Kuutazama Ulimwengu
Maziwa ya Mama Ndiyo Bora
“Maziwa ya mama ndiyo dawa yenye matokeo zaidi kuliko zote,” lasema gazeti Newsweek. “Watoto wanaonyonyeshwa maziwa haya hupata virutubishi wanavyohitaji kwa ukuzi mzuri wa akili, huku yakipunguza hatari zozote kuanzia mizio na maambukizo hadi kuendesha, ukurutu na nimonia.” Hivyo mashirika ya American Academy of Pediatrics na American Dietic Association yawahimiza akina mama wawanyonyeshe watoto wao waliozaliwa kwa angalau mwaka mmoja. “Na bado raslimali hii ya kipekee hutumiwa kwa nadra sana,” lasema gazeti Newsweek. Kwa nini? Mara nyingi ni kwa sababu ya kupotoshwa. Akina mama fulani huwa na wasiwasi kwamba huenda wasiwe na maziwa ya kutosha kuendeleza afya ya watoto wao. Wengine hufikiri kwamba vyakula vinginevyo huhitajiwa mapema zaidi. “Uhakika ni kwamba, akina mama wengi wanaweza kuandaa mahitaji ya mtoto ya virutubishi mpaka anapofikia umri wa miezi 6, wakati ambapo vyakula vigumu huongezwa hatua kwa hatua kwenye lishe,” yasema makala hiyo. “Na hata iwe wanakula chakula gani kingine, watoto wapatao umri wa miaka 2 wanaweza kunufaika na fingo na asidi za mafuta zilizo katika maziwa ya mama.” Akina mama pia hunufaika: Kunyonyesha hupunguza hatari za kupatwa na kansa ya matiti na huharakisha kupungua kwa uzito baada ya kujifungua.
Umaskini Huathiri Nchi Zenye Utajiri na Zenye Umaskini Pia
Kulingana na gazeti International Herald Tribune, ripoti ya karibuni ya Umoja wa Mataifa inafunua kwamba umaskini unazidi kuongezeka, hata katika nchi zilizo tajiri zaidi ulimwenguni. Watu wengi katika nchi zilizoendelea kiviwanda hukosa “mahitaji ya msingi,” kama vile kazi ya kuajiriwa, elimu, na utunzaji wa afya. Kulingana na ripoti hiyo asilimia 16.5 ya Wamarekani huishi katika hali za umaskini. Katika Uingereza tarakimu ni asilimia 15. Katika nchi zilizoendelea kiviwanda, watu milioni 100 hawana makao, milioni 37 hawana kazi za kuajiriwa, na takriban watu milioni 200 “wanatarajia kuishi muda unaopungua miaka 60.”
Kweli Hapasi Kukaribiwa
“Ikiwa unafikiri kwamba simba au nyati ndio wanyama hatari zaidi katika Afrika, unapaswa kuchunguza upya maoni yako,” lasema The Wall Street Journal. “Kiboko ndiye hatari zaidi.” Ingawa katuni na hadithi za watoto huonyesha viboko kuwa wanyama wenye urafiki na wenye furaha, na wanapendwa kama vile vitu vya watoto kuchezea, viboko ndio husababisha vifo vingi zaidi katika Afrika kuliko mnyama mwingine yeyote. Watu wenye kuelekeza wasafiri husema kwamba eneo lililo hatari zaidi kwenye bara ni “sehemu iliyo kati ya kiboko na njia anayofuata anapoenda kutafuta maji” na la “pili labda ni sehemu iliyo kati ya mama kiboko na ndama wake.” Ingawa viboko huonekana kuwa watulivu wanapolala pamoja karibu na vilindi vilivyo katikati ya mto, wao hujua mipaka yao na mara nyingi wanakuwa wajeuri wanaposhtuliwa au kukabiliwa. Wana nguvu nyingi sana. “Kiboko mwenye kichaa aweza kumkata mamba vipande viwili kwa meno yake. Naye aweza kukata mtumbwi vipande vipande,” asema mtu mmoja mwenye kuelekeza wasafiri. Basi kwa nini usafiri kwa mtumbwi mahali palipo na viboko? Kunatokeza mandhari ya kustaajabisha ya mto huo na wanyama walio kwenye ufuo, asema mtu huyo mwenye kuelekeza wasafiri, na “labda si hatari sana kuliko shughuli nyinginezo ambazo watalii hujishughulisha nazo katika sehemu hii: kwa kielelezo mchezo wa kuruka banji meta 110 kutoka kwenye daraja la Victoria Falls.”
Ishara za Kuonya za Kabla ya Maangamizi Makubwa Zaibuka Tena
“Siku hizi kuna mazoea yenye kuogofya katika ukiukaji wa haki za kibinadamu, yanayoleta kumbukumbu isiyopendeza ya siku zenye uovu za miaka ya 1930 wakati mambo kama hayo yalitangulia kuonyesha yale Maangamizi Makubwa,” asema Irwin Cotler, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha McGill na mwenyekiti msaidizi wa shirika la Canadian Helsinki Watch Group, kulingana na The Toronto Star. Anasema kwamba uchunguzi mmoja uliofanywa katika nchi 41 na shirika la Helsinki Federation of Human Rights waonyesha hatari iliyo wazi—kuongezeka kwa mazungumzo yenye chuki dhidi ya vikundi vidogo-vidogo. Mara nyingi kwa njia ya kuchochea chuki inayoenezwa na watangazaji na vichapo vya serikali, husababisha mnyanyaso wa vikundi vidogo-vidogo. Kuhusu mwelekeo huo Cotler asema: “Hili ni somo la Vita ya Ulimwengu ya Pili ambalo hatujajifunza.” Anasema kwamba somo jingine lililosahauliwa ni “ubaridi kuelekea ukiukaji wa haki za kibinadamu, kunyamaza kwa jumuiya kuhusu ukiukaji huu.”
Watoto—Makafara wa Vita
“Kulingana na mwakilishi maalum wa UM Olara Otunnu, vita na mapambano katika mwongo uliopita viliua watoto milioni mbili, vikasababisha watoto zaidi ya milioni moja kuwa mayatima, na kujeruhi vibaya au kulemaza wengine milioni sita,” laripoti gazeti la kila siku la Ujerumani Grevener Zeitung. Baraza la Usalama la UM limelaumu mazoea yote yanayofanya watoto wawe shabaha ya kufanyiwa ujeuri. Jambo linalohangaisha hata zaidi ni kwamba ulimwenguni pote watoto zaidi ya 300,000 wanachukuliwa kuwa askari-jeshi. Wengi wao wanasemekana kuwa wanalazimishwa kuingia katika utumishi wa kijeshi, thuluthi moja kati yao wakiwa ni wasichana. Mara nyingi watoto walio askari-jeshi huelekea kuuawa wanapokuwa vitani. Muungano ulioanzishwa hivi karibuni wa mashirika yasiyo ya kiserikali unadai kuwepo kwa mkataba wa kimataifa ambao utaongeza kiwango cha chini cha umri wa askari-jeshi kuwa miaka 18.
Vatikani Yaunganishwa Kwenye Mfumo wa Internet
Mwaka wa 1994 Vatikani ilitia sahihi mkataba wa kupata Mahali katika mfumo wa Internet. Huduma za kidini, kama vile ungamo la moja kwa moja na kushauriana na makasisi kuhusu “shaka lolote” juu ya mambo ya kidini, sasa zinapatikana katika Internet, laripoti gazeti la habari El Financiero. Kwenye mahali fulani pa mfumo huo, “Wakatoliki wanaotumia Internet” wanaweza kuomba sala zitolewe kwa niaba yao. Pia inawezekana kutazama papa akitoa baraka za Jumapili. Kisha kuna matangazo yanayotoa “fursa za kununua na kuuza vitu vya kidini.” “Tatizo ni kwamba ni mahali pachache sana pa Kikatoliki katika mfumo wa Internet ambapo hufikiwa mara nyingi,” lasema gazeti El Financiero. “Watu wanaopungua 25 huvinjari mahali pa Vatikani kila siku, na watazamaji wengi huwa ni waandishi wa habari Wakatoliki.”
