Maisha na Huduma ya Yesu
Miujiza Mingi Zaidi Katika Kapernaumu
KATIKA Sabato iliyotokea baada ya Yesu kuwaita wanafunzi wake wanne wa kwanza—Petro, Andrea, Yakobo, na Yohana—wote wanaenda kwenye sinagogi la kwao katika Kapernaumu. Huko Yesu anaanza kufundisha, nao watu wanashangaa sana kwa sababu anawafundisha kama mtu mwenye mamlaka wala si kama waandishi.
Katika sabato hii mtu aliyepagawa na pepo yupo. Baada ya muda fulani, yeye anapaaza sauti akisema: “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu.”
Kwa kweli pepo anayeongoza mtu huyo ni mmoja wa malaika za Shetani. Akimkemea pepo huyo, Yesu anasema: “Fumba kinywa, umtoke”!
Basi, pepo huyo anamtupa chini na kumtetemesha mwili kweli kweli na kupiga ukelele mkubwa. Lakini anamtoka mtu huyo bila kumuumiza. Kila mtu anashangaa sana! “Nini hii?” wanauliza. “Kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii.” Habari za jambo hilo zinatapakaa katika sehemu zote zinazokaribiana na eneo hilo.
Wakiondoka kwenye sinagogi, Yesu na wanafunzi wake wanaenda nyumbani kwa Simoni, au Petro. Huko mama-mkwe wa Petro ni mgonjwa sana akiwa na homa kali. ‘Tafadhali msaidie,’ wanamsihi. Kwa hiyo anasogea, anamshika mkono, na kumwinua. Papo hapo anapona na kuanza kuwatayarishia chakula!
Baadaye, jua limeshuka, watu kutoka sehemu zote wanaanza kuja nyumbani kwa Petro wakiwa na wagonjwa wao. Baada ya muda mfupi mji mzima umekusanyika mlangoni! Naye Yesu anaponya wagonjwa wao wote, bila kujali wana magonjwa gani. Hata anaweka watu huru kwa kuwaondolea pepo waliowapagaa. Wanapowatoka, pepo aliowafukuza wanapaaza sauti: “Wewe u Mwana wa Mungu.” Lakini Yesu anawakemea wala hawaruhusu waseme kwa sababu wanajua yeye ndiye Kristo. Marko 1:21-34; Luka 4:31-41; Mathayo 8:14-17.
◆ Ni jambo gani linalotukia katika sinagogi siku ya Sabato baada ya Yesu kuwaita wanafunzi wake wanne?
◆ Yesu anaenda wapi anapoondoka hekaluni, na ni muujiza gani anaoufanya humo?
◆ Ni jambo gani linalotukia baadaye jioni iyo hiyo?
[Picha ya ukurasa nzima katika ukurasa wa 9]