Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • ip-1 sura 17 kur. 215-229
  • “Babeli Umeanguka”!

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • “Babeli Umeanguka”!
  • Unabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “Maono Magumu”
  • “Umeanguka”!
  • Kutafuta Habari Kutoka kwa Mlinzi
  • Usiku Waja Juu ya Uwanda wa Jangwani
  • Mlinzi Akasema: “Umeanguka!”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
  • “Ee Mlinzi Habari Gani za Usiku?”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
  • Kutumikia Pamoja na Mlinzi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
  • Yehova Anyenyekeza Jiji Lenye Kujigamba
    Unabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
Pata Habari Zaidi
Unabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
ip-1 sura 17 kur. 215-229

Sura ya 17

“Babeli Umeanguka”!

Isaya 21:1-17

1, 2. (a) Kichwa kikuu cha Biblia ni nini, lakini ni kichwa kipi chenye kuunga mkono kinachopatikana katika Isaya? (b) Biblia yakuzaje kichwa cha kuanguka kwa Babiloni?

BIBLIA yaweza kufananishwa na wimbo maarufu ulio na kichwa kikuu na vichwa vidogo-vidogo vinavyotiwa ndani ili kuufanya uwe wimbo wa pekee. Vivyo hivyo, Biblia ina kichwa kikuu​—kutetewa kwa enzi kuu ya Yehova kupitia serikali ya Ufalme wa Kimesiya. Pia ina vichwa vingine muhimu, vinavyorudiwa-rudiwa. Kimojawapo ni kuanguka kwa Babiloni.

2 Kichwa hicho chaanzia katika Isaya sura ya 13 na 14. Charudiwa katika sura ya 21 na tena katika sura ya 44 na 45. Karne moja baadaye, Yeremia aongezea kwenye kichwa hicho, na kitabu cha Ufunuo chakileta kwenye upeo usio na kifani. (Yeremia 51:60-64; Ufunuo 18:1–19:4) Kila mwanafunzi wa Biblia anayechukulia mambo kwa uzito apasa kuhangaikia kichwa hicho muhimu kinachounga mkono kichwa kikuu cha Neno la Mungu. Isaya sura ya 21 yatusaidia kufanya hivyo, kwa kuwa yaandaa mambo mengi yenye kupendeza kuhusu kuanguka kulikotabiriwa kwa serikali hiyo kubwa ya ulimwengu. Baadaye, tutaona kwamba Isaya sura ya 21 yakazia kichwa kingine muhimu cha Biblia—kinachotusaidia kuchanganua kukesha kwetu tukiwa Wakristo leo.

“Maono Magumu”

3. Kwa nini Babiloni laitwa ‘nyika ya bahari,’ na jina hilo laashiria nini kuhusu wakati wake ujao?

3 Isaya sura ya 21 yaanza kwa taarifa inayoashiria mabaya: “Ufunuo juu ya bara [“nyika,” “NW”] ya bahari. Kama tufani za Negebu zikaribiavyo kwa kasi, inakuja kutoka bara, toka nchi itishayo.” (Isaya 21:1) Jiji la Babiloni lasambaa pande mbili za Mto Frati, huku upande wake wa mashariki ukiwa katika eneo lililo kati ya mito miwili mikubwa, Frati na Tigris. Jiji hilo liko hatua fulani kutoka kwenye bahari halisi. Mbona basi, laitwa ‘nyika ya bahari’? Kwa sababu eneo la Babiloni lilikuwa na kawaida ya kufurika kila mwaka, likisababisha “bahari” kubwa, yenye matope. Hata hivyo, Wababiloni wamedhibiti nyika hiyo yenye maji mengi kwa kuchimba mitaro, milizamu na mifereji mingi. Wao hutumia maji hayo kwa ustadi yawe sehemu ya mfumo wa kulinda jiji. Ijapokuwa hivyo, hakuna jitihada yoyote ya binadamu itakayookoa Babiloni isihukumiwe na Mungu. Alikuwa nyika—naye atakuwa nyika tena. Maafa yanamwandama, yakijikusanya kama mojawapo ya dhoruba kali ambazo nyakati nyingine huikumba Israeli kutoka kwenye nyika inayotia hofu iliyo upande wa kusini.—Linganisha Zekaria 9:14.

4. Ono la Ufunuo juu ya “Babiloni Mkubwa” latiaje ndani mambo kama vile “maji” na “nyika,” na “maji” yamaanisha nini?

4 Kama tulivyojifunza katika Sura ya 14 ya kitabu hiki, Babiloni la kale lafanana na Babiloni jingine la kisasa—“Babiloni Mkubwa,” milki ya ulimwengu ya dini isiyo ya kweli. Katika Ufunuo, Babiloni Mkubwa vivyo hivyo aonekana akiwa na uhusiano na “nyika” na “maji.” Mtume Yohana apelekwa nyikani kuonyeshwa Babiloni Mkubwa. Aambiwa kwamba yeye “hukaa juu ya maji mengi” yanayowakilisha “vikundi vya watu na umati na mataifa na lugha.” (Ufunuo 17:1-3, 5, 15) Sikuzote kuendelea kwa dini isiyo ya kweli kumetegemea uungaji mkono kutoka kwa watu walio wengi, lakini “maji” hayo hayatamlinda hatimaye. Kama Babiloni la kale, hatimaye atabaki tupu, mwenye kupuuzwa, na mkiwa.

5. Babiloni apataje sifa ya kuwa mwenye ‘kutenda hila’ na “mharibu”?

5 Katika siku ya Isaya, Babiloni bado haijawa serikali kubwa ya ulimwengu, lakini tayari Yehova aona kimbele kuwa wakati wake ufikapo, itatumia mamlaka yake kwa njia mbaya. Isaya aendelea: “Nimeonyeshwa maono magumu; atendaye hila anatenda hila, mharibu anaharibu.” (Isaya 21:2a) Kwa hakika Babiloni ataharibu na kutenda hila dhidi ya mataifa anayoyashinda, kutia ndani Yuda. Wababiloni watateka Yerusalemu nyara, wapore hekalu lake, na kuchukua watu wake mateka hadi Babiloni. Wakiwa huko, mateka hao wasio na uwezo watatendewa hila, watadhihakiwa kwa sababu ya imani yao, nao hawatapewa tumaini lolote la kurudi nchini kwao.—2 Mambo ya Nyakati 36:17-21; Zaburi 137:1-4.

6. (a) Yehova atakomesha huzuni gani? (b) Ni mataifa gani yaliyotabiriwa yatashambulia Babiloni, na hilo latimizwaje?

6 Naam, Babiloni astahili kabisa hayo “maono magumu,” yatakayomsababishia magumu. Isaya aendelea: “Panda juu, Ee Elamu; husuru, Ee Umedi; mimi ninakomesha maombolezo yake yote.” (Isaya 21:2b) Wale wanaoonewa na milki hiyo yenye hila watapata kitulizo. Hatimaye, huzuni yao itakoma! (Zaburi 79:11, 12) Kitulizo hicho kitakujaje? Isaya ataja mataifa mawili yatakayoshambulia Babiloni: Elamu na Umedi. Karne mbili baadaye, mwaka wa 539 K.W.K., Koreshi Mwajemi ataongoza jeshi la mwungano wa Waajemi na Wamedi dhidi ya Babiloni. Kwa habari ya Elamu, watawala wa Uajemi watamiliki angalau sehemu ya nchi hiyo kabla ya mwaka wa 539 K.W.K.a Basi, majeshi ya Uajemi yatatia ndani Waelami.

