Mwenye Hekima Alikuwa na Maana Gani?
HEKIMA inaweza kumfaa sana mtu aliye nayo. Mfalme Sulemani aliandika akauliza, “Ni nani aliye kama mwenye hekima? Naye ni nani ajuaye kufasiri neno? Hekima ya mtu humng’ariza uso wake, na ugumu wa uso wake hubadilika.”—Mhu. 8:1.
Mtu mwenye hekima kweli kweli anakuwa hana kifani katika jamii ya kibinadamu. Mtu wa pekee aliye kama yeye ni yule aliye na hekima pia. Yeye anajua “kufasiri neno,” yaani, ana busara inayohitajiwa ili kutatua matatizo yanayofadhaisha watu maishani.
Hata uso wa mwenye hekima unapendeza. Uso wake unang’aa kuonyesha kwamba ana furaha ndani na ametosheka. Kwa hiyo, badala ya kuwa na uso uliokunjamana na wenye kutisha, uso wake unapendeza watu.
Jinsi ya Kuvumilia Utawala wa Kibinadamu Usiokamilika
Kwa kuwa Sulemani alikuwa mfalme, ilifaa sana akatoa mashauri juu ya jinsi ya kutendea watawala mambo ya hekima. Alisema: “Uishike amri ya mfalme; na hiyo kwa sababu umeapa kwa Mungu. Usifanye haraka kutoka mbele ya uso wake; usiendelee kufanya lililo baya; maana yeye hufanya lo lote limpendezalo. Kwa kuwa neno la mfalme lina nguvu; naye ni nani awezaye kumwambia huyo, Wafanya nini?”—Mhu. 8:2-4.
Katika Israeli ya kale, wazee wenye kuwakilisha taifa hilo wangeweza kufanya agano na mfalme, wakubali kushikamana naye nyakati zote. Kwa mfano, tunasoma hivi juu ya Daudi: “Wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni; naye mfalme Daudi akapatana pao huko Hebroni mbele za [Yehova].” (2 Sam. 5:3) Kwa hiyo, kuasi amri ya mfalme kungekuwa na maana ya kukosa kushikamana na kiapo kilichofanywa mbele za Yehova. Kwa upande mwingine, utii ulionyesha heshima kwa Mungu wa kweli, ambaye agano lilifanywa mbele zake. Vivyo hivyo, Wakristo wa kweli wanaendelea kunyenyekea serikali za ulimwengu kwa sababu ya kumheshimu Yehova, huku wakijua kwamba Yeye ndiye ameziruhusu serikali hizo ziwepo. —Rum. 13:1, 2.
Shauri ambalo Sulemani anatupa kwa kutuambia tusiwe na haraka ya kuondoka mbele za mfalme linaendelea kuelezwa katika Mhubiri 10:4: “Roho yake mtawala ikiinuka kinyume chako, usiondoke mara mahali pako ulipo; kwa maana roho ya upole hutuliza machukizo yaliyo makubwa [au, “dhambi kubwa, NW].” Huenda mtu akasahihishwa au kurudiwa na mkuu. Huenda akachukizwa na jambo hilo na kutaka kuacha cheo alicho nacho au hata kubadili maoni yake juu ya mtawala huyo. Lakini, Sulemani anapendekeza watu wasiachane na wasimamizi wao wala wasijiuzulu katika vyeo vyao haraka haraka. Kanuni iyo hiyo inaweza kutumiwa leo katika uhusiano wa matajiri na wafanya kazi wao.
Mfalme Sulemani mwenye hekima anaendelea kushauri watu ‘wasiendelee kufanya jambo’ linaloonekana na mtawala kuwa baya. Kwa sababu ya mamlaka aliyo nayo, agizo la mfalme lina maana kuliko neno la ye yote wa raia zake. Sauti yake ndiyo yenye amri; mamlaka yake si ya kujibiwa. Ndiyo sababu hakuna mtu awezaye kumwuliza kwa ukaidi, “Wafanya nini?”
Mtu anayeendelea kufuata sheria hapaswi kumwogopa mtawala. Sulemani anasema: “Aishikaye amri hatajua neno baya.” (Mhu. 8:5) Raia mtiifu hataona “neno baya” kwa maana hatapata adhabu inayotokana na kuasi sheria ya mfalme. Shauri la mwenye hekima linalingana na maneno ya mtume Paulo: “Amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu. Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake.”—Rum. 13:2, 3.
Lakini namna gani ikiwa mtawala ni dhalimu’ Sulemani aliendelea kusema yafuatayo, akitaja hali yake mwenyewe: “Moyo wa mwenye hekima hujua wakati na hukumu. Kwa maana kwa kila shauri kuna wakati na hukumu; kwa sababu mashaka ya mwanadamu yaliyo juu yake ni makubwa; kwa kuwa hajui yatakayokuwako; kwa maana ni nani awezaye kumweleza jinsi yatakavyokuwa?”—Mhu. 8:5-7.
Mwenye hekima hafanyi haraka kuasi. Kwa kuwa moyo wake unaongozwa na hekima, anajua kwamba kuna wakati unaofaa wa kuchukua hatua, na kuna njia inayofaa ya kuvumilia mtawala, mwonezi. Kumwasi waziwazi kungekuwa kama kutafuta msiba. Kwa upande mwingine, uamuzi mzuri utazuia mtu asichukue hatua wakati usiofaa. (Zab. 37:1-7) “Kila jambo” lina wakati na uamuzi (au hukumu) au njia inayofaa kulishughulikia. Basi mtu anajitafutia matata akipuza uhakika huo na kuchukua hatua za haraka haraka. Wanadamu wasiokamilika wana matatizo ya kuwatosha, kwa hiyo hawahitaji kuongezewa mengine na mtu mwenye haraka haraka, anayepuza uhakika wa kwamba “kwa kila shauri kuna kati na hukumu.” Tena, hakuna mtu anayeweza kuwa na hakika juu ya mambo yatakayotokea wakati ujao. Hata wakuu wanakufa. Kukumbuka hivyo kunaweza kusaidia mtu avumilie hali yenye kumtatiza. Mtawala mwonezi hawezi kuendelea kutawala milele. Kila kitu katika taratibu hii isiyokamilika kina mwisho wake.
Kuchunguza Sana Utawala wa Kibinadamu Wenye Uonezi
Baada ya Sulemani kufanya uchunguzi mwingi, ndipo alipokata maneno juu ya utawala wa mwanadamu wenye uonezi. Yeye alifikiria sana utawala wote wa kibinadamu na matokeo unayoletea wanadamu. Kwa hiyo angeweza kusema hivi: “Mambo hayo yote nimeyaona, nikatia moyo wangu katika kila kazi iliyofanyika chini ya jua. Kuna wakati ambapo mtu mmoja anayo mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasara yake.”—Mhu. 8:9.
Walakini, watawala waonezi hawawezi kuendeleza utawala wao milele. Sulemani aliendelea kusema: “Pia [baada ya kuona mwanadamu akitawala mwenzake kwa hasara yake] nikaona waovu wamezikwa, nao wamefika kaburini; tena waliofanya mema wameondoka katika patakatifu, nao wamesahauliwa mjini. Hayo nayo ni ubatili.” (Mhu. 8:10) Wakati walipokuwa hai, waovu walikuwa wakiingia patakatifu na kutoka, napo patakatifu hapo palikuwa mji wa Yerusalemu, na hekalu la Yehova siku za Sulemani. (Mt. 24:15) Wasingalipaswa kuzoea uovu mahali hapo. Wanapozikwa wanauacha kabisa. Waovu wajapokuwa na cheo kikubwa, wangekufa, wazikwe na kusahauliwa baada ya muda mfupi na watu waliokuwa hai katika mji wa kwao. Hivyo ndivyo maisha yao ya kutawala watu kwa kuwaonea yangekuwa ya ubatili, ya bure tu.