Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 6/22 kur. 18-19
  • Langilangi—Kutoka Kisiwa cha Manukato

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Langilangi—Kutoka Kisiwa cha Manukato
  • Amkeni!—1998
  • Habari Zinazolingana
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • “Tupeleke Kadi”
    Amkeni!—1993
  • Maua Huonyesha Kwamba Mtu Fulani Anajali
    Amkeni!—1997
  • Ni Maridadi na Matamu!
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 6/22 kur. 18-19

Langilangi—Kutoka Kisiwa cha Manukato

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA MAYOTTE

JE, UMEWAHI kuyasikia? Huenda umewahi kuyatumia. Angalau umewahi kuyanusa! Hayo ni nini? Ni mti na ni marashi.

Mlangilangi ni mti ambao huchanua maua ambayo hutumiwa kutengeneza marashi ya anasa. Watu wengine husema mlangilangi ulitoka kisiwa cha Madagaska; wengine husema kwamba ulitoka Malasia, ambako mti huo hukuzwa pia. Lakini hapa katika Visiwa vya Komoro, katikati ya Afrika na Madagaska, na hasa katika kisiwa cha Mayotte, tabia ya nchi inafaa sana ukuzaji wa milangilangi yenye marashi bora sana—wengine husema marashi hayo ni bora zaidi ulimwenguni.

Mayotte, ambayo wakati mwingine huitwa kisiwa cha manukato, ndiyo mtengenezaji mkuu wa marashi hayo yenye thamani na inashinda mazao ya ulimwengu wote. Milangilangi imefunika mashamba na milima inayoinuka kwa uanana katika kisiwa hiki maridadi. Lakini, kitu cha kwanza mtu huona ni maumbo ya ajabu ya miti hiyo. Matawi huonekana kana kwamba mkono mkubwa uliyapinda kuelekea chini na kuyakunja-kunja kwenye mashina yaliyopinda-pinda, yenye rangi ya kijivu-hafifu. Lakini hayo si maumbo yao ya kawaida. Milangilangi imefanyizwa kwa utaratibu iwe hivyo.

Mara tu mlangilangi ufikiapo urefu wa bega la mtu, ambapo maua yake yaitwayo langilangi yaweza bado kufikiwa vizuri, matawi yanapindwa yaelekee chini. Hilo lisipofanywa, mlangilangi hukua kama umenyooka na kuwa mrefu, ikifanya malangilangi yake yawe juu sana hata yasiweze kuchumwa kwa urahisi. Kisha mti huo hufaa tu kutumiwa kama gogo.

Hata kabla ya kuweza kutofautisha mlangilangi na mimea mingine ya kijani-kibichi, manukato yake makali yakuvutia. Ingawa malangilangi yake hayavutii sana, manukato yake makali hayasahauliki. Kwa kweli, mtu asiyezoea hawezi kuona malangilangi kwa urahisi, kwa vile hayo hayawezi kutofautishwa na majani. Ni wakati tu maua yakomaapo ndipo yaanzapo kuwa na rangi ya kimanjano. Na huo ndio wakati wa kuyachuma.

Katika kisiwa chetu cha kitropiki, milangilangi huanza kuchanua malangilangi ikiwa na miaka miwili au mitatu. Wingi wa malangilangi yake ni wonyesho mzuri ajabu wa roho ya ukarimu ya Muumba! Kati ya Mei na Desemba, watu waweza kukusanya kutoka kwa kila mlangilangi kilogramu 1 hadi 2 ya malangilangi kila baada ya siku 15. Pia huchipua tangu Januari hadi Aprili, lakini hayo huharibiwa na mvua ya kitropiki.

Malangilangi yachumwapo wote katika familia husaidia, hasa wanawake na watoto. Ni rahisi kuchuma malangilangi kwa kuwa matawi yako chini. Malangilangi hayo hukusanywa ndani ya kangas—kikapu kikubwa kilichotengenezwa kwa makuti. Je, waweza kuwazia mtoto akibeba kichwani kangas nyepesi yenye kujaa chekwa? Maua yenye kilogramu 20 hadi 30 huonekana kufunika kabisa kichwa chake kidogo wakati yeye na wengine wanapofuatana barabarani wakielekea mahali ambapo marashi ya langilangi yatatoneshwa.

Sasa ndipo ianzapo kazi nyingi ya mchana na usiku ya kutonesha marashi. Chini ya chombo kikubwa cha utoneshaji kiitwacho alambic, moto huwaka daima. Ndani ya alambic, kilogramu 200 za malangilangi yaliyokomaa huelea katika maji yenye kuchemka ya lita 70. Ufito uliopindwa wa utoneshaji ni lazima upoe kufikia halijoto ifaayo kabisa ili marashi hayo yawe bora. Kufikia lita moja ya marashi yaliyokolea sana yaweza kutolewa kwenye malangilangi ya kiasi hicho, kiasi hasa kikitegemea eneo ambalo yametoka. Marashi zaidi yasiyokolea sana yaweza pia kutolewa kwenye maji hayohayo. Hatimaye, marashi hayo hupelekwa Ulaya ili yatumiwe katika kutengeneza marashi ya anasa.

Labda sasa unaweza kuelewa kwa nini kisiwa hicho cha Mayotte kinaitwa kisiwa cha manukato. Kwa kweli, manukato yenye kupendeza ya milangilangi yanayotanda hewa ya kisiwa hiki yaongezea uthamini wetu kwa uumbaji wa Muumba.

[Ramani katika ukurasa wa 18]

AFRIKA

MADAGASKA

VISIWA VYA KOMORO

Kisiwa Kikuu cha Komoro

Mohéli

Anjouan

Mayotte

[Picha katika ukurasa wa 18]

Malangilangi

[Picha katika ukurasa wa 19]

Shamba la milangilangi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki