Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Watoto Waondokapo Nyumbani Nilifarijiwa na mfululizo wa makala “Watoto Waondokapo Nyumbani.” (Januari 22, 1998) Watatu kati ya watoto wetu wanne waliondoka nyumbani miaka mitatu iliyopita. Ingawa niliwalea nikitazamia kwamba wakati ungefika kwao kuondoka nyumbani, sikufikiri kamwe kwamba hao watatu wangeondoka wakati uleule! Kwa kweli, nathamini hangaiko ambalo Watch Tower Society inaonyesha kwa hisia za wazazi.
M. S., Japani
Kwa wakati uliopo, mimi na mke wangu tunatumikia tukiwa mapainia wa pekee, au waeneza-evanjeli wa wakati wote, nje ya jimbo letu. Shauri lenu juu ya jinsi ya kuwaonyesha wazazi wetu kwamba bado wao ni wapendwa wetu hata ingawa tuko mbali sana, lafanya kazi kwelikweli.
M. M. S., Brazili
Nina umri wa miaka 11. Sikuwa nikiona kazi za kila siku za nyumbani kuwa mazoezi ya kuwa mtu mzima. Lakini makala hizi zimenisaidia nifikiri kwa njia tofauti. Asanteni kwa kutujali sisi tulio vijana.
D. U., Yugoslavia
Sokwe Ile makala “Kuzuru Sokwe wa Mlimani” (Januari 22, 1998) ilifurahisha kusoma. Sikufikiri kamwe mwanadamu aweza kukaribia sana sokwe bila kushambuliwa. Katika sinema kwa kawaida wanyama hawa huonyeshwa wakiwa wakali. Asanteni kwa makala bora.
R. P., Venezuela
Kugugumiza Natoa shukrani nyingi za moyo mweupe kwa makala “Jinsi Ninavyokabiliana na Kugugumiza.” (Januari 22, 1998) Masimulizi ya Sven Sievers yalinitia moyo mimi hasa, kwa kuwa nakabili pambano kama hilo. Kwa miaka iliyopita, Shule ya Huduma ya Kitheokrasi imenisaidia niwe msemaji mwenye ufasaha.
E. Z. S., Brazili
Shule ya Huduma ya Kitheokrasi hufanywa kila juma katika Majumba ya Ufalme ya Mashahidi wa Yehova.—Mhariri.
Mtazamo mzuri wa Sven Sievers ulinivutia licha ya vipingamizi alivyokabili. Katika kutaniko letu kuna ndugu mmoja anayepambana na kugugumiza. Sasa nitasema naye kwa heshima zaidi na kumjali zaidi.
K. K., Japani
Mimi pia nimekuwa nikigugumiza tangu utotoni. Mlitaja jambo la maana sana mliposema kwamba mtu apaswa kumwelewa mwenye kugugumiza badala ya kumsikitikia. Asanteni kwa makala hii.
E. C., Italia
Upinzani wa Wazazi Nimepokea tu toleo la Januari 22, 1998 nikasoma “Vijana Huuliza . . . Namna Gani Ikiwa Wazazi Wangu Wapinga Ndoa Yangu?” Nilifikiri nilikosea katika kupinga ndoa ya binti yangu. Lakini makala hiyo ilitia ndani mambo yote yaliyonihangaisha—umri wake mchanga, utu wa mwenzi ambaye angemwoa, tazamio la kufungiwa nira isiyosawazika pamoja na asiyeamini, uwezekano wa kuambukizwa UKIMWI, na tofauti za kitamaduni. Nasali kwamba makala hii iguse moyo wa binti yangu.
N. B., Marekani
Ni makala iliyoandikwa vizuri kama nini! Mligusia habari inayohitaji kushughulikiwa kwa busara na mkafanya hivyo kwa njia nzuri sana. Masuala tofauti-tofauti yalitajwa, yakimsaidia msomaji awe na akili iliyofunguka kuelekea mambo haya.
S. C., Marekani
Nimekuwa mweneza-evanjeli wa wakati wote kwa miaka minane. Wazazi wangu ni Wakristo pia, na nilikosana nao kuhusu uamuzi wangu wa kufunga ndoa. Asanteni sana kwa kuandaa habari hii yenye kusaidia.
T. C. F., Tanzania