Je! Uhusiano Pamoja na Mungu Unatufaidi Sasa
“[Yehova] yu karibu na wote wamwitao, . . . naye atakisikia kilio chao na kuwaokoa.”—Zab. 145:18, 19.
1, 2. Maneno ya Daudi yanatuonyeshaje hali bora ya mtu aliye na uhusiano wa karibu sana na Mungu?
MFALME DAUDI, aliyekuwa vilevile nabii alisema juu ya furaha ya mtu ambaye Mungu amhesabia kuwa na “haki pasipo matendo,” akisema: “Heri waliosamehewa makosa yao na waliositiriwa dhambi zao. Heri mtu yule ambaye [Yehova] hamhesabii dhambi.” (Rum. 4:6-8; Zab. 32:1, 2) Mtu kama huyo anasamehewa dhambi zake—anakuwa safi machoni pa Mungu. Yehova anamkubalia kuwa msiri wake, akimwona kuwa mtu asiye na udhalimu, kwa kuwa kutokuwa mwenye haki kunamtenganisha mtu na Mungu.
2 Akitaja wema wa kuwa na msimamo kama huo pamoja na Mungu, Daudi aliendelea kusema hivi: “Ee nafsi yangu, umhimidi [Yehova], wala usizisahau fadhili zake zote, akusamehe maovu yako yote, aukomboa uhai wako na kaburi, akutia taji ya fadhili na rehema, aushibisha mema uzee wako, ujana wako ukarejezwa kama tai.”—Zab. 103:2-5.
RAFIKI ZA MUNGU
3. (a) Wale ambao wamesamehewa dhambi zao kupitia kwa dhabihu ya Kristo wanaweza kuruhusiwa wamwiteje Mungu? (b) Mtu huyo anahifadhije msimamo huo?
3 Mtu kama huyo aweza kumwita Mungu Baba. (Mt. 6:9) Anapokosa na kutenda dhambi, kama wafanyavyo wanadamu wote, akijua kwamba amefanya hivyo, aweza kumsihi Mungu amsamehe na kumsafisha, hivyo auhifadhi msimamo huo mwema. Mtume Yohana aliandika juu ya hili: “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.”—1 Yohana 1:8, 9.
4. Kristo alionyeshaje uhusiano wa karibu aliokuwa nao pamoja na wanafunzi wake?
4 Katika maisha ya kila siku, uhusiano wa karibu sana na Mungu ‘unashibishaje mema uzee wako’? Nao uhusiano huo ukoje? Yesu alifunua namna ya uhusiano wa karibu sana aliokuwa nao pamoja na mitume wake waaminifu alipowaambia: “Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.” (Yohana 15:15) Zaidi ya hayo, “haoni haya kuwaita ndugu zake.” (Ebr. 2:11) Ni kweli kwamba Biblia inawataja Wakristo kuwa watumwa wa Mungu na Kristo. Walakini mara nyingi Biblia inatumia mitajo ya kibinadamu, yaani, mitajo tunayofahamiana nayo, ili tuyafahamu mambo fulani. Sababu yake ni kutokamilika kwetu na kutokomaa katika maarifa na ufahamu wa Kikristo. (Linganisha Warumi 6:19; 1 Wakorintho 3:1, 2; angalia pia Luka 17:7-10.) Kwa hiyo, ijapokuwa neno “mtumwa” linatumiwa, kwa kweli Yesu Kristo anatupenda sisi kuliko vile bwana ye yote amepata kumpenda mtumwa wake, naye anatamani tuhakikishwe kwamba anatuona kuwa rafiki zake.
5. Yesu alifunuaje uhusiano wa karibu na upendo wa Mungu kwa wale wanaompenda?
5 Yesu alionyesha kwamba vilevile Mungu yu karibu na wale wanaokuja kwa Kristo, aliposema: “Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake.” (Yohana 14:23) Mtu angetamani uhusiano gani ulio karibu zaidi? (Linganisha Ufunuo 3:20.) Baada ya kuwaambia wanafunzi wake kwamba angeenda zake akawe pamoja na Baba yake, Yesu alionyesha kwamba Mungu yuko karibu zaidi nao kuliko walivyodhania aliposema: “Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu. Hayo nimesema nanyi kwa mithali; saa yaja ambapo sitasema nanyi tena kwa mithali, lakini nitawapa waziwazi habari ya Baba. Na siku ile mtaomba kwa jina langu; wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba; kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba.”—Yohana 16:23-27.
ULINZI KUTOKANA NA KUFANYA MAKOSA
6, 7. (a) Je! kwa kweli Mungu anamjaribu mtu atende dhambi? (b) Yeye anatuwekeaje mlinzi na mngojeaji juu yetu?
6 Bila shaka mtu anayefurahia uhusiano wa karibu sana na Mungu atalindwa asiangukie katika mabaya. Yesu alisema kwamba inatupasa kusali kwa Mungu hivi: “Usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu.” (Mt. 6:13) Hiyo inalingana na sala ya mtunga zaburi: “Ee [Yehova], uweke mlinzi kinywani pangu, mngojezi mlangoni pa midomo yangu. Usiuelekeze moyo wangu kunako jambo baya.”—Zab. 141:3, 4.
7 Ijapokuwa aliruhusu Kristo apatwe na majaribu, jambo ambalo linawapata watu wote, Mungu hamjaribu ye yote kwa maovu. (Yak. 1:13) Kwa upande mwingine, yeye hatamzuia mtu kwa nguvu asichague mwendo mbaya. Mahali pake, yanapotokea majaribu, Mungu anamlinda mtu huyo aliye na uhusiano wa karibu naye kwa kufumbua macho yake wazi aione hatari inayomwelekea. ‘Anamwekea mlinzi na mngojezi juu yake.’ Mtu anayeshirikiana na Mungu atapewa maonyo yenye nguvu.
8. Mungu anajibuje sala, “Usitutie majaribuni”?
8 Kwa mfano, mtu anayepatwa na jaribu la kuiba au la kuwa mchongezi atakumbushwa mara hiyo juu ya mambo ya hakika na yenye kushtua: tendo hilo baya litaharibu uhusiano wake mwema pamoja na Mungu; matendo kama hayo yanapingana na sheria ya upendo; yanaleta lawama juu ya jina zuri la Mungu na Kristo, kwa kuwa Mkristo huyo anajidai kuwawakilisha; akijiachilia ashindwe na tamaa hizo mbaya atajiletea lawama yeye mwenyewe pamoja na wapenzi wake; ataliaibisha kundi la Kikristo, ambalo yeye ni mshiriki wake. Dhamiri njema aliyoomba alipoiamini dhabihu ya Kristo inayofunika dhambi itaumizwa sana. Mawazo haya yenye kuonya yanatokea kwa sababu Mkristo anaisoma Biblia sikuzote na kwa kuongozwa na roho ya Mungu, au nyakati nyingine kwa kuonywa na Mkristo mwenzake. Yatamzuia asifuate kwa upumbavu tamaa za kimwili, kama vile ingalikuwa kwa mtu asiyelindwa na uhusiano mwema na Mungu.—Linganisha Mithali 7:22, 23 na yaliyompata Daudi, katika 1 Samweli 25:32-35.
UHURU WA MAWAZO NA WA KUSEMA
9. Uwezo wa Neno la Mungu unaonyeshwaje tunapochunguza mataifa ya Jumuiya ya Wakristo?
9 Baraka kubwa inayotokana na kuwa na uhusiano mwema na Mungu ni ile ya kufurahia uhuru zaidi wa mawazo na wa kusema. Ili kupata ushuhuda wa uwezo wa Neno la Mungu katika jambo hili, ebu tazama mataifa yanayoitwa Jumuiya ya Wakristo. Yajapokuwa kwa kweli hayajakuwa karibu na Mungu, kwa kawaida yameruhusu Neno la Mungu lienezwe kwa uhuru katika muda wa karne mbili zilizopita. Biblia imepatikana katika kila nyumba, na ijapokataliwa na wengi sasa, kumekuwako wanaume, hata kati ya wale walio na vyeo vya utawala, ambao wamejaribu kutumia kanuni bora za adili za Biblia. Hilo limesaidia sana kuleta uhuru wa mawazo na wa kusema nalo limewafungua watu kutokana na utumwa wa mapokeo ya kidini na ushirikina wa enzi zilizokuwa na giza. Hali za maisha ya watu katika nchi hizi imepata maendeleo kulingana na kadiri ya uenezaji wa Biblia.
10. (a) Wanasayansi na wengine wanaojifunza maajabu ya uumbaji wamemfahamu Mungu kadiri gani? (b) Mtu anayetaka kweli kweli kuwa na uhusiano wa karibu na Mungu lazima afanye nini?
10 Ijapokuwa uhusiano kama huo wa vivi hivi pamoja na Mungu kupitia kwa Neno lake huleta nuru na hali bora za maisha, watu ambao huisoma Biblia kweli kweli na kuitumia kama uongozi maishani mwao wanafaidika zaidi. Mzee wa ukoo Ayubu anaonyesha kwamba kunahitajiwa zaidi ya maarifa ya juujuu tu ya Mungu. Baada ya kutaja juu ya mambo ya hakika ya uumbaji yenye kustaajabisha ambayo wanasayansi wanaweza kufahamu na kuyaeleza baada tu ya kufanya uchunguzi mwingi sana, anasema hivi: “Tazama, hivi ni viunga tu vya njia [za Mungu]; na jinsi yalivyo madogo manong’ono tuyasikiayo katika habari zake!” Baadaye, Ayubu anaonyesha kwamba ili kupata hekima ya kweli tunahitajiwa kujifunza zaidi ya “viunga tu vya njia zake”—kitu kilicho zaidi ya mambo ya hakika tu ya kisayansi. Lazima tupate kujua wema wa utu wa Mungu, na kumwogopa kwa kuwa Ndiye anayezitegemeza kanuni bora, tena inatupasa kufuata kanuni hizi. Hekima hii inaweza kupatikana tu kwa kujifunza Neno lake. Ayubu asema hivi: “Kumcha [Yehova] ndiyo hekima, na kujitenga na uovu ndio ufahamu.” (Ayubu 26:14; 28:28) Mtunga zaburi anaandika hivi kwa habari ya mtu ambaye hutafuta kuwa na uhusiano na Mungu kwa kuiangalia Biblia: “Heri mtu yule umchaguaye, na kumkaribisha akae nyuani mwako. Na tushibe wema wa nyumba yako.”—Zab. 65:4.
NANI ANAYEWEZA KUFURAHIA UHUSIANO WA KARIBU SANA NA MUNGU?
11, 12. Ni mtu wa namna gani atakayekubaliwa na Mungu kuwa na uhusiano wa karibu na wa urafiki pamoja naye?
11 Kwa hiyo, uhusiano ambao katika huo Mungu anakubali mtu kuwa rafiki yake ungekuwa na baraka nyingi na zenye kudumu. Mtu ambaye angechaguliwa na Mungu awe na uhusiano wa karibu sana kama huo anaelezwa katika Zaburi ya 15:
“[Ee Yehova], ni nani atakayekaa
Katika hema yako?
Ni nani atakayefanya maskani yake Katika kilima chako kitakatifu?
Ni mtu aendaye kwa ukamilifu,
Na kutenda haki.
Asemaye kweli kwa moyo wake,
Asiyesingizia kwa ulimi wake,
Wala hakumtenda mwenziwe mabaya,
Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa,
Bali huwaheshimu wamchao [Yehova].
Ingawa ameapa kwa hasara yake,
Hayabadili maneno yake.
Hakutoa fedha yake apate kula riba,
Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia.
Mtu atendayo mambo hayo Hataondoshwa milele.”—Zab. 15:l-5
12 Ni mtu wa namna hiyo tu atakayepata kumwogopa Mungu na kupata kumjua kweli kweli. Rafiki kama huyo wa Mungu anapatwa na magumu ya kawaida yanayowapata watu wote. Walakini yeye haachwi bila msaada.
MSAADA WAKATI WA UGONJWA
13. Mungu anamfanyiaje Mkristo aliye mgonjwa sana, naye anakuonaje kuvumilia ugonjwa?
13 Huenda Mkristo akawa mgonjwa sana. Mara nyingi, ugonjwa wa mwili unakuwa na matokeo mabaya katika afya ya kiroho ya mtu. Inakuwa vigumu kuendeleza usawa mzuri wakati wa ugonjwa. Mungu anamhurumia sana mgonjwa huyo. Na zaidi ya hayo yeye anamsaidia. Mtunga zaburi anasema hivi: “[Yehova] atamtegemeza alipo mgonjwa kitandani. Katika ugonjwa wake umemtandikia.” (Zab. 41:3) Mungu haahidi kwamba mtumishi wake atarudia afya kamili katika hali zote. Walakini anamhakikishia Mkristo kwamba atamtegemeza na kumwezesha kuvumilia ugonjwa wake. Maneno yanayotumiwa na mtunga zaburi yanamkumbusha mtu juu ya mwuguzi wa kike ambaye humwangalia mgonjwa wakati wote ili kila sehemu ya mwili ikae vizuri, au mzazi anayemtunza mtoto mgonjwa kwa upendo, akimweka katika hali nzuri, na kumsafisha, kubadilisha matandiko ya kitanda chake na kukilainisha, hivi kwamba anajisikia kuburudishwa na kuchangamshwa. Ikiwa itamfaa mtu huyo, Mungu aweza kumwinua mtu huyo kutoka katika kitanda chake cha ugonjwa na kukibadilisha kuwa kitanda cha kupatia afya. Walakini hata asipopona, Mungu anafanya mambo yote yatendeke kwa faida yake. (Rum. 8:28) Anatiwa nguvu kiroho, na kuvumilia ugonjwa huo, akiuona kama namna ya adabu au mazoezi yanayomgeuza ili awe Mkristo mwenye nguvu zaidi, na mwenye kuwafikiria na kuwahurumia wengine zaidi. Yeye anakumbuka kwamba Kristo naye aliteseka. Yaliyompata Yesu yalimfaidi na yalitufaidi sisi pia. Mungu hakumwacha Yesu, nayo zawadi yake kwa sababu ya kuvumilia kwa ustahimilivu ilikuwa kubwa.—Ebr. 4:15; 5:8, 9.
MSAADA WAKATI WA MATESO
14. Je! Inatupasa kushangaa mateso yakitupata, nasi tuna uhakikisho gani wa kupata msaada?
14 Huenda upinzani hata mateso yakatokea kwa sababu ya Mkristo kuchukua msimamo wake upande wa kanuni za Biblia. Hilo lilimpata Daudi, ambaye aliwindwa kama mnyama na Mfalme Sauli, akasalitiwa na rafiki yake mkubwa nao wanawe wakamfanyia hila alipokuwa mgonjwa. (1 Sam. 24:2; Zab. 41:9; 2 Sam. 15:31; 1 Fal. 1:1, 5) Hata hivyo kutokana na yaliyompata, yeye aliweza kuandika hivi: “Mradi [Yehova] atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, atanisitiri katika sitara ya hema yake.” “Baba yangu na mama yangu [wakiniacha], [hata Yehova] atanikaribisha kwake.”—Zab. 27:5, 10.
UHURU WA KUTOOGOPA MAMBO YA KIUCHUM!
15. Sababu gani haimpasi Mkristo kuogopa kwamba atakosa kupata mambo ya lazima ya maisha?
15 Hata hali ya uchumi haipaswi kumhangaisha sana Mkristo. Mtume Paulo aliandika hivi: “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema, [Yehova] ndiye anisaidiaye, sitaogopa; mwanadamu atanitenda nini?” (Ebr. 13:5, 6) Daudi vilevile alitangaza hivi: “Wamtafutao [Yehova] hawatahitaji kitu cho chote kilicho chema.” Tena, alisema hivi: “Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, lakini sijamwona mwenye haki ameachwa, wala mzao wake akiomba chakula.”—Zab. 34:10; 37:25.
AMANI, NA FURAHA YA KUWASAIDIA WENGINE
16. Ni gani nyingine za faida zenye thamani sana alizo nazo Mkristo sasa kwa sababu ya kuwa na uhusiano na Mungu?
16 Kati ya faida zilizo kubwa zaidi za wakati huu za kuwa na uhusiano wa karibu sana na Mungu ni amani ya akili na kutoogopa mambo yanayoupata ulimwengu na mtu binafsi. Mkristo ambaye amepata kuona uangalizi wenye upendo wa Mungu pamoja na ulinzi wake kwa wale walio na uhusiano wa karibu sana naye, ana tumaini hakika la mambo bora yajayo. Kulingana na ahadi ya Mungu, yeye anatazamia mbingu mpya na dunia mpya ambamo haki itakaa. (2 Pet. 3:13) Yeye anatumaini kwamba, ajapokufa, atafufuliwa katika taratibu hiyo ya mambo yenye haki. (Matendo 24:15) Kila siku yeye anaona uhakika wa yale yaliyosemwa na mtume Paulo kutokana na aliyoyaona: “Amani ya Mungu ipitayo akili zote [kila kitu kilicho chema ambacho Mkristo angeweza kuwazia], itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”—Flp. 4:7.
17. Ni furaha gani nyingine anayoweza kuwa nayo Mkristo kwa sababu ya kuwa na uhusiano wa karibu sana na Mungu?
17 Akiufurahia uhusiano huu mwema, Mkristo anaweza kuwasaidia wengine wajifunze mambo haya. Hakuna furaha iliyo kubwa zaidi kuliko ile ya kuwasaidia wengine waijue kweli ya Mungu na kuvutwa wawe na uhusiano na Yehova na Mwanawe. Ndiyo sababu Mashahidi wa Yehova huwatembelea watu nyumbani kwao duniani pote, na kuwaambia “habari njema,” na kuwatembelea tena waongoze mafunzo ya Biblia. Hivyo, wale wapya wanapoletwa washirikiane na kundi la Kikristo, wao, pia, wanaona furaha ya kumjua sana Baba na yeye aliyempeleka,. Yesu Kristo. Kwa hao wote, ‘hilo lamaanisha uzima wa milele.’—Yohana 17:3. —Kutoka The Watchtower Apr. 15, 1979,
[Picha katika ukurasa wa 19]
Mungu anamlinda mtu aliye na uhusiano wa karibu naye kwa kufumbua macho yake yaone waziwazi hatari inayomwelekea
[Picha katika ukurasa wa 21]
Kama vile mzazi amtunzavyo kwa upendo mtoto aliye mgonjwa Mungu huwatendea mema Wakristo walio wagonjwa