Maendeleo na Ukuzi Wao wa Kisasa
Historia ya kisasa ya Mashahidi wa Yehova ilianza zaidi kidogo ya miaka 100 iliyopita. Mapema miaka ya kuanzia 1870, kikundi kidogo cha kujifunza Biblia kilianza katika Jiji la Allegheny Pennsylvania, U.S.A., ambalo sasa ni sehemu ya Pittsburgh. Charles Taze Russell ndiye aliyekuwa mwanzilishi mkuu wa kikundi hicho. Julai 1879, toleo la kwanza la gazeti Zion’s Watch Tower and Herald of Christ’s Presence lilitokea. Kufikia 1880 makundi mengi yalikuwa yameenea kutokana na kikundi hicho kimoja cha kujifunza Biblia mpaka kwenye majimbo ya jirani. Katika 1881 shirika la Zion’s Watch Tower Tract Society lilianzishwa, na katika 1884 likaandikishwa kisheria kuwa shirika, Russell akiwa msimamizi. Baadaye jina la Sosaiti hiyo lilibadilishwa likawa Watch Tower Bible and Tract Society. Wengi walikuwa wakitoa ushahidi nyumba kwa nyumba wakitolea watu vitabu vya Biblia. Watu 50 walikuwa wakifanya hivyo wakati wote katika 1888—sasa hesabu ulimwenguni pote ni zaidi ya 530,000.
Kufikia 1909 kazi hiyo ilikuwa imeenea katika mataifa yote, na makao makuu ya Sosaiti yalihamishwa yakawa yalipo sasa katika Brooklyn, New York. Mahubiri yaliyochapwa yalikuwa yakiandikwa katika magazeti mbalimbali, na kufikia 1913 yakaandikwa katika lugha nne katika magazeti 3,000 katika United States, Kanada, na Ulaya. Vitabu, vijitabu, na trakti vilikuwa vimetawanywa kwa mamia ya mamilioni.
Katika 1912 kazi ya kutengeneza Photo-Drama of Creation (mwigizo kupitia picha juu ya uumbaji) ilianza. Ilisimulia habari tangu kuumbwa dunia mpaka mwisho wa Utawala wa Miaka Elfu wa Kristo. Maonyesho yalianza katika 1914, watu 35,000 wakawa wakiiona kila siku. Hiyo ndiyo sinema iliyotangulia kutayarishwa kabla ya sinema nyingine zote za picha zenye mwendo na sauti.
MWAKA 1914
Wakati wa maana sana ulikuwa ukikaribia. Katika 1876 mwanafunzi wa Biblia Charles Taze Russell alichanga makala “Nyakati za Mataifa: Zitakwisha Lini?” katika Bible Examiner, lililotangazwa katika Brooklyn, New York. Lilisema hivi katika ukurasa 27 wa toleo lalo la Oktoba, “Zile nyakati saba za mataifa zitamalizika A.D. 1914.” Nyakati za Mataifa ndicho kipindi ambacho Yesu alikitaja kuwa “nyakati zilizowekwa za mataifa.” (Luka 21:24, New World Translation) Si mambo yote yaliyotazamiwa kutukia katika 1914 yaliyotukia, lakini mwaka huo ulitia alama mwisho wa Nyakati za Mataifa na ulikuwa mwaka wenye maana ya pekee. Wanahistoria wengi na wafafanuzi hukubaliana kwamba 1914 ulikuwa kipindi cha badiliko kubwa katika historia ya kibinadamu. Manukuu yafuatayo yaonyesha hilo:
“Mwaka wa mwisho ‘kuwa wa kawaida’ kamili katika historia ulikuwa 1913, mwaka uliotangulia mwanzo wa Vita ya Ulimwengu 1.” —Safu ya mhariri katika Times-Herald, Washington, D.C., Machi 13, 1949.
“Tangu 1914, kila mtu anayejua mitindo iliyo katika ulimwengu amesumbuliwa sana na ule ambao umeonekana kuwa kama mwendo wenye msiba na ulioamuliwa kimbele kuelekea msiba mkubwa zaidi. Watu wengi wenye kufikiri kwa uzito wamefikia kuhisi kwamba hakuna linaloweza kufanywa kuzuia kutumbukia katika uharibifu.”—Bertrand Russell, The New York Times Magazine, Septemba 27, 1953.
