Sura 23
Miujiza Zaidi Katika Kapernaumu
KATIKA Sabato iliyofuata baada ya Yesu kuwaita wanafunzi wake wanne wa kwanza—Petro, Andrea, Yakobo, na Yohana—wote waenda kwenye sinagogi la kwao katika Kapernaumu. Huko Yesu aanza kufundisha, nao watu washangaa sana kwa sababu awafundisha kama mtu mwenye mamlaka wala si kama waandishi.
Katika Sabato hii mtu aliyepagawa na roho mwovu yupo. Baada ya muda fulani, yeye apaaza sauti akisema: “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu.”
Kwa kweli roho mwovu aongozaye mtu huyo ni mmoja wa malaika za Shetani. Akimkemea roho mwovu huyo, Yesu asema: “Fumba kinywa umtoke!”
Basi, roho mwovu huyo amtupa chini na kumtetemesha mwili kweli kweli na kupiga makelele makubwa. Lakini amtoka mtu huyo bila kumuumiza. Kila mtu ashangaa sana! “Nini hii?” wauliza. “Kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu [roho waovu, NW], nao wamtii.” Habari za jambo hilo zazambaa katika sehemu zote zinazokaribiana na eneo hilo.
Wakiondoka kwenye sinagogi, Yesu na wanafunzi wake waenda nyumbani kwa Simoni, au Petro. Huko mama-mkwe wa Petro ni mgonjwa sana akiwa na homa kali. ‘Tafadhali msaidie,’ wamsihi. Kwa hiyo Yesu asogea, amshika mkono, na kumwinua. Papo hapo apona na kuanza kuwatayarishia chakula!
Baadaye, jua limeshuka, watu kutoka sehemu zote waanza kuja nyumbani kwa Petro wakiwa na wagonjwa wao. Baada ya muda mfupi mji mzima umekusanyika mlangoni! Naye Yesu aponya wagonjwa wao wote, bila kujali wana magonjwa gani. Hata aweka huru waliopagawa na roho waovu. Wanapowatoka, roho aliowafukuza wapaaza sauti hivi: “Wewe u Mwana wa Mungu.” Lakini Yesu awakemea wala hawaruhusu waseme kwa sababu wajua yeye ndiye Kristo. Marko 1:21-34; Luka 4:31-41; Mathayo 8:14-17.
▪ Ni jambo gani latukia katika sinagogi siku ya Sabato baada ya Yesu kuwaita wanafunzi wake wanne?
▪ Yesu aenda wapi aondokapo katika sinagogi, na ni muujiza gani afanya humo?
▪ Ni jambo gani latukia baadaye jioni iyo hiyo?