nao wameshirikisha maonyesho ya kingono na maisha mazuri, lakini huu ni “upotovu [mwingine] wa maoni ya kingono” wa karne ya 20, kama lisemavyo jarida Family Relations.

Kubadilika kwa Hali Hubadili Mitazamo

Kubadilika kwa mazingira ya kijamii na kutokezwa kwa vibonge vya kudhibiti uzazi katika masoko mwaka wa 1960 kulibadili tabia ya kingono ya mamilioni ya wanawake. Vibonge hivyo vilifanya wanawake waone kwamba walikuwa sawa kingono na wanaume, vikawapa uhuru wa kingono au ujitegemezo ambao hawakupata kamwe kuwa nao hapo awali. Kama ilivyo na wanaume, wao sasa waliweza kuwa na mahusiano ya muda mfupi-mfupi, bila woga wa kushika mimba zisizotakiwa. Wakijitosa katika shamrashamra za kufanya ngono kwa uhuru, wote wanaume na wanawake walitupilia mbali madaraka yao ya kawaida ya kifamilia na ya kingono.

Mwandikaji mmoja wa Biblia wa karne ya kwanza alisema hivi juu ya watu kama hao: “Wana macho yenye kujaa uzinzi na yasiyoweza kuachana na dhambi . . . Wana moyo uliozoezwa katika kutamani. . . . Wakiacha pito lililo nyoofu, wameongozwa vibaya.”—2 Petro 2:14, 15.

Mafunzo ya Ngono Shuleni

Uchunguzi mmoja wa Marekani uliofanyiwa wanawake waseja wapatao 10,000 wenye umri wa kwenda shule za sekondari ulifunua kwamba “ujuzi, kama uonyeshwavyo na mitaala ya mafunzo ya ngono na ujuzi juu ya vibonge vya kudhibiti uzazi ambao matineja husema wanao,” haukuathiri kiwango cha matineja kushika mimba nje ya ndoa. Hata hivyo, baadhi ya shule za umma zinakabili mweneo huo mkubwa wa matineja kushika mimba kwa kuwapa wanafunzi kondomu bila malipo, ingawa hatua hiyo inabishaniwa vikali.

Mwanafunzi mmoja mwenye umri wa miaka 17 wa shule ya sekondari aliyehojiwa na gazeti la habari Calgary Herald alisema hivi: “Ni kweli kwamba wengi wa matineja katika shule za sekondari wanafanya ngono . . . , hata baadhi ya wale wenye umri wa miaka 12.”

Upendo na Uwajibikaji Ni Nini?

Upendo, tumaini, na uandamani wenye kutamaniwa si matokeo ya moja kwa moja ya uvutio wa ghafula wa kingono wala si matokeo ya kujitosheleza kingono. Kufanya ngono kwenyewe hakuwezi kutokeza upendo wa kweli. Upendo na ukaribiano hutokezwa na mioyo miwili ya watu wawili wenye kujali ambao wanataka kujenga uhusiano wa kudumu.

Mahusiano ya muda mfupi-mfupi hatimaye hayampi mtu usalama, humfanya awe mpweke, na labda kumwambukiza maradhi ya kupitishwa kingono kama vile UKIMWI. Wateteaji wa mapenzi ya kiholela waweza kufafanuliwa na maneno yapatikanayo kwenye 2 Petro 2:19: “Huku wao wakiwaahidi uhuru, wao wenyewe wanakuwako wakiwa watumwa wa ufisadi. Kwa maana yeyote yule anayewezwa na mwingine hufanywa mtumwa na huyu.”

Kamati ya Kanisa la Uingereza yenye kushughulikia uwajibikaji wa kijamii ilitoa ripoti katika Juni 1995, yenye kichwa “Jambo la Kusherehekewa.” Tofauti kabisa na shauri la Biblia, kamati hiyo ilihimiza kanisa “lifute maneno yasemayo ‘kuishi katika dhambi’ na liache kuhukumu-hukumu wale ambao wanaishi pamoja bila kufunga ndoa,” kulingana na The Toronto Star. Ripoti hiyo ilipendekeza kwamba “makutaniko yapaswa kukaribisha wale wanaoishi pamoja bila kufunga ndoa, wawasikilize, wajifunze kutokana nao, . . . ili kwamba wote waweze kugundua kuwapo kwa Mungu katika maisha zao.”

Yesu angewaitaje viongozi wa kidini kama hao? Bila shaka “viongozi vipofu.” Na vipi juu ya wale wanaofuata miongozo kama hiyo? Yeye alisababu hivi: “Basi, ikiwa kipofu aongoza kipofu, wote wawili wataanguka ndani ya shimo.” Kwa hakika, Yesu alisema waziwazi kwamba “uzinzi” na “uasherati” ni miongoni mwa mambo “yanayotia mtu unajisi.”—Mathayo 15:14, 18-20.

Kukiwa na mambo haya kadhaa yanayopotosha na kuonyesha vibaya ngono, mtu anaweza, hasa vijana, kuachaje ashiki ya kingono? Ni nini siri ya kuwa na mahusiano ya muda mrefu yenye furaha? Makala ifuatayo itakazia kile ambacho wazazi waweza kufanya ili kusaidia vijana kujitayarisha kwa ajili ya wakati ujao.

[Blabu katika ukurasa wa 5]

Katika Marekani pekee, maradhi yanayopitishwa kingono huambukiza matineja wapatao milioni tatu kila mwaka

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Mitindo-Maisha ya Kingono

Waraibu wa Mapenzi: Wao hupenda kushikwa na mapenzi, kwa hiyo wao huanzisha mapenzi na watu tofauti-tofauti mara tu msisimko wa mahaba yao upoapo. Maneno ya Kiingereza, attraction junkies, yamaanishayo waraibu wa mapenzi, yalibuniwa na Dakt. Michael Liebowitz, wa New York State Psychiatric Institute.

Watu Wenye Kufunga Mfululizo wa Ndoa: Watu ambao hupitia mahusiano mengi ya mapenzi yanayohusisha mambo ya kisheria ya ndoa, talaka, na ndoa nyingine huitwa hivyo na wanasoshiolojia.

Waoteaji wa Kingono: Wao hutafuta kuonyesha uwezo wao wa kufanya ngono kwa kuwa na wenzi wengi, aonelea Luther Baker, profesa wa uchunguzi wa familia aliye pia mtaalamu wa ngono. Neno hilo sasa latumiwa kumaanisha wasumbuaji wa watoto kingono.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Ponografia huraibisha na kutokeza maoni yaliyopotoka kuhusu mwenendo wa kingono

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki