Hakuna Fedha kwa Vipofu
Asilimia 80 ya vipofu wa ulimwengu huishi katika nchi zinazositawi. Wengi wao hupatikana katika Asia ya Kusini-Mashariki. Huko, mmoja kati ya kila watu 25 ni kipofu au kwa sehemu ni kipofu, laripoti WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni). Visababishi vikuu ni nini? Kutopata chakula kinachofaa na maambukizo yanayoletwa na uchafu wa kiafya.
Kulingana na gazeti la Kidachi Internationale Samenwerking, WHO hudai kwamba likiwa na dola za U.S. milioni elfu mbili kwa mwaka, lingeweza kufanya kampeni yenye kufaulu ya kuzuia upofu katika nchi zinazositawi. Ingawa kiasi hicho ni kidogo zaidi ya kile ambacho serikali za ulimwengu hutumia kwa ajili ya makusudi ya kijeshi kwa siku moja, WHO hujulisha rasmi linashindwa kupata fedha zinazohitajiwa.
Kwa hiyo, kwa kukosa uwezo wa kutosha, linayoweza kufanya tu sasa ni kujaribu kuzuia upofu kwa kutawanya vidonge vya vitamini A kwa watoto. Karibu watoto 400,000 katika India, Indonesia, Bangladesh, na Ufilipino hupatwa na maradhi ya macho yanayosababishwa na ukosefu wa vitamini A. Lakini WHO latabiri kwa kukosa tumaini kwamba, kama hesabu ya sasa ikiendelea, ulimwengu utakuwa na vipofu na watu walio vipofu kwa sehemu milioni 84 kufikia mwaka 2000.