Maendeleo Yao na Ukuzi Wao Leo
HISTORIA ya kisasa ya Mashahidi wa Yehova ilianza zaidi ya miaka mia moja iliyopita. Mapema miaka ya kuanzia 1870, kikundi kidogo cha kujifunza Biblia ambacho hakikujulikana sana kilianza katika Allegheny, Pennsylvania, Marekani, ambayo sasa ni sehemu ya Pittsburgh. Charles Taze Russell ndiye aliyekuwa mwanzilishi wa kikundi hicho. Mwezi wa Julai 1879, toleo la kwanza la gazeti Zion’s Watch Tower and Herald of Christ’s Presence lilitokea. Kufikia mwaka wa 1880, makundi mengi yalikuwa yameenea kutokana na kikundi hicho kimoja cha kujifunza Biblia mpaka kwenye majimbo jirani. Katika mwaka wa 1881 shirika la Zion’s Watch Tower Tract Society lilianzishwa, na katika mwaka wa 1884 likaandikishwa kisheria kuwa shirika, Russell akiwa msimamizi. Baadaye jina la Shirika hilo lilibadilishwa likawa Watch Tower Bible and Tract Society. Wengi walikuwa wakitoa ushahidi nyumba kwa nyumba wakitolea watu vitabu vya Biblia. Watu 50 walikuwa wakifanya hivyo wakati wote mwaka wa 1888—sasa hesabu ya wastani ulimwenguni pote ni 700,000 hivi.
Kufikia mwaka wa 1909 kazi hiyo ilikuwa imeenea katika mataifa mengi, na makao makuu ya Sosaiti yalihamishwa hadi Brooklyn, New York. Mahubiri yaliyochapwa yalikuwa yakiandikwa katika magazeti mbalimbali, na kufikia mwaka wa 1913 yakaandikwa katika lugha nne katika magazeti 3,000 huko Marekani, Kanada, na Ulaya. Vitabu, vijitabu, na trakti vilikuwa vimegawanywa kwa mamia ya mamilioni.
Mwaka wa 1912, kazi ya kutengeneza “Photo-Drama of Creation” (mwigizo kupitia picha juu ya uumbaji) ilianza. Ilisimulia habari tangu kuumbwa kwa dunia mpaka mwisho wa Utawala wa Miaka Elfu wa Kristo. Maonyesho yalianza mwaka wa 1914, na watu 35,000 waliiona kila siku. Hiyo ndiyo sinema iliyotangulia kutayarishwa kabla ya sinema nyingine zote za picha zenye mwendo na sauti.
MWAKA WA 1914
Wakati wa maana sana ulikuwa ukikaribia. Mwaka wa 1876 mwanafunzi wa Biblia Charles Taze Russell alichanga makala “Nyakati za Mataifa: Zinakwisha Lini?” katika Bible Examiner, iliyotangazwa katika Brooklyn, New York. Ilisema hivi katika ukurasa wa 27 wa toleo lake la Oktoba, “Zile nyakati saba za mataifa zitamalizika A.D. 1914.” Nyakati za Mataifa ndicho kipindi ambacho tafsiri nyingine ya Biblia inakiita “nyakati zilizowekwa rasmi za mataifa.” (Luka 21:24) Si mambo yote yaliyotazamiwa kutukia mwaka wa 1914 yaliyotukia, lakini mwaka huo ulionyesha mwisho wa Nyakati za Mataifa na ulikuwa mwaka wenye umuhimu wa kipekee. Wanahistoria wengi na wafafanuzi hukubaliana kwamba 1914 ulikuwa kipindi cha badiliko kubwa katika historia ya kibinadamu. Manukuu yafuatayo yaonyesha hilo:
“Mwaka wa mwisho ‘kuwa wa kawaida’ kabisa katika historia ulikuwa 1913, mwaka uliotangulia mwanzo wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza.”—Safu ya mhariri katika Times-Herald, Washington, D.C., Machi 13, 1949.
“Wanahistoria wanaendelea kukiona kipindi cha miaka 75 tangu mwaka wa 1914 hadi 1989, ambacho kilihusisha vita viwili vya ulimwengu na ile vita baridi, kuwa kipindi kimoja maalumu, kipindi cha wakati ambapo mataifa mengi ya ulimwengu yalikuwa yakipigana vita, yakipata nafuu kutokana na madhara ya vita au yakijitayarisha kupigana vita.”—The New York Times, Mei 7, 1995.
“Ulimwengu mzima uliharibika kweli kweli wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza na tungali hatujui ni kwa nini. Kabla ya wakati huo, wanadamu walifikiri hali bora zinazowaziwa zilikuwa karibu. Kulikuwako amani na ufanisi. Ndipo kila kitu kikaharibika kweli kweli. Tangu wakati huo tumekuwa tukiishi katika hali yenye mashaka-mashaka . . . Watu wengi zaidi wameuawa katika karne hii kuliko katika historia yote.”—Dakt. Walker Percy, American Medical News, Novemba 21, 1977.
Miaka zaidi ya 50 baada ya mwaka wa 1914, Konrad Adenauer mwanasiasa mweledi Mjerumani aliandika hivi: “Usalama na utulivu umetoweka katika maisha za watu tangu mwaka wa 1914.”—The West Parker, Cleveland, Ohio, Januari 20, 1966.
Msimamizi wa kwanza wa Sosaiti, C. T. Russell, alikufa mwaka wa 1916 na mwaka uliofuata Joseph F. Rutherford akawa mwandamizi wake. Mabadiliko mengi yalitukia. Gazeti-jenzi la Mnara wa Mlinzi, lililoitwa The Golden Age, lilianzishwa. (Sasa laitwa Amkeni!, likiwa na mwenezo wa nakala zaidi ya 20,000,000 katika lugha zaidi ya 80.) Mkazo mkubwa zaidi uliwekwa juu ya kutoa ushahidi mlango kwa mlango. Ili wajitofautishe na madhehebu mengi ya Jumuiya ya Wakristo, mwaka wa 1931, Wakristo hao walilikubali kwa moyo jina Mashahidi wa Yehova. Msingi wa jina hilo ni Isaya 43:10-12, NW.
Redio ilitumiwa sana miaka ya kuanzia 1920 na 1930. Kufikia mwaka wa 1933 Sosaiti ilikuwa ikitumia vituo vya redio 403 kusambaza mihadhara ya habari za Biblia. Baadaye, matumizi ya redio yaliachwa na badala yake Mashahidi wakaanza ziara nyingi za nyumba kwa nyumba wakiwa na santuri zenye kuchukulika kwa mikono na hotuba za Biblia zilizorekodiwa. Mafunzo ya Biblia nyumbani yalianzishwa na mtu yeyote aliyependezwa na kweli ya Biblia.
USHINDI MWINGI WA MAHAKAMANI
Wakati wa miaka ya kuanzia 1930 na 1940, Mashahidi wengi walikamatwa kwa kufanya kazi hiyo, na kesi mahakamani zilijadiliwa kwa kupigania kuhifadhiwa kwa uhuru wa kusema, wa vyombo vya kusambaza habari, wa kukusanyika, na wa kuabudu. Nchini Marekani, rufani kutoka mahakama ndogo zilifanya Mashahidi washinde kesi 43 mbele ya Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani. Hali moja na hiyo, mahakama kuu katika nchi nyingine zimefanya maamuzi mazuri yakiunga mkono Mashahidi. Kwa habari ya ushindi huo mwingi wa mahakamani, Profesa C. S. Braden, alisema hivi juu ya Mashahidi katika kitabu chake These Also Believe: “Wametolea demokrasia utumishi mkubwa kwa kupigania hifadhi ya haki zao za uraia, maana katika harakati yao wamefanya kazi kubwa ya kupatia kila kikundi cha walio wachache katika Marekani haki hizo.”
PROGRAMU ZA PEKEE ZA MAZOEZI
J. F. Rutherford alikufa mwaka wa 1942 na N. H. Knorr akawa mwandamizi katika usimamizi. Mazoezi ya jitihada ya pamoja yakaanza. Mwaka wa 1943, shule ya pekee ya kuzoeza wamishonari, inayoitwa Shule ya Biblia ya Gileadi ya Watchtower, ilianzishwa. Tangu wakati huo na kuendelea, wenye kuhitimu shule hiyo wametumwa katika nchi nyingi duniani kote. Makutaniko mapya yametokea katika nchi ambako hakukuwako hata moja, na ofisi za tawi zilizoanzishwa duniani sasa ni zaidi ya 100. Pindi kwa pindi, mitalaa ya pekee imefanywa ya kuzoeza wazee wa makutaniko, wafanyakazi wa kujitolea kwenye ofisi za tawi, na wale wanaoshiriki wakati wote (wakiwa mapainia) katika kazi ya kutoa ushahidi. Idadi fulani ya mitalaa ya kutoa mazoezi maalumu imefanywa kwenye kituo cha elimu kinachoendeshwa huko Patterson, New York.
N. H. Knorr alikufa mwaka wa 1977. Mojawapo mabadiliko ya mwisho ya kitengenezo ambayo alishiriki kabla ya kufa kwake ni upanuzi wa Baraza Linaloongoza, lililo katika makao makuu ya ulimwengu katika Brooklyn. Mwaka wa 1976 madaraka ya usimamizi yaligawanywa na kupewa kwa halmashauri mbalimbali ambazo zafanyizwa na washiriki wa Baraza Linaloongoza, ambao wote wana miongo mingi ya uzoefu wakiwa wahudumu.
VIFAA VYA KUPIGIA CHAPA VYAPANUKA
Historia ya Mashahidi wa Yehova katika nyakati za kisasa imejaa matukio makubwa sana. Tangu kile kikundi kimoja kidogo cha kujifunza Biblia katika Pennsylvania mwaka wa 1870, kufikia mwaka wa 2000 Mashahidi walikuwa wameongezeka kuwa makutaniko yapatayo 90,000 ulimwenguni pote. Hapo kwanza vitabu vyote vilichapishwa kwa kutumia kampuni za kibiashara; kisha mwaka wa 1920, Mashahidi walichapa vichapo fulani katika majengo ya kiwanda ya kukodi. Lakini tangu mwaka wa 1927 na kuendelea, vitabu vingi zaidi vilichapwa katika jengo la kiwanda lenye orofa nane katika Brooklyn, New York, likiwa ni mali ya Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc. Sasa kazi hiyo imepanuliwa kufika katika majengo mengine ya viwanda na ofisi kubwa. Kuna majengo zaidi karibu na hapo katika Brooklyn yaliyo makao ya wahudumu wanaojitolea kuendesha vifaa vya kuchapia. Kuongezea hilo, mwunganisho wa mashamba na mahali pa matbaa zinaendeshwa karibu na Wallkill, katika wilaya iliyo nje ya New York. Hushughulikia kuchapa magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! na huzalisha baadhi ya chakula cha kulisha wahudumu wanaotumikia katika sehemu mbalimbali. Kila mfanyakazi wa kujitolea hupokea rudishio dogo la gharama kila mwezi ili kulipia gharama ndogo-ndogo.
MIKUSANYIKO YA KIMATAIFA
Mwaka wa 1893, mkusanyiko mkubwa wa kwanza ulifanywa katika Chicago, Illinois, Marekani. Ulihudhuriwa na watu 360, na wapya 70 wakabatizwa. Mkusanyiko mmoja mkubwa wa mwisho wa kimataifa ulifanywa katika New York City mwaka wa 1958. Ulitumia uwanja wa Yankee Stadium na ule wa Polo Grounds uliokuwako wakati huo. Kilele cha hudhurio kilikuwa 253,922; wapya waliobatizwa wakawa 7,136. Tangu wakati huo mikusanyiko ya kimataifa hufanywa mfululizo katika nchi nyingi. Kwa jumla, mifululizo hiyo huenda ikahusisha mikusanyiko ipatayo elfu moja katika nchi mbalimbali duniani.
[Blabu katika ukurasa wa 8]
Utumishi wenye kutokeza wa kuleta uhuru wa kiraia
[Picha katika ukurasa wa 6]
“Mnara wa Mlinzi,” kutoka nakala 6,000 katika lugha moja kufikia nakala zaidi ya 22,000,000 katika lugha zaidi ya 132
[Picha kaitika ukurasa wa 7]
Kipindi cha badiliko katika historia ya kibinadamu
[Picha kaitka ukurasa wa 10]