Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 5/22 kur. 14-15
  • Jikinge na Vimelea!

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Jikinge na Vimelea!
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuzuia Ni Bora Kuliko Kuponya
  • Fanya Ulaji Wako Uwe Salama
    Amkeni!—1990
  • Kichocho—Je, Kitaondolewa Karibuni?
    Amkeni!—1997
  • Unayopaswa Kujua Kuhusu Malaria
    Amkeni!—2015
  • Upofu wa Mtoni-Kuishinda Tauni Mbaya Mno
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 5/22 kur. 14-15

Jikinge na Vimelea!

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA HONDURAS

WEWE huamka ukihisi kichefuchefu. Unachoka haraka. Tumbo lako limefura kidogo. Je, hizo ni dalili za mimba? Labda. Lakini kama unaishi katika au karibu na nchi za joto ulimwenguni, huenda tatizo likawa aina fulani ya vimelea vya tumbo. Vimelea vya tumbo ni nini, na unaweza kujuaje ikiwa una vimelea?

Kwa lugha rahisi, vimelea ni vijiumbe ambavyo hunufaika kutokana na kiumbe kingine ambacho vinategemea. Aina mbili za vimelea vya tumbo ni protozoa zinazotia ndani amiba, na minyoo. Madhara yanayompata mtu hutegemea aina ya vimelea na idadi ya vimelea ambavyo vimemwambukiza na vilevile umri wake na afya yake.

Kwa mfano, mnyoo aina ya mchango mkuu wa kike aweza kutaga mayai yapatayo 200,000 kwa siku. Lakini, ni lazima mayai yapevuke kwenye udongo ili yaweze kutokeza minyoo. Idadi ya michango mikuu katika mtu hutegemea idadi ya mayai yaliyopevuka au viluwiluwi vyake vilivyoingia mwilini. Watu wengi wana michango mikuu kadhaa na hata hawajui. Lakini michango mikuu wengi wanaweza kusababisha hatari ya kuziba utumbo.

Baadhi ya dalili za kawaida za vimelea vya tumbo ni maumivu ya tumbo, kichefuchefu, kukosa hamu ya kula, tumbo lililofura, uchovu, tatizo la kudumu la kutomeng’enya chakula tumboni, kuhara, au kufunga choo. Kupoteza uzito, shida ya kupata usingizi, kuwashwa, kupumua kwa nguvu, na homa zaweza pia kuwa dalili za vimelea. Bila shaka, dalili hizo zaweza pia kuwa ishara ya magonjwa mengine. Lakini vimelea vinaweza kutambuliwa kwa kupima choo mara kadhaa.

Inafaa mnyoo utambuliwe vizuri. Kwa mfano, ikiwa kuna mchango mkuu pamoja na aina nyingine za vimelea, mchango mkuu wahitaji kutibiwa kwanza. Kwa nini? Kwa sababu baadhi ya dawa haziui minyoo hao bali huwaathiri tu, nao huhamia viungo vingine vya mwili ambako wanasababisha madhara mabaya.

Kuzuia Ni Bora Kuliko Kuponya

Ingawa dawa zimefanikiwa kuua vimelea, ni bora uepuke kuambukizwa. Basi, unaweza kujikingaje na vimelea?

Usafi ndio kinga bora. Mavi yasiachwe bila kufunikwa. Vyoo viwe mbali na mahali pa maji. Mavi ya wanadamu yasitumiwe kama mbolea. Usafi wa mwili ni muhimu vilevile. Kwa kuongezea, usiruhusu watoto wale udongo. Mtoto mmoja akipatikana ana vimelea, ingekuwa vizuri watu wengine wote katika familia wapimwe.

Utahadhari unaponunua na kutayarisha vyakula. Jaribu kununua bidhaa ambazo zinakuzwa katika eneo linalojulikana kuwa safi. Nyama zapasa kupikwa vizuri hadi ndani kabisa. Usile kamwe nyama mbichi. Matunda na mboga mbichi zisafishwe kabisa kwanza. Uwe mwangalifu usitumie maji ayo hayo kwa kuwa huenda yana vijidudu.

Maji ya kunywa yachemshwe kabisa. Baada ya maji kupoa, yanaweza kuongezewa hewa. Vichujio vingi vya nyumbani haviondoi vimelea vyote. Usafi wa maji ya chupa yanayouzwa hutegemea kiwango cha usafi unaofuatwa kwenye kiwanda cha kuyaweka maji kwenye chupa.

Unahitaji kutahadhari zaidi unaposafiri au wakati huli nyumbani. Vinywaji vya chupa au vya karatasi huwa salama maadamu havitiliwi barafu. Kwa kuwa vimelea fulani huweza kustahimili baridi kali ya kuganda, usafi wa barafu hutegemea maji yanayoifanyiza. Ni vizuri kutahadhari juu ya kula vyakula vinavyouzwa na wachuuzi mitaani. Nanasi au tikiti ambalo limekatwa laweza kutamanisha, lakini mara nyingi matunda hayo hunyunyiziwa maji ili yasikauke—maji ambayo huenda ikawa yana vijidudu. Uwe mwangalifu, lakini usihangaike kupita kiasi hata usiweze kufurahia safari yako. Kwa kuchukua tahadhari zifaazo, unaweza kufanya mengi ili kujikinga na vimelea.

[Picha katika ukurasa wa 14]

Usafi ndio kinga bora kabisa

[Picha katika ukurasa wa 15]

Usafi wa barafu hutegemea maji yanayoifanyiza

[Picha katika ukurasa wa 15]

Amiba na minyoo ni aina mbili za vimelea

[Hisani]

DPDx, the CDC Parasitology Website

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki