Kuutazama Ulimwengu
Matineja wa Kanada na Mungu
“Kwa kushangaza asilimia 80 ya matineja wa Kanada huamini katika Mungu,” huku “ni asilimia 15 peke yake ndio wanaohudhuria ibada za kidini kwa ukawaida,” lasema gazeti Vancouver Sun. Kwa nini kuna hali hiyo ya kutofautiana kabisa? Wengine huamua kuacha dini kwa sababu ya “uchoshi mtupu wa ibada nyingi za kidini,” na “kutopendezwa kwa vijana na mafundisho yasiyobadilika.” Gazeti hilo laongezea: “Bila shaka pia sifa ya jinsi tengenezo la kidini linavyoonekana imeharibiwa sana na vichwa vikuu vya magazeti vinavyohusu kutendwa vibaya kingono na makasisi wa Kikristo, ghasia za Makalasinga, Wayahudi wenye siasa kali na wanamgambo wa Kihindu. Kura zafunua kwamba ni asilimia 39 tu ya matineja wa Kanada walio na imani katika viongozi wa kidini, kwa kulinganishwa na asilimia 62 katika mwaka wa 1984.” Ripoti hiyo yamalizia kwa kusema: “Ama makasisi hawawakaribishi vijana kihalisi, kawaida ya misa ni yenye uhasama dhidi ya matengenezo ya kidini ama ujumbe wa kiroho hauvutii vijana wengi. Au sababu zote zilizotajwa juu zahusika.”
Kombamwiko Wenye Mwendo wa Kasi
Mtu yeyote ambaye amejaribu kuwashika kombamwiko anajua kwamba si jambo rahisi. Siri yao ni nini? Kwanza, mavuzi madogo sana yaliyo kwenye kila upande wa fumbatio lao hugundua mwendo mdogo wa hewa unaosababishwa na maadui wao na kutambua unatoka upande gani. Pia, mfumo wao wa neva unaonekana kuwa hufanya kazi kwa matokeo sana, kwa kuwa kombamwiko huhitaji tu sehemu moja kwa mia ya sekunde ili kuitikia na kukimbia. Sasa, kwa kutumia kamera zenye mwendo wa kasi, Jeffrey Camhi na wenzake kwenye Hebrew University of Jerusalem wamejifunza mengi zaidi, laripoti gazeti Berliner Morgenpost. Waliona kwamba kombamwiko wanaweza kukimbia kwa mwendo wa meta moja kwa sekunde moja na wakiwa katika mwendo huo wanaweza hata kubadili upande wanakoelekea mara 25 kwa sekunde moja. “Hatujui mnyama mwingine yeyote anayeelewa mazingira aliye na uwezo wa marudio ya hali ya juu namna hiyo ya kubadili mwendo wa mwili wake,” akasema Camhi, aliyenukuliwa katika New Scientist. “Kama si vile kombamwiko hatakiwi katika nyumba, bila shaka angependwa sana anavyostahili.”
Je, Hii Ndiyo Bakteria Kubwa Zaidi Ulimwenguni?
Heide Schulz, mwanasayansi mmoja kutoka taasisi ya Max Planck Institute for Marine Microbiology, amegundua bakteria kubwa sana kwenye masimbi ya sakafu ya bahari kando ya pwani ya Namibia, Afrika. Kiumbehai hicho kina kipenyo chenye ukubwa wa sehemu tatu kwa mia ya inchi na ni kikubwa zaidi mara 100 kuliko bakteria yoyote inayojulikana. “Ikiwa bakteria ya wastani ingetoshana na panya aliyetoka tu kuzaliwa, ile mpya ingetoshana na nyangumi-samawi,” laripoti The Times la London. Viumbehai hao, wanaoitwa Thiomargarita namibiensis, hushikana, kama mfuatano wa lulu. Kulingana na The Times, bakteria hiyo “hujikimu kwa salfaidi, zinazochanganywa na oksijeni kwa kutumia naitreti zinazopatikana kwenye maji ya bahari.”
Mto Ganges una Maiti Nyingi Sana
“Kwa karne nyingi, Wahindu wamewatumbukiza wafu wao katika mto Ganges wakiamini kwamba jambo hilo hutoa uhakikisho wa Moksha, au uhuru wa nafsi kutoka kwa duru za kuwapo katika mwili,” lasema Electronic Telegraph. “Mkondo wenye nguvu wa Mto Ganges wenye urefu wa kilometa 2,500 ulibeba mamia ya miili iliyokuwa ikioza, maadamu uliendelea kuwa wenye kina. Lakini katika miaka ambayo imepita mto huo umekuwa ukisonga polepole zaidi na kuwa na kina kifupi zaidi kwa sababu ya takataka ya viwandani na takataka nyingine zinazotupwa ndani yake.” Jambo hilo limesababisha maiti “zinaswe kwenye magugu na takataka kwa majuma kadhaa.” Katika miaka ya mwisho-mwisho ya 1980 serikali ilijaribu kutatua tatizo hilo kwa kuweka maelfu ya kasa wanaokula nyama katika Mto Ganges. Lakini mradi huo ulikomeshwa mnamo mwaka wa 1994 kwa sababu kulikuwa na maiti nyingi sana kiasi cha kulemea kasa hao, na kasa hao wenyewe walikuwa wakichukuliwa na wawindaji haramu. Katika kampeni mpya, watu wanasihiwa wawachome jamaa zao waliokufa au kuwazika kwenye changarawe kandokando ya mto huo.
Je, Hakuna Ahera Tena?
Ahera—mahali ambapo kulingana na pokeo la Katoliki nafsi za wafu za vitoto vichanga visivyobatizwa huenda—imetoweka kwenye theolojia ya Katoliki. Ijapokuwa ahera haikuwahi kuwa fundisho lisilobadilika, ilikuwa “tokeo la utabiri wa wanatheolojia wa karne ya 12” waliotaka kupata mahali “katika Ahera” kwa wale ambao hawakukusudiwa kwenda mbinguni au kwenye helo. Watu waliotiwa ndani ni “watoto wachanga waliozaliwa wasiokuwa na hatia ambao walikufa kabla ya kubatizwa” na wale “wasioamini walioishi maisha manyofu.” “Mara tu ilipobuniwa, Ahera ikachangia fungu muhimu katika fundisho lililofundishwa na kanisa,” aandika mwelezaji wa Vatikani Marco Politi, katika gazeti La Repubblica. Lakini katika katekisimu za hivi karibuni zaidi, kutia ndani katekisimu ya ulimwenguni pote iliyotangazwa wazi mwaka wa 1992, Ahera haitajwi hata kidogo. “Kwa kweli, dhana nzima ya Ahera imebadilishwa katika miongo michache iliyopita,” aeleza Politi. Wanatheolojia wengi sasa wanasema kwamba vitoto vichanga vinavyokufa bila kubatizwa huenda mbinguni moja kwa moja. Mwanatheolojia Mwitalia Pino Scabini asema: “Leo, kuna mwelekeo wa kufikiria mambo muhimu kati ya yale yaliyofunuliwa—uhai wa milele, ambao Yesu alizungumza juu yake, na ufufuo.”
Biashara ya Utekaji Nyara
“Utekaji nyara ni . . . biashara ambayo inanawiri katika sehemu kama vile, Mexico, Kolombia, Hong Kong, na Urusi,” lasema U.S.News & World Report. “Ulimwenguni pote, idadi ya waliotekwa nyara ili kupata fidia iliongezeka kuliko wakati mwingine wowote katika kila miaka mitatu iliyopita.” Idadi kubwa zaidi hutukia huko Amerika ya Latini, ambako kulikuwa na visa vya utekaji nyara 6,755 kati ya mwaka wa 1995 na 1998. Inafuatwa na Asia na Mashariki ya Mbali (617), Ulaya (271), Afrika (211), Mashariki ya Kati (118), na Amerika Kaskazini (80). Ingawa wengi wa wale waliotekwa nyara ni wafanyabiashara wa mahali hapo na wenye kumiliki mashamba, mtu yeyote—wafanyakazi wa kigeni, wafanyabiashara wanaosafiri, au watalii—aweza kuwa hatarini. Makampuni ya kimataifa sasa yananunua hati za bima za kutekwa nyara na za fidia ili kushughulikia fidia na vilevile malipo ya wataalamu-wapatanishi na washauri wa saikolojia. Watekaji nyara wamepangwa kitengenezo, wakifanya utafiti wa soko na kukabili hatari ya kukadiria bei ya watu watakaowateka nyara. Mara nyingi wao huwatendea mateka wao kwa njia inayofaa, wakitambua kwamba kufanya hivyo hupunguza uwezekano wao kutoroka na pia wanakuwa na uwezekano wa kupata faida kubwa zaidi. “Ni kisa 1 tu kati ya visa 10 vya utekaji nyara ulimwenguni pote ambapo mtu aliyetekwa nyara huuawa,” lasema gazeti hilo, lakini linatoa tahadhari hii: “Jihadhari na polisi wa kwenu. Mara nyingi wao hushirikiana na watekaji nyara.”
Mwongozo wa Kusali Mahali Katika Internet
Hivi karibuni, Church of England lilipata mahali pake katika Internet. Sehemu hiyo ina mwongozo wa jinsi ya kusali. Likisisitiza kwamba Mungu husikiliza sala zote, kanisa hilo huwasihi sana watu wawe wabunifu wanaposali. “Tumia muziki, jiwe, unyoya, ua, au mshumaa ili ukusaidie kukaza fikira,” na “tumia mkono wako. Vidole vyako vyaweza kutumiwa kukukumbusha vitu tofauti-tofauti vya kusali juu yake.” Kwa mfano, linasema kwamba kidole gumba, kwa kuwa ndicho kidole chenye nguvu zaidi, chaweza kudokeza sala kwa ajili ya mambo ambayo ni yenye uzito maishani mwako, kama vile nyumba na familia. Kidole kirefu cha kati kingeweza kukukumbusha usali juu ya “watu wenye mamlaka ulimwenguni,” na kidole kidogo zaidi kingeweza kukukumbusha juu ya “sala yako ya kibinafsi.” Likitoa maelezo juu ya ubunifu huo, The Times lasema: “Mambo yaliyomo katika Internet ni udhihirisho wa jinsi Kanisa linavyohisi taifa limependa sana mambo ya ulimwengu. Sehemu hiyo katika Internet inalinganisha nidhamu ya kusali na kufuatia kanuni za mlo, au kung’oa magugu shambani: ‘Sala fupi zinazotolewa mara nyingi, ni bora zaidi, lakini usivunjike moyo.’”
Asidi na Kuoza kwa Meno
“Watu wanapaswa kuacha kufikiri kwamba sukari peke yake ndiyo husababisha mashimo, na kuendelea kula vyakula vinavyoacha asidi midomoni mwao,” asema Mike Edgar, mmojawapo wa waandishi wa Oral Health: Diet and Other Factors. Ripoti hiyo yashauri kwamba watu wanaokunywa maji ya machungwa wakati wa kifungua-kinywa au wanaokula vyakula vyenye asidi hawapaswi kupiga meno yao mswaki kwa angalau nusu saa baada ya hapo. Kwa nini? Kwa sababu asidi iliyoko mdomoni inapoanza kuongezeka na kuzidi kiwango fulani, tabaka ya juu ya jino huanza kuwa nyororo na kupiga meno mswaki kutamomonyoa tabaka ya juu. Badala yake inapendekezwa kwamba mtu azuie asidi hiyo kwa kula vyakula vyenye protini, kama vile jibini au njugu karanga, dakika 20 baada ya kula vyakula hivyo vyenye asidi, lasema The Times la London.
Je, Wajapani Wamepata Suluhisho la Mwanasesere?
Kwa babu na nyanya wanaoishi mbali na wajukuu wao na ambao huwaona mara chache, kiwanda kimoja cha biashara huko Japani kina suluhisho: Pelekea kiwanda hicho picha ya mtoto, na katika majuma sita utapokea mwanasesere anayefanana na mtoto huyo. “Lakini mwanasesere huyo ana kitu kingine,” laripoti New Scientist. “Kifaa cha kurekodia cha kompyuta kilicho ndani ya mwanasesere huyo hurekodi sauti ya mapema ya mtoto, hivyo kikisikika kama mtoto wako. Ushikilie tu mkono wa mwanasesere huyo naye atarudia kucheza sauti ya mtoto—au chochote kile unachorekodi. Kulingana na The Nikkei Weekly, mwanasesere huyo anayegharimu dola za Marekani 400 huagizwa hasa na babu na nyanya wanaowaona wajukuu wao kwa nadra sana.”