Kuna Tumaini Gani kwa Vipofu?
JOHN MILTON alitunga masimulizi yake ya kihekaya Paradise Lost na Paradise Regained hata ingawa alikuwa kipofu kabisa. Ingawa alikuwa kipofu na kiziwi pia hilo halikumzuia Helen Keller asijitahidi kuwasaidia wale wenye upungufu mbalimbali wa kimwili. Ndiyo, watu wengi walio vipofu hukabiliana vema na hali hiyo. Lakini ingekuwa jambo la ajabu kama nini ikiwa kila mtu angeweza kuona vizuri! Huenda ukakubali hasa ikiwa una mpendwa au rafiki aliye kipofu au mwenye kasoro ya macho.
Ni kweli kwamba, katika mabara fulani programu za kurudisha hali nzuri hufundisha stadi za maisha ya kila siku kwa watu wenye kasoro ya macho. Braille (maandishi ya vipofu) na mbwa waliozoezwa kuwaongoza vipofu husaidia vipofu kushughulikia mengi ya mahitaji yao. Hata hivyo, watu wengi huona upofu kuwa ndio ulemavu wenye kuhofisha zaidi. Mwandikaji mmoja alidai hivi: “Kuwa kipofu ni kupoteza uwezo wa kuwasiliana na sehemu ya maana zaidi ya ulimwengu wetu wa hisi.” Wakati uleule, vipofu wengi hulazimika kutegemea wengine zaidi na zaidi.
Huenda ukajiuliza, kwa nini upofu umeenea sana? Je! umesikia juu ya trakoma (ugonjwa unaopinda kope la jicho)? Huo husababisha karibu visa milioni tisa vya upofu. The New Encyclopædia Britannica yasema hivi juu yao: “Ugonjwa huo unaambukiza na unaenea sana mahali ambapo vikundi vya watu vimesongamana pamoja katika mazingira yasiyo yenye afya nzuri. Upungufu wa maji ya kuoshea vitu, na inzi wengi sana wanaovutiwa na kinyesi cha kibinadamu, husaidia kueneza ugonjwa huo. Katika njia fulani-fulani trakoma ni tatizo la kijamii zaidi kuliko kuwa tatizo la kitiba; ikiwa hali za maisha zaweza kuboreshwa, msongamano wa watu kupunguzwa, inzi kuzuiwa, na maji ya kutosha kuhakikishwa, kutokea kwa trakoma kwapungua upesi.” Watu wengine wapatao milioni moja hupatwa na upofu wa mto. Au namna gani ekrofithalmia? Ingawa jina hilo ni gumu, jambo ni kwamba hicho ni kisababishi cha kawaida cha upofu. Ugonjwa wa sukari, diftheria (unaoathiri koo na moyo), surua, homa isababishayo vipele vyekundu ngozini, na magonjwa yanayopitishwa kingono huenda pia yakasababisha upofu.
Tunapokuwa wenye umri mkubwa zaidi, huenda uwezo wetu wa kuona ukafifia kwa sababu ya maradhi kama vile kudhoofika kwa sehemu ya jicho inayopokea mwangaza na glaukoma (ugonjwa unaotanua mboni ya jicho), na hatuwezi kuacha katarakti (watoto jichoni). The New Encyclopædia Britannica yaonyesha hivi: “Mtoto jichoni bado husababisha visa vingi vya upofu katika nchi nyingi ulimwenguni, na jambo hilo linahuzunisha zaidi kwa sababu hali hiyo yaweza kuponywa kwa urahisi sana kupitia upasuaji.”
Yajapokuwa magunduzi mapya katika matibabu ya magonjwa ya macho, yaonekana kwamba kuondolewa mbali kwa upofu hakuko karibu sana. Ensaiklopedia iyo hiyo yasema hivi: “Maendeleo katika kuzuia na kutibu upofu kitiba na kwa njia ya upasuaji kwaweza kuwanufaisha wale tu wawezao kupata utunzaji wa kitiba. Mpaka hali za kilishe na za kiafya za sehemu iliyo kubwa ya watu ulimwenguni ziweze kuboreshwa, upofu uwezao kukingwa utaendelea kwenye kiwango chao cha juu kilichopo sasa.”
Ingawa kwa hakika madawa ya kuua viini vya magonjwa na upasuaji vyafaa katika kupigana dhidi ya upofu, tumaini la ponyo la kudumu linahusiana na jambo fulani lililotokea yapata miaka elfu mbili iliyopita.
Kuwaponya Vipofu Katika Siku ya Yesu
Wazia mtu wa miaka yake ya mapema-mapema ya 30 akitembea kando ya barabara yenye mavumbi. Wakiwa wamesikia kwamba anapitia hapo, wanaume vipofu wawili walio kando ya barabara wapaaza sauti: “Uturehemu!” Ingawa wale wanaotazama wanawaamuru wanyamaze, wale vipofu wapaaza sauti: “Uturehemu!” Mtu huyo auliza hivi kwa fadhili: “Mnataka niwafanyie nini?” Kwa hamu wao wajibu: “Twataka macho yetu yafumbuliwe.” Sasa wazia: Huyo mtu agusa macho yao, na mara iyo hiyo wao wapokea uwezo wa kuona!—Mathayo 20:29-34.
Ni shangwe iliyoje kwa watu hao waliokuwa vipofu hapo awali! Hata hivyo, upofu umeenea sana. Hilo lilikuwa tukio moja tu. Kwa nini lastahili uangalifu wetu? Kwa sababu ni Yesu wa Nazareti aliyewapa vipofu hao pendeleo la kuona. Kwa kweli, zaidi ya ‘kutiwa mafuta ili kuwahubiri maskini habari njema,’ Yesu ‘alitumwa kuwezesha vipofu kupata kuona tena.’—Luka 4:18.
Watu walistaajabishwa na maponyo hayo ya kimuujiza yaliyofanywa kupitia roho takatifu ya Mungu yenye nguvu. Twasoma hivi: “Mkutano wakastaajabu, walipowaona mabubu wanasema, vilema wanakuwa wazima, viwete wanakwenda, na vipofu wanaona; wakamtukuza Mungu wa Israeli.” (Mathayo 15:31) Bila kulipisha chochote au kujivuna au kujaribu kujiletea utukufu katika maponyo hayo, Yesu alikazia upendo na rehema ya Yehova Mungu. Hata hivyo, Yesu alikuwa na huruma pia kuelekea watu waliokuwa vipofu na hoi kiroho waliokuwa “wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji.”—Mathayo 9:36.
Ingawa huenda historia hiyo iwe yenye kupendeza sana, huenda ukajiuliza, Namna gani leo? Kwa kuwa leo hakuna anayeponya watu kama Yesu alivyofanya, je, maponyo hayo yana maana kwetu sisi? Je! kuna tumaini lolote kwa vipofu? Tafadhali soma makala ifuatayo.
[Blabu katika ukurasa wa 4]
“Mpaka hali za kilishe na za kiafya za sehemu iliyo kubwa ya watu ulimwenguni ziweze kuboreshwa, upofu uwezao kukingwa utaendelea kwenye kiwango chao cha juu kilichopo sasa.”—The New Encyclopædia Britannica