Ukimwi—Wazidi Kuenea
KAREN alikulia magharibi mwa Marekani.a Akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, alidumisha viwango vya juu vya maadili muda wote alipokuwa kijana. Katika mwaka wa 1984, alipokuwa na umri wa miaka 23, aliolewa na Bill, ambaye alikuwa amekuwa Shahidi kwa muda wa miaka miwili pekee. Walibarikiwa kupata watoto wawili, mvulana na msichana.
Kufikia mwaka wa 1991 upendo wao ulikuwa umeongezeka, na walikuwa na uradhi na furaha. Mwisho-mwisho wa mwaka huo, Bill alipatwa na doa ulimini mwake lililodumu. Akaenda kumwona daktari.
Muda mfupi baada ya hapo, Karen na watoto wake walikuwa nje wakikusanya majani. Bill aliketi kwenye ngazi ya baraza na kumwita Karen aje aketi kando yake. Alizungusha mikono yake kiunoni mwake na akilengwalengwa na machozi alisema kwamba alimpenda na alitaka kuishi milele pamoja naye. Basi mbona machozi hayo? Daktari alishuku kwamba Bill alikuwa ameambukizwa HIV, kirusi kinachosababisha UKIMWI.
Familia hiyo ilipimwa. Matokeo yalionyesha kwamba Bill na Karen waliambukizwa. Bill alikuwa ameambukizwa kabla hajawa mmoja wa Mashahidi wa Yehova; kisha akamwambukiza Karen. Matokeo yakaonyesha kwamba watoto hawakuambukizwa. Bill alikufa baada ya miaka mitatu. Karen asema: “Sijui jinsi ya kueleza namna ilivyo kumwona mtu aliyekuwa na sura nzuri, umpendaye na unayenuia kuishi milele pamoja naye, akidhoofika polepole na kukonda kama ufito. Nililia sana kwa siku nyingi. Alikufa miezi mitatu tu kabla ya ukumbusho wetu wa ndoa wa miaka kumi. Alikuwa baba mzuri na mume mzuri.”
Ingawa daktari alimwambia Karen kwamba baada ya muda mfupi angekufa kama mume wake, bado angali hai. Ambukizo hilo liko katika hatua za mapema za UKIMWI.
Karen ni mmoja tu kati ya watu wapatao milioni 30 ambao sasa wana HIV/UKIMWI, tarakimu iliyo kubwa kuliko idadi ya watu wa Australia, Ireland, na Paraguai ikiunganishwa pamoja. Makadirio yanaonyesha kwamba kati ya wahasiriwa hawa, milioni 21 wanapatikana Afrika. Kulingana na tarakimu za Umoja wa Mataifa, kufikia mwanzoni mwa karne ya 21, idadi hiyo ingeweza kuongezeka na kufikia watu milioni 40. Ripoti moja ya UM yasema kwamba maradhi hayo yanalingana na magonjwa mengine ya kuenea yaliyo makubwa zaidi katika historia. Watu wazima ulimwenguni wenye kutenda kingono walio na umri wa kati ya miaka 15 hadi 49, 1 kati ya 100 tayari ameambukizwa HIV. Kati ya hawa ni 1 kati ya 10 anayetambua kwamba ameambukizwa. Katika sehemu fulani za Afrika, asilimia 25 ya watu wazima wameambukizwa.
Tangu ugonjwa huu wa kuenea ulipoanza katika mwaka wa 1981, watu wanaokadiriwa kuwa milioni 11.7 wamekufa kwa UKIMWI. Inakadiriwa kwamba katika mwaka wa 1997 pekee, watu wapatao milioni 2.3 walikufa. Hata hivyo, kuna sababu mpya za kutumainia mema katika pigano dhidi ya UKIMWI. Katika miaka michache iliyopita, visa vipya vya UKIMWI vimepungua katika mataifa tajiri. Kwa kuongezea, dawa zinazoweza kutumainiwa zinawapa watu tumaini la afya bora na maisha marefu.
Unaweza kujilindaje dhidi ya UKIMWI? Kuna maendeleo gani mapya katika tiba na chanjo? Je, maradhi haya yatapata kushindwa? Maswali haya yatajibiwa katika makala zinazofuata.
[Maelezo ya Chini]
a Majina yamebadilishwa.