Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w75 1/15 kur. 41-45
  • Dawa za Vichakani—Je! Wakristo Watafute “Mapozo” Yake?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Dawa za Vichakani—Je! Wakristo Watafute “Mapozo” Yake?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • DAWA ZA VICHAKANI NA DESTURI ZA UCHAWI
  • VISA VIWILI VYA MFANO VYA VIPINDI “VYA KUPONYA”
  • KWA UWEZO WA NANI?
  • WAKRISTO WA KWELI WANAMPA MUNGU IBADA YA PEKEE
  • Dawa za Kienyeji Katika Afrika Je! Zinafaana na Ukristo?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1987
  • Roho Zisizoonekana—Je! Zinatusaidia? Au Zinatuumiza?
    Roho Zisizoonekana—Je! Zinatusaidia? au Zinatuumiza?
  • Kuponya kwa Imani—Je! Kunaleta Matokeo?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1982
  • Uchawi Waenea Pote—Je! Ni Hatari?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
w75 1/15 kur. 41-45

Dawa za Vichakani​—Je! Wakristo Watafute “Mapozo” Yake?

KWA jumla, watu katika Amerika ya Kaskazini na Ulaya wanauona ushirikina ulioko leo kati ya idadi fulani ya watu kama jambo la kuchekesha. Wanazicheka imani za kwamba kushika vyura kunaleta chunjua (uvimbe mdogo mdogo wa mwili), kwamba kulala mwezi ukimulika uso wa mtu kwaweza kusababisha kichaa, na maoni ya namna hiyo. Na hali wengi wao ni wenye ushirikina wa namna ile kwa njia nyingine. Kwa mfano, hofu ya namba 13 “yenye bahati mbaya” yazuia hoteli zisiwe na orofa ya 13 au namba kama hiyo ya chumba. Zaidi ya hayo, wakuu wengi, hata viongozi wa kisiasa, wanawaendea wanajimu na waaguzi.

Katika Amerika ya Kati na ya Kusini, Afrika, Asia na visiwa vya bahari, “dawa za vichakani” na Uchawi vyachukuliwa kwa uzito sana mara nyingi na idadi kubwa ya watu.

Watumiao dawa za vichakani na Uchawi wanasema magonjwa yote au mengi sana yanaletwa na nguvu zenye uwezo upitao ule wa mwanadamu wa kawaida, “wachawi” na roho wabaya. Kwa hiyo, wao wanakimbilia msaada kwa roho zenye uwezo usio wa kibinadamu katika kuponya ugonjwa. Nyakati nyingine kwa kweli wanaelekea kuponya kwa maneno yao ya kunuizia uchawi, desturi na matoleo ya kuku, nguruwe na mbuzi.

Kwa hiyo ulizo linatokea: Je! wale wanaokuwa Wakristo wanaweza kwa kufaa kuzitazamia dawa za vichakani au Uchawi waponywe magonjwa yao?

Jibu kwa ulizo hili lingetegemea chanzo cha “mapozo” hayo na mambo ambayo Biblia inayasema juu yake. Ulizo lote ni juu ya kama mtu huyu anamtolea Mungu wa kweli ibada ya pekee au sivyo​—⁠kama anagawana ibada hiyo na “miungu” mingine. Kwa maana Mungu wa Biblia anasema: “Mimi Yehova Mungu wako ni Mungu mwenye kutaka ibada ya pekee.”​—Kum. 5:9, NW.

Maisha ya sasa ya mtu si ya muhimu sana hata azivunje kanuni za haki na kugeukia miungu mingine kwa msaada. (Mt. 16:25) Kwa mfano, Mkristo wa kweli asingeua au kufanya uzinzi kusudi aokoe uhai wake mwenyewe. Lakini je! dawa za vichakani na Uchawi hazimtaki Mkristo auondoe utii wake kwa Mungu, aushiriki na miungu mingine?​—Linganisha Isaya 42:8.

DAWA ZA VICHAKANI NA DESTURI ZA UCHAWI

Ni kweli kwamba dawa za uchawi zinatumia miti mingi inayojulikana kama yenye kuponya. Na, kwa sababu ya maongozi ya nchi za Magharibi, “waganga” wengi wamekuja kuwa wataalamu wa dawa za miti za magonjwa fulani, kwa kadiri fulani. Lakini “waganga” wa kutumia Uchawi na dawa za vichakani wanashikilia kwamba ile miti na dawa za kunywa wanazozitumia vyenyewe havina nguvu. Watu hawa wanaamini kwamba, zinafanya kazi wakati tu uwezo wa nomma, yaani, nguvu ya uhai ijayo kwa uwezo wa maneno ya mganga inapotumiwa, kama “dawa” hiyo inamezwa, inapakwa au inabebwa kwa kamba nyembamba inayoizunguka shingo. Kwa hiyo, dawa zote za vichakani zilizotolewa kwa “waganga” hao zahusiana na uchawi, na ibada ya miungu ya walozi, hata ingawa huenda vile vile nyingine zikawa na mapozo ya wazi na ya asili ya ugonjwa wenyewe.

Watu waishio vichakani wa !Kung wa Afrika (ile alama ya mshangao yamaanisha mlio “wa kualika”) wanasema kwamba “dawa” hiyo ilitolewa na Mungu kwa waishio vichakani hapo kwanza, lakini kwamba watu wanaweza kuondoa “dawa” moja katika mwili mmoja kuitia katika mwingine. Wakati ambapo, kwa kucheza ngoma, “dawa” inafikia upeo, mvuke unapanda ukipitia katika uti wa mgongo, nao mvuke ufikapo ubongoni, mcheza ngoma anakuwa kana kwamba ana usingizi mzito na anaona njozi. Mmoja aliyataja matokeo kwa kusema hivi:

“Dawa ya aishiye vichakani inaingizwa mwilini kupitia katika uti wa mgongo. Inachemka tumboni mwangu na kuchemka hata kichwani mwangu kama pombe. Wanawake waanzapo kuimba nami naanza kucheza ngoma, kwanza najisikia vema sana. Halafu katikati, dawa yaanza kupanda kutoka tumboni mwangu. Nyumaye nawaona watu wote kama ndege wadogo sana, mahali pote kama panapozunguka-zunguka na ndiyo sababu twakimbia-kimbia tukizunguka-zunguka. . . . Unajisikia damu yako ikipata moto sana kama vile damu inayochemka motoni kisha waanza kupoa . . . kisha nimwekeleapo mikono mgonjwa, dawa iliyomo ndani yangu itamwingia na kumponya.”​—Gazeti la Natural History, Novemba 1967.

Desturi iliyo tofauti na hii ni ile ya “Zionists” wa Afrika ya Kusini, kikundi cha kidini kilichotokana na kazi ya wamisionari wa dhehebu moja katika Zion, Illinois. Wakati wa ngoma ya kuzunguka-zunguka, wacheza ngoma wanazishika sehemu zenye ugonjwa za kundi la watu ‘watakaoponywa.’ Huku “kuwekelea mikono” kwadhaniwa kunatia ndani “roho mtakatifu” awaponye.

Katika Peru, yule curandero au “mwenye kuponya” huenda akawa na mesa au meza iliyogawanywa sehemu tatu. Ya kwanza yadhaniwa inaongozwa na Shetani. Ina vyombo vinavyoshirikiana na ulozi na nguvu mbaya. Sehemu ile nyingine inaitwa “uwanja wa haki ya kimungu,” nayo ina vyombo vinavyoshirikishwa na “uganga.” Yasemekana eneo hili laongozwa na Kristo. Sehemu ya tatu (ya katikati) ni ya namna ya kutokuwa wala upande huu wala ule, ikiongozwa na Mtakatifu Cyprian (anayesemekana kuwa mchawi mwenye nguvu aliyeongolewa akawa Mkristo).

Yule curandero anatenda kama mshauri wa wafuasi wake juu ya upendo, biashara au mambo mengine. Anapofanya haya huenda atumie karata za uaguzi. Lakini kwa ugonjwa au shuku ya kupagawa na roho ya mchawi, huenda akamsugua mgonjwa na mnyama mdogo wa namna ya panya, kisha kulipasua tumbo la mnyama huyo na kufanya uaguzi wa matumbo. Ikiwa uchawi ndio ulioleta maumivu, yatazamiwa kwamba uti wa mgongo wa yule mnyama mdogo utapatikana umevunjika. Ikiwa kuna ugonjwa wa kiungo fulani, kiungo kile kile kilichomo katika mnyama yule mdogo chatazamiwa kuonekana chenye doa au kikiwa cheusi.

VISA VIWILI VYA MFANO VYA VIPINDI “VYA KUPONYA”

Mchunguzi mmoja, akiandika katika Natural History (Nov. 1972), anasimulia kuhudhuria kipindi “cha kuponya” katika Peru, kilichofanywa usiku. Mtu mmoja alikuwa amekuwa mgonjwa asiweze kutembea. Biashara yake ilikuwa ikiharibika nao watoto wake walikuwa wamekwisha shindwa kuendelea na kazi na katika shule. Uchunguzi wa yule curandero ulikuwa kwamba mlozi alikuwa amenuiza maneno ya ulozi na kwamba hii ndiyo iliyokuwa sababu ya taabu ya jamaa. Mnamo kawaida iliyofuata “ya kuponya,” kijana wa kike wa jamaa ile alianza kukohoa na kubabaika, akiyatapika majimaji yaliyochemshwa ya mmea wa namna ya mpungate wa San Pedro aliyokuwa ameyanywa (vile vile alikuwa amekunywa mchanganyiko wa mmea huo na majimaji ya tumbako ya vichakani). Akaanza kuegemea nyuma kwa uwazimu. Mtu fulani akapiga yowe kwamba dubwana lilikuwa likimvuta kijana yule wa kike nywele kutokea nyuma. Sasa, yule curandero akashika upanga kutoka mezani na kuingia katika pigano la nguvu sana kana kwamba anapigana na adui asiyeonekana, akikatakata kwa upanga kwa ukali mwingi na kwa nguvu sana. Yeye alisema, hii ilikuwa ni kuyatangua maneno yaliyonuizwa ya mlozi. Mchunguzi huyo asema kwamba alipoiona jamaa ile nyumaye, afya ya mtu yule na vile vile ya jamaa yake na biashara ilikuwa imepata maendeleo.

Mchunguzi mwingine, Louis C. Whiton aliyeongoza safari sita za kwenda Surinam akachunguze habari za watu wajulikanao kama Bush Negroes (Weusi wa Vichakani), aeleza habari ya yaliyompata mwenyewe akiwa na mchawi mmoja katika Paramaribo. (Natural History Aug.-Sept. 1971) “Wengi wa watu wa mjini walioelimishwa zaidi waliutumia ujuzi wake wajapokuwa walihudhuria makanisa ya Kikristo,” anaandika. Whiton alikuwa amelemaa naye akawa na maumivu makali kiunoni mwake na mguuni. Kwa kipindi cha zaidi ya miezi kumi na minane, wataalamu na tabibu wa Whiton mwenyewe walikuwa wameshindwa kuleta kitulizo. Ifuatayo ni muhtasari ya kawaida “ya kuponya.”

Sherehe yenyewe ilianza usiku wa manane. Udongo uliokuwa umebarikiwa kulingana na kawaida ili upate uwezo wa kuondosha uovu ulipakwa katika mwili wake wote. Kuimba na sala kwa miungu ya vichakani vikafuata. Ndipo “nafsi”‏ ya mgonjwa ilipohojiwa juu ya maisha yake yaliyopita. Yule mchawi alisali kwa mungu Misa ‘amlinde Mtoto huyu wa Dunia, ajapokuwa ametenda dhambi, ili asije akapatwa na madhara.’ Madhabahu ya Uchawi ilipangwa kukizunguka kichwa chake Whiton nazo bendera za miungu ya Kihindi zikapepewa juu yake. Nyuma ya karibu saa mbili aliambiwa miungu ilikuwa imewasili. Akaambiwa alale chini, naye “mwenye kuponya” akalala akielekea upande ule mwingine, tosi za vichwa vyao zikiwa zimegusana. Kisha kinu kikubwa sana sana na kizito kikawekwa kifuani pa yule mchawi, huku mmojawapo wa wadogo wake akisimama juu ya tumbo lake na mwingine juu ya mapaja yake, wakikitwanga kinu kwa michi mikubwa ya kutwangia. Waliamini kwamba kutwanga huko kungeufanya moyo wake uendelee kupiga kwa kawaida wakati wa mateso hayo, ambapo yule roho mbaya alitazamiwa amwache mgonjwa na kumwingia mchawi.

Mchawi, sasa aliyedhaniwa amepagawa na yule roho mbaya aliyekuwa katika mgonjwa, akawa mgomvi, akizungumza Kiingereza, pahali pa lugha yake ya kienyeji ya Taki-Taki, kwa kutumia maneno ya hasira na ya uadui. Kisha, alipaswa yule roho mbaya aondolewe kwake apelekwe kwenye madhabahu ya mifupa ya nyoka, na mwishowe, kwenye mwili wa kifaranga wa kuku, aliyenyanyuliwa kwa manyoya yake ya shingoni mbele ya mgonjwa. Ikiwa yule roho mbaya alikuwa amefukuzwa kabisa, yule kifaranga angekufa bila ya kudhuriwa na mchawi kwa njia yo yote. Kifaranga hakufa, kwa hiyo mgonjwa akaambiwa kwamba labda si ubaya wote ‘ulioondolewa kwake.’ Kwa hiyo ilimpasa kuufunua mdomo wa kifaranga na kutema mate kinywani mwake. Akakubali, nalo hili lilipokwisha kutukia, yule ndege alipigapiga mabawa yake kwa nguvu, akachechema na kufa. Whiton asema kwamba ilipokwisha kupita miaka miwili tangu kawaida hiyo ilipofanywa maumivu hayajapata kumrudia tena mguuni mwake wala kiunoni.

KWA UWEZO WA NANI?

Yaonekana wazi kutokana na taarifa hizi kwamba kuna namna fulani ya uwezo katika dawa za vichakani na kawaida za Uchawi. Lakini uwezo wa nani? Je! ndio uwezo wa Yehova Mungu, Muumba wa mbingu na dunia, au wa “roho njema” nyingine? Kwa kweli ni nani wanaoitwa na wale wanaojaribu kuponya kwa kutumia dawa za vichakani au Uchawi? Kwa kujibu, ebu na tuangalie kimojawapo cha vipindi vya Uchawi​—si kawaida ya kuponya, lakini kinachofanywa muda kwa muda kuiridhisha miungu yao, inayoitwa loas. Yaonyesha n’nani kweli anayeingia katika uongozi wa wale wanaozoea Uchawi na dawa za vichakani:

Wanapowaomba loas watokee, waabudu wanaanza kucheza ngoma nyimbo zinapoimbwa na ngoma kuvuma. Ngoma zinapozidi kuvuma sana, mkazo unaongezeka. Wacheza ngoma wanakuwa kana kwamba wanaona njozi, wanaruka-ruka, na kuanza kufanya vigelegele. Ndipo loas ‘wanapotokea,’ wakiingia ndani ya wacheza ngoma mmoja baada ya mwingine, au, kama wasemavyo, ‘wakiwapanda na kutembea’ juu yao. Mtu yule anakuwa ndiye “farasi” wa loa. Kisha anaonyesha wazi tabia za loa yule aliyempanda, nao ni wengi, mmoja anayesimamia neema, mwingine, mtawala wa bahari, mwingine, msimamizi wa ukulima, kikundi cha wale ambao ni miungu ya vita, ya kifo, na mungu wa kike wa mambo yawapasayo wanaume na wanawake, tukitaja tu kwa uchache. ‘Aliyepandwa’ anamweka yule loa; kwa hiyo yeye anakuwa loa yule. Ndipo anapoweza kuanza kuropoka maneno ya kijinga na ya matusi sana na matendo. Mara nyingi mtu aliyepagawa na mmojawapo wa loas wa moto aweza kutembea juu ya kuni za moto mkubwa miguu mitupu, akiwa ameshika koleo zilizogeuzwa nyekundu na moto mkononi mwake, akichekacheka na kurudi tena akitembea polepole, asidhurike.

Angalia kwamba Yesu Kristo alikubali kwamba mashetani yako kweli, watu hawa wabaya wa kiroho wakiwa chini ya usimamizi wa Shetani Ibilisi, adui ya Mungu, uhakika ambao hata Wayahudi waliukubali. (Luka 11:14-20) Watu wengi ambao kutoka kwao Yesu alifukuza mashetani walikuwa na maradhi ya kimwili au ya akili “yasiyoponyeka.” Wengine walikuwa na kifafa au waliopooza. (Mt. 4:24; 17:14-16, 18; Luka 9:38-43) Wengine walikuwa wakali, wajeuri na hatari. (Mt. 8:28-32; Marko 5:2-13) Mashetani yalikuwa yamefanya wengine wakapofuka na kuwa bubu.​—Mt. 12:22; Luka 11:14.

Yesu alifukuza mashetani kutoka katika wale waliopagawa nayo, si kwa njia ya kawaida yo yote, wala siyo kwa kuiomba “miungu,” bali katika jina la Mungu wa kweli, Baba yake, Yehova. (Yohana 10:25) Yeye hakujaribu kuwaridhisha roho ama kutumia kawaida fulani aupate msaada. wao. ‘Alikemea’ roho mchafu kwa mamlaka iliyotoka kwa Mungu. Wakati mmoja alimponya kijana wa kiume mwenye kifafa aliyetaabishwa na shetani mwenye nguvu sana ambaye asingeweza kufukuzwa na wanafunzi wa Yesu. Lakini kwa wepesi Yesu “akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile.”​—Mt. 17:14-18; Luka 9:42.

Kwa hiyo, je! mtu anayeiita “miungu” afukuze roho wabaya, anatumikia nani, au yeye afanyaye uaguzi kwa kutumia karata au matumbo, atazamaye nyakati mbaya na kutoa dhabihu?

Yehova Mungu alionyesha wazi nia yake juu ya namna zote za uaguzi, uchawi, unajimu na mazoea ya mafumbo alipoliambia hivi taifa la Israeli lilipokaribia kuiingia nchi ya Kanaani:

“Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo [Yehova], Mungu wako, usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale. Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. . . . Maana mataifa haya utakaowamiliki, huwasikiliza wanaoshika nyakati mbaya na kutazama bao; bali wewe, [Yehova], Mungu wako, hakukupa ruhusa kutenda hayo.”​—Kum. 18:9-14.

Mtume Paulo aliwaonya Wakristo juu ya hatari ya kuigawanya ibada yao kwa kuitazamia miungu mingine mahali pa Yehova: “Hamwezi kunywea kikombe cha [Yehova] na kikombe cha mashetani. Hamwezi kushirikiana katika meza ya [Yehova] na katika meza ya mashetani. Au twamtia [Yehova] wivu? Je! tuna nguvu zaidi ya yeye?”​—1 Kor. 10:20, 21, 22.

WAKRISTO WA KWELI WANAMPA MUNGU IBADA YA PEKEE

Je! maoni ya Mkristo wa kweli yanamaanisha kwamba Mkristo anakatazwa na Biblia asitafute mapozo kwa wenye maarifa ya dawa za mimea, matabibu, wenye kuponya uti wa mgongo, na vivyo hivyo? Hapana. Lakini Wakristo wa kweli wataepuka Uchawi, dawa za vichakani, wachawi na namna zote za uchawi, kutia na zile zinazoonwa na matabibu kama “roho njema.” (Ufu. 21:8) Bila shaka mimea fulani yaweza kuponya na ziko dawa nyingine. Lakini Wakristo wanajua kwamba mapozo hayapaswi kutafutwa kwa wachawi, waganga wa kienyeji, curanderos au tabibu mwingine ye yote atumiaye namna yo yote ya mazoea ya kichawi, hirizi, talasimu au kawaida za mambo hayo, hata iwapo daktari huyo anatia ndani na mimea au namna nyingine yo yote ya dawa pamoja nayo au sivyo.

Huenda wengine wakajisikia kwamba wamepata mapozo, au mapozo kidogo, kwa ugonjwa fulani kutokana na dawa za vichakani. Lakini, wale ambao hapo kwanza walitumia dawa za vichakani wanakubali kwamba “mapozo” ya pekee ambayo kwa jumla wachawi wenye kuponya wanadai kuyafanya ni yale ya magonjwa yanayoletwa na roho, mashetani. Ni kweli, wengine wanatumia mimea yenye uwezo wa kuponya, pamoja na uchawi wao. Lakini wao wanasema faida zinazopatikana zimeletwa na uwezo wao wa kichawi, wala si ile mimea. Hivyo wanamdanganya mgonjwa aamini ni uchawi kweli, si ile mimea yenyewe, ulioleta kitulizo. Watu wanaowaendea waganga hao wanakuja chini ya uongozi wa roho hao, mashetani waovu, kwa maana wamewaomba mashetani kupitia kwa mchawi, nao wakakikubali kilichotolewa na mashetani.​—Rum. 6:16; 1 Kor. 10:20, 21.

Watu wengi katika Afrika, Asia, Amerika ya Kusini na sehemu nyingine za dunia ambako dawa za vichakani, namna mbalimbali za Uchawi zinakozoewa wanakombolewa kutoka katika ushirikina wao na hofu juu ya wachawi na miungu ya Uchawi kwa kujifunza kweli ya Biblia. Kama vile Yesu alivyosema: “Mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.” (Yohana 8:32) Uhuru wa hofu juu ya mashetani unawapa maoni mazuri juu ya maisha nao waongezea sana afya yao ya kimwili na ya akili. Kwa upande mwingine, wanaona utovu wa heshima ambao umeletwa kwa watu na mazoea ya dawa za vichakani, pamoja na mvuto wake kwenye roho, kwa kweli kwenye mashetani waovu. Wao wanajua kwamba ni kupitia kwa dhabihu ya ukombozi ya Kristo peke yake mwanadamu anavyoweza kuponywa kutokamilika kwake na magonjwa kwa umilele. Vile vile wanajifunza kwamba matumizi ya faida hizo za ukombozi yatakuja mnamo utawala wa Kimasihi wa miaka elfu, unaokaribia sasa.

Kama mfano wa kujiepusha huku kunakofaa na mambo haya na azimio la kumpa Muumba ibada ya pekee, mmojawapo wa mashahidi wa Yehova katika Afrika aliombwa apige chapa maagizo fulani yaliyotolewa na mchawi amweleze mfuasi wake namna ya kutumia dawa ya pekee aliyokuwa ameitayarisha. Shahidi alikataa kushiriki utabibu huo, akimwambia “mganga” kwamba yeye mwenyewe alikuwa amekwisha acha kutumia dawa hizo za kunywa naye hakutaka kuwa lawamani mbele za Mungu kwa kumtia mtu mwingine moyo azitumie. Mwendo huo waonyesha imani ya kweli na utiifu, ukihakikisha baraka za Mungu.

Kwa hiyo jibu la waziwazi kwa ulizo, ‘Je! Wakristo watafute mapozo ya dawa za vichakani?’ ni “Hapana.” Yawapasa Wakristo wajue kwamba hawawezi kuushikilia Ukristo wa kweli wakati ule ule wakimwomba mungu mwingine ye yote kama namna ya “kuchanganya imani,” hata ikiwa wanadhani mapozo fulani ya magonjwa fulani ya kimwili yatatokana na chanzo hicho. Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, alisema: “Mtu awaye yote atakaye kuuhifadhi uhai wake mwenyewe ataupoteza, na mtu awaye yote aupotezaye uhai wake kwa ajili yangu mimi atauona.” Tena: “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili.”​—Mt. 16:25, AT; 6:24.

Wakristo wa kweli wanajua kwamba ukubali wa Mungu wapaswa kutafutwa kuliko mambo mengine yote. Wao wanaepuka majaribio ya kuponywa au ya kitu kingine cho chote kwa njia ambayo ni ya uasi machoni pa Mungu, ambayo yaweza kuigawanya ibada yao. Wao wanaitumaini taratibu mpya yake iliyoahidiwa, kwa maana humo wanaweza kufurahia mapozo ya milele, si kwa miaka michache tu.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki