Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 8/07 kur. 16-18
  • Kisiwa cha Krismasi—Sababu Yetu ya Kukitembelea

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kisiwa cha Krismasi—Sababu Yetu ya Kukitembelea
  • Amkeni!—2007
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Siri ya Ndege Hao Yagunduliwa
  • Sababu Yetu ya Kutembea
  • Krismasi Inamaanisha Nini Kwako?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Je! Ni Lazima Wewe Usherehekee Krismasi?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
  • Ni Nini Kilichoipata Krismasi ya Kidesturi?
    Amkeni!—1993
  • Krismasi (Noёl) Ilianza Zamani Sana
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2007
g 8/07 kur. 16-18

Kisiwa cha Krismasi—Sababu Yetu ya Kukitembelea

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FIJI

KISIWA cha Kiritimati (linatamkwa Ki-ris-masʹ, au Krismasi) ndicho kisiwa kikubwa zaidi kati ya visiwa 33 vya nchi ya Kiribati katika Bahari ya Pasifiki.a Kisiwa hicho kina ukubwa wa karibu kilomita 388 za mraba, ukubwa unaolingana na wa vile visiwa vingine 32 vikiwa pamoja. Visiwa vyote vya Kiribati vina wakazi 92,000 hivi. Kisiwa cha Krismasi kina wakazi 5,000 hivi.

Visiwa vyote vya Kiribati ni visiwa vya matumbawe isipokuwa kimoja tu. Kisiwa cha Krismasi ndicho kisiwa kikubwa zaidi cha matumbawe, si kati ya visiwa vya Kiribati tu bali ulimwenguni pote!

Kwa kuongezea, Kisiwa cha Krismasi kinajulikana kwa sababu kiko karibu na mstari wa tarehe wa kimataifa. Wakazi wake huwa wa kwanza duniani kuona siku mpya, mwaka mpya, na sikukuu nyingine za kila mwaka, kama vile kifo cha Yesu Kristo.b

Isitoshe, kisiwa hicho cha matumbawe ni mojawapo ya sehemu muhimu zaidi katika maeneo ya Tropiki ambapo ndege wa baharini huzaliana. Wakati fulani uliopita ilisemekana kwamba membe milioni 25 hivi walitua huko kwa kawaida.

Siri ya Ndege Hao Yagunduliwa

Mvumbuzi Nahodha James Cook alipofika kwenye kisiwa hicho siku moja kabla ya Krismasi mnamo 1777, hakuna mtu aliyekuwa akiishi huko. Lakini kulikuwa na ndege wengi. Cook alikiita Kisiwa cha Krismasi.c Kwa miaka mingi ni ndege tu waliojua mahali ambapo kisiwa hicho kilikuwa.

Tulipotembelea eneo hilo wakati mmoja, askari mmoja wa Kikosi cha Kutunza Wanyama-Pori alitutembeza. Alipotutembeza kwenye ufuo, membe weupe waliruka kutuelekea kana kwamba walikuwa wakitukaribisha. Walitazama kila kitu tulichofanya, huku wakiruka-ruka karibu nasi.

Hapo mbele ya ufuo kulikuwa na kundi la membe. Mamia ya maelfu ya ndege hao huja kwenye Kisiwa cha Krismasi kuzaliana. Wanapofika, wanaruka kwa kuzunguka usiku na mchana kwa majuma kadhaa huku wakipiga kelele juu ya eneo hilo wakingoja ndege wote wawasili kabla ya kushuka na kujenga viota kwenye mchanga.

Makinda ya membe huanza kusafiri juu ya bahari wakiwa na umri wa miezi mitatu hivi. Hayarudi kwenye nchi kavu hadi miaka mitano au saba inapokwisha, wanapokuwa tayari kuzaliana. Kwa miaka hiyo yote, wao hutumia muda mwingi wakiwa angani. Hawawezi kuelea majini kwa kuwa manyoya yao hayana mafuta mengi.

Tuliwaona buabua weusi wakiwa wameketi juu ya viota vyao, wakiwa na makinda yao na mayai ambayo bado hayajaanguliwa. Ingawa ndege hawa wa baharini hujenga viota kwa ajili ya makinda yao, membe weupe hawajengi. Membe hao hutaga mayai juu ya matawi. Makinda huanguliwa yakiwa na miguu yenye kucha zinazofaa kujishikilia kwenye tawi. Tulifurahishwa mara moja tulipoona makinda hayo. Wakiwa na manyoya meupe na mdomo mweusi, wazazi wa makinda hao wanavutia sana.

Tulipoendelea kutembea, ndege anayeitwa Christmas shearwater alitukazia macho huku akiwa amekalia yai lake. Kisiwa cha Krismasi kina ndege wengi zaidi ulimwenguni wanaoitwa wedge-tailed shearwater. Na hilo ndilo eneo pekee linalojulikana ambapo aina mbalimbali za koikoi huja kuzaliana. Ndege wengine wengi ambao huzaliana huko wanatia ndani ndege wa tropiki anayeitwa red-tail, polisi bawajeusi, polisi kahawia, polisi anayeitwa red-foot, buabua kahawia, na frigate.

Ndege aina ya frigate waliruka juu yetu, wakijipindapinda hewani, wakiiba samaki wa ndege wengine hewani, na waking’ang’ania vipande vidogo-vidogo vilivyotupwa na wavuvi. Ndege hao wa frigate hulazimika kujifunza ustadi huo kwani hawatui juu ya maji. Kama vile membe, manyoya yao hushika maji kwa urahisi, nao hawawezi kupaa kwa urahisi kwa sababu ya mabawa yao makubwa.

Tuligundua kwamba ndege mdogo mwenye rangi ya kahawia tuliyekuwa tumemwona anaitwa kiluwiluwi-dhahabu wa Pasifiki. Huyo ni mmoja kati ya ndege wengi wahamaji ambao hutua kwenye Kisiwa cha Krismasi ili kula na kujikinga na majira ya baridi kali baada ya kusafiri kwa muda mrefu kutoka kwenye eneo la kuzaliana lililoko kilomita nyingi sana, juu ya Mzingo wa Aktiki. Ingawa eneo hilo liko kilomita 2,100 hivi kusini ya Honolulu, Hawaii, ndege hao hufaulu kufika huko kutokana na uwezo wa ajabu wa kutambua maeneo.

Sababu Yetu ya Kutembea

Sababu yetu ya kutembelea Kisiwa cha Krismasi mara nyingi, haikuwa kutazama ndege bali kuwatembelea Mashahidi wa Yehova wa huko na kushirikiana nao katika mikutano na mahubiri. Mashahidi hao huwa na hali ngumu kwa sababu eneo hilo liko mbali na maeneo mengine. Kwa mfano, miaka fulani iliyopita ndugu mmoja alipokufa ghafula, mke wake alijipa ujasiri na kutoa hotuba ya mazishi kwa sababu hakukuwa na mtu mwingine wa kufanya hivyo. Alitaka watu wengi waliohudhuria wasikie kuhusu tumaini la Biblia kwa ajili ya wafu.—Yohana 11:25; Matendo 24:15.

Hakuna vitabu vingi vinavyotegemea Biblia katika lugha ya kienyeji isipokuwa tu tafsiri tatu nzuri za Biblia. Hata hivyo, Mashahidi wa Yehova huchapisha gazeti la Mnara wa Mlinzi mara moja kwa mwezi katika lugha ya Gilbertese pamoja na vichapo vingine vya Biblia. Watu wengi hushangazwa kusikia hilo kwani lugha hiyo inazungumzwa na watu wasiozidi 100,000 ulimwenguni pote. Vichapo hivyo vinavyotegemea Biblia huwawezesha Mashahidi hao wachache kufanya mikutano yao ya ibada kwa kawaida na kutimiza utume wao waliopewa na Yesu wa kuhubiri habari njema ya Ufalme wa Mungu.—Mathayo 24:14; Waebrania 10:24, 25.

Wageni huona ikiwa vigumu kusafiri kwenye kisiwa hicho. Hata hivyo, unaweza kusafiri kwa gari kutoka London hadi Poland kupitia Tennessee katika muda wa saa tatu tu! Hilo linawezekanaje? Banana, London, Paris, Poland, Tennessee, na Tabwakea ni majina yenye kupendeza ya vijiji katika kisiwa hicho, yakionyesha mahali ambapo wahamiaji fulani wa kwanza walikuwa wametoka.

Wakati mmoja tulipotembelea kisiwa hicho, daktari mmoja alitukaribisha tusafiri pamoja naye kwenda Poland, na hivyo tukaweza kuhubiri huko kwa mara ya kwanza. Kwa kuwa tungekaa huko Poland kwa muda wa saa mbili tu, tulikimbia kutoka nyumba moja hadi nyingine ili tuweze kuhubiri nyumba zote. Kila mtu tuliyezungumza naye alisikiliza ujumbe wetu wa Biblia kwa makini na kukubali vichapo. Walistaajabu kuona kwamba vichapo hivyo vilikuwa katika lugha yao.

Tunawapenda sana watu walio kwenye kisiwa hicho cha Krismasi kilicho mbali sana. Pia, tunavutiwa sana na ndege maridadi wanaotua huko. Ingawa zamani Nahodha Cook alihisi kwamba kisiwa hicho kinawafaa tu ndege, leo watu wengi sana hawakubaliani na maoni yake. Kama tu ndege hao, hayo ndiyo makao yao.

[Maelezo ya Chini]

a Hapo awali Visiwa vya Kiribati viliitwa Visiwa vya Gilbert. Sasa Kiribati inatia ndani visiwa 16 vya Gilbert, vile vya Phoenix, vya Line, na Banaba (Kisiwa cha Bahari).

b Kwa kutii amri ya Yesu, Mashahidi wa Yehova hukumbuka kifo chake mara moja kwa mwaka, siku inayolingana na ile aliyokufa.—Luka 22:19.

c Kuna kisiwa kingine kinachoitwa Krismasi kwenye Bahari ya Hindi.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Kisiwa cha Krismasi

Banana

Tabwakea

London

Paris

Poland

Mstari wa tarehe wa kimataifa

[Picha katika ukurasa wa 16]

Ndege wanaoitwa “frigate”

[Hisani]

GaryKramer.net

[Picha katika ukurasa wa 17]

Membe mweupe

[Hisani]

©Doug Perrine/ SeaPics.com

[Picha katika ukurasa wa 17]

Polisi kahawia

[Hisani]

Valerie & Ron Taylor/ ardea.com

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kuhubiri na Mashahidi wa huko

[Picha katika ukurasa wa 18 zimeandaliwa na]

GaryKramer.net

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki