Kuutazama Ulimwengu
Kipindupindu Charudi Tena
Baada ya kutokuwapo kwa zaidi ya miaka 100, kipindupindu kimerudi tena kwa ghafula katika Amerika Kusini. “Tangu 1991, visa milioni 1.4 vimeripotiwa kule, vikisababisha vifo 10,000,” lataarifu The Times la London. Wasiwasi ulioongezeka kwa wenye mamlaka ya kitiba ulikuwa kule kutokea kwa 1992 kwa kikundi kipya cha bakteria za kipindupindu katika India, Bangladesh, na nchi jirani, ambacho kwa sasa kimeathiri watu 200,000. Kipindupindu ni maradhi yanayofanya mtu aharishe sana, na kifo hutokea kwa asilimia 70 ya visa isipokuwa matibabu ya kutosha yanapatikana. Lakini kinga ni bora kuliko ponyo. Kuchemsha maji ya kunywa na maziwa, kufukuza nzi, na kuosha chakula ambacho hakijapikwa katika maji yaliyo na klorini ni hali za msingi za usalama.
Maongezi Kuhusu Amani ya Ulimwengu
Vita vya maeneo ambavyo hapo awali vilichangia sehemu kubwa katika ile Vita Baridi vyaonekana kuwa vimeisha, kulingana na Yearbook 1997 ya Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Kimataifa ya Stockholm. Katika 1989, mwaka wa mwisho wa Vita Baridi, kulikuwa na “mapambano makuu ya kijeshi” 36. Idadi ilipungua kufikia 27 katika 1996, na yote ila moja, lile pambano kati ya India na Pakistan, lilikuwa la ndani, vita vya nchini. Zaidi ya hilo, kama inavyokadiriwa na idadi ya vifo, mengi ya mapambano haya yalipungua katika ukali, au yaliendelea kwa kiwango cha chini. “Hakuna kizazi kingine ambacho kimekaribia sana kufikia amani ya ulimwengu,” likamalizia gazeti la habari The Star, la Afrika Kusini. Gazeti Time lasema: “Utawala wa Kimarekani . . . umepatia ulimwengu amani chini ya uvutano wa Amerika, muhula wa amani ya kimataifa na utulivu ambao haujaonekana katika karne hii, usioonekana kwa urahisi katika historia ya kibinadamu.”
Bado Ni Nambari Moja
“Nakala zaidi za Biblia bado zinazidi kuchapishwa kuliko kitabu kingine chochote,” laripoti ENI Bulletin. Nchi zilizo na ugawanyaji wa juu zaidi wa Biblia ni China, Marekani, na Brazili. Kulingana na ripoti kutoka Muungano wa Sosaiti za Biblia (UBS), nakala milioni 19.4 za Biblia nzima ziligawanywa katika 1996. Hii ilikuwa rekodi mpya na ongezeko la asilimia 9.1 zaidi ya 1995. Licha ya “ukuzi wa ajabu katika kuigawanya katika sehemu hususa za ulimwengu,” akasema John Ball, mratibu wa huduma za uchapishaji kwenye UBS, “bado kuna kazi nyingi zaidi ya kufanywa ikiwa tutaandalia kila mtu njia rahisi zaidi ya kupata Maandiko.”
“Wajumbe wa Kifo”
Nchi za Magharibi zilizo tajiri zinatokeza “mzigo wenye kulemea maradufu” wa maradhi kwa nchi zinazositawi, yasema ripoti ya 1997 ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO). Kama ilivyoripotiwa katika The Daily Telegraph la London, maradhi ya moyo, mishtuko ya akili, ugonjwa wa kisukari, na kansa fulani, yanaendelea kuongezeka sana kadiri nchi zinazositawi zinavyojitwalia mitindo-maisha ya Magharibi ya kuvuta sigareti, milo yenye kizio na mafuta mengi, na kupunguza kufanya mazoezi ya kimwili. Ijapokuwa tufeni pote watu sasa wanaishi maisha marefu zaidi, ‘hii ni zawadi iliyo bure, bila ubora wa maisha,’ asema Dakt. Paul Kleihues, mkurugenzi wa WHO. Aongezea: “Wale ambao wanasema sisi kwa kweli ni wajumbe wa kifo wanasema kweli.” Shirika la WHO linatetea kampeni iliyoongezeka ya ulimwenguni pote ya kutia moyo mitindo-maisha yenye afya. Kama sivyo, lasema, kutakuwako “tatizo la kuteseka kwa kiwango cha tufeni pote.”
Mkuu wa Wabuddha Ashauri Kutafuta Kweli
“Ukaidi si mzuri” kuhusiana na dini, asema Eshin Watanabe, kasisi mkuu kuliko wote na kiongozi wa mojawapo ya mafarakano ya Kibuddha ya Japani yaliyo ya kale zaidi. Alipoulizwa ikiwa alimaanisha ya kwamba uaminifu-mshikamanifu kwa itikadi ni mzuri lakini kushikilia itikadi kwa ukaidi ni vibaya, Mainich Daily News ilinukuu maelezo yake: “Unapaswa kufikiria kwa uzito ikiwa itikadi zako ni sawa au ni zenye makosa. Ni jambo muhimu kupitia uhusiano wake na itikadi nyingine. Wapaswa kufikiria pia ikiwa itikadi zako zawakilisha kweli au sivyo. Lazima tuchunguze mambo haya tena.” Watanabe huongoza farakano la Ubuddha la Tendai, lililoanzishwa Japani kutoka China miaka 1,200 iliyopita.
Kemikali ya Kiasili ya Kuzuia Kukua kwa Bakteria
Watu fulani bila kufikiri huramba majeraha yao wajikatapo, kama vile wanyama wafanyavyo. Kwa kupendeza, watafiti katika Hospitali ya St. Bartholomew katika London wamegundua kwamba kwa hakika mate ni kemikali ya kiasili ya kuzuia kukua kwa bakteria. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti la habari The Independent, wataalamu wa madawa waliuliza wajitoleaji 14 warambe pande zote za mikono yao nao wakapata kwamba viwango vya nitrojeni oksaidi kwenye ngozi viliongezeka sana. Nitrojeni oksaidi, kemikali yenye nguvu inayoweza kuua viini, hufanyizwa wakati naitreti iliyopo katika mate ikutanapo na sehemu ya juu ya ngozi iliyo na asidi. Utendanaji huongezwa na kemikali nyingine, askobiti, ambayo pia hupatikana katika mate.
Bangi—Ni Dawa ya Kulevya Yenye Uraibu?
Kwa muda mrefu watumiaji wa bangi wameshindana kwamba dawa hii ya kulevya kwa kadiri ni isiyodhuru. Hata hivyo, “uthibitisho mpya hudokeza [kwamba] matokeo [ya bangi] katika ubongo hufanana na yale ya madawa ya kulevya ‘yenye uraibu’ kama vile heroini,” laripoti jarida Science. Wanasayansi kutoka Marekani, Hispania, na Italia waliongoza uchunguzi huo. Miongoni mwa matokeo ya uchunguzi wao walipata kwamba “kiambato kitendaji katika bangi—sehemu ya kemikali inayojulikana kama THC—husababisha matokeo yaleyale ya msingi ya biokemia ambayo huonekana kuimarisha uraibu katika dawa nyingine za kulevya, kutoka nikotini hadi heroini: ikiachilia dopamini katika sehemu ya “kijia cha ‘thawabu’ cha ubongo,” ambacho hufanya watumizi wa madawa ya kulevya waendelee kuyatumia zaidi. Wakati matumizi ya bangi ya muda mrefu yanapokomeshwa, kiwango cha kemikali nyingine, peptidi inayoitwa corticotropin-releasing factor (CRF), huongezeka katika ubongo. CRF imehusianishwa na mkazo wa kihisia-moyo na hangaiko linalotokana na kuacha kutumia dawa ya kutia usingizi, alkoholi, na kokeni. Kulingana na hayo, mtafiti mmoja alisema: “Ningeridhika ikiwa, baada ya kuchunguza uthibitisho wote huu, watu wasingeifikiria tena THC kuwa dawa ya kulevya ‘isiyo na’ uraibu.” Kila mwaka, karibu watu 100,000 katika Marekani hutafuta matibabu kwa ajili ya uraibu unaotokana na bangi.
Barafu Katika Misri ya Kale
Ijapokuwa Wamisri wa kale hawakuwa na utiaji baridi bandia, waliweza kutokeza barafu kwa kutumia njia ya asili ya ajabu ambayo hutokea katika tabia za nchi zilizo kavu,” likaonelea The Countyline, gazeti la habari la Bryan, Ohio. Walifanyaje hivyo? “Karibu na mshuko-jua, wanawake Wamisri waliweka maji ndani ya trei za udongo zilizo na kina kifupi kwenye tuta la nyasi. Mvukizo wa haraka kutoka kwa uso wa maji na kutoka kwenye pande za trei zilizo na unyevunyevu uliungana na kupunguka kwa halijoto ya usiku ili kugandisha maji—ingawa halijoto ya mazingira haikupunguka kamwe kukaribia kiwango cha kuganda.”
Kuchomwa kwa Jua
“Kansa ya ngozi imeibuka kama sehemu ya magonjwa ya mlipuko katika Amerika ya Kaskazini,” lasema gazeti la habari The Vancouver Sun, na “kati ya [Wakanada] saba, mmoja angekuwa katika hatari” ya kupatwa na kansa ya ngozi wakati fulani maishani mwake. “Kuchomwa kwa jua kwaaminiwa kuwa huchangia asilimia 90 ya visa vya uvimbe unaoua,” laongezea hilo gazeti la habari. Ngozi ambayo imegeuka rangi ikawa hudhurungi imeharibika, yasema ripoti hiyo, na huongoza kwenye kuzeeka kwa ngozi kabla ya wakati vilevile kukandamizwa kwa mfumo wa kinga. Ukaguzi wa kitaifa uliohusisha Wakanada zaidi ya 4,000 hufunua kwamba asilimia 80 wanafahamu hatari za kuchomwa kwa jua kwenye ngozi zao, na bado karibu nusu huchukua hatua za kujikinga mara chache sana ikiwa wanafanya hivyo kwa vyovyote. Profesa na Dakt. mwenzi Chris Lavato, wa Chuo Kikuu cha British Columbia ambaye alikuwa mmoja wa wakuu katika ukaguzi huo, aonya kwamba “tunahitaji kufanya usalama wa kujikinga na jua kuwa zoea” na kutia ndani “njia za busara na zenye usalama za kufurahia kuwa nje wakati wa jua.”
Zoea Lenye Gharama Kubwa
Kuvuta sigareti hugharimu. Kwa kiasi gani? Kulingana na University of California Berkeley Wellness Letter, hatimaye, ingeweza kufikia dola 230,000 au dola 400,000—ikitegemea ikiwa unavuta pakiti moja au mbili za sigareti kwa siku. “Tuseme wewe ni mchanga na unaanza kuvuta sigareti leo na kuendelea kwa miaka 50, tukikata kauli kwamba haikuui kabla ya hapo,” lasema Wellness Letter. “Kwa pakiti moja kila siku inayogharimu dola 2.50 (kusahilisha mambo, acha tuondoe ongezeko la bei), hiyo ingejumlika kufikia zaidi ya dola 900 kwa mwaka, au dola 45,000 kwa miaka 50. Ikiwa utaweka dola 900 kwenye benki kila mwaka kwa riba ya asilimia 5, jumla ingeweza kwa urahisi kuongezeka mara nne.” Kuongeza gharama za ziada za bima ya maisha na gharama nyingine za ziada za usafi (kwa ajili ya nyumba, mavazi, na meno) hujumlika kufikia tarakimu zilizotajwa juu. Barua hiyo yaongezea: “Na hilo halitii ndani gharama za kitiba zinazohusiana na uvutaji wa sigareti ambazo utahitaji kulipia ikiwa bima yako ya afya hailipii kila kitu.”