Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w77 7/1 kur. 296-298
  • Nilipata Kimbilio la Kweli Nikiwa Mzee

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Nilipata Kimbilio la Kweli Nikiwa Mzee
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • MASOMO YA KWANZA NA NDOA
  • SIKUTAKA MAMBO YA KIROHO
  • KUZIITIKIA KWELI ZA BIBLIA
  • MAADUI, UZEE NA KIFO
  • Kumtumikia Mungu Nyakati za Magumu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1981
  • Shangwe na Matatizo ya Kuwalea Watoto Wanane Ili Wafuate Njia za Yehova
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2006
  • Jinsi Nilivyonufaika Kutokana na Utunzaji wa Mungu
    Amkeni!—1995
  • Nilipata Kitu Bora Kuliko Utajiri
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
w77 7/1 kur. 296-298

Nilipata Kimbilio la Kweli Nikiwa Mzee

Imesimuliwa na Louisa Gregorio

NIMEISHI karibu miaka mia moja na miwili​—muda mrefu zaidi kuliko miaka 70 tuliyopewa. (Zab. 90:10) Lakini niliweza kupata nilichotaka sikuzote nilipopita umri wa miaka 70, yaani, kimbilio na tumaini la kweli.

Mimi ni mzao wa watoro waliotafuta uhuru wa ibada miaka mingi iliyopita. Mwanzoni mwa utawala wa Malkia Victoria, aliyetawala Uingereza kutoka mwaka 1837 mpaka 1901, wakazi wa Madeira, kisiwa cha Ureno, waliteswa na Wakatoliki kwa sababu ya dini. Biblia zao zilichomwa moto, wakatendwa mabaya mengine. Baadaye, Malkia Victoria alipeleka meli kisiwani ili wote wenye kutaka kuondoka wafanye hivyo.

Kati ya waliopanda meli hiyo walikuwako wasichana wawili wadogo. Meli ilikuwa ikielekea British West Indies. Watoro wengine walitoka walipofika kisiwa cha Antigua. Wale wengine, kutia na wale wasichana wawili, walikuja hapa Trinidad. Walikuwa wenye bidii na unyofu. Walichukua mawe kutoka mto wa karibu ulioitwa East Dry River wakajenga St, Ann’s Church of Scotland, kanisa ambalo hata leo hii lipo.

Mmoja wa wasichana hao watoro alikuwa nyanya yangu mkubwa. Alizaa binti, Marceliana, naye huyo alikuwa ndiye nyanya yangu. Marceliana alipoolewa akazaa watoto, mama’ngu Maria alizaliwa. Baadaye, aliolewa na Manuel Pereira, naye akawa ndiye baba yangu. Jamaa yetu ikawa na wasichana watatu na mvulana aliyekufa akiwa mdogo. Baba pia alikufa, kwa hiyo mama yangu akatafuta kazi katika duka ili aangalie jamaa yake na nyumba yake.

MASOMO YA KWANZA NA NDOA

Tuliishi katika pembe ya barabara mbili, Henry Street na Duke Street, ambayo sasa iko upande wa chini wa mji wenye biashara katika Port of Spain. Hapo karibu ilikuwako shule iliyoitwa Girls Model School katika Victoria Street, na hapo ndipo niliposomea. Nilipokuwa na umri wa miaka kumi na sita, vijana wawili wa ujirani walianza kupendezwa nami. Mmoja alikuwa wa jamaa tajiri; yule mwingine alikuwa kijana maskini. Mimi nilimpenda Albert Gregorio, yule kivulana maskini. Tulioana nilipokuwa na umri wa miaka 20, nami sijapata kusikitika kwamba nilimchagua huyo.

Albert nami tulifurahi pamoja tukajitahidi tujipatie nyumba nzuri kwa ajili ya jamaa yetu iliyokuwa ikiongezeka. Tulikuwa na wavulana watatu na wasichana watatu. Albert alifuga farasi na alikuwa na magari ya kukokotwa na farasi ili atupatie riziki. Nyumba yetu katika Belmont ilikuwa ya kiasi, lakini tulikuwa jamaa yenye furaha na umoja mwingi.

Baada ya miaka kadha Albert alifungua nyumba ndogo ya kuwekea maiti katika Belmont, na kwa muda mrefu nyumba hiyo iliyoitwa Gregorio’s Funeral Home ikawa mashuhuri katika Observatory Street. Mume wangu alijulikana kuwa rafiki ya maskini, kwa maana hata ikiwa jamaa haikuweza kulipa pesa za maziko, Albert bado alifanya mipango kuwasaidia na mazishi.

SIKUTAKA MAMBO YA KIROHO

Wakati wa vita ya Ulimwengu ya Kwanza mtu mmoja aitwaye Evander J. Coward alikuwa Trinidad akavuta watu wengi kwa kuwatolea hotuba za Biblia. Alikuwa mmojawapo Wanafunzi wa Biblia, ambao sasa wanaitwa Mashahidi wa Yehova. Dada yangu Annie, na mumewe, Wilfred Ferreira, na vilevile mama yangu, walianza kushirikiana na Wanafunzi wa Biblia. Wilfred, ambaye alijulikana kama Willie, akawa Mwanafunzi wa Biblia mwenye juhudi nyingi, akasafiri kwenda visiwa vile vingine akihubiri. Ingawa nilikuwa nikimsikiliza Willie, sikuitikia.

Mwaka 1931 mume wangu alipatwa na ugonjwa wa baridi ya mapafu (pneumonia). Alijitahidi mpaka mwisho kuinuka na kutembea-tembea, lakini baada ya muda mfupi alizimia akafia nyumbani mwetu. Yeye hakuwa Mwanafunzi wa Biblia wakati wo wote, lakini kwangu alikuwa mume mwema sana. Nilisikitika sana alipokufa. Sasa mzigo wa kuitunza nyumba ukawa wangu peke yangu. Nikawa nikitengeneza blausi, marinda na vitu vingine, na kuviuza kwa bei nafuu. Ndivyo nilivyojipatia riziki miaka mingi.

KUZIITIKIA KWELI ZA BIBLIA

Miaka ya mwisho ya 1940 ndipo mwishowe nilipojua mahali ambapo kimbilio na tumaini la kweli lingepatikana, ingawa ningaliweza kujua hivyo mapema zaidi kama ningalitaka. Mashahidi wa Yehova walikuwa wamefungua shule ya pekee katika United States inayoitwa Gileadi, kuzoeza wamisionari waende nchi nyingine na kufundisha Biblia watu wo wote waliotaka, bila malipo. Mwaka 1946 baadhi ya wamisionari hao walitumwa Trinidad.

Mmoja wao alikuwa kijana mwanamke aitwaye Ann Blizzard. Mimi nilimpenda nikakubali toleo lake la kujifunza nami Biblia, tena nilizithamini kweli nilizoanza kujifunza. Siku moja tulijifunza Petro wa Pili 3:13, panaposema hivi: “Lakini, kama ilivyo ahadi yake, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake.” Nilifurahi sana nilipofikiria mbingu na dunia hiyo yenye haki. Nilitaka niwe katika mpango huo wenye haki. Wakati huo nilikuwa na umri karibu wa miaka 76.

Nilimtia moyo binti-mjukuu wangu, ajiunge nasi katika funzo langu. Alifurahi, naye karibuni akazikubali kweli za Biblia tulizokuwa tukijifunza. Mwishowe nilianza kuhudhuria mikutano yote ya Mashahidi wa Yehova katika 6-B Norfolk Street katika Belmont, nikaifurahia sana.

Nilifurahia pia kueleza wengine mambo mazuri sana niliyokuwa nikijifunza. Niliona mambo mengi ya kupendeza nilipokuwa nikitembelea watu nyumba kwa nyumba na kuongoza mafunzo ya nyumbani ya Biblia. Nakumbuka kwamba nilijifunza Biblia na Alma Ford. Mwanamke huyo aliikubali kweli kwa moyo mwema, akawa shahidi wa Yehova mwenye bidii.

Nilimtia moyo Ivy binti yangu, aliyeishi San Fernando karibu maili 30 kusini mwa Port of Spain, ajifunze na wamisionari wa huko. Alikubali, kisha yeye na binti yake Jean wakazikubali kweli za Biblia walizojifunza, na mwishowe hata mumewe Jack alizikubali. Pita, mwana-mjukuu wangu, alisikiliza akaamini. Nakumbuka nilivyofurahi siku hiyo, Novemba 25, 1950, wakati Ivy binti yangu na binti-wajukuu wangu wawili, Joy na Jean, walipobatizwa wote katika kusanyiko la Mashahidi wa Yehova.

MAADUI, UZEE NA KIFO

Miaka yote ya 1950 na mwanzoni mwa miaka ya 1960 nilihudhuria mikutano na kushiriki kuhubiri na kufundisha watu kweli za Biblia karibu na nyumbani kwangu. Ndipo udhaifu wa uzee uliponipata sana. Mimi najua sana kwamba Zaburi 90:10 yasema kweli: “Siku za miaka yetu ni miaka sabini, na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; na kiburi chake ni taabu na ubatili.”

Lililoniongezea taabu ni kwamba, mmojawapo wana wangu aligonjweka sana asipate nafuu. Wakati ule ule alipoonekana kama apata nafuu, ndipo alipogonjweka tena akafa. Ingawa nilijua kwamba Biblia yaahidi ufufuo na dunia ya paradiso, nilihuzunika sana kwa kufiwa na Cecil.

Halafu siku moja nilipokuwa nimepita umri wa miaka 96, nilianza kufungua dirisha katika sebule letu. Kwa ghafula, niliteleza nikaanguka, nikaumia sana. Daktari aliitwa akapanga bila kukawia kunipeleka kwenye makao ya kutunzia watu. Nilikuwa nimevunjika kiuno kwa hiyo nikalazimika kupasuliwa.

Madaktari na wauguzi wa kike walinikaza nitiwe damu mishipani, wakisema ningekufa tu nisipokubali. Nilikataa, kwa sababu Neno la Mungu lakataza kula damu. (Mwa. 9:4; Law. 17:10; Matendo 15:20, 29) Namshukuru Yehova kwamba niliweza kuendelea kuwa hai nilipopasuliwa na kuendelea kupona. Wakati uo huo, mabibi wawili wazee waliokuwa katika umri wa miaka 80 walikuwa katika makao ayo hayo kwa sababu ya kuvunjika viuno. Wote wawili walikubali kutiwa damu mishipani. Wote wawili walikufa.

Basi, mguu mmoja ulikuwa mfupi zaidi ya mwingine nilipopona kiuno. Nilitengenezewa kiatu cha pekee nikapewa chombo cha kutembelea. Kwa kutumia vitu hivyo niliweza kutembeatembea nyumbani mwangu na kufanya kazi nyingi za nyumba na kupika vyakula. Ulikuwa wakati wenye magumu, lakini washiriki wa kundi la kwetu walinifadhili wakanitia moyo sana. Niliendelea kutamani sana niokoke pigano la Har–​Magedoni niingie katika taratibu mpya ya Mungu.

Ndipo mwana’ngu Vivian alipokufa, na muda mfupi baadaye Kenneth pia akafa, nikaachwa bila wana. Dada zangu watatu walikuwa wamekufa pia. Vifo vyote hivyo vya wapendwa wangu vilinihuzunisha mno, lakini najua nitawaona watakapofufuliwa. Natazamia pia kumwona mume wangu tena katika taratibu mpya ya Mungu yenye haki. Tumaini hilo la Biblia limenipa ushujaa mwingi. Nafurahia kusoma Zaburi 56:11: “Nimemtumaini Mungu, sitaogopa.”

Kwa sasa mimi ni dhaifu sana mwilini, maana siwezi kwenda nje nikiwa peke yangu. Nyakati nyingine nafikiri ni afadhali kufa katika umri huu. Sikuzote nilitaka nipite Har–​Magedoni nikiwa hai, lakini huenda isiwezekane katika umri nilio nao. Kwa hiyo natazamia kufufuliwa wakati ambao furaha zangu zote zitatimizwa na wakati ambao hali za sasa zenye kuhuzunisha hazitakumbukwa kamwe.​—Ufu. 21:3, 4.

[Picha Louisa Gregorio katika ukurasa wa 296]

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki