Sura 6
Dini ya Buddha—Jitihada ya Kutafuta Mnurisho Bila ya Mungu
1. (a) Dini ya Buddha imejidhihirishaje katika jumuiya ya nchi za Magharibi? (b) Ni nini visababishi vya usitawi huo wa nchi za Magharibi?
IKIWA yajulikana kidogo nje ya Asia mwanzoni mwa karne ya 20, Dini ya Buddha leo imechukua fungu la kuwa dini ya ulimwengu. Kwa kweli, watu wengi katika nchi za Magharibi hushangaa sana kukuta Dini ya Buddha ikisitawi katika ujirani wao wenyewe. Sehemu kubwa ya hilo imekuwa ni kwa sababu ya kuhama kwa wakimbizi wa kimataifa. Jumuiya kubwa-kubwa za Kiasia zimejiimarisha katika Ulaya ya Magharibi, Amerika ya Kaskazini, Australia, na sehemu nyinginezo. Wahamiaji zaidi na zaidi wanapotia mizizi katika mabara mapya, wanaleta pia dini yao. Wakati uo huo, wengi zaidi ya watu katika nchi za Magharibi wanakutana uso kwa uso na Dini ya Buddha kwa mara ya kwanza. Hilo, pamoja na uendekezaji na uzorotaji wa makanisa ya kimapokeo, limesababisha watu fulani wawe waongofu wa hiyo dini “mpya.”—2 Timotheo 3:1, 5.
2. Wafuasi wa Dini ya Buddha watapatikana wapi leo?
2 Kwa hiyo, kulingana na 1989 Britannica Book of the Year, Dini ya Buddha hujidai kuwa na washiriki wapatao milioni 300 ulimwenguni pote, kukiwa na wapatao 200,000 katika Ulaya ya Magharibi na hesabu iyo hiyo katika Amerika ya Kaskazini, 500,000 katika Amerika ya Latini, na 300,000 katika Soviet Union. Hata hivyo, waumini wengi wa Dini ya Buddha, wangali wanapatikana katika nchi za Kiasia, kama vile Sri Lanka, Myanmar (Burma), Thailand, Japan, Korea, na China. Lakini, Buddha alikuwa nani? Dini hii ilianzaje? Mafundisho na mazoea ya Dini ya Buddha ni nini?
Swali la Chanzo Chenye Kutegemeka
3. Ni chanzo gani cha habari kinachopatikana juu ya maisha ya Buddha?
3 “Yanayojulikana juu ya maisha ya Buddha yanategemea hasa uthibitisho wa maandishi yanayokubalika, yenye kueleza kirefu na kutia mambo mengi yakiwa ni yale yaliyoandikwa katika Kipali, lugha ya India ya kale,” chasema kitabu World Religions—From Ancient History to the Present. Kinachomaanishwa na hilo ni kwamba hakuna chanzo cha habari za wakati wake cha kutueleza chochote juu ya Siddhārtha Gautama, mwanzilishi wa dini hii, ambaye aliishi katika India ya kaskazini katika karne ya sita K.W.K. Bila shaka, hilo latokeza tatizo. Hata hivyo, lenye uzito zaidi ni swali la kwamba ni wakati gani na jinsi gani hayo “maandishi yanayokubalika” yalivyofanyizwa.
4. Fundisho asilia la Dini ya Buddha lilihifadhiwaje hapo kwanza?
4 Pokeo la Dini ya Buddha husema kwamba muda mfupi tu baada ya kifo cha Gautama, baraza la watawa 500 walikusanyika waamue ni nini lililokuwa fundisho asilia la Bwana wao. Kama baraza hilo liliketi hasa ni habari inayobishaniwa sana kati ya wasomi wa Dini ya Buddha na wanahistoria. Hata hivyo, jambo la maana tunalopaswa kuangalia ni kwamba hata maandishi ya Dini ya Buddha yanakubali kwamba fundisho asilia lililoamuliwa halikuandikwa bali lilikaririwa na wanafunzi. Kuandikwa hasa kwa maandishi hayo matakatifu kulingojea kipindi kirefu.
5. Maandishi ya Kipali yaliandikwa wakati gani?
5 Kulingana na maandishi ya tarehe za matukio ya Sri Lanka ya karne ya nne na sita W.K., ya mapema zaidi kati ya hayo “maandishi yanayokubalika” yaliandikwa wakati wa utawala wa Mfalme Vattagamani Abhaya katika karne ya kwanza K.W.K. Masimulizi mengine ya maisha yake Buddha hayakuandikwa mpaka labda karne ya kwanza au hata ya tano W.K., karibu miaka elfu moja baada ya wakati wake.
6. Ni uchambuzi gani unatolewa kuhusu “maandishi yanayokubalika”? (Linganisha 2 Timotheo 3:16, 17.)
6 Kwa hiyo, chasema Abingdon Dictionary of Living Religions, “Chanzo cha ‘nyasifa’ ni cha baadaye tena chajaa habari ya kihekaya na kingano nayo maandishi ya kale zaidi yanayokubalika ni mazao ya hatua ndefu za kupokezana kwa mdomo ambayo kwa wazi yalitia ndani usahihisho fulani na nyongeza nyingi.” Msomi mmoja hata “alishikilia kwamba hakuna neno hata moja la fundisho lililoandikwa linaloweza kusemwa kwa uhakika kamili kuwa ni la Gautama mwenyewe.” Je! machambuzi hayo ni ya haki?
Mimba na Kuzaliwa kwa Buddha
7. Kulingana na maandishi ya Dini ya Buddha, mama yake Buddha alipataje mimba yake?
7 Fikiria madondoo yafuatayo kutoka Jataka, sehemu ya maandishi yanayokubalika ya Kipali, na Buddha-charita, maandishi ya Sanskrit ya karne ya pili W.K. juu ya maisha yake Buddha. Kwanza, ni simulizi la jinsi mama ya Buddha, Malkia Maha-Maya, alivyopata kuchukua mimba yake katika ndoto.
“Malaika wanne walinzi walikuja na kumnyanyua, pamoja na kitanda chake, wakampeleka kwenye Milima ya Himalaya. . . . Kisha wakaja wake za malaika hao walinzi, na wakamwongoza kwenye Ziwa Anotatta, wakamwogesha, ili kumwondoa kila dosari ya kibinadamu. . . . Si mbali kutoka hapo kulikuwa Kilima Fedha, na ndani yacho jumba la dhahabu. Humo wakatandika kitanda cha kimungu kichwa chacho kikielekea mashariki, wakamlaza juu yacho. Sasa Buddha wa wakati ujao alikuwa amekuwa tembo murua mweupe . . . Akakwea Kilima Fedha, na . . . na mara tatu akatembea kuzunguka kitanda cha mamaye, upande wake wa kulia kukielekea, na akimgongagonga upande wake wa kulia, akaonekana ni kama anaingia tumbo lake la uzazi. Kwa njia hiyo mtungo wa mimba ukatukia katika sikukuu ya katikati ya kiangazi.”
8. Ni nini kilichotabiriwa kuhusu wakati ujao wa Buddha?
8 Malkia alipomwambia mumeye, mfalme, ndoto hiyo, yeye aliita makuhani mashuhuri Wahindu 64, akawalisha na kuwavisha, akawaomba tafsiri. Jibu lao lilikuwa hili:
“Usiwe na wasiwasi, mfalme mkuu! . . . Utapata mwana. Na yeye, akiendelea kuishi maisha ya nyumbani, atakuwa maliki wa ulimwengu wote mzima; lakini akiacha maisha ya nyumbani na kujiepusha na ulimwengu, atakuwa Buddha, na kukunja mawingu ya dhambi ya upumbavu wa ulimwengu huu.”
9. Ni matukio gani yasiyo ya kawaida yaliyosemekana yalifuata tamko kuhusu wakati ujao wa Buddha?
9 Baada ya hilo, yasemekekana miujiza 32 ilikuwa imetokea:
“Jumla ya malimwengu elfu kumi ghafula yakatetemeka, yakatitima, na kutikisika. . . . Mioto ikazimika katika helo zote; . . . maradhi yakakoma kati ya binadamu; . . . ala zote za muziki zikavuma bila ya kuvumishwa; . . . katika bahari kuu maji yakawa matamu; . . . malimwengu mazima elfu kumi yakawa tungamo moja la shada la maua la uzuri upendezao kabisa uwezekanao.”
10. Maandishi matakatifu ya Dini ya Buddha huelezaje kuzaliwa kwa Buddha?
10 Kisha ukafika uzawa usio wa kawaida wa Buddha katika bustani ya miti ya chumvi iitwayo Msitu wa Lumbini. Wakati malkia alipotaka kushika tawi la mti wa chumvi uliokuwa mrefu zaidi katika msitu huo, mti huo ulikubali kwa kuinama akaufikia. Akiwa ameshikilia tawi hilo na amesimama, akazaa.
“Akatoka katika tumbo la uzazi la mamaye kama mhubiri anayeshuka kutoka kwenye kiti chake cha kuhubiri, au kama mwanamume anayeshuka ngazini, akinyoosha mikono yote miwili na miguu yote miwili, asichafuliwe na unajisi wowote kutoka kwa tumbo la uzazi la mamaye. . . . ”
“Mara tu akiisha kuzaliwa, [Buddha wa wakati ujao] aweka imara nyayo zote mbili kwenye ardhi, achapua hatua saba kuelekea kaskazini, kukiwa chandalua cheupe kilichobebwa juu ya kichwa chake, na akagua kila sehemu ya ulimwengu, akipaaza sauti zisizo na kifani: Katika ulimwengu wote mimi ndimi mkuu, bora na wa kwanza; huu ndio uzawa wangu wa mwisho; Sitazaliwa tena kamwe.”
11. Wasomi fulani wamefikia mkataa gani kuhusu masimulizi juu ya maisha ya Buddha kama yapatikanavyo katika maandishi matakatifu?
11 Pia kuna hadithi nyingine hali moja na hiyo zenye madoido kuhusu utoto wake, kukutana kwake na wastaajabiwa wachanga wa kike, kutanga-tanga kwake, na karibu kila tukio maishani mwake. Labda ndiyo sababu haishangazi kwamba wasomi walio wengi husema masimulizi hayo yote ni hekaya na ngano. Ofisa mmoja wa British Museum hata adokeza kwamba kwa sababu ya “fungu kubwa la hekaya na miujiza, . . . maisha ya kihistoria ya Buddha hayawezi kujulikana.
12, 13. (a) Ni nini simulizi la kimapokeo juu ya maisha ya Buddha? (b) Ni jambo gani linalokubalika na wengi kuhusu wakati ambao Buddha alizaliwa? (Linganisha Luka 1:1-4.)
12 Ijapokuwa ngano hizi, simulizi la kimapokeo la maisha ya Buddha limetawanywa sana. Maandishi ya kisasa, A Manual of Buddhism, yaliyochapishwa katika Colombo, Sri Lanka, hutoa simulizi jepesi lifuatalo.
“Wakati wa siku ya mwezi-mpevu ya Mei katika mwaka 623 K.K. katika wilaya ya Nepali alizaliwa Mwana-Mfalme Msakya wa Kihindi, jina lake Siddhattha Gotama.a Mfalme Suddhodana alikuwa baba yake, na Malkia Mahā Māyā alikuwa mama yake. [Mama yake] alikufa siku chache baada ya kuzaliwa kwa mtoto huyo na Mahā Pajāpati Gotamī akawa mama yake mlezi.
“Akiwa na miaka kumi na sita alimwoa binamu yake, Yasodharā Binti-Mfalme mrembo.
“Kwa karibu miaka kumi na mitatu baada ya ndoa yake ya furaha aliishi maisha ya anasa, akiwa na raha mustarehe hakujua kubadilikabadilika kwa maisha yaliyo nje ya malango ya jumba lake la kifalme.
“Baada ya muda, ukweli ukampambazukia hatimaye. Katika mwaka wake wa 29, ambao ukaleta badiliko la mtindo wake wa maisha, mwana wake Rāhula alizaliwa. Aliuchukua uzao wake kuwa kizuizi, kwa maana alitambua kwamba lazima wote wazaliwe, wawe wagonjwa, na kufa. Hivyo akitambua huzuni inampata kila mtu, akaamua kutafuta maponya ya ugonjwa huo unaopata binadamu wote.
“Kwa hiyo akiacha kabisa anasa zake za kifalme, aliondoka nyumbani usiku mmoja . . . akanyoa nywele zake, na kuvaa joho la vivi hivi la mtu anayejiepusha na anasa, akatanga-tanga akiwa Mtafuta-Ukweli.”
13 Kwa wazi habari chache hizo za kindani za wasifu huo zinatofautiana kabisa na masimulizi mazuri ajabu yanayopatikana katika “maandishi yanayokubalika.” Na isipokuwa mwaka wa kuzaliwa kwake, kwa ujumla hayo yanakubaliwa.
Mnurisho—Jinsi Ulivyotokea
14. Ni jambo gani lililoleta badiliko kubwa katika maisha ya Gautama?
14 “Badiliko la mtindo wake wa maisha” lililotangulia kutajwa, ni nini? Ilikuwa wakati, kwa mara ya kwanza maishani mwake, alipoona binadamu mgonjwa, binadamu mzee, na binadamu aliyekufa. Maono hayo yalimfanya aumizwe moyo sana juu ya ni nini maana ya maisha—Ni kwa nini wanadamu walizaliwa, na ndipo tu wateseke, wazeeke, na kufa? Kisha, ilisemekana kuwa aliona binadamu mtakatifu, ambaye alikuwa amekataa kabisa ulimwengu ili afuatie ukweli. Hilo lilimsukuma Gautama aache familia yake, mali zake, na jina lake la kimwana-mfalme atumie miaka sita iliyofuata akitafuta jibu kutoka kwa walimu na waguru Wahindu, lakini asifanikiwe. Simulizi hilo latuambia kwamba alifuatia mwendo wa kutafakari, kufunga, Yoga, na kujikana kabisa, na bado asipate amani au mnurisho wowote wa kiroho.
15. Gautama alifikiaje mwishowe kile alichoita mnurisho?
15 Hatimaye akaja kutambua kwamba mwendo wake wa kujikana kabisa haukufaa kitu sawa na vile maisha ya kula raha aliyokuwa amekuwa nayo mbeleni. Sasa akaanza aliyoiita Njia ya Katikati, akiepuka mitindo ya maisha ya kupita kiasi ambayo alikuwa amefuata. Kwa kuamua kwamba jibu lingepatikana katika fahamu zake mwenyewe, aliketi akitafakari chini ya mpipali, au mtini wa Kihindi. Akikinza mashambulizi na vishawishi vya ibilisi Mara, aliendelea imara katika kutafakari kwake kwa majuma manne (wengine husema saba) hadi yasemekana kuwa akatwaa maarifa na ufahamu wote na kufikia mnurisho.
16. (a) Gautama akawa nini? (b) Ni maoni gani tofauti yanayoshikiliwa kuhusu Buddha?
16 Kwa hatua hiyo, katika istilahi ya Dini ya Buddha, Gautama akawa ndiye Buddha—Aliyeamka, au Aliyenurishwa. Alikuwa amefikia mradi wa upeo, Nirvana, hali ya amani na mnurisho kamili, bilia na tamaa na kuteseka. Pia amekuja kujulikana kuwa Sakyamuni (mtabiri wa kabila la Sakya), na mara nyingi alijitaja kuwa Tathagata (mtu ambaye kwa njia hiyo akaja [kufundisha]). Hata hivyo, faraka tofauti-tofauti za Dini ya Buddha zina maoni tofauti juu ya habari hiyo. Baadhi yazo humwona kuwa binadamu kamili aliyepata njia ya mnurisho akafundisha wafuasi wake hiyo. Nyingine humwona kuwa wa mwisho wa mfululizo wa Mabuddha aliyekuja katika ulimwengu kuhubiri au kuhuisha dharma (Kipali, Dhamma), fundisho au njia ya Buddha. Bado nyingine humwona kuwa bodhisattva, mtu aliyekuwa amefikia mnurisho lakini akaahirisha kuingia Nirvana kusudi asaidie wengine katika mfuatio wao wa mnurisho. Lolote liwalo, tukio hilo, huo Mnurisho, ni lenye umaana wa msingi kwa mafundisho yote ya Dini ya Buddha.
Mnurisho Huo—Ni Nini?
17. (a) Buddha alihubiri wapi na kwa nani mahubiri yake ya kwanza? (b) Eleza kifupi Kweli Bora Nne.
17 Baada ya mnurisho, na baada ya kushinda kusita alikokuwa nako hapo kwanza, Buddha aliondoka akafundishe wengine ukweli wake mpya, dharma yake, aliokuwa ametoka kuupata. Mahubiri yake ya kwanza na yawezekana ndiyo ya maana zaidi yalitolewa katika jiji la Benares, katika msitu wa paa, kwa mabhikku watano—wanafunzi au watawa. Katika hayo, alifundisha kwamba ili kuokolewa, ni lazima mtu aepuke mwendo wa anasa za mwili na ule wa kujiepusha na anasa na kufuata Njia ya Katikati. Halafu, ni lazima mtu aelewe na kufuata Kweli Bora Nne (ona kisanduku, ukurasa unaoangaliana huu), ambazo muhtasari wake kwa ufupi ndio huu:
(1) Uhai wote unateseka.
(2) Kuteseka hutokana na tamaa au uchu.
(3) Kwisha kwa tamaa humaanisha mwisho wa kuteseka.
(4) Kwisha kwa tamaa kunafikiwa kwa kufuata Njia Inayojumlisha Nane, mtu kudhibiti mwenendo, kufikiri, na imani yake.
18. Buddha alisema nini juu ya chanzo cha mnurisho wake? (Linganisha Ayubu 28:20, 21, 28; Zaburi 111:10.)
18 Mahubiri hayo juu ya Njia ya Katikati na juu ya Kweli Nne Bora yanajumlisha maana ya Mnurisho huo na huonwa kuwa taarifa ya mafundisho yote ya Buddha. (Kwa utofautisho, linganisha Mathayo 6:25-34; 1 Timotheo 6:17-19; Yakobo 4:1-3; 1 Yohana 2:15-17.) Gautama hakudai upulizio wowote wa Mungu kwa mahubiri yake bali alijipa sifa mwenyewe kwa maneno “yamevumbuliwa na Tathagata.” Yasemekana kwamba akiwa katika kitanda cha kufia, Buddha aliwaambia wanafunzi wake hivi: “Tafuteni wokovu pekee katika ukweli; msitafute msaada kwa yeyote isipokuwa kwenu wenyewe.” Kwa hiyo, kulingana na Buddha, mnurisho hutoka, si kwa Mungu, bali kwa jitihada ya kibinafsi kwa kusitawisha fikira na vitendo vizuri.
19. Ni kwa nini ujumbe wa Buddha ulikaribishwa wakati huo?
19 Si vigumu kuona ni kwa nini fundisho hilo lilikaribishwa katika jumuiya ya Kihindi ya wakati huo. Lilaani mazoea ya kidini yenye pupa na yenye ufisadi yaliyositawishwa na Wabrahmani Wahindu, au mfumo wa kitabaka wa kikuhani, upande mmoja, na ujiepushaji na anasa wenye kupita kiasi wa wafuasi wa Dini ya Jaini na vidhehebu vingine vya kimafumbo kwa upande ule mwingine. Pia lilikomesha dhabihu na sherehe za ibada, makumi maelfu mengi ya vijimungu na vijimungu-vike, na mfumo wa kitabaka wenye kulemea ambao ulitawala na kutumikisha kila sehemu ya maisha za watu. Kwa ufupi, liliahidi kukombolewa kwa kila mtu aliyekuwa na nia ya kufuata njia ya Buddha.
Dini ya Buddha Yaeneza Uvutano Wayo
20. (a) Zile “Johari Tatu” za Dini ya Buddha ni nini? (b) Shughuli ya Buddha ya kuhubiri ilienea kadiri gani?
20 Mabhikku watano walipokubali fundisho la Buddha, wakawa sangha wa kwanza, au daraja la watawa. Kwa hiyo “Johari Tatu” (Triratna za Dini ya Buddha zilikamilishwa, yaani, Buddha, dharma, na sangha, ambazo zilifikiriwa zinasaidia watu waingie kwenye njia ya mnurisho. Akiwa tayari hivyo, Gautama Buddha alienda mapana na marefu ya Bonde Ganges akihubiri. Watu kutoka kila ngazi na hadhi ya kijamii wakaja kumsikia, nao wakawa wanafunzi wake. Kufikia wakati wa kifo chake akiwa na miaka 80, alikuwa amejulikana sana na kuheshimiwa sana. Iliripotiwa kwamba maneno yake ya mwisho kwa wanafunzi wake yalikuwa haya: “Kuoza ni urithi wa vitu vyote vilivyofanyizwa. Jifanyieni wokovu wenu wenyewe kwa bidii yenye kuendelea.”
21. (a) Ni nani aliyetumika kama chombo cha kuenezea Dini ya Buddha? (b) Matokeo ya jitihada zake yalikuwa nini?
21 Katika karne ya tatu K.W.K., karibu miaka 200 baada ya kifo cha Buddha, mteteaji mkuu zaidi wa Dini ya Buddha alitokea, Maliki Asóka, ambaye alitawala sehemu kubwa ya India. Akiwa amehuzunishwa na machinjo na misukosuko iliyosababishwa na jitihada zake za kushinda, alikubali Dini ya Buddha na akatumia Serikali kuitegemeza. Alijenga vikumbusho vya kidini, akakutanisha mabaraza, na kuwapa mawaidha watu waishi kulingana na maagizo ya Buddha. Asóka pia aliwatuma wamisionari wa Dini ya Buddha kwenye sehemu zote za India na Sri Lanka, Shamu, Misri, na Ugiriki. Hasa kupitia jitihada za Asóka, Dini ya Buddha ilikua kutoka kuwa faraka la Kihindi mpaka kuwa dini ya ulimwengu. Kwa haki, ameonwa na wengine kuwa mwanzilishi wa pili wa Dini ya Buddha.
22. Dini ya Buddha ilikujaje kuimarishwa katika Asia yote?
22 Kutoka Sri Lanka, Dini ya Buddha ilienea kuelekea mashariki kuingia Myanmar (Burma), Thailand, na sehemu nyingine za Uhindi-Uchina. Kuelekea kaskazini, Dini ya Buddha ilienea mpaka Kashmir na Asia ya kati. Kutoka sehemu hizo, na mapema ya karne ya kwanza W.K., watawa wa Dini ya Buddha walisafiri kuvuka milima na majangwa yenye matatizo makubwa na kuipeleka dini yao ndani ya China. Kutoka China, ilikuwa rahisi kwa Dini ya Buddha kuenea mpaka Korea na Japan. Dini ya Buddha pia ilianzishwa Tibet, nchi jirani ya kaskazini mwa India. Kwa kuchanganywa na imani za hapo, ikatokea ikiwa Dini ya Lama, ambayo ilitawala maisha ya kidini na ya kisiasa ya huko. Kufikia karne ya sita au saba W.K., Dini ya Buddha ilikuwa imeimarishwa katika Asia ya Kusini-mashariki yote na Mashariki ya Mbali. Lakini India kulikuwa kukitukia nini?
23. Dini ya Buddha ilipatwa na nini katika India?
23 Dini ya Buddha ilipokuwa ikieneza uvutano wayo katika mabara mengine, ilikuwa inapungua nguvu polepole katika India. Wakiwa wanajishughulisha mno na mambo ya falsafa na ya kimetafizikia, watawa walianza kupoteza uhusiano wao na wafuasi wao wa kawaida. Kuongezea hilo, kupoteza udhamini wa kifalme na kuingizwa kwa mawazo na mazoea ya Kihindu yote hayo yaliharakisha kufa kwa Dini ya Buddha katika India. Hata sehemu takatifu za Dini ya Buddha, kama vile Lumbini, ambako Gautama alizaliwa, na Buddh Gaya, ambako alipata “mnurisho,” zikawa magofu. Kufikia karne ya 13, karibu Dini ya Buddha ilikuwa imetokoweka India, bara ilikoanzia.
24, 25. Ni matukio gani zaidi katika Dini ya Buddha yalionekana katika karne ya 20?
24 Wakati wa karne ya 20, Dini ya Buddha ilipata badiliko jingine la sura. Msukosuko wa kisiasa katika China, Mongolia, Tibet, na nchi nyingine katika Asia ya Kusini-mashariki uliipiga dharuba ya kuangamiza. Maelfu ya makao ya watawa na mahekalu yaliharibiwa na mamia ya maelfu ya watawa wa kiume na wa kike walifukuzwa, wakafungwa gerezani, au hata kuuawa. Hata hivyo, uvutano wa Dini ya Buddha ungali wahisiwa sana katika kufikiri na tabia za watu wa mabara hayo.
25 Katika Ulaya na Amerika ya Kaskazini, wazo la Dini ya Buddha la kutafuta “ukweli” ndani ya mtu mwenyewe yaonekana linavutia wengi, na zoea hilo la kutafakari linatoa njia ya kuepea makelele ya maisha ya nchi za Magharibi. Yapendeza kwamba katika utangulizi wa kitabu Living Buddhism, Tenzin Gyatso, Dalai Lama wa Tibet aliye uhamishoni, aliandika: “Labda leo Dini ya Buddha yaweza kuwa na sehemu ya kutimiza katika kuwakumbusha watu wa nchi za magharibi maisha zao ni zenye kadiri gani ya kiroho.”
Njia za Dini ya Buddha za Namna Mbalimbali
26. Ni katika njia zipi Dini ya Buddha imegawanyika?
26 Ingawa ni desturi kuzungumza juu ya Dini ya Buddha kuwa dini moja, kwa kweli imegawanyika katika vikundi vingi vyenye mawazo tofauti. Kwa kutegemea tafsiri tofauti-tofauti za asili ya Buddha na mafundisho yake, kila kimoja kina imani, mazoea, na maandiko yacho yenyewe. Vikundi hivi vyenye mawazo tofauti vimegawanywa zaidi kuwa vikundi na faraka nyingi, vingi vya hivyo vikiongozwa sana na utamaduni na mapokeo ya mahali pavyo.
27, 28. Ungeeleza jinsi gani juu ya Dini ya Buddha ya Theravada? (Linganisha Wafilipi 2:12; Yohana 17:15, 16.)
27 Kikundi chenye mawazo tofauti cha Dini ya Buddha Theravada (Njia ya Wazee), au Hinayana (Kichukuzi Kidogo Zaidi), husitawi katika Sri Lanka, Myanmar (Burma), Thailand, Kampuchea (Kambodia), na Laos. Wengine hukiona hiki kuwa kikundi chenye mawazo tofauti ya kuhifadhi mambo ya kale. Hukazia kupata hekima na mtu kujifanyia wokovu wake mwenyewe kwa kukataa katakata ulimwengu na kuishi maisha ya mtawa, kujitoa kwa kutafakari na kujifunza katika makao ya kitawa.
28 Ni jambo la kawaida katika baadhi ya mabara hayo kuona vikundi vya wanaume vijana wenye vichwa vilivyonyolewa, wamevaa majoho mekundu-dhahabu na nyayo zisizo na viatu, wamebeba vibakuli vyao vya kuomba fedha ili wapokee riziki yao ya kila siku kutoka kwa waumini wa kawaida ambao fungu lao ni kuwategemeza. Ni desturi wanaume kutumia angalau sehemu fulani ya maisha yao katika makao ya kitawa. Mradi wa upeo wa maisha katika makao ya kitawa ni kuwa arhat, yaani, mtu ambaye amefikia ukamilifu wa kiroho na kukombolewa kutoka maumivu na mateso yaliyo katika marudio ya kuzaliwa tena. Buddha ameonyesha njia; ni juu ya kila mmoja kuifuata.
29. Ni tabia gani zilizo za Dini ya Buddha ya Mahayana? (Linganisha 1 Timotheo 2:3, 4; Yohana 3:16.)
29 Kikundi chenye mawazo tofauti cha Dini ya Buddha Mahayana (Kichukuzi Kikubwa Zaidi) kwa ujumla chapatikana China, Korea, Japan, na Vietnam. Kinaitwa hivyo kwa sababu hukazia fundisho la Buddha kwamba “ukweli na njia ya kwenda kwenye wokovu ni kwa ajili ya kila mtu awe anaishi ndani ya pango, makao ya kitawa, au nyumba . . . Si kwa ajili ya wale tu wanaoukataa ulimwengu.” Wazo la msingi la Mahayana ni kwamba upendo na huruma ya Buddha ni kubwa mno kwamba hawezi kunyima yeyote wokovu. Hufundisha kwamba kwa sababu asili ya Buddha imo ndani yetu sisi sote, kila mtu aweza kuwa Buddha, aliyenurishwa, au bodhisattva. Mnurisho hautokani na nidhamu ya kujikana mno, bali kwa imani katika Buddha na kuhurumia vitu vyote vilivyo hai. Kwa wazi hiki chavutia zaidi umati mkubwa wa watu wenye kutaka kufanya mambo kwa uhalisi wayo. Hata hivyo kwa sababu ya kuwa na mtazamo huu ulio mkunjufu zaidi, vikundi na vidhehebu vingi vimetokea.
30. Wajitoaji wa Dini ya Buddha wa “Bara Lenye Utakato” hutafuta mradi gani? (Linganisha Mathayo 6:7, 8; 1 Wafalme 18:26, 29.)
30 Kati ya faraka nyingi za Mahayana ambazo zimesitawi katika China na Japan ni kikundi chenye mawazo tofauti cha Dini ya Buddha ya Bara Lenye Utakato na Zen. Kiini cha itikadi ya kile kilichotangulia ni imani katika nguvu zenye kuokoa za Amida Buddha, aliyeahidi wafuasi wake kuzaliwa tena katika Bara Lenye Utakato, au Paradiso ya Magharibi, bara lenye shangwe na upendezi lenye kukaliwa na vijimungu na wanadamu. Kutoka hapo, ni hatua rahisi kwenda Nirvana. Kwa kurudia sala “Naweka imani yangu katika Amida Buddha,” nyakati nyingine mara maelfu kwa siku moja, mjitoaji hujitakasa mwenyewe kusudi afikie mnurisho au apate kuzaliwa tena katika Paradiso ya Magharibi.
31. Ni mambo gani yanayohusu Dini ya Buddha ya Zen? (Linganisha Wafilipi 4:8.)
31 Dini ya Buddha ya Zen (katika China kikundi chenye mawazo tofauti cha Ch’an) ilitoa jina layo kutoka kwa zoea la kutafakari. Maneno ch’an (Kichina) na zen (Kijapan) ni miachano ya neno dhyãna la Sanskrit, linalomaanisha “kutafakari.” Nidhamu hiyo hufundisha kwamba kujifunza, matendo mema, na desturi hazina ustahili mkubwa. Mtu aweza kufikia mnurisho kwa kufikiria tu vitendawili visivyowazika kama, ‘Mkono mmoja upigao makofi una sauti gani?’ na, ‘Twapata nini mahali patupu?’ Asili ya kimafumbo ya Dini ya Buddha ya Zen imejionyesha katika sanaa bora za kupanga maua, mwandiko wa ustadi, kusawiri kwa wino, kutunga mashairi, kulima bustani, na kadhalika, na mambo hayo yamepokewa vizuri katika nchi za Magharibi. Leo, vitovu vya utafakari wa Zen vyapatikana katika nchi nyingi za Magharibi.
32. Dini ya Buddha ya Tibet inazoewaje?
32 Hatimaye, kuna Dini ya Buddha ya Tibet, au Dini ya Lama. Namna hii ya Dini ya Buddha nyakati nyingine huitwa Mantrayana (Kichukuzi cha Mantra) kwa sababu ya matumizi maarufu ya mantra, mfululizo wa silabi zenye maana au zisizo nayo, katika ukariri mrefu. Badala ya kukazia hekima au huruma, namna hii ya Dini ya Buddha hukazia matumizi ya sherehe za ibada, sala, mizungu, na uwasiliani-roho katika ibada. Sala hurudiwa mara maelfu kwa siku moja kwa kutumia shanga za sala na magurudumu ya sala. Sherehe hizo za ibada zilizotatanika zaweza kujifunzwa tu chini ya maagizo ya mdomo ya walama, au viongozi wa makao ya kitawa, kati yao wajulikano zaidi ni Dalai Lama na Panchen Lama. Baada ya kifo cha lama, mtoto hutafutwa ambaye yasemekana lama amezaliwa tena katika umbo lake ili awe kiongozi wa kiroho mwandamizi. Hata hivyo, usemi huo kwa ujumla pia hutumiwa kwa watawa wote, ambao, kulingana na kadirio moja, wakati mmoja walifikia hesabu yapata sehemu moja ya tano ya idadi yote ya watu wa Tibet. Malama pia walitumika wakiwa wafundishaji, madaktari, wenyeji wa mashamba, na wanasiasa.
33. Ni jinsi gani migawanyiko ya Dini ya Buddha inafanana na ile ya Jumuiya ya Wakristo? (Linganisha 1 Wakorintho 1:10.)
33 Migawanyiko hiyo mikubwa ya Dini ya Buddha nayo inagawanywa kuwa vikundi vingi, au faraka. Vingine vimejitoa kwa kiongozi fulani, kama vile Nichiren katika Japan, aliyefundisha kwamba ni Lotus Sutra ya Mahayanani pekee ndiyo yenye mafundisho kamili ya Buddha, na Nun Ch’in-Hai katika Taiwan, mwenye umati mkubwa wa wafuasi. Katika jambo hilo, Dini ya Buddha haitofautiani sana na Jumuiya ya Wakristo yenye vikundi na faraka nyingi. Kwa kweli ni kawaida kuona watu wanaodai kuwa wafuasi wa Dini ya Buddha wakishiriki katika mazoea ya Dini ya Tao, Dini ya Shinto, ibada ya wazazi wa kale waliokufa, na hata yale ya Jumuiya ya Wakristo.b Faraka zote hizi za Dini ya Buddha hudai kutegemeza itikadi na mazoea yazo juu ya mafundisho ya Buddha.
Vikapu Vitatu na Maandiko Mengine ya Dini ya Buddha
34. Tunapaswa kukumbuka nini tunapofikiria mafundisho ya Dini ya Buddha?
34 Mafundisho yanayosemwa kuwa ya Buddha yalipokezanwa kwa neno la mdomo na yalianza kuandikwa tu karne nyingi baada ya yeye kufa. Hivyo, kwa ujumla yanawakilisha yale ambayo wafuasi wake katika vizazi vilivyofuata walidhani yeye alisema na kufanya. Hilo latatanishwa zaidi na uhakika wa kwamba, kufikia wakati huo, Dini ya Buddha ilikuwa imefarakana kuwa vikundi vingi vyenye mawazo tofauti. Kwa njia hiyo, maandishi tofauti yaeleza Dini ya Buddha kwa kutofautiana sana.
35. Ni yapi maandishi matakatifu ya Dini ya Buddha yaliyo ya mapema zaidi?
35 Ya mapema kabisa kati ya maandishi ya Dini ya Buddha yaliandikwa katika Kipali, kinachosemekana kuwa lugha ya kuzaliwa ya Buddha, karibu na karne ya kwanza K.W.K. Yanakubaliwa na kikundi chenye mawazo tofauti cha Theravada kuwa maandishi asilia. Jumla ni vitabu 31 vilivyopangwa katika mikusanyo mitatu inayoitwa Tipitaka (Sanskrit, Tripitaka), kumaanisha “Vikapu Vitatu,” au “Mikusanyo Mitatu.” Vinaya Pitaka (Kikapu cha Nidhamu) hushughulika hasa na kanuni na virekebi kwa ajili ya watawa wa kiume na wa kike. Sutta Pitaka (Kikapu cha Mahubiri) ni kuhusu mahubiri, mifano ya maneno, na mithali zilizotolewa na Buddha na wanafunzi wake mashuhuri. Hatimaye, Abhidhamma Pitaka (Kikapu cha Fundisho la Upeo) ni kuhusu maelezo juu ya mafundisho ya Dini ya Buddha.
36. Ni nini kinachoonyesha tabia ya Maandiko ya Dini ya Buddha ya Mahayana?
36 Kwa upande mwingine, maandiko ya kikundi chenye mawazo tofauti cha Mahayana kwa sehemu kubwa ni katika Sanskrit, Kichina, na Kitibet, nayo ni mengi mno. Maandishi ya Kichina pekee ni jumla ya mabuku zaidi ya 5,000. Yana mawazo mengi ambayo hayakuwako katika maandishi ya mapema zaidi, kama vile masimulizi ya Mabuddha wengi kama mchanga wa Ganges, ambao yasemekana waliishi kwa mamilioni yasiyohesabika ya miaka, kila mmoja akisimamia ulimwengu wake wa Buddha. Si kutia chumvi wakati mwandikaji mmoja anaposema kwamba maandishi hayo “yamejaa utofautiano, mawazo yenye kuzidi mno, watu waliorembwa kupita kiasi, na kurudia-rudia mambo mno.”
37. Ni matatizo gani yaliyotokezwa na maandishi ya Mahayana? (Linganisha Wafilipi 2:2, 3.)
37 Bila shaka ni watu wachache wanaoweza kuelewa tungo hizo za kudhania. Matokeo ni kwamba, mambo hayo yaliyositawi baadaye yameondosha Dini ya Buddha mbali na alichokusudia Buddha mwenyewe hapo awali. Kulingana na Vinaya Pitaka, Buddha mwenyewe alitaka mafundisho yake yaeleweke na kila namna ya mtu, si tabaka la waelimu peke yao. Kwa sababu hiyo, yeye alisisitiza kwamba mawazo yake yafundishwe katika lugha ya watu wa kawaida, wala si lugha takatifu isiyotumika ya Uhindu. Kwa hiyo, wafuasi wa Dini ya Buddha ya Theravada wanapotoa kipingamizi kwamba vitabu hivi havikuwa vyenye kukubalika, jibu la wafuasi wa Mahayana ni kwamba Gautama Buddha kwanza alifunza watu wa vivi hivi na wasiojua kitu, lakini kwa walioelimika na wenye hekima alifunua mafundisho yaliyoandikwa baadaye katika vitabu vya Mahayana.
Mrudio wa Karma na Samsara
38. (a) Ni jinsi gani mafundisho ya Dini ya Buddha na Uhindu yalivyo yakilinganishwa? (b) Wazo la Dini ya Buddha kinadharia na kihalisi juu ya nafsi ni nini?
38 Ingawa Dini ya Buddha ilikomboa watu kwa kadiri fulani kutoka kwa pingu za Uhindu, mawazo yayo ya msingi yangali ni urithi wa mafundisho ya Kihindu ya Karma na samsara. Dini ya Buddha, kama ambavyo hapo awali ilifunzwa na Buddha mwenyewe, yatofautiana na Uhindu kwa sababu hukataa kuwapo kwa nafsi isiyoweza kufa lakini huzungumza juu ya mtu kuwa “mchanganyiko wa kani au nishati za kimwili na kiakili.”c Hata hivyo, mafundisho yayo yangali yategemea mawazo ya kwamba binadamu wote hutanga-tanga kutoka maisha haya mpaka haya kupitia kuzaliwa tena kusikohesabika (samsara) na kuteseka kwa sababu ya vitendo vya wakati uliopita na vya wakati huu (Karma). Hata ingawa ujumbe wayo wa mnurisho na kukombolewa katika mrudio huo waweza kuonekana kuwa wenye kuvutia, wengine huuliza: Msingi ni timamu kadiri gani? Kuna uthibitisho gani kwamba mateso yote ni kwa sababu ya vitendo vya mtu vya maisha yaliyotangulia? Na, kwa kweli, kuna uthibitisho gani kwamba kuna maisha ya wakati uliopita?
39. Maandishi fulani ya Dini ya Buddha hufafanuaje sheria ya Karma?
39 Ufafanuzi mmoja juu ya sheria ya Karma husema:
“Kamma [katika Kipali ni kisawe cha Karma] yenyewe ni sheria. Lakini si lazima kuweko mtoa-sheria. Sheria za kawaida za asili, kama uvutano, hazihitaji mtoa-sheria. Sheria ya Kamma pia haina mtoa-sheria. Hiyo hujitendesha yenyewe katika uwanja wayo bila ya kuingiliwa na kitenzi fulani cha nje kitawalacho, chenye kujitegemea.”—A Manual of Buddhism.
40. (a) Kuwapo kwa sheria za asili kunaonyesha nini? (b) Biblia yasema nini juu ya kisababishi na tokeo?
40 Je! huko ni kusababu timamu? Je! sheria za asili hazihitaji kweli kuwe mtoa-sheria? Mtaalamu wa roketi Dakt. Wernher von Braun alieleza hivi wakati mmoja: “Sheria za asili za ulimwengu wote ni sahihi kabisa hata kwamba hatutatiziki kuunda chombo cha angani kiruke kwenda kwenye mwezi na twaweza kupangia mruko huo kwa usahihi kabisa wa kisehemu cha sekunde. Lazima sheria hizo ziwe ziliwekwa na mtu fulani.” Pia Biblia husema juu ya sheria ya kisababishi na tokeo. Hutuambia, “Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.” (Wagalatia 6:7) Badala ya kusema sheria hiyo haihitaji mtoa-sheria, yataja kwamba “Mungu hadhihakiwi,” kuonyesha kwamba sheria hiyo ilianzishwa na Mfanyizi wayo, Yehova.
41. (a) Ni ulinganifu gani unaoweza kufanywa kati ya sheria ya Karma na sheria ya mahakama? (b) Tofautisha Karma na ahadi ya Biblia.
41 Kuongezea hayo, Biblia hutuambia kwamba “mshahara wa dhambi ni mauti,” na “aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi [zake].” Hata mahakama za hukumu zatambua kwamba hakuna anayepaswa kuhatarishwa maradufu kwa ajili ya uhalifu wowote. Basi, kwa nini mtu ambaye tayari amekwisha lipia dhambi zake kwa kufa azaliwe tena ili apatwe upya na matokeo ya vitendo vyake vya wakati uliopita? Isitoshe, bila ya kujua ni kwa ajili ya vitendo gani vya wakati uliopita mtu anaadhibiwa, atawezaje kutubu na kufanya maendeleo? Je! hiyo yaweza kuonwa kuwa haki? Je! yapatana na rehema, inayosemekana kuwa ndiyo sifa yenye kutokeza ya Buddha? Kinyume cha hilo, Biblia, baada ya kutaja kwamba “mshahara wa dhambi ni mauti,” yaendelea kusema: “Bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Ndiyo, inaahidi kwamba Mungu atakomesha kuharibika kwote, dhambi, na kifo naye ataleta uhuru na ukamilisho kwa ajili ya ainabinadamu wote.—Warumi 6:7, 23; 8:31; Isaya 25:8.
42. Msomi mmoja wa Dini ya Buddha hufafanuaje kuzaliwa tena?
42 Kuhusu kuzaliwa tena, kuna ufafanuzi fulani wa msomi wa Dini ya Buddha Dakt. Walpola Rahula:
“Mtu si kitu ila ni mchanganyiko wa kani au nishati za kimwili na kiakili. Tunachoita kifo ni jumla ya kutotenda kwa mwili wa kimnofu. Je! kani na nishati zote hizo hukoma kabisa mwili uachapo kutenda? Dini ya Buddha husema ‘La.’ Nia, uchaguzi, tamaa, kiu ya kuishi, kuendelea, kuzidi, ni kani yenye nguvu inayosukuma uzima wote, maisha zote, inayosukuma hata ulimwengu mzima. Hiyo ndiyo kani kubwa kabisa, nishati kubwa zaidi katika ulimwengu. Kulingana na Dini ya Buddha, kani hiyo haikomi mwili unapoacha kutenda, yaani kifo; bali huendelea kujidhihirisha katika umbo jingine, ikitokeza maisha mengine yanayoitwa kuzaliwa tena.”
43. (a) Kibayolojia, visadifu vya mtu huamuliwaje? (b) Ni “uthibitisho” gani unaotolewa safari nyingine kuunga mkono kuzaliwa tena? (c) Je! “uthibitisho” huo wa kuzaliwa tena wapatana na ambayo sote hujionea?
43 Dakika ile ya kutungwa mimba, mtu hurithi asilimia 50 ya visadifu vyake (tabia zinazorithiwa) kutoka kwa kila mzazi. Kwa hiyo haiwezekani kamwe awe asilimia 100 kama mtu mwingine aliyekuwapo katika maisha yaliyotangulia. Hakika, kuzaliwa tena hakuwezi kuungwa mkono na kanuni yoyote inayojulikana ya sayansi. Pindi nyingi, wale wanaoamini fundisho la kuzaliwa tena hutaja kuwa uthibitisho maono ya watu wanaodai hukumbuka nyuso, matukio, na mahali ambako hapo awali hawajapata kupajua. Je! hilo ni jambo la kusababu vizuri? Kusema kwamba mtu anayekumbuka mambo ya nyakati zilizopita lazima awe aliishi katika enzi hiyo, mtu angepaswa kusema pia kwamba mtu anayeweza kutabiri ya wakati ujao—na kunao wengi wanaodai hufanya hivyo—lazima awe aliishi katika wakati ujao. Kwa wazi sivyo ilivyo.
44. Linganisha fundisho la Biblia kuhusu “roho” na fundisho la Dini ya Buddha la kuzaliwa tena.
44 Miaka zaidi ya 400 kabla ya Buddha, Biblia ilinena juu ya kani ya uhai. Ikieleza yanayotukia wakati wa kifo cha mtu, yasema: “Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa.” (Mhubiri 12:7) Neno hilo “roho” limetafsiriwa kutoka neno la Kiebrania ruʹach, linalomaanisha kani ya uhai inayotendesha viumbe vyote vilivyo hai, binadamu na mnyama. (Mhubiri 3:18-22) Hata hivyo, tofauti ya maana ni kwamba ruʹach ni kani isiyo na utu; haina nia yayo yenyewe au haibaki ikiwa na utu au tabia zozote za mtu aliyekufa. Haitoki kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine wakati wa kufa bali “[h]umrudia Mungu aliyeitoa.” Kwa maneno mengine, mataraja ya uhai wa wakati ujao wa mtu huyo—tumaini la ufufuo—yamo mikononi mwa Mungu tu.—Yohana 5:28, 29; Matendo 17:31.
Nirvana—Kufikia Kisichofikika
45. Wazo la Dini ya Buddha la Nirvana ni nini?
45 Hilo latuleta kwenye fundisho la Buddha juu ya mnurisho na wokovu. Kwa semi za Dini ya Buddha, wazo la msingi la wokovu ni kukombolewa na sheria za Karma na samsara, na pia kufikia Nirvana. Na Nirvana ni nini? Maandishi ya Dini ya Buddha husema kwamba haiwezekani kufafanua au kusimulia ila tu mtu aweza kujionea. Si mbingu fulani aendako mtu baada ya kifo bali mfikio unaowezekana kwa wote, mara hii. Neno lenyewe lasemekana kumaanisha “kuzima kwa kupulizia, kuzimisha.” Kwa hiyo, wengine hueleza Nirvana kuwa kwisha kwa harara na tamaa yote; maisha yasiyo na hisia za neva, kama vile maumivu, hofu, kutaka, upendo, au chuki; hali ya amani ya milele, pumziko, na kutobadilika. Kwa ujumla, husemekana kuwa kukoma kwa kuwako kwa mtu.
46, 47. (a) Kulingana na mafundisho ya Dini ya Buddha, ni nini chanzo cha wokovu? (b) Ni kwa nini maoni ya Dini ya Buddha juu ya chanzo cha wokovu yanapingana na mambo ambayo sote tumejionea?
46 Buddha mwenyewe alifundisha kwamba mnurisho na wokovu—ukamilifu wa Nirvana—hutokana, si na Mungu yeyote wala kani ya nje, bali ndani ya mtu kupitia jitihada yake mwenyewe kwa vitendo vyema na mawazo sahihi. Hilo latokeza swali hili: Je! kuna kikamilifu kinachoweza kutokana na kitu kisicho kikamilifu? Je! mambo ya kawaida tuliyojionea hayatuambii, kama ambavyo nabii Mwebrania Yeremia alivyotuambia, kwamba “njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu”? (Yeremia 10:23) Ikiwa hakuna anayeweza kuongoza kabisa vitendo vyake hata katika mambo mepesi ya kila siku, je! ni kusababu kuzuri kufikiri kwamba yeyote aweza kujifanyia wokovu wake wa milele kwa kujitegemea tu?—Zaburi 146:3, 4.
47 Sawa na mtu aliyekwama katika tope lenye kunata asivyoelekea kujikwamua kwa jitihada yake mwenyewe, ndivyo ainabinadamu wote walivyonaswa katika dhambi na kifo, na hakuna anayeweza kujinasua kwa mtego huo. (Warumi 5:12) Hata hivyo, Buddha mwenyewe alifundisha kwamba wokovu wategemea jitihada ya mtu mwenyewe peke yake. Waidha lake la kuaga wanafunzi wake lilikuwa “jitegemeeni wenyewe wala msitegemee msaada wa kutoka nje; ushikeni kabisa ukweli kuwa taa; tafuteni wokovu peke yake katika ukweli; msitafute msaada kwa yeyote isipokuwa kwenu wenyewe.”
Mnurisho au Mzinduko
48. (a) Kitabu kimoja chaelezaje juu ya matokeo yaliyotatanika ya mawazo ya Dini ya Buddha kama vile Nirvana? (b) Ni nini yamekuwa matokeo ya kupendezwa kwa karibuni na mafundisho ya Dini ya Buddha katika maeneo fulani?
48 Ni nini matokeo ya fundisho hilo? Je! linachochea waumini walo kwenye imani na ujitoaji wa kweli? Kitabu Living Buddhism charipoti kwamba katika nchi fulani za Dini ya Buddha, hata “watawa hawafikirii sana mambo bora sana ya dini yao. Kufikia Nirvāna kunafikiriwa na wengi kuwa mradi ambao hakuna tumaini la kuufikia, na kutafakari kunazoewa mara chache. Mbali na uchunguzi mbadilifu wa kawaida wa Tipitaka, wao wanajishughulisha kuwa uvutano wenye hisani na wenye upatani katika jumuiya.” Hali moja na hiyo, World Encyclopedia (Kijapan), katika kueleza juu ya mvuvumko wa karibuni wa kupendezwa na mafundisho ya Dini ya Buddha, chasema: “Kadiri uchunguzi wa Dini ya Buddha uzidivyo kuwa aina pekee ya kujifunza, ndivyo izidivyo kuondoka kwenye kusudi layo la awali—kuongoza watu. Kwa maoni hayo, mtindo wa hivi karibuni wa uchunguzi mkali wa Dini ya Buddha haumaanishi kwa lazima kufufuliwa kwa imani iliyo hai. Badala yake, lazima iangaliwe kwamba wakati dini inapokuwa kitu cha usomi uliotatanika wa kimetafizikia, uhai wayo halisi wa imani unapoteza nguvu zao.”
49. Kwa wengi, Dini ya Buddha imekuwa nini?
49 Wazo la msingi la Dini ya Buddha ni kwamba maarifa na ufahamu huongoza kwenye mnurisho na wokovu. Lakini mafundisho yaliyotatanika ya vikundi mbalimbali vyenye mawazo tofauti vya Dini ya Buddha yametokeza tu hali iliyotajwa juu “hakuna tumaini la kuufikia,” jambo ambalo waumini walio wengi hawawezi kulipata. Kwao, Dini ya Buddha imekuwa ni kufanya wema na kufuata sherehe chache za maagizo mepesi. Haitatui maswali ya maisha yenye kutatanisha, kama vile: Sisi hutoka wapi? Kwa nini tupo hapa? Na wakati ujao ni nini kwa binadamu na dunia?
50. Ni swali gani linalokuja akilini kwa sababu ya mambo kadhaa waliyojionea wafuasi wa Dini ya Buddha fulani wenye moyo mweupe? (Linganisha Wakolosai 2:8.)
50 Wafuasi fulani wa Dini ya Buddha wenye mioyo myeupe wametambua vurugu na mzinduko unaotokana na mafundisho tata na sherehe zenye kulemea za Dini ya Buddha kama inavyozoewa leo. Jitihada za kibinadamu za vikundi na vyama vya Dini ya Buddha katika baadhi ya nchi huenda zikawa zimeleta faraja kutoka maumivu na taabu kwa wengi. Lakini ikiwa chanzo cha mnurisho na ukombozi wa kweli kwa ajili ya wote, je! Dini ya Buddha imetimiza ahadi yayo?
Mnurisho Bila ya Mungu?
51. (a) Kituko kimoja chaeleza nini juu ya mafundisho ya Buddha? (b) Ni jambo gani la maana lililoachwa ambalo ni wazi halikutajwa katika mafundisho ya Buddha? (Linganisha 2 Mambo ya Nyakati 16:9; Zaburi 46:1; 145:18.)
51 Masimulizi ya maisha ya Buddha yaeleza kwamba katika pindi moja yeye na wanafunzi wake walikuwa katika msitu. Alichukua gao la majani na kuwaambia wanafunzi wake hivi: “Mambo ambayo mimi nimewafunza yanalingana na majani haya katika mkono wangu, mambo ambayo sijawafunza yanalingana na kiasi cha majani katika msitu huu.” Bila shaka, wazo ni kwamba Buddha alikuwa amefundisha kisehemu tu cha yale aliyojua. Hata hivyo, kuna jambo moja la maana lililoachwa—Gautama Buddha karibu hakuwa na chochote cha kusema juu ya Mungu; wala yeye hakudai kamwe kuwa Mungu. Kwa kweli, yasemekana kwamba aliwaambia wanafunzi wake, “Kama kuna Mungu, haiwaziki kwamba Yeye angehangaishwa na shughuli zangu za siku baada ya siku,” na “hakuna vijimungu viwezavyo au vitakavyosaidia binadamu.”
52. (a) Maoni ya Dini ya Buddha juu ya Mungu ni nini? (b) Dini ya Buddha imepuuza nini?
52 Kwa maana hiyo, fungu la Dini ya Buddha katika kusaidia ainabinadamu katika jitihada ya kutafuta Mungu ni dogo mno. The Encyclopedia of World Faiths chasema kwamba “Dini ya Buddha ya mapema yaelekea haikufikiria swali la Mungu, na bila shaka haikufunza ama kutaka imani katika Mungu.” Katika kukazia kila mtu kujitafutia wokovu kwa kujitegemea, kugeukia ndani katika akili au fahamu zake mwenyewe kwa ajili ya mnurisho, Dini ya Buddha kwa kweli ni uagnosti, kama si uatheisti. (Ona kisanduku, ukurasa 145.) Katika kujaribu kutupilia mbali pingu za Uhindu za ushirikina na vijimungu vyao vingi vyenye kubumbuaza, Dini ya Buddha imevuka ng’ambo ile nyingine. Ilipuuza wazo la msingi la Mtu Aliye Mkuu Kabisa, ambaye kwa mapenzi yake kila kitu kinaishi na kutenda.—Matendo 17:24, 25.
53. Ni nini laweza kusemwa juu ya kutafuta mnurisho bila ya Mungu? (Linganisha Mithali 9:10; Yeremia 8:9.)
53 Kwa sababu ya njia hii ya kufikiri ya kujielekezea fikira na ya kujitegemea, matokeo ni mvurugo halisi wa hekaya, mapokeo, mafundisho yaliyotatanika, na fasiri zilizotokezwa na vikundi vingi vyenye mawazo tofauti na faraka muda wa karne nyingi. Kilichokusudiwa kiwe utatuzi mwepesi wa matatizo ya maisha yaliyotatanika kimekuwa mfumo wa kidini na kifalsafa ambao watu walio wengi hawawezi kuuelewa. Badala yake, mfuasi wa wastani wa Dini ya Buddha hujishughulisha tu na kuabudu sanamu na vitu vya ukumbusho vya watakatifu, vijimungu na mashetani, roho na wazazi wa kale waliokufa, na kufanya sherehe za kiibada na mazoea mengine mengi yasiyohusiana na yale ambayo Gautama Buddha alifundisha. Kwa wazi, jitihada ya kutafuta mnurisho bila ya Mungu haileti mafanikio.
54. Ni mafundisho gani ya wafikiriaji-dini wengine wa nchi za Mashariki yatafikiriwa halafu?
54 Karibu na wakati uo huo ambao Gautama Buddha alikuwa akifanya jitihada ya kutafuta njia ya mnurisho, katika sehemu nyingine ya kontinenti ya Asia waliishi wanafalsafa wawili ambao mawazo yao yalikuja kuvuta mamilioni ya watu. Wao walikuwa ni La-tzu na Confucius, watu hao wawili wenye hekima nyingi wameheshimiwa mno na vizazi vingi vya Wachina na wengine. Wao walifundisha nini, nao walikuwa na uvutano gani juu ya jitihada ya ainabinadamu kutafuta Mungu? Hayo ndiyo tutachunguza katika sura inayofuata.
[Maelezo ya Chini]
a Huu ni mwendelezo wa Kipali uliotoholewa wa jina lake. Katika Sanskrit utohozi huo ni Siddhārtha Gautama. Hata hivyo, tarehe yake ya kuzaliwa imetolewa ikitofautiana-tofautiana kuwa 560, 563, au 567 K.W.K. Wasomi wengi hukubali tarehe 560 au angalau huweka kuzaliwa kwake katika karne ya sita K.W.K.
b Wafuasi wa Dini ya Buddha wengi katika Japan husherehekea “Krismasi” yenye ushaufu.
c Mafundisho ya Dini ya Buddha, kama vile anatta (hakuna hatinafsi), hukanusha maisha yasiyobadilika au nafsi ya milele. Hata hivyo, wafuasi wa Dini ya Buddha walio wengi leo, hasa wale katika Mashariki ya Mbali, huamini kuhama kwa nafsi isiyoweza kufa kuingia katika mwili mwingine. Zoea lao la kuabudu wazazi wa kale waliokufa na imani katika helo baada ya kifo hudhihirisha hili.
[Sanduku katika ukurasa wa 139]
Kweli Bora Nne za Budha
Buddha alifafanua fundisho lake la msingi katika zile zinazoitwa Kweli Bora Nne.Hapa tunanukuu kutoka Dhammacakkappavattana Sutta (Msingi wa Ufalme wa Uadilifu), katika tafsiri ya T. W. Rhys Davids:
◼ “Sasa huu, Ewe Bhikkus, ndio ukweli bora kuhusu kuteseka. Kuzaliwa hufuatana na maumivu, uozi una maumivu, maradhi yana maumivu, kifo kina maumivu. Kuungana na kisichopendeza kuna maumivu, kutenganishwa na chenye kupendeza kuna maumivu; na uchu wowote usiotoshelezwa, una maumivu pia. . . .
◼ “Sasa huu, Ewe Bhikkus, ndio ukweli bora kuhusu asili ya kuteseka. Kwa kweli, ni kile kiu, kinachosababisha kufanywa upya kwa maisha, kikifuatana na na upendezi wa kianasa, kutafuta utoshelezo sasa hapa, sasa pale—ndiyo kusema, kuwa na uchu wa kutoshelezwa kwa harara, au uchu wa uhai, au uchu wa kufanikiwa. . . .
◼ “Sasa huu, Ewe Bhikkus, ndio ukweli bora kuhusu uharibifu wa kuteseka. Kwa kweli, ni uharibifu, ambao katika huo harara hubaki, wa kiu iki hiki; kuweka kando, kuondosha, kuwa huru na, kutoendelea kuwa na kiu hiki . . .
◼ “Sasa huu, Ewe Bhikkus, ndio ukweli bora kuhusu njia inayoongoza kwenye uharibifu wa huzuni. Kwa kweli, njia hii bora yenye sehemu nane; ndiyo kusema: maoni sahihi; miradi sahihi, usemi sahihi; mwenendo sahihi; riziki sahihi; jitihada sahihi; wanio sahihi; na ufikiri sahihi.”
[Sanduku katika ukurasa wa 145]
Dini ya Buddha na Mungu
Dini ya Buddha hufundisha njia inayoongoza kwenye wema kamilina hekima bila ya Mungu mwenye utu; maarifaya juu kabisa bila ya ‘ufunuo’; . . . uwezekanowa kukombolewa bila ya mkombozi wa wengine, wokovuambao katika huo kila mtu ndiye mwokozi wake mwenyewe.”—The Message ofBuddhism, cha Bhikkhu Subhadra, kama ilivyonukuliwa katika What Is Buddhism?
Basi je! wafuasi wa Dini ya Buddha ni waatheisti? Kitabu What Is Buddhism? kilichochapishwa na Buddhist Lodge, London, hujibu: “Ikiwa kwa atheisti unamaanisha mtu anayekataa wazo la Mungu mwenye utu, basi ndivyo tulivyo.” Ndipo kinapoendelea kusema: “Akili inayokua yaweza kuelewa wazo la Ulimwengu Wote Mzima unaoongozwa na Sheria isiyo na kigeu-geu, sawa na inavyoweza [kuelewa] wazo la Mtu aliye mbali ambaye huenda isipate kumwona kamwe, anayekaa mahali isipojua, na ambaye wakati fulani ameumba kutoka kwa kitu kisichokuwapo Ulimwengu Wote Mzima uliojaa uadui, ukosefu wa haki, ukosefu wa usawa wa nafasi, na kuteseka na mizozo isiyo na mwisho.”
Kwa hiyo, kinadharia, Dini ya Buddha haitetei imani katika Mungu au Muumba. Hata hivyo, mahekalu ya Dini ya Buddha na makuba ya vinara yanapatikana leo katika karibu kila nchi ambayo Dini ya Buddha inazoewa, na mifano na vitu vya ukumbusho vya Mabuddha na mabodhisattva yamekuwa vitu vya kutolewa sala, sadaka, na ujitoaji wa wafuasi wa Dini ya Buddha wenye kufuata dini. Buddha, ambaye hakujidai kamwe kuwa Mungu, amekuwa kijimungu katika kila maana ya neno hilo.
[Ramani katika ukurasa wa 142]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Kufikia karne ya saba W.K., Dini ya Buddha ulikuwa umeenea kutoka India hadi Asia yote ya mashariki
INDIA
Benares
Buddh Gaya
KARNE YA 3 K.W.K. SRI LANKA
KARNE YA 1 K.W.K. KASHMIR
ASIA YA KATI
KARNE YA 1 W.K. CHINA
MYANMAR
THAILAND
KAMPUCHEA
JAVA
KARNE YA 4 W.K. KOREA
KARNE YA 6 W.K. JAPAN
KARNE YA 7 W.K. TIBET
[Picha katika ukurasa wa 131]
Mahekalu ya Dini ya Buddha hutofautiana katika mtindo ulimwenguni pote
Chengteh, China kaskazini
Kofu, Japan
Jiji New York, U.S.A.
Chiang Mai, Thailand
[Picha katika ukurasa wa 133]
Mchongo wa jiwe, Ndoto ya Maya, kutoka Gandhara, Pakistan, waonyesha Buddha wa wakati ujao akiwa kama akiwa kama tembo mweupe nwenye mwenye duara ya nuru akiingia upande wa kulia wa Malkia wa Malkia Maya ili amtie mimba
[Picha katika ukurasa wa 134]
Watawa wa Dini ya Buddha na waabudu katika hekalu katika Jiji New York
[Picha katika ukurasa wa 141]
Mifano ya Buddha yenye ishara za kistaili
akiingia Nirvana
akifundisha
akitafakari
akikinza kishawishi
[Picha katika ukurasa wa 147]
Mwandamano kwa heshima ya siku ya kuzaliwa ya Buddha, katika Tokyo, Japan. Tembo mweupe kule nyuma anawakilisha Buddha
[Picha katika ukurasa wa 150]
Kurasa za Lotus Sutra (karne ya 10), katika Kichina, zaeleza nguvu za bodhisattva Kuan-yin za kuokoa kutoka moto na furiko. Bodhisattva Ksitigarbha, kulia, alikuwa maarufu Korea katika karne ya 14
[Picha katika ukurasa wa 155]
Hati-kunjo ya Dini ya Buddha kutoka Kyoto, Japan, yaonyesha mateso katika “helo”
[Picha katika ukurasa wa 157]
Wafuasi wa Dini ya Buddha leo huabudu, kama inavyoonekana kulingana na mzunguko wa kisaa kutoka juu kushoto, mbele ya lingam katika Bangok, Thailand; Jino la Buddha la ukumbusho katika Kandy, Sri Lanka; mifano ya Buddha katika Singapore na New York
[Picha katika ukurasa wa 158]
Mwanamke mfuasi wa dini ya Buddha akisali mbele ya madhabahu ya familia, na watoto wakishiriki katika ibada ya hekaluni