“Ulimwengu mzima uliharibika kweli kweli kufikia Vita ya Ulimwengu 1 na tungali hatujui ni kwa nini. Kabla ya wakati huo, wanadamu walifikiri hali bora zinazowaziwa zilikuwa zikitazamiwa. Kulikuwako amani na ufanisi. Ndipo kila kitu kikaharibika kweli kweli. Tangu wakati huo tumekuwa tukiishi katika hali yenye mashaka-mashaka . . . Watu wengi zaidi wameuawa katika karne hii kuliko katika historia yote.”—Dakt. Walker Percy, American Medical News, Novemba 21, 1977.
Miaka zaidi ya 50 baada ya 1914, Konrad Adenauer waziri wa serikali Mjerumani aliandika hivi: “Usalama na utulivu umetoweka katika maisha za watu tangu mwaka 1914.”—The West Parker, Cleveland, Ohio, Januari 20, 1966.
Msimamizi wa kwanza wa Sosaiti, C. T. Russell, alikufa katika 1916 na mwaka uliofuata Joseph F. Rutherford akawa mwandamizi wake. Mabadiliko mengi yalitukia. Gazeti-jenzi la Mnara wa Mlinzi, lililoitwa The Golden Age, lilianzishwa. (Sasa laitwa Amkeni!, likiwa na mwenezo wa nakala 12,980,000 katika lugha zaidi ya 60.) Mkazo mkubwa zaidi uliwekwa juu ya kutoa ushahidi mlango kwa mlango. Ili wajitofautishe na madhehebu mengi ya Jumuiya ya Wakristo, Wakristo hao walilikubali kwa moyo jina Mashahidi wa Yehova katika 1931. Msingi wa jina hilo ni Isaya 43:10-12.
Redio ilitumiwa sana miaka ya kuanzia 1920 na 1930. Kufikia 1933 Sosaiti ilikuwa ikitumia vituo vya redio 403 kusambaza mihadhara ya habari za Biblia. Baadaye, matumizi ya redio yaliachwa na badala yake Mashahidi wakaanza ziara nyingi za nyumba kwa nyumba wakiwa na santuri zenye kuchukulika kwa mikono na hotuba za Biblia zilizorekodiwa. Mafunzo ya Biblia nyumbani yalianzishwa kwa watu wenye kupendezwa.
USHINDI MWINGI WA MAHAKAMANI
Wakati wa miaka ya kuanzia na 1930 na 1940, Mashahidi wengi walikamatwa kwa kufanya kazi hiyo na kesi mahakamani zilijadiliwa kwa kupigania kuhifadhiwa kwa uhuru wa kusema, wa vyombo vya kusambaza habari, wa kukusanyika, na wa kuabudu. Katika United States, rufani kutoka mahakama ndogo zilifanya Mashahidi washinde kesi 43 mbele ya Mahakama Kuu Zaidi ya United States. Hali moja na hiyo, mahakama kuu katika mabara mengine zimefanya maamuzi mazuri yakiunga mkono Mashahidi. Kwa habari ya ushindi huo mwingi wa mahakamani, Profesa C. S. Braden, alisema hivi juu ya Mashahidi katika kitabu chake These Also Believe: “Wametolea demokrasia utumishi mkubwa kwa kupigania hifadhi ya haki zao za uraia, maana katika harakati yao wamefanya kazi kubwa ya kupatia kila kikundi cha walio wachache katika Amerika haki hizo.”
PROGRAMU ZA PEKEE ZA MAZOEZI
J. F. Rutherford alikufa katika 1942 na N.H. Knorr akawa mwandamizi katika usimamizi. Mazoezi ya jitihada iliyounganishwa pamoja yakaanza. Katika 1943 shule ya pekee ya kuzoeza wamisionari, inayoitwa Watchtower Bible School of Gilead, ilianzishwa. Tangu wakati huo na kuendelea, wenye kuhitimu shule hiyo wametumwa kwenye mabara zaidi ya 140 ya dunia. Makundi mapya yametokea katika nchi ambako hakukuwako hata moja, na matawi yamesimamishwa katika mataifa yote, sasa yakiwa zaidi ya 90. Pindi kwa pindi, mitaala ya pekee imefanywa ya kuzoeza wazee wa makundi, wafanya kazi wa kujitolea kwenye matawi, na wale wanaoshiriki wakati wote (wakiwa mapainia) katika kazi ya kutoa ushahidi.
N. H. Knorr alikufa katika 1977. Mojawapo mabadiliko ya mwisho ya kitengenezo ambayo alishiriki kabla ya kufa kwake ni upanuzi wa Baraza Linaloongoza, lililo katika makao makuu ya ulimwengu katika Brooklyn. Katika 1976 madaraka ya usimamizi yaligawanywa na kupewa kwa halmashauri mbalimbali ambazo zafanyizwa na washiriki wa Baraza Linaloongoza. Kila mmoja wa washiriki walo 12 (katika 1989) amekuwa akitumia wakati wake wote akifanya kazi ya kutoa ushahidi kwa miaka zaidi ya 45.
VIFAA VYA KUPIGIA CHAPA VYAPANUKA
Historia ya Mashahidi wa Yehova katika nyakati za kisasa imejaa matukio makubwa sana. Tangu kile kikundi kimoja kidogo cha kujifunza Biblia katika Pennsylvania katika 1870, kufikia mwaka 1990 Mashahidi walikuwa wameongezeka kuwa makundi zaidi ya 63,000 ulimwenguni pote. Hapo kwanza vitabu vyote vilichapishwa kwa kutumia kampuni za kibiashara; kisha katika 1920, vitabu fulani vya Mashahidi vikachapwa katika majengo ya kiwanda cha kukodi. Lakini tangu 1927 na kuendelea, vitabu vingi zaidi vilianza kuchapwa katika jengo la kiwanda lenye orofa nane katika Brooklyn, New York, likiwa ni mali ya Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc. Sasa limepanuliwa kuwa majengo saba ya kiwanda na mfumo mkubwa wa ofisi. Kuna majengo mengine karibu katika Brooklyn yaliyo makao ya wafanya kazi wapatao 3,000 wanaohitajiwa ili kuendesha vifaa vya kuchapia. Kuongezea hilo, mwunganisho wa mashamba na kiwanda wenye wafanya kazi 1,000 hivi waendeshwa karibu na Wallkill katika wilaya iliyo nje ya New York. Hushughulikia kuchapa magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! na hulima chakula cha kulisha wafanya kazi wote 4,000 wa kujitolea. Kila mfanya kazi wa kujitolea hupokea posho dogo la kila mwezi ili kulipia gharama ndogo.
MIKUSANYIKO YA MATAIFA YOTE
Katika 1893 mkusanyiko mkubwa wa kwanza ulifanywa katika Chicago, Illinois, U.S.A. Ulihudhuriwa na watu 360, na wapya 70 wakabatizwa. Mkusanyiko mmoja mkubwa wa mwisho wa mataifa yote ulifanywa katika Jiji la New York katika 1958. Ulitumia uwanja wa Yankee Stadium na ule wa Polo Grounds uliokuwako wakati huo. Kilele cha hudhurio kilikuwa 253,922; wapya waliobatizwa wakawa 7,136. Tangu wakati huo makusanyiko ya mataifa yote imefanywa ikiwa mfululizo wa mikusanyiko katika nchi nyingi nyingi. Sasa mfululizo wa mikusanyiko ya mataifa yote huhusisha mikusanyiko yapatayo 1,000 katika nchi zaidi ya 80.
[Blabu katika ukurasa 6]
Sinema za mapema
[Blabu katika ukurasa 7]
Kipindi cha badiliko katika historia ya kibinadamu
[Blabu katika ukurasa wa 8]
Utumishi wenye kutokeza wa kuleta uhuru wa kiraia
[Picha katika ukurasa 6]
“Mnara wa Mlinzi,” kutoka nakala 6,000 katika lugha moja kufikia zaidi ya 15,290,000 katika lugha zaidi ya 111 zenye sauti
[Picha katika ukurasa wa 10]
Matbaa katika Wallkill, New York,
. . . na katika Brooklyn, New York