Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 10/8 kur. 24-27
  • Upofu wa Mtoni-Kuishinda Tauni Mbaya Mno

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Upofu wa Mtoni-Kuishinda Tauni Mbaya Mno
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maradhi Mabaya Mno
  • Kupambana na Nzi Mweusi
  • Tembe Moja au Mbili Mara Moja kwa Mwaka
  • Mataraja ya Wakati Ujao
  • Kuna Tumaini Gani kwa Vipofu?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Kufumbua Macho ili Kuona Habari Njema
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Hakuna Fedha kwa Vipofu
    Amkeni!—1991
  • Magonjwa Je! Kuna Siku Yatakapokwisha?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1984
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 10/8 kur. 24-27

Upofu wa Mtoni-Kuishinda Tauni Mbaya Mno

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA NIGERIA

MANDHARI ilikuwa ile ya kawaida katika vijiji vingi vya kando ya mto katika Afrika Magharibi. Kikundi cha watu kimekalia benchi chini ya mti mkubwa unaowapa kivuli kutokana na jua lenye kuchoma. Watano kati yao—wanaume wanne na mwanamke mmoja—walikuwa vipofu kabisa na daima.

“Watu hawakujua kwa nini walikuwa wakipofuka katika kijiji cha kale,” akasema chifu wa kijiji, ambaye alikuwa amevalia joho refu jeupe. “Wengi wa wazee huko walikufa wakiwa vipofu. . . . Walifikiri kwamba ibilisi fulani alikuwa dhidi yao. Waliomba viabudiwa vyao viwalinde. Babu zao waliwaambia wapatie viabudiwa hivyo chakula. Kwa hiyo walichinja kuku na kondoo kuwa dhabihu. Lakini waliendelea tu kuwa vipofu.”

Hatimaye, madaktari wakaja na kueleza kwamba chanzo cha huo upofu hakikuwa viumbe roho. Ulikuwa matokeo ya ugonjwa uitwao onchocerciasis, au upofu wa mtoni, ukiitwa hivyo kwa sababu nzi wadogo mno, wanaouma wenye kuueneza hutaga mayai yao katika mito yenye maji yapitayo kwa kasi.

Kwa uzuri, upofu wa mtoni si rahisi kuambukizwa kama ilivyo na maradhi mengine ya kitropiki. Hautokezi tisho lolote kwa wakazi wa jijini au kwa wale wanaozuru kwa muda mfupi mahali palipo na ambukizo. Upofu hutokea tu baada ya maambukizo ya tena na tena kwa kipindi cha miaka mingi.

Hata hivyo, upofu wa mtoni ni maradhi mabaya sana ya kitropiki, yenye kuharibu uhai wa mamilioni. Ingawa umeenea sana katika baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati na Amerika ya Kati na ya Kusini, walioathiriwa mno ni wale wanaofanya kazi na kuishi karibu na mito iliyojaa nzi katika Afrika ya Magharibi. Katika vijiji fulani karibu kila mtu ana maradhi hayo. Kulingana na makadirio yaliyofanywa na The Carter Center katika Atlanta, Georgia, Marekani, watu wapatao milioni 126 wako hatarini mwa kuambukizwa. Wengine wapatao milioni 18 wana minyoo ya kimelea isababishayo upofu wa mtoni miilini mwao. Idadi ya watu walio vipofu kabisa au nusu yakadiriwa kuwa kati ya milioni moja na milioni mbili.

Sasa, tauni hiyo ya karne nyingi inadhibitiwa na jitihada zilizounganishwa za WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni) na mashirika mengine, pamoja na serikali za nchi kadhaa. Dhidi ya hali za uhasama na kukosa tumaini katika sehemu nyingi za Afrika, hii ni programu ya kudhibiti-maradhi iliyo na matokeo. Programu hiyo inashangiliwa kuwa “moja ya ushindi wa kitiba na maendeleo wa karne ya ishirini.”