7. Maono ya Isaya yamwathirije, ikimaanisha nini?

7 Ona maelezo ya Isaya kuhusu athari ya maono hayo kwake: “Kwa sababu hiyo viuno vyangu vimejaa maumivu, utungu umenishika, kama utungu wa mwanamke azaaye; ninaumwa sana, nisiweze kusikia; nimefadhaishwa kwa hofu, nisiweze kuona. Moyo wangu unapiga-piga, utisho umenitaabisha, gizagiza la jioni nilipendalo limegeuka likanitetemesha.” (Isaya 21:3, 4, Chapa ya 1989) Yaonekana nabii huyo hufurahia saa za gizagiza la jioni, wakati mzuri unaofaa kwa kutafakari kimya-kimya. Lakini sasa jioni imepoteza msisimko wake, badala yake inaleta tu hofu, maumivu, na kutetemeka. Yeye apata utungu kama wa mwanamke azaaye, na moyo wake “unapiga-piga.” Msomi mmoja afasiri usemi huo kuwa “moyo wangu unapiga ovyo ovyo,” na kutaarifu kuwa usemi huo warejezea “mpigo wa moyo wenye kuyumba-yumba na usio wa kawaida.” Mbona msononeko huo? Yamkini hisia za Isaya ni za unabii. Katika usiku wa Oktoba 5/6, 539 K.W.K., Wababiloni watakumbwa na hofu kama hiyo.

8. Kama ilivyotabiriwa, Wababiloni watendaje, hata ingawa adui zao wako nje ya kuta?

8 Giza liingiapo usiku huo wenye maafa, Wababiloni hawana hofu hata kidogo. Isaya atabiri hivi karne mbili mapema: “Wanaandika meza, wanaweka ulinzi, wanakula, wanakunywa.” (Isaya 21:5a) Naam, Mfalme Belshaza mwenye kiburi aandaa karamu. Viti vimepangwa kwa ajili ya wakuu wake elfu, na pia wake na masuria wengi. (Danieli 5:1, 2) Wenye kusherehekea wafahamu kuwa kuna jeshi nje ya kuta, lakini waamini kwamba jiji lao haliwezi kupenywa. Kuta zake kubwa mno na mahandaki yake ya maji yenye kina kirefu yafanya lionekane kuwa lisiloweza kamwe kutekwa; miungu yake mingi yafanya kutekwa kusiwazike hata kidogo. Basi, acha ‘wale na wanywe’! Belshaza alewa, na labda wengine pia. Ile haja ya kuwaamsha maofisa wa ngazi za juu yadokeza kuwa wamepumbazika, kama vile maneno yafuatayo ya Isaya yaonyeshavyo kwa njia ya unabii.

9. Kwa nini kuna uhitaji wa ‘kutia ngao mafuta’?

9 “Simameni, enyi wakuu, itieni ngao mafuta.” (Isaya 21:5b) Karamu yaisha ghafula. Yawapasa wakuu wajiamshe! Danieli, nabii mzee, ameitwa, naye aona jinsi Yehova anavyomtia hofu Mfalme Belshaza wa Babiloni, hofu kama ile ambayo Isaya alieleza. Wakuu wa mfalme wavurugika huku majeshi ya mwungano wa Wamedi, Waajemi, na Waelami yashindapo kinga za jiji. Babiloni laanguka mara moja! Lakini, ‘kutia ngao mafuta’ kwamaanisha nini? Nyakati nyingine Biblia humrejezea mfalme wa taifa kuwa ngao yake kwa sababu yeye ndiye anayekinga na kulinda nchi.b (Zaburi 89:18) Basi labda mstari huo katika Isaya watabiri uhitaji wa mfalme mpya. Kwa nini? Kwa sababu Belshaza auawa “usiku uo huo.” Kwa hiyo, kuna uhitaji wa ‘kutia ngao mafuta,’ au kumteua mfalme mpya.—Danieli 5:1-9, 30.

10. Waabudu wa Yehova waweza kupata faraja gani kutokana na utimizo wa unabii wa Isaya unaohusu mwenye kutenda hila?

10 Masimulizi hayo huwafariji wote wapendao ibada ya kweli. Babiloni wa leo, Babiloni Mkubwa, ni mwenye kutenda hila na mharibu kama vile Babiloni ya zamani ilivyokuwa. Hadi leo hii viongozi wa dini hupanga njama Mashahidi wa Yehova wapigwe marufuku, wanyanyaswe, au watozwe kodi kali. Lakini kama unabii huo unavyotukumbusha, Yehova huona matendo hayo yote ya hila, naye bila shaka atawaadhibu. Ataangamiza dini zote zisizomwakilisha ifaavyo na ambazo huwatenda vibaya watu wake. (Ufunuo 18:8) Je, hilo lawezekana? Ili kujenga imani yetu, twahitaji tu kuona jinsi ambavyo maonyo yake kuhusu kuanguka kwa Babiloni ya kale na kule kwa mwenzake wa leo pia kumekwisha timizwa.

“Umeanguka”!

11. (a) Mlinzi ana wajibu gani, naye ni nani leo? (b) Magari ya vita ya punda na ya ngamia huwakilisha nini?

11 Yehova sasa amzungumzia nabii huyo. Isaya aripoti: “Maana Bwana ameniambia hivi, Enenda, weka mlinzi; aonayo na ayatangaze.” (Isaya 21:6) Maneno hayo yaanzisha kichwa kingine muhimu cha sura hiyo—kinachohusu mlinzi. Wakristo wote wa kweli leo wanapendezwa na maneno hayo, kwa kuwa Yesu aliwasihi wafuasi wake ‘wafulize kulinda.’ “Mtumwa mwaminifu na mwenye busara” hakuwahi kamwe kuacha kutangaza yale aonayo kuhusu kukaribia kwa siku ya Mungu ya hukumu na hatari za mfumo huu wenye ufisadi. (Mathayo 24:42, 45-47) Mlinzi kwenye maono ya Isaya aona nini? “Akiona kundi [“gari la vita,” “NW”] la wapanda farasi, wakienda wawili wawili, na kundi [“gari la vita,” “NW”] la punda, na kundi [“gari la vita,” “NW”] la ngamia; asikilize sana, akijitahidi kusikiliza.” (Isaya 21:7) Labda kila gari moja la vita lawakilisha kundi la magari yanayosonga mbele katika mpangilio wa kivita kwa mwendo wa farasi waliozoezwa. Gari la vita la punda na lile la ngamia yawakilisha ipasavyo serikali mbili, Umedi na Uajemi, zitakazoungana kuanzisha shambulio hilo. Isitoshe, historia yathibitisha kuwa jeshi la Uajemi lilitumia punda na pia ngamia katika vita.

12. Mlinzi kwenye maono ya Isaya adhihirisha sifa gani, na ni nani wanaohitaji sifa hizo leo?

12 Basi, mlinzi alazimika kutoa ripoti. “Akalia kama simba, Ee Bwana, mimi nasimama daima juu ya mnara wakati wa mchana, na kila usiku ninakaa katika zamu ya ulinzi wangu. Na, tazama, linakuja kundi [“gari la vita,” “NW”] la watu, wapanda farasi, wakienda wawili wawili.” (Isaya 21:8, 9a) Mlinzi huyo kwenye maono atangaza kwa moyo mkuu, “kama simba.” Yahitaji moyo mkuu ili kutangaza ujumbe wa hukumu dhidi ya taifa lenye kutisha kama vile Babiloni. Jambo jingine lahitajika pia—uvumilivu. Mlinzi asimama mahali pake usiku na mchana, pasipo kuruhusu kamwe kukesha kwake kufifie. Vivyo hivyo, jamii ya mlinzi katika siku hizi za mwisho imehitaji moyo mkuu na uvumilivu. (Ufunuo 14:12) Wakristo wote wa kweli wahitaji sifa hizo.

13, 14. (a) Babiloni la kale lapatwa na nini, na sanamu zake zavunjwaje? (b) Babiloni Mkubwa alipatwaje na anguko kama hilo, nalo lilitukia lini?

13 Mlinzi kwenye maono ya Isaya aona gari la vita likija. Kuna habari gani? “Akajibu na kusema, Babeli umeanguka, umeanguka; na sanamu zote za miungu yake zimevunjwa chini”! (Isaya 21:9b) Ripoti hiyo yasisimua kama nini! Mwishowe, mwenye hila huyo anayeharibu watu wa Mungu ameanguka!c Hata hivyo, mifano na sanamu za Babiloni zavunjwaje? Je, wavamizi wa Umedi na Uajemi wataingia katika mahekalu ya Babiloni na kuvunja-vunja sanamu zake nyingi? La, jambo hilo halihitajiki. Miungu ya sanamu ya Babiloni itavunjwa kwa njia ya kwamba itaonyeshwa kuwa isiyo na uwezo wa kulinda jiji hilo. Na Babiloni ataanguka wakati anaposhindwa kuendelea kuwaonea watu wa Mungu.

14 Namna gani Babiloni Mkubwa? Alipopanga njama ya kuonea watu wa Mungu wakati wa Vita ya Kwanza ya Ulimwengu, kwa kweli aliwashikilia uhamishoni kwa muda fulani. Kazi yao ya kuhubiri ilikaribia kukomeshwa kabisa. Msimamizi na maofisa wengine mashuhuri wa Watch Tower Society walifungwa gerezani kwa mashtaka ya uwongo. Lakini kukawa na mabadiliko yenye kushangaza mwaka wa 1919. Maofisa hao walifunguliwa kutoka gerezani, ofisi ya makao makuu ikafunguliwa tena, na kazi ya kuhubiri ikaanzishwa tena. Kwa hiyo, Babiloni Mkubwa alianguka kwa njia ya kwamba mshiko wake juu ya watu wa Mungu ulivunjwa.d Katika Ufunuo, malaika atangaza anguko hilo mara mbili akitumia maneno ya tangazo lililo kwenye Isaya 21:9.—Ufunuo 14:8; 18:2.

15, 16. Watu wa Isaya ‘wamefikichwaje,’ nasi twaweza kujifunza nini kutokana na mtazamo wa Isaya kwao?

15 Isaya amalizia ujumbe huo wa unabii kwa taarifa yenye huruma kwa watu wake mwenyewe. Asema: “Ewe niliyekufikicha, na nafaka ya sakafu yangu [“na mwana wa sakafu yangu ya kupuria,” “NW”]; Hayo niliyoyasikia kwa BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, nimewapasha habari zake.” (Isaya 21:10) Katika Biblia, mara nyingi kupura hufananisha kutia nidhamu na kusafisha watu wa Mungu. Watu wa agano wa Mungu watakuwa ‘wana wa sakafu ya kupuria,’ ambapo ngano yatenganishwa kwa nguvu kutoka kwa makapi, ikiacha tu nafaka iliyosafishwa na yenye kutamaniwa. Isaya hafurahii nidhamu hiyo. Badala yake, awahurumia hao watakaokuwa ‘wana wa sakafu ya kupuria,’ ambao baadhi yao wataishi maisha yao yote wakiwa mateka katika nchi ya kigeni.

16 Jambo hilo laweza kuwa kikumbusha kinachotufaa sisi sote. Katika kutaniko la Kikristo leo, huenda wengine wakawa na mwelekeo wa kutowahurumia wakosaji. Na mara nyingi huenda wale wanaopokea nidhamu wakawa na mwelekeo wa kuikataa. Hata hivyo, tukizingatia kuwa Yehova huwatia watu wake nidhamu ili kuwasafisha, hatutaidharau nidhamu hiyo na wale wanaoipokea kwa unyenyekevu, wala sisi wenyewe hatutakataa kutiwa nidhamu hiyo. Acheni tukubali nidhamu ya Mungu kuwa ni wonyesho wa upendo wake.—Waebrania 12:6.

Kutafuta Habari Kutoka kwa Mlinzi

17. Kwa nini Edomu yaitwa kwa kufaa “Duma”?

17 Ujumbe wa pili wa unabii wa Isaya sura ya 21 wakazia mlinzi. Waanza hivi: “Ufunuo juu ya Duma. Mtu ananililia toka Seiri, Ee mlinzi, habari gani za usiku? Ee mlinzi, habari gani za usiku?” (Isaya 21:11) Duma uko wapi? Yaonekana kulikuwa na miji kadhaa yenye jina hilo katika nyakati za Biblia, ingawa Duma unaotajwa hapa si mmoja wa miji hiyo. Duma hauko Seiri, ambalo ni jina jingine la Edomu. Hata hivyo, neno “Duma” lamaanisha “Kimya.” Basi yaonekana kwamba, kama vile ilivyokuwa katika ufunuo wa hapo awali, eneo hilo lapewa jina linalodokeza wakati wake ujao. Edomu, ambayo kwa muda mrefu ilikuwa adui mlipiza-kisasi dhidi ya watu wa Mungu, itakimya hatimaye—kimya cha kifo. Hata hivyo, kabla hilo halijatukia, baadhi ya watu wake watataka sana kujua juu ya wakati ujao.

18. Ufunuo unaosema, “Mchana unakuja na usiku pia,” watimizwaje juu ya Edomu ya kale?

18 Wakati wa kuandikwa kwa kitabu cha Isaya, Edomu iko kwenye njia ya jeshi la Ashuru lenye nguvu. Baadhi ya watu huko Edomu wana hamu ya kujua wakati ambapo usiku wa kuonewa kwao utaisha. Kuna jibu gani? “Mlinzi akasema, Mchana unakuja na usiku pia.” (Isaya 21:12a) Mambo si mema kwa Edomu. Nuru hafifu ya asubuhi itachomoza kwenye upeo wa macho, lakini itakuwa ya muda mfupi, yenye kudanganya. Usiku—wakati mwingine wenye giza la uonezi—utafuatia upesi baada ya asubuhi. Hilo lawakilisha ipasavyo kama nini wakati ujao wa Edomu! Ukandamizaji wa Ashuru utaisha, lakini Babiloni itafuatia Ashuru ikiwa serikali ya ulimwengu nayo itaharibu Edomu. (Yeremia 25:17, 21; 27:2-8) Mambo hayo yatarudiwa. Ukandamizaji kutoka kwa Babiloni utafuatwa na ukandamizaji kutoka kwa Uajemi kisha kwa Ugiriki. Kisha kutakuwepo “asubuhi” fupi katika nyakati za Roma, wakati akina Herode—wenye asili ya Edomu—watakapochukua mamlaka huko Yerusalemu. Ingawa “asubuhi” hiyo haitadumu. Hatimaye, Edomu atashuka kwenye kimya cha kudumu, atokomee kabisa kutoka katika historia. Mwishowe jina Duma litamfaa.

19. Huenda mlinzi amaanisha nini asemapo, “Mkitaka kuuliza, ulizeni; njoni tena”?

19 Mlinzi amalizia ujumbe wake mfupi kwa maneno haya: “Mkitaka kuuliza, ulizeni; njoni tena.” (Isaya 21:12b) Usemi “njoni tena” labda warejezea ‘masiku’ yanayofuatana bila kikomo yaliyo mbele ya Edomu. Au kwa sababu usemi huo waweza pia kutafsiriwa “rudi,” huenda nabii huyo adokeza kwamba Waedomi wowote wanaotaka kuponyoka uharibifu wa taifa hilo wapaswa kutubu na ‘kumrudia’ Yehova. Kwa vyovyote vile, mlinzi akubali maulizo zaidi.

20. Kwa nini ufunuo uliorekodiwa kwenye Isaya 21:11, 12 ni muhimu kwa watu wa Yehova leo?

20 Ufunuo huo mfupi umemaanisha mambo mengi kwa watu wa Yehova leo.e Twajua kuwa wanadamu wako ndani sana ya usiku wenye giza la upofu wa kiroho na kutengwa kutoka kwa Mungu ambao utaongoza kwenye kuharibiwa kwa mfumo huu wa mambo. (Waroma 13:12; 2 Wakorintho 4:4) Wakati huu wa usiku, nuru yoyote ile ya kutumaini eti huenda kwa njia fulani mwanadamu akaleta amani na usalama ni kama ile nuru ya mapambazuko yenye kudanganya ambayo hufuatwa tu na nyakati zenye giza hata zaidi. Mapambazuko ya kweli yanakaribia—mapambazuko ya Utawala wa Mileani wa Kristo juu ya dunia hii. Lakini maadamu usiku upo, ni sharti tufuate mwongozo wa jamii ya mlinzi kwa kudumu tukiwa macho kiroho na kutangaza kwa moyo mkuu kukaribia kwa mwisho wa mfumo huu wa mambo wenye ufisadi.—1 Wathesalonike 5:6.

Usiku Waja Juu ya Uwanda wa Jangwani

21. (a) Huenda usemi “ufunuo juu ya uwanda wa jangwani” ukawa na maana gani mbili? (b) Misafara ya Wadedani ni nini?

21 Ufunuo wa mwisho wa Isaya sura ya 21 waelekezwa dhidi ya “uwanda wa jangwani.” Waanza hivi: “Ufunuo juu ya Arabuni [“uwanda wa jangwani,” “NW”]. Ndani ya msitu wa Arabuni mtalala, Enyi misafara ya Wadedani.” (Isaya 21:13) Yamkini uwanda wa jangwani unaorejezewa ni Arabia, kwa sababu ufunuo huo wahusu makabila kadhaa ya Kiarabu. Nyakati nyingine neno limaanishalo “uwanda wa jangwani” laweza kutafsiriwa “jioni,” neno linalofanana nalo kabisa katika Kiebrania. Wengine hudokeza kwamba hilo ni neno lenye maana mbili, kana kwamba jioni yenye giza—wakati wa matatizo—yakaribia kuja juu ya eneo hilo. Ufunuo huo waanza kwa mandhari ya usiku ikionyesha misafara ya Wadedani, kabila maarufu la Kiarabu. Misafara hiyo hufuata njia za biashara zitokazo kwenye chemchemi moja ya jangwani hadi nyingine, huku ikiwa imebeba vikolezo, lulu, na hazina nyingine mbalimbali. Lakini hapo twawaona wakilazimika kuacha njia zao ambazo zimesafiriwa mara nyingi na kulala mafichoni usiku. Kwa nini?

22, 23. (a) Ni mzigo gani mzito ulio karibu kulemea makabila ya Kiarabu, nayo yataathiriwaje? (b) Msiba huo utakuja upesi kadiri gani, nao utasababishwa na nani?

22 Isaya aeleza: “Waleteeni wenye kiu maji, Enyi wenyeji wa nchi ya Tema; nendeni kuwalaki wakimbiao na chakula chao. Kwa maana wanakimbia mbele ya panga, upanga uliofutwa, na upinde uliopindwa, na mbele ya ukali wa vita.” (Isaya 21:14, 15) Naam, mzigo mzito wa vita utayalemea makabila hayo ya Kiarabu. Tema, iliyo kwenye mojawapo ya chemchemi za jangwani zenye maji mengi zaidi katika eneo hilo, yalazimika kuwaletea maji wakimbizi hao wa vita wenye kupatwa na msiba. Taabu hiyo itakuja lini?

23 Isaya aendelea: “Bwana ameniambia hivi, Katika muda wa mwaka, kama miaka ya mtu mwenye kuajiriwa, utaangamia utukufu wote wa Kedari. Na mabaki ya hesabu ya wavuta pinde, hao mashujaa wa Kedari watakuwa wachache; maana BWANA, Mungu wa Israeli, amenena neno hili.” (Isaya 21:16, 17) Kedari ni kabila maarufu sana hivi kwamba nyakati nyingine hutumiwa kuwakilisha Arabia yote. Yehova ameazimia kuwa idadi ya wapiga upinde na watu wenye nguvu wa kabila hilo itapungua kabisa na kubaki wachache tu. Lini? “Katika muda wa mwaka,” si zaidi, kama vile tu mtu mwenye kuajiriwa asivyofanya kazi kuzidi wakati wa malipo yake. Hakuna uhakika kamili kuhusu namna ambavyo hayo yote yalitimizwa. Watawala wawili wa Ashuru—Sargoni wa Pili na Senakeribu—walidai kuwa walitiisha Arabia. Huenda mmoja wao aliangamiza mengi ya makabila hayo ya Kiarabu yenye kiburi, kama ilivyotabiriwa.

24. Twawezaje kuwa na uhakika kwamba unabii wa Isaya dhidi ya Arabia ulitimizwa?

24 Hata hivyo, twaweza kuwa na uhakika kwamba unabii huo ulitimizwa kikamili. Hakuna jambo liwezalo kukazia hoja hiyo kwa nguvu sana kuliko maneno ya kumalizia ya ufunuo huo: “BWANA, Mungu wa Israeli, amenena neno hili.” Machoni pa watu katika siku ya Isaya, huenda isiwezekane kuwa Babiloni itainuka juu ya Ashuru kisha ipinduliwe kutoka mamlakani wakati wa jioni moja yenye karamu. Vivyo hivyo, huenda ikaonekana kuwa vigumu kwa Edomu yenye nguvu kutokomea katika kimya cha kifo au kwa usiku wenye magumu na njaa kuyakumba makabila ya Kiarabu yenye utajiri. Lakini Yehova asema yatatukia, nayo yatukia. Leo, Yehova atuambia kuwa milki ya ulimwengu ya dini isiyo ya kweli itaangamizwa. Huo si uwezekano tu; ni uhakika. Yehova mwenyewe amenena!

25. Twaweza kuigaje kielelezo cha mlinzi?

25 Basi, sisi na tuwe kama mlinzi yule. Acheni tudumu katika kukesha, kana kwamba tuko juu ya mnara mrefu, tukichunguza kwa makini kuelekea upeo wa macho iwapo kuna ishara yoyote ya hatari inayokuja. Na tujiunge kwa ukaribu na jamii ya mlinzi, Wakristo watiwa-mafuta ambao bado wako duniani leo. Acheni tuungane nao katika kutangaza kwa moyo mkuu yale hasa tuyaonayo—uthibitisho mwingi mno unaoonyesha kwamba Kristo anatawala mbinguni; kwamba karibuni atakomesha usiku mrefu, wenye giza, wa kujitenga kwa mwanadamu kutoka kwa Mungu; na kwamba baada ya hapo ataleta mapambazuko ya kweli, Utawala wa Mileani juu ya dunia paradiso!

[Maelezo ya Chini]

a Nyakati nyingine Mfalme Koreshi wa Uajemi aliitwa “Mfalme wa Anshani”—Anshani lilikuwa eneo au mji katika Elamu. Huenda Waisraeli wa siku ya Isaya—karne ya nane K.W.K.—hawakufahamu Uajemi, ingawa labda walijua Elamu. Huenda hilo likaeleza sababu Isaya hapa ataja Elamu badala ya Uajemi.

b Waelezaji wengi wa Biblia hufikiri kuwa maneno “itieni ngao mafuta” yarejezea zoea la zamani la kijeshi la kutia mafuta kwenye ngao zao za ngozi kabla ya vita ndipo silaha nyingi zinazorushwa ziteleze. Ingawa fasiri hiyo huenda ikawa kweli, yapasa ikumbukwe kuwa usiku ambao jiji hilo lilianguka, Wababiloni hawakuwa na wakati wa kupigana, sembuse wa kujitayarishia vita kwa kutia ngao zao mafuta!

c Unabii wa Isaya uhusuo kuanguka kwa Babiloni ni sahihi sana hivi kwamba wahakiki fulani wa Biblia wametunga nadharia ya kuwa haikosi uliandikwa baada ya tukio hilo. Lakini kama asemavyo msomi wa Kiebrania F. Delitzsch, makisio hayo hayafai ikiwa twakubali kwamba nabii aweza kupuliziwa kutabiri matukio mamia ya miaka mapema.

d Ona Ufunuo—Upeo Wao Mtukufu U Karibu!, ukurasa wa 164-169.

e Kwa muda wa miaka 59 ya kwanza ya kuchapishwa kwake, gazeti la Mnara wa Mlinzi lilionyesha andiko la Isaya 21:11 kwenye jalada lake. Andiko hilohilo lilikuwa kichwa cha hotuba ya mwisho iliyoandikwa na Charles T. Russell, msimamizi wa kwanza wa Watch Tower Society. (Ona kielezi kwenye ukurasa unaotangulia.)

[Picha katika ukurasa wa 219]

“Wanakula, wanakunywa”!

[Picha katika ukurasa wa 220]

Ndipo mlinzi “akalia kama simba”

[Picha katika ukurasa wa 222]

“Mimi nasimama daima . . . wakati wa mchana, na kila usiku”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki