Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kijana Mwenye Kansa Nina umri wa miaka 18, na ningependa kuwashukuru kwa ajili ya simulizi la Matt Tapio, katika makala “Hakukata Tamaa.” (Oktoba 22, 1998) Niliguswa sana na imani yake, kuthamini kwake mambo ya kiroho, na hisi yake ya uharaka. Ninatumaini kwamba nitamshukuru Matt binafsi baada ya yeye kufufuliwa katika Paradiso.
E. G. G., Hispania
Ningependa kuwashukuru kwa ajili ya makala hiyo kwa niaba ya familia yangu. Tulinufaika sana tuliposoma pamoja na vijana wetu matineja kielelezo cha imani cha Matt Tapio. Ilitupa fursa ya kuchanganua mambo tunayotanguliza tukiwa mtu mmoja-mmoja na tukiwa familia.
M. F. N. G., Brazili
Makala hiyo ilitutia moyo sana tukiwa vijana kwa sababu ilikazia bidii ya kijana ambaye, licha ya ugonjwa wake, hakukoma kusema juu ya Yehova.
D. M., Italia
Ingawa Matt Tapio alikuwa na ugonjwa wa kufisha, hakukata tamaa maishani ili aweze kumsifu na kumtumikia Yehova. Ni kielelezo bora kwetu tulio na afya njema.
D. P., Puerto Riko
Uangalifu wangu ulivutwa na ile makala juu ya Matt, ambaye alihitaji kufanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe uliokuwa kwenye ubongo akiwa na umri wa miaka 14. Baadhi ya maneno yake ya mwisho yalikuwa, “Msikome kamwe kutoa ushahidi juu ya Yehova.” Maneno haya yalinitia moyo nisikate tamaa na yalinisaidia kung’amua jinsi ilivyo muhimu kujifunza Biblia na kutwaa ujuzi uongozao kwenye uhai!
D. V., Filipino
UKIMWI Nilitaka kuwashukuru sana kwa ajili ya ule mfululizo “Vita Dhidi ya Ukimwi—Je, Itashinda?” (Novemba 8, 1998) Ulikuwa wenye kuarifu sana. Nina umri wa miaka 19 na nimefundishwa mengi shuleni na nyumbani kuhusu UKIMWI na kirusi cha HIV, lakini bado nilikuwa nimetatanika. Makala hii ilinisaidia kuthamini jinsi ilivyo muhimu kuchagua mwenzi wa ndoa kwa hekima na kuishi maisha safi kiadili.
S. T., Marekani
Makala zenu zilikuwa zenye kuarifu, sahihi, na kweli. Nimeugua UKIMWI kwa zaidi ya miaka kumi. Rafiki yangu ananifunza Biblia kwa msaada wa vichapo vyenu. Asanteni kwa sababu ya kutohofu kuchapisha makala hizi.
B. W., Marekani
Singeweza kuiweka Amkeni! hii chini hadi nilipomaliza kusoma makala juu ya UKIMWI. Sijawahi kamwe kusoma habari sahihi kama hiyo juu ya UKIMWI. Na hilo ni jambo la pekee kwangu, kwa kuwa mimi ni muuguzi. Asanteni sana.
D. E., Ujerumani
Ninathamini sana makala hizo kwa sababu mwanangu aliacha njia ya Ukristo na alipoirudia alikuwa ameathiriwa sana na UKIMWI. Kwa msaada wa Yehova, sasa ana msimamo mzuri wa kiroho. Afya yake imeimarishwa na matibabu. Twajua kwamba kuna watu wengi walioambukizwa na ambao bado hawajui hivyo. Mtu yeyote anayefikiria kufunga ndoa anapaswa kuhangaikia sana jambo hili.
N. J., Marekani
Madaraja Baada tu ya Kimbunga Mitch kuharibu takriban asilimia 80 ya madaraja yote huku Honduras, tulipokea lile toleo la Novemba 8, 1998, lenye makala “Madaraja—Hali Ingekuwaje Bila Madaraja?” Sikuzote mimi na mume wangu husafiri huku, na tulijifunza mara moja jinsi madaraja yalivyo muhimu kwa kazi yetu. Tungependa kuwashukuru kwa ajili ya makala hiyo yenye kupendeza iliyofika kwa wakati unaofaa. Kama vile fungu la mwisho linavyosema, hatutayachukulia madaraja kijuu-juu tena!
C. H., Honduras