SIKU YA UPATANISHO (ATONEMENT DAY)
Siku ya Upatanisho (Kieb., yohm hak·kip·pu·rim′, “siku ya ufunikaji”) ilikuwa ya kupatanisha au kufunika dhambi, iliyoadhimishwa na Israeli katika siku ya kumi ya mwezi wa saba wa kalenda takatifu, au katika Tishri 10. (Tishri kwa kulinganishwa ni kama Septemba-Oktoba.) Katika siku hii kuhani mkuu wa Israeli alitoa dhabihu ziwe kifuniko cha dhambi kwa ajili yake mwenyewe, kwa ajili ya wale Walawi wengine, na kwa ajili ya watu wengineo. Pia ulikuwa ni wakati wa kulitakasa hema au mahekalu yale ya baadaye kutokana na matokeo ya dhambi yenye kutia unajisi.
Siku ya Upatanisho ilikuwa ni siku ya kusanyiko takatifu na ya kufunga kula, kama inavyoonyeshwa na uhakika wa kwamba wakati huo watu walipaswa ‘kuzitesa nafsi zao.’ Huu ndio uliokuwa mfungo pekee ulioagizwa chini ya Sheria ya Musa. Ilikuwa pia ni sabato, wakati wa kujiepusha na kazi mbalimbali za kawaida.—Law 16:29-31; 23:26-32; Hes 29:7; Mdo 27:9.
Kuhani mkuu aliruhusiwa kuingia chumba cha Patakatifu Zaidi cha hema au cha hekalu katika siku moja tu kwa mwaka, katika Siku ya Upatanisho. (Ebr 9:7; Law 16:2, 12, 14, 15) Mwaka wa Yubile, ulipofika, ulianza na Siku ya Upatanisho.—Law 25:9.
Haruni, ndugu ya Musa, alikuwa kuhani mkuu wa Israeli wakati mwadhimisho huo ulipoanzishwa katika jangwa la Rasi ya Sinai katika karne ya 16 K.W.K. Aliyoagizwa afanye ndiyo yaliyokuwa kiolezo cha maadhimisho ya baadaye ya Siku ya Upatanisho. Mtu akipiga picha akilini kuhusu matukio yenye kuvutia ya siku hiyo, jambo hilo linamwezesha aelewe vizuri zaidi siku hiyo ilimaanisha nini kwa Waisraeli. Bila shaka, hapo walichochewa wawe na ufahamu mkubwa zaidi juu ya hali yao ya kuwa na dhambi na uhitaji wa ukombozi na vilevile wathamini zaidi rehema nyingi ya Yehova katika kufanya mpango huo wa kufunika dhambi zao za mwaka uliotangulia.
Sehemu Mbalimbali za Siku ya Upatanisho. Haruni alipaswa kuingia katika patakatifu akiwa na fahali mchanga kwa ajili ya toleo la dhambi na kondoo-dume kwa ajili ya toleo la kuteketeza. (Law 16:3) Katika Siku ya Upatanisho yeye alivua vazi lake la kawaida la kikuhani, akaoga na maji, na kujivika mavazi matakatifu ya kitani. (Law 16:4) Kisha kura zilitupwa na kuhani mkuu juu ya mbuzi wawili (wana-mbuzi wa kiume) waliofanana kabisa katika hali yao ya kuwa timamu na bila waa, waliopatikana kutoka kwa kusanyiko la wana wa Israeli. (Law 16:5, 7) Kuhani mkuu alitupa kura juu yao ili kuamua ni yupi kati yao wawili angetolewa dhabihu kwa Yehova awe toleo la dhambi na ni yupi angeachiliwa nyikani, abebe dhambi zao akiwa ‘mbuzi wa Azazeli.’ (Law 16:8, 9; linganisha 14:1-7; ona AZAZELI.) Kisha yeye alimtoa dhabihu yule fahali mchanga kuwa toleo la dhambi kwa ajili yake mwenyewe na nyumba yake, iliyotia ndani kabila zima la Lawi, ambalo nyumba yake ilikuwa sehemu yalo. (Law 16:6, 11) Kisha alichukua uvumba wenye manukato na chetezo ya moto ikiwa imejaa makaa yenye kuwaka kutoka kwenye madhabahu na kuingia ndani ya pazia, na kupaingia Patakatifu Zaidi. Uvumba ulichomwa katika chumba cha ndani zaidi, ambamo palikuwa na lile sanduku la ushuhuda, lile wingu la uvumba wenye kuchomeka likifunika kifuniko cha lile Sanduku la Agano la dhahabu ambalo juu yake kulikuwa na makerubi wawili waliofanyizwa kwa dhahabu. (Law 16:12, 13; Kut 25:17-22) Tendo hilo lilimfungulia Haruni njia ya baadaye ya kuingia tena akiwa salama katika Patakatifu Zaidi.
Haruni, akiwa anarudi kutoka Patakatifu Zaidi, alichukua sehemu ya damu ya yule fahali, na kuingia chumba hicho akiwa nayo, na kunyunyiza sehemu ya damu hiyo kwa kidole chake mara saba mbele ya kifuniko cha Sanduku la Agano katika upande wa Mashariki. Hivyo ndivyo upatanisho wa ukuhani ulivyokamilishwa, hilo likiwafanya makuhani wawe safi na kuweza kufanya upatanisho kati ya Yehova na watu wake.—Law 16:14.
Mbuzi ambaye kura hiyo ilianguka juu yake “kwa ajili ya Yehova” alitolewa dhabihu kuwa toleo la dhambi kwa ajili ya watu. (Law 16:8-10) Kisha kuhani mkuu alichukua damu ya yule mbuzi kwa ajili ya Yehova hadi ndani ya Patakatifu Zaidi, na kuitumia humo kufanya upatanisho kwa ajili ya makabila 12 ya Israeli yasiyo ya kikuhani. Katika njia inayofanana na jinsi ilivyoshughulikiwa damu ya yule fahali, damu ya yule mbuzi ilinyunyizwa “kukielekea kifuniko na mbele ya kifuniko” cha Sanduku la Agano.—Law 16:15.
Kupitia njia hizo Haruni pia alifanya upatanisho kwa ajili ya patakatifu na hema la kukutania. Kisha, akichukua sehemu ya damu ya yule fahali na ya yule ‘mbuzi kwa ajili ya Yehova,’ yeye alifanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu ya toleo la kuteketezwa, akiweka sehemu fulani ya damu hiyo juu ya pembe za hiyo madhabahu. Pia alipaswa ‘kutapanya sehemu ya damu juu yake kwa kidole chake mara saba na kuisafisha na kuitakasa kutokana na uchafu wa wana wa Israeli.’—Le 16:16-20.
Kisha kuhani mkuu aligeuza fikira zake kuelekea yule mbuzi aliyebaki, aliye kwa ajili ya Azazeli. Aliweka mikono yake juu ya kichwa chake, akaungama juu yake “makosa yote ya wana wa Israeli na maasi yao yote na dhambi zao zote,” na kuyaweka juu ya kichwa cha mbuzi huyo, na kisha kumtuma aende zake “mpaka nyikani kwa mkono wa mtu aliye tayari.” Hivyo, mbuzi huyo alibeba makosa ya Waisraeli hadi nyikani, na kutokomea huko. (Law 16:20-22) Baada ya hayo yule mtu aliyemwongoza mbuzi huyo aende zake alipaswa kuosha mavazi yake na kuoga mwili wake na maji kabla ya kuingia tena ndani ya kambi.—Law 16:26.
Kisha Haruni angeingia ndani ya hema la kukutania, ayavue mavazi ya kitani, aoge, na kuvaa mavazi yake ya kawaida. Halafu angetoa toleo lake la kuteketezwa na toleo la kuteketezwa la watu (akitumia kondoo-dume waliotajwa katika Law 16:3, 5) na kufanya upatanisho, naye angefanya mafuta ya toleo la dhambi yafuke moshi juu ya madhabahu. (Law 16:23-25) Sikuzote Yehova Mungu alidai mafuta ya dhabihu yawe yake, na Waisraeli walikatazwa kuyala. (Law 3:16, 17; 4:31) Mabaki ya mizoga ya fahali na mbuzi wa toleo la dhambi ilichukuliwa kutoka ua wa hema hadi mahali fulani nje ya kambi, ambako ilitekeketezwa. Mtu aliyefanya uteketezaji alipaswa kuosha mavazi yake na kuoga mwili na maji, kisha angeweza kuingia ndani ya kambi. (Law 16:27, 28) Dhabihu za ziada za siku hiyo zinatajwa katika Hesabu 29:7-11.
Kukomeshwa kwa Mwadhimisho Halali. Ingawa wafuasi wa dini ya Kiyahudi wangali husherehekea Siku ya Upatanisho, sherehe hiyo inafanana kidogo na ile iliyoanzishwa na Mungu, kwa maana wao hawana hema, hawana madhabahu, hawana sanduku la agano, hawatoi fahali na mbuzi kuwa dhabihu, na hakuna ukuhani wa Kilawi. Hata hivyo, Wakristo wanatambua kwamba watumishi wa Yehova hawako sasa chini wajibu huo. (Ro 6:14; Ebr 7:18, 19; Efe 2:11-16) Isitoshe, kuangamizwa kwa hekalu la Yerusalemu mwaka wa 70 W.K. kulilazimisha kuwe na kikomo cha utumishi mbalimbali wa ukuhani wa kweli wa Walawi, na hapana njia yoyote ya kujua ni nani ambao kwa kufaa wangeweza kutenda wakiwa makuhani hao. The Encyclopedia Americana (1956, Buku 17, ukur. 294) chasema hivi kuhusu Walawi: “Baada ya kuharibiwa kwa hekalu katika ule uhamisho, walitokomea kutoka katika historia, wakachanganyikana na umati wa mateka waliotawanyika katika ulimwengu wa Roma.”
Utimizo Uliofananishwa. Ilipoadhimishwa kwa njia inayofaa, Siku ya Upatanisho ya kila mwaka, kama vile sehemu nyinginezo za Sheria ya Musa, ilikuwa picha ya kitu kikubwa zaidi. Uchunguzi wa uangalifu wa mwadhimisho huo kulingana na maelezo ya mtume Paulo yaliyoongozwa na roho unaonyesha kwamba kuhani mkuu wa Israeli na wanyama waliotumiwa kuhusiana na sherehe hiyo walifananisha Yesu Kristo na kazi yake ya ukombozi kwa niaba ya jamii ya wanadamu. (Ebr 5:4-10) Mtume huyo pia anaonyesha kwamba uingiaji wa kuhani mkuu ndani ya Patakatifu Zaidi mara moja kwa mwaka akiwa na damu ya wanyama wa dhabihu ulitangulia kufananisha uingiaji wa Yesu Kristo mbinguni kwenyewe akiwa na damu yake mwenyewe, kwa njia hiyo afanye upatanisho kwa ajili ya wale wanaodhihirisha imani katika dhabihu yake. Bila shaka, Kristo, akiwa bila dhambi, hakuhitaji kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zozote za kibinafsi, kama alivyofanya kuhani mkuu wa Israeli.—Ebr 9:11, 12, 24-28.
Haruni alitoa yule fahali kuwa dhabihu kwa ajili ya makuhani na wale wengine wa kabila la Lawi, akinyunyiza damu yake katika Patakatifu Zaidi. (Law 16:11, 14) Kwa kulinganisha Kristo alitoa thamani ya damu yake ya kibinadamu kwa Mungu mbinguni, ambako ingeweza kutumiwa kufaidi wale ambao wangekuja kutawala pamoja naye wakiwa makuhani na wafalme. (Ufu 14:1-4; 20:6) Yule mbuzi kwa ajili ya Yehova alitolewa dhabihu pia na damu yake ilinyunyizwa mbele ya Sanduku la Agano katika Patakatifu Zaidi, jambo hilo likifanywa ili kufaidi yale makabila ya Israeli yasiyo ya kikuhani. (Law 16:15) Hali moja na hiyo, ile dhabihu moja ya Yesu Kristo hufaidi pia jamii ya wanadamu zaidi ya kufaidi Israeli wa kikuhani wa kiroho. Mbuzi wawili walihitajiwa, kwa maana mbuzi mmoja tu hangeweza kutumika akiwa dhabihu na bado atumiwe kuchukua dhambi za Israeli. Mbuzi wote wawili walitajwa kuwa toleo moja la dhambi. (Law 16:5) nao walitendewa kwa njia ileile moja hadi wakati wa kutupwa kwa kura juu yao, jambo ambalo linaonyesha kwamba wakiwa pamoja walifananisha kitu kimoja. Si kwamba tu Yesu Kristo alitolewa dhabihu bali pia alichukua dhambi za wale ambao alikufa kama dhabihu kwa ajili yao.
Mtume Paulo alidhihirisha kwamba, ingawa haikuwezekana kwa damu ya mafahali na ya mbuzi kuchukua dhambi, Mungu alitayarisha mwili kwa ajili ya Yesu (ambao yeye alionyesha nia ya kuutoa dhabihu alipojitoa abatizwe), na kulingana na mapenzi ya kimungu, wafuasi wa Kristo ‘wametakaswa kupitia toleo la mwili wa Yesu Kristo mara moja kwa wakati wote.’ (Ebr 10:1-10) Kama vile mabaki ya miili ya fahali na mbuzi waliotolewa kwenye Siku ya Upatanisho ilivyoteketezwa hatimaye nje ya kambi ya Israeli, mtume huyo anaonyesha kwamba Kristo aliteseka (akitundikwa) nje ya lango la Yerusalemu.—Ebr 13:11, 12.
Kwa hiyo, ni wazi kwamba, ingawa Siku ya Upatanisho ya Kiyahudi haikutokeza ondoleo la dhambi lililo kamili na la kudumu hata kwa Israeli, zile sehemu mbalimbali za sherehe hiyo ya kila mwaka zilikuwa ni ufananisho wa kimsingi. Zilitangulia kufananisha ule upatanisho mtukufu uliofanywa kwa ajili ya dhambi kupitia Yesu kristo, aliye Kuhani Mkuu ambaye Wakristo humuungama.—Ebr 3:1; ona UPATANISHO; FIDIA.