Maradhi Mabaya Mno

Upofu wa mtoni huenezwa na aina kadhaa za nzi mweusi wa kike (jenasi Simulium). Nzi aliyeambukizwa amwumapo binadamu, huacha buu la mnyoo wa kimelea (Onchocerca volvulus). Pole kwa pole, chini ya ngozi ya watu walioambukizwa, buu hao hukomaa na kuwa minyoo yenye urefu wa hadi sentimeta 60.

Baada ya kutungishwa, kila mnyoo wa kike huanza kutokeza minyoo midogo mno iitwayo mikrofilaria; huendelea kufanya hivyo kwa miaka 8 hadi 12, wakitokeza mamilioni ya hizo. Hizo mikrofilaria hazikomai isipokuwa zichukuliwe na nzi mweusi, zipitie ukuzi ndani ya nzi huyo, na kurudishwa kwa binadamu. Kwa sehemu kubwa, minyoo hawa wasiokomaa walio wadogo mno, huingia kupitia ngozi kwa wingi mno na huenda hatimaye wakashambulia macho. Kiasi kikubwa kufikia milioni 200 hujikusanya katika mtu mmoja. Ni wengi mno hivi kwamba uyakinishaji hutia ndani kukata kwa makasi vijipande vya ngozi kwa ajili ya uchunguzi. Chini ya hadubini, kiolezo cha ngozi chaweza kuonyesha mamia ya minyoo yenye kujizungusha-zungusha.

Vimelea hivi hutesa majeruhi wavyo wa kibinadamu. Baada ya miaka ngozi ya mtu aliyeambukizwa hunenepa na kuwa na magamba. Mara nyingi viraka vya kuisha kwa rangi huonekana. Majeruhi husitawisha kile kifafanuliwacho kwa wazi sana kuwa ngozi ya mamba, ngozi ya mjusi, au ngozi ya chui. Kuwashwa ni kwingi mno, kunaripotiwa kufanya wengine wajiue. Minyoo hiyo michanga ikivamia macho, baada ya kupita kwa wakati, mwono hudhoofika na jeruhi huwa kipofu kabisa.

Katika sehemu zenye umaskini za mashambani, mahali ambapo nzi weusi wameenea sana, upofu hasa ni mzigo mzito sana kustahimili. Sababu moja ni kwamba wanakijiji wengi huamini kishirikina kwamba upofu ni tokeo la adhabu ya kimungu na kwamba vipofu hawana maana katika jamii zao. Sababu nyingine ni kwamba serikali hazitoi misaada ya kijamii, hilo likifanya majeruhi wategemee familia zao katika hali zote. Sata, jeruhi wa kike wa upofu wa mtoni katika Burkina Faso, asema hivi: “Kwa kipofu, awe mwanamume au mwanamke, mteseko ni uleule. Mwanamke mchanga akiwa kipofu na hajaolewa, hatapata mume. Niliolewa kabla ya kuwa kipofu, lakini mume wangu alikufa. Ndugu yangu alikuwa kipofu alipokuwa mchanga na kwa hiyo hangeweza kupata mke. Sote tunategemezwa na familia yetu—kwa chakula, kwa kila kitu. Ni hali mbaya mno.”

Katika maeneo ambapo upofu wa mtoni ni wa kawaida, watu mara nyingi huacha vijiji vyao, wakilazimishwa kutoroka na nzi hao na maradhi. Ardhi yenye rutuba kando ya maji hupuuzwa na kuwa ardhi isiyo na faida. Hatimaye hili huchangia umaskini na njaa.

Kupambana na Nzi Mweusi

Jitihada za kimataifa za kudhibiti upofu wa mtoni katika nchi saba za Afrika Magharibi zilianza mapema katika miaka ya 1970. Vikiwa vimejihami kwa viuawadudu vitumiwavyo kuulia mabuu, vikundi vya helikopta, ndege ndogo, na malori vilishambulia nzi weusi, kichukuzi cha maradhi hayo. Lengo lilikuwa kushambulia na kuua nzi weusi wakati ambapo walikuwa rahisi zaidi kuuawa—katika hatua yao ya buu.

Halikuwa jambo la lazima kusumisha mito yote. Wataalamu walijua kwamba nzi weusi wa kike walitaga mayai yao juu ya maji na kwamba mayai hayo hukwama kwenye matawi na miamba chini tu ya mikondo yenye nguvu ya mto. Ni maji yenye kupita kwa kasi tu yanayoandalia buu wanaotokeza oksijeni nyingi wanayohitaji ili kuendelea kuishi. Hili lilimaanisha kwamba mahali pa uzaaji kando ya mito palikuwa pachache na palipoweza kutambulika.

Kusudi la kupulizia dawa kwenye mahali pa uzaaji halikuwa kumaliza nzi weusi kabisa, kazi ambayo haiwezekani. Lakini kwa kupunguza idadi ya nzi, wataalamu walitumaini kwamba mweneo wa vimelea ungeweza kukomeshwa. Kuwa na nzi wachache zaidi kungemaanisha kuwa na maambukizo mapya machache zaidi. Kwa mafafanusi ya akili, ikiwa hao nzi wangeweza kukandamizwa hadi vimelea vilivyopo vife pole kwa pole katika watu walioambukizwa tayari, kungekuwa na wakati ambapo hakungekuwa na vimelea vilivyobaki. Kwa hiyo, kama nzi angemwuma mtu, hangechukua vimelea vyovyote vya kupitisha kwa wengine.

Mradi huo ulikuwa mgumu. Nzi huzaa katika mahali pengi mno ambapo ni vigumu kwa wataalamu kupafikia. Pia, kwa kuwa hao nzi wanaweza kupuruka mamia ya kilometa, kupambana na nzi weusi kwahitaji kufanywa katika eneo kubwa mno. Isitoshe, uangalifu upitao wa kawaida utahitajika kwa kuwa hata kukosa kupuliza dawa kwa mwezi mmoja kungetokeza kurudi tena kwa idadi ya nzi, ikiharibu miaka mingi ya kazi.

Zikianza katika miaka ya 1970, ndege zilipulizia dawa kwa kuchagua zaidi ya kilometa 19,000 za njia za maji zisizofikilika. Kama tokeo, maradhi hayo yalimalizwa kutoka asilimia 80 ya maeneo yaliyoambukizwa katika nchi zilizoshiriki.

Tembe Moja au Mbili Mara Moja kwa Mwaka

Kisha, kuanzia mwaka 1987, silaha nyingine ilitokezwa katika pigano dhidi ya upofu wa mtoni. Wakati huu badala ya kushambulia nzi weusi, shabaha ilikuwa vimelea vilivyo ndani ya mwili wa binadamu. Silaha hiyo ilikuwa dawa salama na yenye matokeo iitwayo Mectizan (ivermectin), iliyotokezwa katika maabara za kampuni fulani ya madawa ya Marekani.

Ili kusimamisha kusitawi kwa maradhi hayo, mtu aliyeambukizwa ahitaji kumeza kiasi kimoja—tembe moja au mbili—kila mwaka. Mectizan haiui minyoo ya kimelea iliyokomaa mwilini, bali huua minyoo midogo mno na kuzuia utokezaji wa mikrofilaria wa minyoo iliyokomaa. Jambo hili husimamisha uendeleaji wa maradhi katika jeruhi na kupunguza upitishaji wa maradhi kwa wengine. Dawa hiyo pia hufanya kazi kuondoa uvimbe wa mapema katika sehemu nyeupe ya jicho na kuzuia vimbe nyingine kutokana na kuwa mbaya zaidi. Hata hivyo, haiwezi kurekebisha vimbe za zamani za macho, wala kuondoa upofu mara upatikanapo.

Hata hivyo, taabu ilikuwa usambazaji—kupelekea dawa watu wenye uhitaji. Halaiki zinazoishi katika vijiji vya mbali mno na vilivyojitenga zaweza kufikiwa tu kwa kutembea. Kutumia gari mara nyingi huhitaji kukata vichaka au hata kujenga madaraja. Nyakati fulani vita vya wenyewe kwa wenyewe, ukosefu wa fedha, na siasa za mahali huongezwa kwenye magumu ya usambazaji. Hata hivyo, licha ya vizuizi hivi, kufikia mapema mwa 1995 tembe za Mectizan milioni 31 hivi zilikuwa zimesambazwa, sanasana katika Afrika.

Mataraja ya Wakati Ujao

Katika miaka 20 iliyopita, Programu ya Udhibiti wa Upofu wa Mtoni imepambana na upofu wa mtoni katika nchi 11 za Afrika Magharibi, eneo lililo mara tatu ukubwa wa Ufaransa. Matokeo yamekuwa nini? Kulingana na tarakimu za WHO, utumizi uliounganishwa wa viuamabuu na Mectizan umefanya kazi ili kukinga zaidi ya watu milioni 30, ambao wakati mmoja walitishwa na tauni hii ya kale na iliyo mbaya. Zaidi ya watu milioni 1.5 ambao walikuwa wameambukizwa vibaya mno na vimelea sasa wamepata nafuu kabisa. Isitoshe, kushindwa kwa upofu wa mtoni pia ni kupatikana kwa ekari milioni 60 hivi za bara liwezalo kulimwa kwa ajili ya ukaaji tena na ukulima—bara lenye kutosha kulisha watu milioni 17 hivi kwa mwaka.

Hiyo vita haijakwisha hata kidogo. Mataifa ya Afrika ambayo yameng’ang’ana kushinda upofu wa mtoni yana watu chini ya nusu wanaotishwa na maradhi hayo.

Katika miaka ya majuzi jitihada za kushindana na maradhi zimeongezeka. Katika miaka miwili tu, kutoka 1992 hadi 1994, idadi ya watu waliotibiwa na Mectizan ilirudufika, kutoka milioni 5.4 hadi milioni 11. Kufikia mwishoni mwa 1994 nchi zipatazo 32 katika Afrika, Amerika ya Kilatini, na Mashariki ya Kati zilikuwa zimeanzisha programu za utibabu wa kutumia Mectizan, ambao kwa kupita kwa wakati waweza kukinga watu wengi mno kufikia milioni 24 dhidi ya upofu.

Shirika liitwalo Pan American Health Organization latumaini kuondoa maradhi hayo kutokana na kuwa tisho la afya ya umma katika Amerika kufikia mwaka 2002. Katika Afrika, bila shaka, kazi hiyo ni kubwa zaidi. Hata hivyo, Wakf wa Watoto wa Umoja wa Mataifa waonelea hivi: “Tayari ni wazi kwamba kwa kizazi kinachokua sasa upofu hautokezi tisho kubwa la wakati ujao ambalo ulitokeza wakati mmoja, katika eneo ambalo kupoteza mwono kumekuwa sehemu ya kawaida ya kuzeeka.”

Inachangamsha moyo kujua juu ya jitihada zinazofanywa ili kusaidia watu ambao walitishwa na upofu. Wakati wa huduma yake ya kidunia, Yesu Kristo pia alionyesha ufikirio wenye upendo kwa watu kwa kuwarudishia wengi waliokuwa vipofu mwono kimuujiza. (Mathayo 15:30, 31; 21:14) Hili lilionyesha kwa kiwango kidogo kile kitakachotukia duniani chini ya Ufalme wa Mungu. Kwa hakika, wakati unakuja ambapo hakuna mtu atakayeteseka kwa upofu wa aina yoyote. Neno la Mungu latabiri hivi: “Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa.”—Isaya 35:5.

[Blabu katika ukurasa wa 25]

“Walikuwa wakilaumu viumbe wa kiroho kwa kusababisha upofu. Sasa, wanajua kwamba ni minyoo”

[Blabu katika ukurasa wa 27

Tembe moja au mbili kwa mwaka zaweza kuzuia upofu wa mtoni

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki