Appendix
Damu: Uchaguzi wa Nani na Dhamiri ya Nani?
na J. Lowell Dixon, M.D.
Imechapwa upya kwa ruhusa ya New York State Journal of Medicine, 1988; 88:463-464, haki ya kunakili ya Medical Society of the State of New York.
MATABIBU wamejitoa watumie maarifa, stadi, na ujuzi wao katika kupigana na magonjwa na kifo. Hata hivyo, vipi ikiwa mgonjwa anakataa utibabu uliopendekezwa? Inaelekea hilo litatukia ikiwa mgonjwa ni Shahidi wa Yehova na utibabu ni damu nzima, chembe nyekundu za damu zilizopakiwa, plazima, au visahani-damu.
Inapohusu kutumia damu, huenda tabibu akahisi kwamba uchaguzi wa mgonjwa wa utibabu usiotumia damu utazuia wafanya kazi wa kitiba waliojitoa wasiweze kufanya lolote. Hata hivyo, ni lazima mtu asisahau kwamba mara nyingi wagonjwa wengine wasio Mashahidi wa Yehova huchagua kutofuata mapendekezo ya daktari wao. Kulingana na Appelbaum na Roth1 asilimia 19 ya wagonjwa katika mahospitali ya kufundishia walikataa angalau utibabu mmoja au njia ya kufuatwa, hata ingawa asilimia 15 ya makatao hayo “yalikuwa na uwezekano wa kuhatarisha uhai.”
Maoni ya ujumla ya kwamba “daktari ajua vizuri zaidi” hufanya wagonjwa walio wengi wastahi ustadi na maarifa ya daktari wao. Lakini ingekuwa hatari yenye hila kama nini kwa tabibu kuendelea kana kwamba fungu hili la maneno ni uhakika wa kisayansi na kutibu wagonjwa kulingana nalo. Ni kweli, mazoezi yetu ya kitiba, kupewa leseni, na ujuzi hutupa mapendeleo yanayostahili kuangaliwa katika uwanja wa kitiba. Ingawa hivyo, wagonjwa wetu wanazo haki. Na, kama inavyoelekea kuwa twajua, sheria (hata Katiba) huzipa haki umaana ulio mkubwa zaidi.
Kwenye kuta za mahospitali yaliyo mengi, mtu huiona “Sheria ya Haki za Mgonjwa” ikiwa imeangikwa ionekane. Mojapo haki hizo ni idhini baada ya kuarifiwa, ambayo inaweza kuitwa kwa usahihi zaidi uchaguzi baada ya kuarifiwa. Baada ya mgonjwa kuarifiwa juu ya yale yanayoweza kuwa matokeo ya matibabu mbalimbali (au hata kutotibiwa), ni juu yake kuchagua ule ambao atakubalia. Kwenye Hospitali ya Albert Einstein katika Bronx, New York, hati ya mwongozo juu ya utiaji-damu mishipani na Mashahidi wa Yehova ilitaarifu: “Mgonjwa yeyote aliye mtu mzima asiyeondolewa nguvu zake za kufikiri ana haki ya kukataa utibabu hata katao hilo liwe lenye kudhuru afya yake kadiri gani.”2
Ingawa matabibu huenda wakasema juu ya mahangaiko yao juu ya maadili au daraka, mahakama zimekazia ubora wa uchaguzi wa mgonjwa.3 Mahakama ya Rufani ya New York ilitaarifu kwamba “haki za mgonjwa kuamua mwendo wa utibabu wake mwenyewe inapita zote . . . Daktari hawezi kuonwa kuwa amehalifu madaraka yake ya kisheria au ya kikazi anapoheshimu haki ya mgonjwa hodari aliye mtu mzima ya kukataa utibabu.”4 Mahakama hiyo imeonelea pia kwamba “ukamilifu wa kiadili wa wafanya kazi ya kitiba, ingawa ni wa maana, hauwezi kuwa wa maana zaidi ya haki za msingi za watu mmoja mmoja zilizoelezwa kwa imara hapa. Mahitaji na tamaa za mtu mmoja mmoja ndizo za maana zaidi, si matakwa ya shirika fulani.”5
Shahidi anapokataa damu, matabibu huenda wakahisi michomo ya dhamiri kwa taraja la kufanya kile kinachoonekana kuwa punde ya kiwango kikubwa kabisa. Ingawa hivyo, kile ambacho Shahidi anataka madaktari wenye kudhamiria wafanye, ni kuandaa utunzaji mwingine ulio bora zaidi uwezekanao chini ya hali hizo. Mara nyingi lazima sisi tubadili utibabu wetu ili kuruhusu hali, kama vile kanieneo kubwa ya damu, mzio mkali wa dawa za kuua viini, au kutopatikana kwa vifaa fulani vilivyo ghali. Kwa habari ya mgonjwa Shahidi, matabibu wanaombwa washughulikie tatizo la kitiba au la upasuaji kupatana na uchaguzi na dhamiri ya mgonjwa, uamuzi wake wa kiadili/kidini wa kushika mwiko wa damu.
Ripoti nyingi juu ya upasuaji mkubwa waliofanyiwa wagonjwa Mashahidi huonyesha kwamba matabibu wengi wanaweza, kwa dhamiri njema na kwa mafanikio, kuruhusu ombi la kutotumia damu. Kwa kielelezo, katika 1981, Cooley alipitia mipasuo 1,026 ya moyo na mishipa, asilimia 22 waliyofanyiwa watoto wadogo. Yeye aligundua “kwamba hatari ya upasuaji katika wagonjwa wa kikundi cha Mashahidi wa Yehova haikupata kuwa juu zaidi kwa vyovyote kuliko kwa wengine.”6 Kambouris7 aliripoti juu ya upasuaji mkubwa waliofanyiwa Mashahidi, baadhi yao walikuwa “wamenyimwa utibabu wa upasuaji uliohitajiwa kwa haraka sana kwa sababu ya kukataa kupokea damu.” Akasema: “Wagonjwa wote walipokea mahakikishio kabla ya utibabu kwamba imani zao za kidini zingestahiwa, bila kujali hali katika chumba cha kupasulia. Hakukuwa na athari mbaya za mwongozo huo.”
Wakati mgonjwa ni Shahidi wa Yehova, zaidi ya jambo la uchaguzi, dhamiri inahusika. Mtu hawezi kufikiria tu dhamiri ya tabibu. Namna gani ile ya mgonjwa? Mashahidi wa Yehova huuona uhai kuwa zawadi ya Mungu inayowakilishwa na damu. Wao huiamini ile amri ya Biblia ya kwamba lazima Wakristo ‘wajiepushe na damu.’ (Matendo 15:28, 29).8 Kwa sababu hiyo, ikiwa kwa kuchukua daraka la baba tabibu angehalifu masadikisho hayo ya kidini ya mgonjwa yenye kina na yaliyoshikiliwa kwa muda mrefu, matokeo yangeweza kuwa yenye tanzia. Papa John Paul 2 ameonelea kwamba kumlazimisha mtu ahalifu dhamiri yake “ndilo pigo lenye maumivu makali zaidi lililopata kupigwa kwa heshima ya kibinadamu. Katika maana fulani, ni baya zaidi kuliko pigo la kifo cha kimwili, au kuua.”9
Ingawa Mashahidi wa Yehova hukataa damu kwa sababu za kidini, wagonjwa zaidi na zaidi wasio Mashahidi sasa wanachagua kuepuka damu kwa sababu ya hatari kama vile UKIMWI, mchochota wa ini [hepataitisi non-A non-B], na maitikiano yanayohusu kinga. Huenda sisi tukawatolea maoni yetu juu ya kama hatari hizo huonekana ndogo au la, zikilinganishwa na manufaa. Lakini, kama American Medical Association linavyoonyesha, mgonjwa ndiye “mwamuzi wa mwisho kama atajihatarisha kwa utibabu au upasuaji uliopendekezwa na daktari au atahatarisha kuishi bila huo. Hiyo ndiyo haki ya kiasili ya mtu mmoja mmoja, ambayo sheria inatambua.”10
Macklin11 alitokeza suala la hatari/manufaa linalohusiana na hilo kwa habari ya Shahidi “ambaye alipata hatari ya kutokwa damu mpaka kufa bila kutiwa damu mishipani.” Mwanafunzi wa kitiba alisema: “Fikira zake zilikuwa nzima. Ufanye nini wakati imani za kidini zinapopinga kile chanzo pekee cha utibabu?” Macklin alisababu hivi: “Huenda sisi tukaamini kwa imara sana kwamba mtu huyu anakosea. Lakini Mashahidi wa Yehova huamini kwamba kutiwa damu mishipani . . . [huenda kukatokeza] hukumu mbaya ya milele. Sisi tumezoezwa kufanya uchanganuzi wa hatari-manufaa katika tiba lakini ukipima hukumu mbaya ya milele dhidi ya maisha yanayobaki duniani, uchanganuzi huo wachukua maoni tofauti.”11
Vercillo na Duprey12 katika toleo hili la Journal walirejezea In re Osborne ili kukazia upendezo katika kuhakikisha usalama wa wategemeaji, lakini kesi hiyo iliamuliwaje? Ilihusu baba ya watoto wawili wadogo aliyeumizwa sana. Mahakama iliamua kwamba akifa, watu wa ukoo wangetunza watoto wake kimwili na kiroho. Hivyo, kama vile katika kesi nyingine za karibuni,13 mahakama haikupata upendezo lazima wa kiserikali wa kuwa na haki ya kutangua chaguo la mgonjwa kupata utibabu; kujiingiza kwa mahakama ili kutoa mamlaka ya kutumia utibabu wenye kukataliwa sana naye hakukuwa na sababu halali.14 Kwa kutumia utibabu mwingine mgonjwa huyo alipona na akaendelea kutunza jamaa yake.
Je! si kweli kwamba visa vilivyo vingi sana ambavyo matabibu wamekabili, au yaelekea watakabili, vyaweza kushughulikiwa bila damu? Tuliyojifunza na tunayojua vizuri zaidi yanahusiana na matatizo ya kitiba, hata hivyo wagonjwa ni binadamu ambao thamani na miradi yao wakiwa watu mmoja mmoja haiwezi kupuuzwa. Wanajua vizuri zaidi juu ya mambo yao wenyewe ya kutangulizwa, maadili na dhamiri yao wenyewe, mambo ambayo huwapatia maana ya maisha.
Kustahi dhamiri za kidini za wagonjwa Mashahidi huenda kukatokeza tatizo lenye kudai tutumie stadi zetu. Lakini tukabilipo tatizo hili, tunakazia uhuru wenye thamani ambao sisi sote twapenda sana-sana. Kama John Stuart Mill alivyoandika kwa kufaa: “Hakuna jamii ambayo ni huru ikiwa uhuru huu kwa ujumla haustahiwi, hata namna yayo ya serikali iwe nini . . . Kila mmoja ni mtunzi wa afya yake mwenyewe, iwe ya kimwili, au ya kiakili na kiroho. Ainabinadamu ni wafaidikaji wakubwa kwa kuruhusu kila mmoja aishi kama aonavyo kuwa vema kwake, kuliko kwa kushurutisha kila mmoja aishi kama ionekanavyo kuwa vema kwa wengine.”15
[MAREJEZEO]
1. Appelbaum PS, Roth LH: Wagonjwa wanaokataa utibabu katika mahospitali ya kitiba. JAMA 1983; 250:1296-1301.
2. Macklin R: Yanayotendeka ndani ya halmashauri ya maadili: Pigano la karibuni zaidi juu ya Mashahidi wa Yehova. Hastings Cent Rep 1988; 18(1):15-20.
3. Bouvia v Superior Court, 179 Cal App 3d 1127, 225 Cal Rptr 297 (1986); In re Brown, 478 So 2d 1033 (Miss 1985).
4. In re Storar, 438 NYS 2d 266, 273, 420 NE 2d 64, 71 (NY 1981).
5. Rivers v Katz, 504 NYS 2d 74, 80 n 6, 495 NE 2d 337, 343 n 6 (NY 1986).
6. Dixon JL, Smalley MG: Mashahidi wa Yehova. Lile Tatizo la upasuaji/la kiadili. JAMA 1981; 246:2471-2472.
7. Kambouris AA: Mipasuo mikubwa ya fumbatio wanayofanyiwa Mashahidi wa Yehova. Am Surg 1987; 53:350-356.
8. Mashahidi wa Yehova na Suala la Damu. Brooklyn, NY, Watchtower Bible and Tract Society, 1988, kur 1-64.
9. Papa ashutumu tendo la kinidhamu la Polandi. NY Times, Januari 11, 1982, uku A9.
10. Ofisi ya Kushauri Watu Wote: Medicolegal Forms with Legal Analysis. Chicago, American Medical Association, 1973, uku 24.
11. Kleiman D: Mwanafalsafa wa hospitali akabilisha maamuzi ya maisha. NY Times, Januari 23, 1984, kur B1, B3.
12. Vercillo AP, Duprey SV: Mashahidi wa Yehova na utiwaji mishipani vitu vilivyofanyizwa kwa damu. NY State J Med 1988; 88:493-494.
13. Wons v Public Health Trust, 500 So 2d 679 (Fla Dist Ct App) (1987); Randolph v City of New York, 117 AD 2d 44, 501 NYS 2d 837 (1986); Taft v Taft, 383 Mass 331, 446 NE 2d 395 (1983).
14. In re Osborne, 294 A 2d 372 (DC Ct App 1972).
15. Mill JS: Juu ya uhuru, katika Adler MJ (ed): Great Books of the Western World. Chicago, Encyclopaedia Britannica, Inc, 1952, buku 43, uku 273.