Waamua Kubaki Wakiwa Wagonjwa
“Kifua Kikuu ungali ndio ugonjwa namba moja unaoua watu wengi zaidi ulimwenguni,” laripoti gazeti la habari Cape Times. Katika Afrika Kusini ambapo unasambaa kwa haraka miongoni mwa watu walio maskini zaidi, unaua watu zaidi ya 13,000 kila mwaka na kuwafanya wengi wawe wagonjwa sana wasiweze kufanya kazi. Kwa watu wanaokuwa wagonjwa na kutoweza kufanya kazi, serikali inawapa marupurupu ya kuwasaidia na tiba za kifua kikuu. Lakini kwa kuwa kazi ya kuajiriwa ni nadra sana na mara nyingi malipo ni ya chini, wagonjwa fulani huamua kuacha kupokea matibabu ya kifua kikuu kusudi waendelee kupata marupurupu yao. “Malipo hayo ni zaidi ya mara 10 ya pesa wanazopata kwa kufanya vibarua,” akaeleza Ria Grant, mkurugenzi wa shirika la Afrika Kusini Linaloshughulikia Kifua Kikuu. “Wanaamini kwamba ni afadhali kuwa mgonjwa kuliko kuwa na afya njema wanapoona kiasi cha pesa wanazoweza kupata.”
Madereva Wenye Kusinzia
“Wataalamu fulani wanasema kwamba madereva wenye kusinzia ni hatari kama walivyo madereva walevi,” laripoti jarida The Journal of the American Medical Association. “Fungu linalochangiwa na usingizi katika migongano ya [magari] hudharauliwa sana, na madereva wenye kusinzia wanatokeza tisho kubwa kwa afya na usalama wa umma.” Kulingana na The Toronto Star, uchunguzi umeonyesha kwamba watu hawawezi kubashiri wakati watakaposhikwa na usingizi au kukadiria kiwango cha usingizi wao. “Kama vile njaa na kupumua yalivyo mahitaji, ndivyo na usingizi,” asema Stephanie Faul, msemaji wa shirika la American Automobile Association Foundation for Traffic Safety. “Mwili wako unapohitaji usingizi, unajipata umeshikwa na usingizi tu.” Madereva wanapaswa kufanya nini wanapojipata wakipiga miayo mara kwa mara au macho yao yanapojifunga au gari lao linapoanza kwenda kombo? “Majaribio ya kawaida ya kuamka, kama vile kufungua dirisha au kufungulia redio, kwa wazi hayafanyi kazi,” lasema The Toronto Star. “Kafeini humsaidia mtu abaki akiwa macho kwa muda mfupi tu lakini haiwezi kupunguza mahitaji ya kiasili ya kulala.” Madereva wenye kusinzia wanashauriwa wasimamishe magari yao mahali palipo salama na kulala kidogo.
Je, Kuna Bakteria Ngapi?
Bakteria ni namna ya uhai iliyo ya kawaida duniani. Zinapatikana chini ya sakafu ya bahari yenye kina kirefu zaidi na kilometa 60 juu kwenye angahewa. Jumla ya uzito wake unashinda uzito wa namna nyinginezo za uhai. Sasa jaribio la kwanza ambalo limefanywa kwa juhudi la kukadiria idadi yake limechapishwa na wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Georgia, Marekani. Kadirio lao ni tano ikifuatwa na sufuri 30. “Watu wengi hufikiri kwamba bakteria husababisha maradhi,” lasema gazeti The Times la London. “Lakini ni chache ambazo huweza kusababisha maradhi. Hata ikiwa bakteria zote zinazoishi ndani ya wanyama zitajumlishwa, zinafikia asilimia moja hivi ya jumla yake. Nyingi zaidi mbali na kutosababisha madhara huwa za muhimu, zikisaidia katika utendaji kama vile umeng’enyaji.” Kwa kushangaza, asilimia 92 hadi 94 ya bakteria zote hupatikana kwenye mashapo yaliyo sentimeta kumi chini ya bahari na kwenye ardhi iliyoko chini yenye kina kinachozidi meta tisa. Awali maeneo haya yalifikiriwa kuwa hayana uhai kabisa. Karibu nusu ya uzito usio na maji wa bakteria huwa na kaboni, elementi iliyo muhimu kwa uhai. “Kiasi cha kaboni kinachohifadhiwa katika bakteria kinakaribia kutoshana na kile kinachohifadhiwa katika mimea yote ulimwenguni,” lasema gazeti The Times.