Appendix
Mashahidi wa Yehova—Tatizo la Upasuaji/la Kiadili
Imechapwa upya kwa ruhusa ya American Medical Association kutoka The Journal of the American Medical Association (JAMA), Novemba 27, 1981, Buku 246, Na. 21, kurasa 2471, 2472. Copyright 1981, American Medical Association.
Matabibu wanakabili tatizo la pekee katika kutibu Mashahidi wa Yehova. Washiriki wa imani hii wana masadikisho ya kidini yenye kina dhidi ya kupokea damu nzima-nzima kutoka kwa mtu mwingine aliye na damu inayofanana na yake au yake mwenyewe, RBCs [chembe nyekundu za damu], WBCs [chembe nyeupe za damu], au visahani-damu. Wengi wataruhusu utumizi wa kifaa cha kusaidia moyo na mapafu (non-blood-prime), dayalisisi, au kingine kama hicho ikiwa mzunguko wa damu wa nje ya mwili haukatizwi. Wafanya kazi wa kitiba hawapaswi kuhangaikia kupasishwa daraka, kwa maana Mashahidi watachukua hatua za kutosha za kisheria kuwaondolea kupasishwa daraka kwa habari ya katao lao la damu baada ya kuarifiwa. Wao huruhusu umajimaji usio damu badala ya damu yenyewe. Kwa kutumia hizo na mbinu nyingine za uangalifu sana, matatibu wanafanya upasuaji mkubwa wa aina zote juu ya wagonjwa Mashahidi walio watu wazima na watoto wadogo. Hivyo kimesitawishwa kiwango cha kufuatwa kwa ajili ya wagonjwa hao kinachopatana na kanuni ya kutibu “mwanadamu mzima.” (JAMA 1981; 246:2471-2472)
MATABIBU hukabili tatizo lenye kuongezeka ambalo ni suala kubwa la kiafya. Kuna Mashahidi zaidi ya nusu milioni katika United States wasioruhusu kutiwa damu mishipani. Hesabu ya Mashahidi na wale wanaoshirikiana nao inaongezeka. Ijapokuwa hapo kwanza, matabibu wengi na wakuu wa hospitali waliona kukataa kutiwa damu mishipani kuwa tatizo la kisheria na walitafuta mamlaka ya mahakama ili waendelee kama vile walivyoamini kuwa inafaa kitiba, fasihi za kitiba za karibuni hufunua kwamba badiliko kubwa la maoni linatukia. Huenda hili ni tokeo la ujuzi zaidi wa kupasua wagonjwa walio na viwango vya chini sana vya hemoglobini na huenda pia laonyesha hali yenye kuongezeka ya kuijua kanuni ya kisheria ya idhini baada ya kuarifiwa.
Sasa, hesabu kubwa ya visa vya upasuaji wa kujichagulia na visa vya majeraha zinazohusu Mashahidi walio watu wazima na watoto wadogo pia zinashughulikiwa bila kutiwa damu mishipani. Hivi majuzi, wawakilishi wa Mashahidi wa Yehova walikutana na wafanya kazi wa upasuaji na wasimamizi kwenye baadhi ya vitovu vikubwa zaidi vya kitiba nchini. Mikutano hiyo ilisaidia kuendeleza uelewevu na ikasaidia kutatua masuala juu ya kuokoa damu, mapandikizo ya viungo, na kuepuka mapambano ya kitiba/kisheria.
MSIMAMO WA MASHAHIDI JUU YA UTIBABU
Mashahidi wa Yehova huruhusu kutibiwa na kupasuliwa. Kwa kweli, baadhi yao ni matabibu, hata madaktari wapasuaji. Lakini Mashahidi ni watu wenye kufuata dini sana ambao huamini kwamba utiaji-damu mishipani unakatazwa kwao na vifungu vya Biblia kama vile: “Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile.” (Mwanzo 9:3-4); ‘[Lazima nyinyi] mmwage damu yake, na kuifunika mchanga.’ (Walawi 17:13-14); na “wajiepushe na . . . uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu.” (Matendo 15:19-21).1
Ingawa mistari hii haikusemwa kwa semi za kitiba, Mashahidi huiona kuwa hairuhusu kutiwa mishipani damu nzima, RBCs, na plazima, pamoja na WBC na visahani-damu. Hata hivyo, uelewevu wa kidini wa Mashahidi haukatazi kabisa kabisa utumizi wa sehemu kama vile albyumini, globyulini za kinga, na mitayarisho ya hemofiliaki; kila Shahidi lazima aamue kama aweza kupokea hivi.2
Mashahidi huamini kwamba damu iliyoondolewa mwilini yapaswa kumwagwa, kwa hiyo hawaruhusu kutiwa mishipani damu yao wenyewe iliyotangulia kuwekwa. Mbinu za kukusanya damu au mchanganyo wa chembe-damu na umajimaji unaohusu kuweka damu akiba wakati wa upasuaji wanazikataa. Hata hivyo, Mashahidi wengi hurusu utumizi wa kifaa cha dayalisisi na kile cha kusaidia moyo na mapafu (non-blood-prime) pamoja na kuokoa damu wakati wa upasuaji ambapo mzunguko wa damu wa nje haukatizwi; tabibu apaswa kushauriana na mgonjwa aone dhamiri yake inamwogozaje.2
Mashahidi hawahisi kwamba Biblia inatoa maelezo ya moja kwa moja juu ya kupandikizwa viungo; kwa sababu hiyo, lazima maamuzi yafanywe na Shahidi mwenyewe kwa habari ya konea, figo, au mapandikizo mengine ya tishu.
UPASUAJI MKUBWA WAWEZEKANA
Ijapokuwa mara nyingi madaktari wapasuaji wamekataa kutibu Mashahidi kwa sababu msimamo wao juu ya kutumia damu ulionekana kuwazuia kufanya chochote, matabibu wengi wamechagua sasa kuona hali hiyo kuwa tatizo moja linalowadai kutumia ustadi wao. Kwa kuwa Mashahidi hawakatai umajimaji wa koloidi au kristaloidi utumiwe badala ya damu, wala kuchoma kwa umeme, hypotensive anesthesia,3 (kushusha sana kanieneo ya damu kwa kutumia nusukaputi), au kiwango cha chini sana cha hali-joto, njia hizo zimekwisha kutumiwa kwa mafanikio. Matumizi ya sasa na ya wakati ujao ya hetastarch,4 viasi vikubwa vya deksitrani ya chuma vikiingizwa mishipani,5,6 na ‘sonik-skapeli’7 yaelekea kufanikiwa na hayakataliki kidini. Pia, ikiwa kibadala cha damu kinachoitwa Fluorini (Fluosol-DA) kilichositawishwa karibuni kitathibitika kuwa salama na chenye mafanikio,8 utumizi wacho hautahitilafiana na imani za Mashahidi.
Katika 1977, Ott na Cooley9 waliripoti juu ya mipasuo 542 ya moyo na mishipa waliyofanyiwa Mashahidi bila kutia damu mishipani nao wakakata shauri kwamba njia hii yaweza kutumiwa “kukiwa na hatari ndogo sana yenye kuruhusika.” Katika kuitikia ombi letu, hivi majuzi, Cooley alipitia tarakimu za mipasuo 1,026, asilimia 22 ikiwa ya watoto wadogo, naye akagundua “kwamba hatari ya upasuaji katika wagonjwa wa kikundi cha Mashahidi wa Yehova haikupata kuwa juu zaidi kwa vyovyote kuliko kwa wengine.” Vivyo hivyo, Michael E. DeBakey, MD, aliwasilisha “kwamba katika hali zilizo nyingi [zinazohusu Mashahidi] hatari ya upasuaji bila kutia damu mishipani si kubwa kuliko katika wale wagonjwa ambao tunatia damu mishipani” (uwasilisho wa kibinafsi, Machi 1981). Fasihi pia hurekodi upasuaji uliofanikiwa wa viungo vya mkojo10 na wa mifupa.11 G. Dean MacEwen, MD, na J. Richard Bowen, MD, waandika kwamba muunganisho wa ute wa mgongo wa nje “umefanywa kwa mafanikio kwa watoto wadogo [Mashahidi] 20” (habari zisizotangazwa, Agosti 1981). Waongezea: “Daktari mpasuaji anahitaji kusitawisha falsafa ya kustahi haki za mgonjwa za kukataa kutiwa damu mishipani lakini bado afuate njia za upasuaji kwa jinsi inayoruhusu usalama kwa mgonjwa.”
Herbsman12 aripoti fanikio katika visa fulani, kutia vingine vilivyohusu vijana, “wenye kupoteza damu nyingi sana kwa sababu ya majeraha.” Yeye hukiri kwamba kidogo ni kana kwamba “Mashahidi wako katika hali isiyo na mafaa inapohusu matakwa ya damu. Hata hivyo ni wazi pia kwamba tuna matibabu mengine badala ya damu.” Akionelea kwamba madaktari wengi wapasuaji wamehisi wakijizuia kupokea wagonjwa Mashahidi kwa sababu ya “hofu ya matokeo ya kisheria,” yeye aonyesha kwamba hilo si hangaiko halali.
MAHANGAIKO YA KISHERIA NA WATOTO WADOGO
Mashahidi hutia sahihi kwa utayari ile fomu ya American Medical Association wakiondolea matabibu na mahospitali kupasishwa daraka,13 na Mashahidi walio wengi hubeba kadi ya Medical Alert yenye kuandikwa tarehe na kushuhudiwa na mashahidi, iliyotayarishwa kwa kushauriana na mamlaka za kitiba na za kisheria. Hati hizo zinampa mgonjwa (au mali zake) wajibu wa kuzifuata na huwapa ulinzi matabibu, kwa maana Hakimu Warren Burger alithibitisha kwamba shtaka la utibabu mbaya “lingeonekana kutoungwa mkono” ikiwa hati kama hiyo imetiwa sahihi. Pia, akitoa maelezo juu jambo hilo katika uchanganuzi wa “utibabu wa lazima na uhuru wa kidini,” Paris14 aliandika: “Mwelezaji mmoja aliyechunguza fasihi aliripoti, ‘Mimi sikuweza kupata mamlaka yoyote kwa taarifa ya kwamba tabibu angepasishwa daraka . . . la uhalifu . . . kwa kushindwa kumlazimisha mgonjwa asiyetaka atiwe damu mishipani.’ Hatari hiyo huonekana zaidi kuwa zao lenye kubuniwa na akili ya kisheria kuliko kuwa uwezekano halisi.”
Utunzaji wa watoto wadogo hutokeza hangaiko kubwa zaidi, mara nyingi ukitokeza tendo la kisheria dhidi ya wazazi chini ya sheria ya kutojali mtoto. Lakini matabibu na mawakili wengi wa sheria wanaozijua sana kesi za Mashahidi hutilia shaka matendo kama hayo, kwa kuwa wanaamini kwamba wazazi Mashahidi hutafuta utunzaji mzuri wa kitiba kwa ajili ya watoto wao. Kwa kutotaka kuepa daraka lao la kimzazi au kulihamisha kwa hakimu au mtu mwingine, Mashahidi huhimiza kwamba ufikirio utolewe kwa itikadi za kidini za jamaa. Dakt. A. D. Kelly, aliyekuwa Katibu wa Canadian Medical Association, aliandika kwamba15 “wazazi wa watoto wadogo na watu wa jamaa wa karibu wa wagonjwa wasio na fahamu wana haki ya kufasiri penzi la mgonjwa. . . . Mimi sivutiwi na zile hatua za mahakama ya ujadili iyokusanyika saa 8:00 za usiku ili kuondoa mtoto katika utunzi wa mzazi wake.”
Ni wazi kwamba wazazi wana haki ya kujieleza katika utunzaji wa watoto wao, kama vile wakati wa kukabili uwezekano wa hatari-manufaa za upasuaji, mnururisho, au utibabu wa kutumia kemikali. Kwa sababu za kiadili zinazopita lile suala la hatari ya kutiwa damu mishipani,16 wazazi Mashahidi huomba kwamba utibabu usiokatazwa kidini utumiwe. Hilo lapatana na itikadi ya kutibu “mwanadamu mzima,” bila kusahau uwezekano wa dhara lenye kudumu la kiakili na kijamii lifanyizwalo na utaratibu wenye kuvamia ambao huhalifu imani za msingi za jamaa. Mara nyingi, vitovu vikubwa kotekote nchini ambavyo vimepata kushughulika na Mashahidi sasa vinakubali kuhamishwa kwa mgonjwa kutoka shirika lisilotaka kutibu Mashahidi, hata visa vya watoto wadogo.
TATIZO LA TABIBU
Yaeleweka kwamba, kutunza Mashahidi wa Yehova huenda kukatokeza tatizo kwa tabibu aliyejitoa kuhifadhi uhai na afya kwa kutumia mbinu zote alizo nazo. Katika tahariri ya makala mfululizo kuhusu upasuaji mkubwa waliofanyiwa Mashahidi, Harvey17 alikubali hivi, “Mimi huziona kuwa zenye kuudhi zile imani ambazo zaweza kuingilia kazi yangu.” Lakini, aliongeza: “Labda sisi pia husahau vyepesi sana kwamba upasuaji ni ufundi unaotegemea mbinu za kibinafsi za watu mmoja mmoja. Mbinu zaweza kufanyiwa maendeleo.”
Profesa Bolooki18 aliona ripoti yenye kufadhaisha kwamba mojapo hospitali zenye shughuli kuliko zote za kutibu maumivu makali ya majeraha katika Dade County, Florida, ilikuwa na “mwongozo wa kukataa kwa ujumla kutibu” Mashahidi. Yeye alionyesha kwamba “njia zilizo nyingi za upasuaji katika kikundi hiki cha wagonjwa zashirikishwa na hatari ndogo kuliko kawaida.” Aliongezea: “Ingawa madaktari wapasuaji huenda wakahisi kwamba wananyimwa kitumishi cha tiba ya ki-siku-hizi . . . Mimi nasadiki kwamba kwa kupasua wagonjwa hawa watajifunza mengi zaidi.”
Badala ya kuona mgonjwa Shahidi kuwa tatizo, matabibu wanaozidi kuongezeka hupokea hali hiyo kuwa tatizo la kitiba. Katika kukabiliana na tatizo hilo wamesitawisha kiwango cha kufuatwa kwa ajili ya kikundi hiki cha wagonjwa kinachoruhusiwa kwenye vitovu vingi vya kitiba kotekote nchini. Wakati ule ule matabibu hawa wanaandaa utunzaji ulio bora kabisa kwa hali jema ya ujumla ya wagonjwa. Kama vile Gardner et al19 anavyoonelea: “Ni nani angenufaika ikiwa mgonjwa ameponywa ugonjwa wa kimwili lakini uhai wake wa kiroho pamoja na Mungu, kama auonavyo, uhatirishwe, jambo ambalo huongoza kwenye maisha yasiyo na maana na pengine mabaya zaidi ya kifo chenyewe.”
Mashahidi hutambua kwamba, kitiba, sadikisho lao lenye kushikiliwa kwa imara huonekana kuongeza kadiri fulani ya hatari na huenda likatatanisha utunzaji wao. Kwa hiyo, kwa ujumla wao hudhihirisha uthamini usio wa kawaida kwa ajili ya utunzaji wanaopokea. Zaidi ya kuwa na imani yenye kina na nia thabiti ya kuishi, ambazo ni sehemu muhimu, wao hushirikiana kwa nderemo na matatibu na wafanya kazi wa tiba. Hivyo, mgonjwa na tabibu pia huungamana katika kulikabili tatizo hili lisilo na kifani.
MAREJEZO
1. Mashahidi wa Yehova na Suala la Damu. Brooklyn, NY, Watchtower Bible and Tract Society, 1988, kur. 1-64.
2. Mnara wa Mlinzi 1978;16 (Novemba 15):21-23.
3. Hypotensive anesthesia hurahisisha upasuaji wa nyonga, MEDICAL NEWS. JAMA 1978;239:181.
4. Hetastarch (Hespan)—njia mpya ya kutanua plazima. Med Lett Drugs Ther 1981;23:16.
5. Hamstra RD, Block MH, Schocket AL:Kuingiza deksitrani ya chuma mishipani katika utibabu wa kliniki. JAMA 1980;243:1726-1731.
6. Lapin R:Upasuaji mkubwa wanaofanyiwa Mashahidi wa Yehova. Contemp Orthop 1980;2:647-654.
7. Fuerst ML: ‘Sonik-skalpeli’ haiharibu mishipa. Med Trib 1981;22:1, 30.
8. Gonzáles ER: Kile kisa cha ‘damu isiyoasilia’: Fluosol manufaa maalumu kwa Mashahidi wa Yehova. JAMA 1980;243:719-724.
9. Ott DA, Cooley DA:Upasuaji wa moyo na mishipa wanaofanyiwa Mashahidi wa Yehova. JAMA 1977;238:1256-1258.
10. Roen PR, Velcek F: Upasuaji mkubwa wa viungo vya mkonjo na uzazi bila utiaji-damu mishipani. NY State J Med 1972;72:2524-2527.
11. Nelson CL, Martin K, Lawson N, et al: Mbadilisho mzima wa nyonga bila utiaji-damu mishipani. Contemp Orthop 1980;2:655-658.
12. Herbsman H: Kutibu Mashahidi wa Yehova. Emerg Med 1980;12:73-76.
13. Medicolegal Forms With Legal Analysis. Chicago, American Medical Association, 1976, uku. 83.
14. Paris JJ: Utibabu wa kushurutishwa na uhuru wa kidini: Ni sheria ya nani itashinda? Univ San Francisco Law Rev 1975;10:1-35.
15. Kelly AD: Aequanimitas Can Med Assoc J 1967;96:432.
16. Kolins J: Vifo kutokana na utiwaji-damu mishipani. JAMA 1981;245:1120.
17. Harvey JP: Suala la ufundistadi. Contemp Orthop 1980;2:629.
18. Bolooki H: Kutibu Mashahidi wa Yehova: Kielelezo cha utunzi mzuri. Miami Med 1981;51:25-26.
19. Gardner B, Bivona J, Alfonso A, et al: Upasuaji mkubwa wanaofanyiwa Mashahidi wa Yehova. NY State J Med 1976;76:765-766.